[AR - BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HE - HR -
HU - LA - LV - PT - SW - ZH]
Tamko juu ya
uhusiano wa Kanisa
na dini zisizo za kikristo
Paulo Askofu
Mtumishi wa watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima
Utangulizi
1. NYAKATI ZETU (Nostra Aetate), ambapo wanadamu wazidi kuunganika siku kwa siku na unakua utegemeano kati ya watu wa mataifa mbalimbali, Kanisa ladhamiria kwa makini tabia ya uhusiano wake na dini zisizo za kikristo. Ni wajibu wake kuhamasisha umoja na upendo kati ya wanadamu, naam kati ya mataifa ya watu; ndiyo sababu kwanza kabisa linachunguza hivi yale yote ambayo kati ya watu ni ushirika na yawaongoza kuishi pamoja.
Maana, watu wote ni jumuiya moja tu. Wenyewe, asili yao ni moja, kwa sababu Mungu aliwaweka wote wakae juu ya uso wa nchi yote[1]; tena wao wanacho kikomo kimoja tu, yaani Mungu, ambaye maongozi yake, ushuhuda wa wema wake, na azimio lake la wokovu yawaelekea watu wote[2], hadi wateule wapate kukusanyika katika Mji Mtakatifu, ambao utukufu wa Mungu utautia nuru, na ambapo mataifa watatembea katika nuru yake[3].
Watu hungoja majibu kutoka kwa dini mbalimbali kuhusu vitendawili vigumu vya hali ya wanadamu, ambavyo mpaka leo vinafadhaisha sana mioyo ya watu: “Binadamu ni nini?”, “Maana na mwisho wa maisha yetu ndio nini?”, “Tendo jema na dhambi ni nini?”, “Chanzo na lengo la mateso ni nini?”, “Njia gani inatupeleka kwenye furaha ya kweli?”, “Nini mauti, na hukumu, na kulipwa adhabu au tuzo baada ya kifo?”, hatima, “Maana yake nini lile fumbo lisiloelezeka la maisha yetu, yaani, ni wapi tutokako, na ni wapi kule tuendako?”.
Dini mbalimbali zisizo za kikristo
2. Tangu zamani za kale mpaka leo pamekuwepo katika mataifa mbalimbali hisi fulani ya ule Uwezo usioonekana ambao uko katika mkondo wa mambo na matukio ya maisha ya kibinadamu. Pengine hutambulika kwamba Uwezo huo ni Umungu mkuu, au hata ni Baba. Ni hisi na utambuzi vinavyopenyeza katika maisha ya [watu] hisia za kidini. Dini zinazohusiana na maendeleo ya utamaduni, zajitahidi kujibu maswali hayohayo kwa matamko ya akili kali na kauli zenye ufasaha mwingi. Hivyo, katika Uhindu, watu huchunguza fumbo la umungu na kulieleza kwa njia ya hazina maridhawa ya hadithi na kwa njia ya majaribio makali ya falsafa. Wao hutafuta afua kutoka kwa taabu za utu wetu kwa namna mbalimbali za maisha ya kiasketi, kwa njia ya taamuli nzito au kwa kumkimbilia Mungu kwa upendo na imani. Katika Ubudha, kulingana na madhehebu yake mbalimbali, hukirika kule kutoweza kwa asili kwa ulimwengu huu geugeu, na kufundishwa njia ambayo watu, wakiifuata kwa moyo wa ibada na imani, waweza kujipatia hali ya afua kamili au kuifikia ile hali ya mwangaza mkuu, ama kwa njia ya juhudi zao wenyewe, au kwa msaada unaotoka juu. Hali kadhalika dini nyinginezo zilizopo ulimwenguni pote zatafuta kushinda, kwa namna moja au nyingine, mashaka yaliyomo mioyoni mwa watu, kwa kushauri njia, yaani mafundisho au kanuni za maisha na ibada za kidini.
Kanisa Katoliki halikatai yoyote yaliyo kweli na matakatifu katika dini hizo. Lenyewe laheshimu kwa sifa timamu namna zile za kutenda na kuishi, sheria zile na mafundisho yale ambayo, ingawa mara nyingi yanatofautiana na yale ambayo lenyewe laamini na kufundisha, hata hivyo, mara nyingine, yarudisha nuru ya mshale wa ule Ukweli wenye kumwangazia kila mtu. Walakini Kanisa lamtangaza na lazima liendelee kutangaza bila kukoma Kristo, ambaye ndiye “njia, ukweli na uzima” (Yn 14:6), na ambaye ndani yake wanadamu waona utimilifu wa maisha ya utauwa, na ambamo Mungu alivipatanisha vitu vyote na nafsi yake[4].
Kwa hiyo Kanisa linawahimiza wanawe ili, kwa busara na mapendo, kwa njia ya dialogia na ushirikiano na wafuasi wa dini nyinginezo, watoe ushuhuda wa imani na wa maisha ya kikristo, na tena watambue, wahifadhi na kukuza mema ya kiroho na ya kimaadili, na tunu za kijamii na za kitamaduni, ambazo zapatikana kati ya wasio wakristo.
Uislamu
3. Kanisa pia lawatazama kwa heshima Waislamu wanaomwabudu Mungu aliye mmoja, mwenye uhai na mwenye kuwepo, rahimu na mwenyezi, Muumba wa mbingu na dunia[5], aliyenena na wanadamu. Wenyewe hujitahidi kujiweka kwa moyo wote chini ya amri za kisiri za Mungu, kama alivyojiweka chini Ibrahimu, ambaye imani ya kiislamu kwa furaha inajihusisha naye. Ingawa hao hawamkiri Yesu kama Mungu, lakini wanamheshimu kama nabii; wanamsifu mama yake bikira Maria, na mara kwa mara pia humwomba kwa ibada. Aidha wanangoja siku ya kiyama, ambapo Mungu atawapatia thawabu yao wote watakaofufuliwa. Kutokana na hayo yote, wenyewe pia watathmini maisha ya kimaadili na wamtolea Mungu ibada hasa kwa njia ya sala, ya sadaka na ya saumu.
Hata ikiwa katika mkondo wa karne yalitukia magomvi na chuki kwa namna nyingi kati ya Wakristo na Waislamu, Mtaguso Mkuu huwasihi wote wayasahau yaliyopita na kujitahidi kweli kuelewana. Tena, huwasihi ili haki ya kijamii, tunu za kimaadili, amani na uhuru kwa ajili ya watu wote vihifadhiwe na kuhamasishwa kwa juhudi za pamoja.
Wayahudi
4. Mtaguso huu Mkuu, huku ukitafakari fumbo la Kanisa, hukumbuka kile kifungo ambacho hufungamanisha kiroho taifa la Agano Jipya na uzazi wa Ibrahimu.
Kanisa la Kristo linatambua na kufundisha wazi kwamba chanzo cha imani yake na cha kuteuliwa kwake, kutokana na fumbo la wokovu la kimungu, hupatikana tayari katika Mababu, na Musa, na Manabii. Lenyewe laungama kuwa waamini wote wa Kristo, walio wana wa Ibrahimu kwa habari ya imani[6], wameingizwa ndani ya wito wa Babu huyo; tena lakiri kuwa wokovu wa Kanisa umeaguliwa kifumbo katika ‘kutoka’ kwa taifa teule walipohama toka nchi ya utumwa. Ndiyo sababu Kanisa haliwezi kusahau kwamba limepokea ufunuo wa Agano la Kale kwa njia ya watu wale ambao Mungu – katika huruma yake isiyoelezeka – alipenda kufunga agano nao. Tena haliwezi kusahau kwamba linalishwa katika shina la mzeituni ule mwema, ambapo matawi ya mzeituni mwitu, yaliyo mataifa ya wapagani, yamepandikizwa juu yake[7]. Maana, Kanisa huamini kwamba Kristo, aliye amani yetu, aliwapatanisha Wayahudi na [watu wa] Mataifa kwa njia ya msalaba wake, na hivyo akawafanya hao wawili kuwa mmoja ndani ya nafsi yake[8].
Vilevile, Kanisa linayo sikuzote mbele ya macho yake maneno aliyoyasema mtume Paulo akinena juu ya watu wa ukoo wake, “[ambao ni Waisraeli] wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao; katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili” (Rum 9:4-5), mwana wa Bikira Maria. Nalo Kanisa lakumbuka pia kwamba katika taifa la Wayahudi walizaliwa Mitume, walio misingi na nguzo za Kanisa, na mlemle ulizaliwa ule umati wa wafuasi wa kwanza waliotangaza Injili ya Kristo ulimwenguni kote.
Maandiko Matakatifu yashuhudiavyo, Yerusalemu haikutambua majira ya kujiliwa kwake[9]; Wayahudi waliokuwa wengi hawakuikubali Injili, bali wengi wao waliipinga sana isienezwe[10]. Hata hivyo, Mtume [Paulo] husema kwamba Wayahudi, kwa ajili ya Mababu zao, huendelea kuwa wapendwa wake Mungu kwa sababu karama zake hazina majuto, wala mwito wake[11]. Pamoja na Manabii na pamoja na Mtume mwenyewe Kanisa langojea siku ile anayoijua Mungu peke yake, ambapo watu wote watamwimbia Bwana Mungu kwa sauti moja na “watamtumikia bega kwa bega” (Sof 3:9 Vulg.)[12].
Maadam urithi wa kiroho ulio wa shirika kwa Wakristo na kwa Wayahudi ni mkubwa namna hii, Mtaguso Mkuu hutaka kuhimiza na kuthibitisha ubora wa kufahamiana na kuheshimiana kati yao wawili, ambao hupatikana hasa katika mitaala ya Biblia na ya kiteolojia, na kwa dialogia ya kidugu.
Ni kweli kwamba wakuu wa Wayahudi pamoja na watumishi wao walijibidisha ili kufanya Kristo auawe[13]; lakini hata hivyo, siyo halali kuwalaumu moja kwa moja Wayahudi wote wa nyakati zile, wala Wayahudi wa sasa kwa ajili ya yale aliyotendewa [Yesu Kristo] wakati wa mateso. Tena, japo ni kweli kwamba Kanisa ndilo taifa jipya la Mungu, hata hivyo Wayahudi sharti wasinenewe kama watu waliokataliwa na Mungu, wala kama watu waliolaaniwa, kwa kudai ya kuwa hayo yatokana na Maandiko Matakatifu. Kwa hiyo, wote katika katekesi na katika mahubiri ya Neno la Mungu wajihadhari wasifundishe lolote lisilokubaliana na ukweli wa Injili na roho ya Kristo.
Aidha Kanisa, linalolaumu kila namna ya udhalimu dhidi ya mtu awaye yote, likikumbuka ule urithi ulio wa shirika na Wayahudi, na likisukumwa na visa visivyo vya kisiasa, bali vya kidini, yaani upendo wa kiinjili, linashutumu chuki na udhalimu na aina zozote za ukatili dhidi ya Wayahudi (
antisemitismus) wakati wowote [na utendekao] na yeyote yule.
Kanisa limetegemea sikuzote na linaendelea kutegemea kuwa Kristo, kwa ajili ya upendo wake mkuu, alikubali kwa hiari yake kuteswa na kufa kwa minajili ya dhambi za wanadamu wote, ili wote wapate wokovu. Hivyo ni wajibu wa Kanisa, katika mahubiri yake, kukiri kwamba msalaba wa Kristo kweli ni ishara ya upendo wa Mungu kwa watu wote, nao ndio chemchemi ya neema zote.
Udugu wa watu wote
5. Kweli hatuwezi kumwita Mungu kama Baba wa wote, iwapo hatukubali kuwatendea watu wote kama ndugu, walioumbwa kwa sura ya Mungu. Uhusiano wa mwanadamu na Mungu Baba na uhusiano wa mwanadamu na wanadamu wenzake vinafungamana mno, kiasi kwamba Maandiko Matakatifu husema: “Yeye asiyependa, hakumjua Mungu” (1Yoh 4:8).
Huondolewa, kwa hiyo, msingi wowote kwa nadharia au utendaji wa aina yoyote ile vinavyosababisha ubaguzi kati ya mwanadamu na mwenzake, kati ya taifa moja na jingine, mintarafu hadhi ya mwanadamu na haki zitokanazo nayo.
Ndiyo sababu Kanisa hulaumu ubaguzi wa namna yoyote kati ya wanadamu, na vilevile udhalimu utendekao kwa minajili ya ukabila au ya rangi, ya cheo au ya dini: hayo ni matendo yanayopingana kabisa na mapenzi ya Kristo. Kwa hiyo Mtaguso Mkuu, kwa kuzifuata nyayo za Mitume Watakatifu Petro na Paulo, huwasihi sana wakristo ili, “wakiwa na mwenendo mzuri kati ya mataifa” (1Pet 2:12), kama yamkini, kwa upande wao, wakae katika amani na watu wote[14], ili wapate kuwa kweli wana wa Baba aliye mbinguni[15].
Mambo yote yaliyoamuliwa katika tamko hili, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 28 Oktoba 1965
Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki
(zinafuata sahihi za Mababa)