Index

Back Top Print

[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya Ekumeni

 Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

  

UTANGULIZI

 

1. Kuhamasisha URUDISHAJI WA UMOJA (Unitatis Redintegratio) kati ya Wakristo wote ni kusudi mojawapo kubwa la Mtaguso Mkuu wa Vatikano II. Kristo Bwana alianzisha Kanisa moja na pekee; walakini madhehebu mengi ya kikristo yanajieleza mbele ya watu kuwa yenyewe ni urithi halisi wa Yesu Kristo, wote wanathibitisha kuwa wenyewe ni wafuasi wa Bwana, lakini wana fikra tofauti na wanafuata njia zenye kutofautiana, kana kwamba Kristo mwenyewe amegawanyika[1]. Utengano huo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo, nao ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kuhubiri Injili kwa kila kiumbe.

Bwana wa karne zote hulifuatia kwa hekima na subira azimio la neema yake kwetu sisi wenye dhambi. Naye mwisho wa siku hizi ameanza kuwamiminia wakristo waliotengana hisia za toba na hamu ya umoja. Popote duniani watu wengi sana wameonja na kusukumwa na neema hiyo; na pia kati ya ndugu zetu waliojitenga, harakati za urudishaji wa umoja wa wakristo wote zinazidi kupata nguvu siku kwa siku, nayo imewashwa na neema ya Roho Mtakatifu. Wanaoshiriki katika harakati za umoja ziitwazo za kiekumeni, ni wale wamwombao Mungu katika Utatu Mtakatifu na kumwungama Yesu aliye Bwana na Mwokozi; na wanafanya hivyo siyo tu kama harakati za watu binafsi, bali pia kama wajumbe wa makundi yaliyo-jumuika ambamo wamesikiliza Injili na kila mmoja anasema kuwa hayo ni Kanisa lake na la Mungu. Lakini karibu wote, ingawa ni kwa njia mbalimbali, wanatamani Kanisa la Mungu, moja na linaloonekana, liwe kweli la wote, lililotumwa popote duniani, ili ulimwengu upate kuiongokea Injili na hivyo ukombolewe kwa utukufu wa Mungu.

Ndiyo maana Mtaguso Mkuu ulifurahi kuzitambua shughuli hizo, na baada ya kutangaza hati juu ya Kanisa, ukasukumwa na hamu ya kurudisha umoja kati ya wafuasi wote wa Kristo; na sasa Mtaguso huo unataka kuwaonyesha wakatoliki wote njia, namna na misaada ili waweze kuitikia wito na neema hizo za Mungu.

Sura ya Kwanza

KANUNI ZA KIKATOLIKI JUU YA EKUMENI

Umoja na upekee wa Kanisa

2. Katika hili upendo wa Mungu ulionekana kwetu, kwamba Mungu Baba amemtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, auchukue mwili, na kwa njia ya ukombozi awahuishe upya wanadamu na kuwakusanya wawe wamoja[2]. Naye, kabla ya kujitoa kama kafara safi juu ya madhabahu ya msalaba, aliwaombea wamwaminio kwa Baba akisema: “Wote wawe na umoja, kama wewe Baba ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiye uliyenituma” (Yn 17:21). Tena akaiweka katika Kanisa lake sakramenti ya ajabu ya Ekaristi Takatifu, ambayo ni ishara na chemchemi ya umoja wa Kanisa. Na akawapa wafuasi wake amri mpya ya kupendana[3], akawaahidia Roho Mfariji[4], aliye Mungu mtia uzima, ili akae nao daima.

Baada ya kuinuliwa juu msalabani na kutukuzwa, Bwana Yesu alimimina Roho aliyeahidiwa na kwa njia yake akawaita na kuwakusanya watu wa Agano Jipya, ndio Kanisa, katika umoja wa imani, matumaini na mapendo, kadiri ya mafundisho ya Mtume [Paulo], “mwili mmoja, na roho moja, kama mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja” (Efe 4:4-5), kwa maana “ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo... ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu” (Gal 3:27-28). Roho Mtakatifu, akaaye ndani yao waamini na kulijaza na kulitegemeza Kanisa zima, ndiye aundaye ushirika wa ajabu wa waamini na kuwaunganisha wote kwa ndani katika Kristo, kiasi kwamba yeye mwenyewe ni asili ya umoja wa Kanisa. Yeye ndiye mgawaji wa karama mbalimbali za kiroho na huduma[5] na mwenye kulitajirisha Kanisa la Yesu Kristo kwa vipaji mbalimbali: “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe” (Efe 4:12).

Kwa kusudi la kusimika popote Kanisa lake takatifu mpaka mwisho wa nyakati, Kristo alilikabidhi Baraza la Mitume kazi za kufundisha, kuongoza na kutakatifuza[6]. Kati yao alimchagua Petro ambaye juu yake, baada ya kukiri imani yake [kwa Yesu], aliazimia kulijenga Kanisa lake; akamwahidia kumpa funguo za Ufalme wa mbinguni[7]. Na baada ya ushuhuda wa upendo wake, alimkabidhi kondoo wake ili awaimarishe katika imani[8]; na kuwachunga katika umoja kamili[9], Yesu Kristo mwenyewe akiendelea kuwa daima jiwe kuu la pembeni[10] na mchungaji wa roho zetu[11].

Yesu Kristo hutaka taifa lake likue, na ushirika ukamilishwe katika umoja. Nalo litimizwe kwa njia ya kuhubiri kiaminifu Injili, ya kutoa sakramenti, na ya mamlaka inayotekelezwa katika upendo na Mitume na mahalifa wao, yaani maaskofu pamoja na kiongozi wao, halifa wa Petro, kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Nao ushirika hukamilishwa katika kukiri imani moja, katika adhimisho kwa pamoja la ibada kwa Mungu, na katika maafikiano ya kidugu ya familia yake Mungu.

Ndivyo Kanisa, lililo kundi pekee la Mungu, mfano wa bendera iliyotwekwa kati ya mataifa[12], linatia Injili ya amani kuwa huduma ya watu wote[13] na kuitimiza safari yake kwa tumaini mpaka kuufikia uenyeji wake huko mbinguni[14].

Hilo ndilo fumbo tukufu la umoja wa Kanisa katika Kristo na kwa njia yake Kristo, wakati Roho Mtakatifu akigawa karama zake mbalimbali. Mfano mkuu na asili ya fumbo hilo ndio umoja wa Utatu Mtakatifu, aliye Mungu mmoja, Baba na Mwana katika Roho Mtakatifu.

Uhusiano uliopo bado kati ya ndugu waliofarakana katika Kanisa la Yesu Kristo

3. Katika Kanisa hili la Mungu lililo moja na pekee, yalizuka tangu mwanzo mafarakano[15], ambayo Mtume ameyalaumu vikali kuwa yanastahili adhabu[16]. Lakini katika karne zilizofuata mitengano mikali zaidi ilitokea na Jumuiya kubwa zikajitenga na ushirika kamili wa Kanisa Katoliki, pengine si bila kosa la watu wa pande zote mbili. Wanaozaliwa sasa na kufundishwa katika imani ya Kristo kwenye Jumuiya hizo, haiwezekani wahesabiwe dhambi ya utengano, bali Kanisa Katoliki, linawakumbatia kwa heshima na mapendo ya kidugu. Wote wanaomwamini Kristo na kubatizwa kwa mujibu wa kanuni halali wameingizwa kwa namna fulani kwenye ushirika na Kanisa Katoliki, ingawa haujakamilika. Kwa kweli, tofauti za aina mbalimbali zilizomo baina yao na Kanisa Katoliki, kuhusu mafundisho na pengine pia kanuni, ama kwa upande wa muundo wa Kanisa, zinasababisha vizuio vingi, tena vizito kwa ushirika kamili ndani ya Kanisa. Kujaribu kuviondoa vizuio hivyo ni juhudi ya harakati za Ekumeni (motus oecumenicus). Hata hivyo, wale wote waliohesabiwa haki kwa imani katika ubatizo wameingizwa katika mwili wa Kristo[17], kwa sababu hiyo wana haki ya kuitwa wakristo. Tena kwa haki hutambuliwa na waamini wa Kanisa Katoliki kuwa ni ndugu katika Bwana[18].

Zaidi ya hayo, kati ya yale mema ambayo, yakichukuliwa kwa pamoja, Kanisa lenyewe linajengwa na kuhuishwa kwayo, mengine, naam mengi na makuu, yaweza kutokeza nje ya mipaka inayoonekana ya Kanisa Katoliki. Nayo ndiyo neno la Mungu lililoandikwa, maisha ya neema, imani, matumaini, mapendo, na hatimaye karama nyingi nyingine za moyoni, zitokazo kwa Roho Mtakatifu na mambo mengine yanayoonekana: hayo yote yatokayo kwa Kristo na yanayoongoza kwake, kwa haki ni [urithi] wa Kanisa moja la Kristo.

Aidha, ndugu waliojitenga nasi wanaendesha pia matendo mengi ya kiliturujia ya dini ya Kikristo ambayo, kwa njia na namna mbalimbali kufuatana na hali ya kila Kanisa au Jumuiya, kwa uhakika yanaweza kweli kusitawisha maisha ya neema na sharti yatazamwe kuwa na uwezo wa kufungua njia ielekeayo katika ushirika wa wokovu.

Inafuata kwamba Makanisa yenyewe, na Jumuiya, yaliyojitenga[19], bila shaka katika fumbo la wokovu hayakosi kuwa na maana na uzito wake, ingawa twaamini kwamba yana makasoro. Maana Roho wa Kristo hakatai kuyatumia kama vyombo vya wokovu, ambavyo uweza wake hutokana na utimilifu uleule wa neema na ukweli uliokabidhiwa kwa Kanisa Katoliki.

Hata hivyo, ndugu zetu waliojitenga nasi, tukiwachukua mmoja mmoja au kama Jumuiya na Makanisa, hawaufaidii umoja ule ambao Yesu Kristo alitaka kuwajalia wale wote waliotiwa uzima mpya na kuhuishwa pamoja katika mwili mmoja na kwa maisha mapya; nao ndio ule umoja uliothibitishwa waziwazi na Maandiko Matakatifu na Mapokeo matakatifu ya Kanisa. Maana ni kwa njia ya Kanisa Katoliki la Kristo pekee, ambalo ni msaada halisi wa wokovu, ambamo ukamilifu wa njia za wokovu unapatikana. Naam, tunaamini kuwa Bwana alikabidhi baraka zote za Agano Jipya kwa Baraza la Mitume tu, ambalo Petro analisimamia, ili kuunda mwili mmoja wa Kristo hapa duniani. Na katika huo mwili lazima waunganike kiaminifu wote wale ambao, kwa njia fulani, wanahusiana na taifa lake Mungu. Na taifa hilo, ingawa watu wake pindi safari yao inadumu hapa duniani, wanaendelea kuzingirwa na dhambi, linakua katika Kristo na kuongozwa na Mungu kwa wema kufuatana na mapenzi yake, hadi liufikie kwa furaha utimilifu wa utukufu wa milele katika Yerusalemu ya mbinguni.

Juhudi zinazofanywa na Kanisa ili kurudisha umoja kamili: harakati ya kiekumeni

4. Siku hizi, kwa msukumo wa neema ya Roho Mtakatifu, juhudi nyingi zinafanyika sehemu nyingi duniani, kwa njia ya sala, ya maneno, na ya matendo, ili kuufikia ule umoja kamili unaotakiwa na Yesu Kristo. Ndiyo maana Mtaguso unawasukuma waamini Wakatoliki wote ili, wakizitambua ishara za nyakati, washiriki kwa bidii katika juhudi hizo za kuleta umoja wa Wakristo.

Neno “harakati ya kiekumeni” linamaanisha juhudi na shughuli zinazotiwa moyo na kuratibiwa, kulingana na mahitaji mbalimbali ya Kanisa na jinsi nyakati zinavyoruhusu, ili kusitawisha umoja wa Wakristo. Hizo ndizo kwanza, bidii ya kuepukana na maneno, kauli ya hukumu na matendo yasiyo ya haki wala ya kweli kuhusu hali ya ndugu zetu waliojitenga nasi, na hivyo yanafanya uhusiano nao kuwa mgumu zaidi; pili, kwa warsha ya kidini kati ya Wakristo wa Makanisa au Jumuiya mbalimbali, mazungumzo ya ana kwa ana (“dialogia”) yaliyoanzishwa kati ya wataalamu wenye mafunzo imara, ambapo kila mmoja anaelezea kwa undani zaidi mafundisho ya Jumuiya yake na kuonyesha kinaganaga tabia yake halisi ilivyo. Maana, kwa dialogia hiyo wote wanapata elimu yenye ukweli zaidi na heshima iliyo sahihi zaidi ya mafundisho na ya maisha ya Jumuiya hizo. Tena zaidi, Jumuiya hizo zapata kusaidiana katika juhudi zote zinazodaiwa kwa dhamiri ya kila mkristo kwa manufaa ya jamii nzima ya wanadamu. Pia inapokubaliwa, wanakutana ili kusali pamoja. Hatimaye, wote wanachunguza uaminifu wao kwa matakwa ya Kristo kuhusu Kanisa na, kama ilivyo wajibu wao, wanakubali kwa ujasiri kazi ya kujirekebisha na ya kujitengeneza upya.

Hayo yote, wakati yanafuatiliwa kwa busara na subira na waamini wa Kanisa Katoliki chini ya uangalizi wa wachungaji wao, yanasaidia kusitawisha haki na ukweli, upatano na ushirikiano, upendo wa kidugu na umoja. Matokeo yake yatakuwa kwamba, polepole kwa kuviondoa vikwazo vinavyozuilia ushirika kamili wa kikanisa, Wakristo wote wakusanyike kwa adhimisho la pamoja la Ekaristi, katika umoja wa Kanisa lililo moja na pekee, umoja ambao Kristo alilijalia Kanisa lake tangu mwanzo na tunaoamini unadumu na usiotoweka katika Kanisa Katoliki, na tunaotumaini utazidi kuongezeka siku kwa siku mpaka mwisho wa nyakati.

Walakini, ni wazi kwamba kazi ya kuwatayarisha na kuwapatanisha mmoja mmoja wale wanaotamani ushirika kamili wa kikatoliki ni ya aina tofauti na kazi ya kiekumeni; lakini hakuna upinzani kati yao, kwa sababu zote mbili zinatokana na azimio lenye kushangaza la Mungu.

Katika kazi ya kiekumeni, Wakatoliki hakika ni lazima wajishughulishe kwa ajili ya ndugu zao waliojitenga, kusali kwa ajili yao, kushirikiana nao katika mambo ya Kanisa, na kuchukua hatua za kwanza kwa kuwaelekea, lakini kwanza kabisa lazima wachunguze kwa moyo mwangalifu na mnyofu yale yanayohitajika kurekebishwa na kutendwa katika familia ya ukatoliki yenyewe, ili katika maisha yake itoe ushuhuda wenye uaminifu na mweupe zaidi wa mafundisho na mapokeo (doctrina institutisque) yaliyowekwa na Kristo na tuliyopokea kwa njia ya Mitume.

Ingawa Mungu amelijalia Kanisa Katoliki kweli zote zilizofunuliwa pamoja na njia zote za neema, hata hivyo wanakanisa hawazitumii ili kufanya bidii sana katika maisha yao ya kiroho; kwa hiyo sura ya Kanisa hung’ara kwa upungufu mbele za ndugu waliojitenga nasi na mbele ya ulimwengu mzima, na ukuaji wa ufalme wa Mungu hukawishwa. Ndiyo maana Wakatoliki wote lazima wakusudie kufikia ukamilifu wa kikristo[20], na kujitahidi, kila mmoja kufuatana na uwezo wake, ili Kanisa huku likichukua katika mwili wake unyenyekevu na ujihinisho wa Kristo[21], lizidi siku kwa siku kujisafisha na kujirekebisha mpaka Yesu apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na hila wala kunyanzi[22].

Waamini wote katika Kanisa, huku wakihifadhi umoja katika mambo muhimu kufuatana na wajibu aliopewa kila mmoja, katika namna mbalimbali ya maisha ya kiroho na ya nidhamu kama vile katika utofauti wa ibada, naam hata katika ufafanuzi wa kiteolojia juu ya ukweli uliofunuliwa, waweze kuwa na uhuru unaofaa; na katika yote wasitawishe upendo. Kwa kufanya hivyo, watazidi siku kwa siku kuonyesha ukatoliki wa kweli pamoja na mtiririko wa kitume wa Kanisa.

Kwa upande mwingine inawapasa Wakatoliki kukubali kwa furaha na kuthamini tunu zilizo za kikristo kweli, zitokanazo na urithi ulio wa pamoja, tunu ambazo zinapatikana kwa ndugu zetu waliojitenga. Kutambua karama za Kristo na kazi zilizo njema katika maisha ya wengine, wanaotoa ushuhuda kwa Kristo pengine hata kwa kumwaga damu yao, ni tendo la haki na wema: Kwa kuwa Mungu daima ni wa ajabu na wa kustaajabiwa katika kazi zake zote.

Tena inapaswa isisahaulike kwamba yote yanayotendeka na neema ya Roho Mtakatifu kati ya ndugu zetu waliojitenga, yanaweza kusaidia kutuboresha. Lolote lililo kweli la kikristo halipingani kamwe na neema halisi ya imani, bali linawezesha fumbo la Kristo na la Kanisa lifikiwe (attingatur) kwa ukamilifu zaidi.

Walakini matengano kati ya Wakristo yanazuia Kanisa lenyewe lisitimilize Ukatoliki ulio wake katika wanawe wale, ambao, ingawa wameunganika nalo kwa ubatizo, wamejitenga na utimilifu wa ushirika. Tena, Kanisa lenyewe linapata shida kueleza katika fani zake zote utimilifu wa ukatoliki katika maisha yenyewe.

Mtaguso Mkuu huu unatazama kwa furaha kukua siku kwa siku kwa waamini Wakatoliki kushiriki katika kazi ya kiekumeni. Aidha unawakabidhi maaskofu wa pande zote za dunia kazi hiyo, ili waihamasishe kwa bidii na kuiongoza kwa busara.

Sura ya Pili

EKUMENI KATIKA UTENDAJI

Wote wanahusika katika kuurudisha umoja

5. Juhudi ya kuufikia umoja ni wajibu wa Kanisa zima, yaani waamini kwa wachungaji. Kila mmoja anapaswa kuutimiza kadiri ya uwezo wake, ama katika maisha ya kikristo ya kila siku ama kwa masomo ya kiteolojia na ya kihistoria. Juhudi hiyo inaonyesha kwa namna fulani uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Wakristo wote na inasukuma kwenye umoja kamili na timilifu kufuatana na fadhili za Mungu.

Marekebisho ya Kanisa

6. Marekebisho yoyote ya Kanisa[23] maana yake ni hasa ukuzaji wa uaminifu katika wito wake; bila shaka hiyo ndiyo asili ya jitihada kwa umoja. Kanisa linalosafiri [hapa duniani] laitwa na Kristo kuendeleza hayo matenengezo bila kukoma, ambayo yahitajika daima nalo kwa vile ni taasisi ya kibinadamu na ya kidunia. Kufuatana na hayo, ikiwa kwa wakati na mazingira fulani kumekuwepo na makasoro katika maadili au katika nidhamu ya Kanisa au hata katika namna ambayo mafundisho ya Kanisa yalitayarishwa – namna ambayo ni lazima itofautishwe kwa uangalifu na hazina yenyewe ya imani – ni lazima yarekebishwe kwa wakati wake na kwa njia sahihi.

Marekebisho hayo yana maana ya pekee kwa Ekumeni. Marekebisho hayo yanaonekana tayari katika sehemu mbalimbali za maisha ya Kanisa, kwa mfano harakati za kibiblia na za kiliturujia (motus biblicus et liturgicus), mahubiri ya Neno la Mungu na katekesi, utume wa walei, mtindo mpya wa maisha ya kitawa, maisha ya kiroho katika ndoa, mafundisho na matendo ya Kanisa kuhusu jamii. Hayo yote lazima yatazamwe kama ahadi na amana zinazoashiria kwa furaha maendeleo yajayo ya ekumeni.

Marekebisho ya moyo

7. Ekumeni ya kweli haipatikani pasipo wongofu wa moyo. Kwa maana hamu ya umoja inaanza na kukomaa kutokana na kufanywa wapya katika nia[24] kwa kujikana na kutoa upendo mwingi kwa hiari. Hivyo inatupasa kumwomba Roho Mtakatifu atujalie neema ya kujikana kweli, ya unyenyekevu na upole katika utumishi na ya ukarimu wa moyo wa kidugu kwa wengine; “Kwa hiyo nawasihi – amesema Mtume wa mataifa – mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani” (Efe 4:1-3). Himizo hili linawahusu hasa wale walioteuliwa katika daraja takatifu ili wauendeleze utume wa Yesu Kristo, ambaye “hakuja kati yetu ili kutumikiwa, bali kutumika” (Mt 20:28).

Mt. Yohane alishuhudia kwamba “tukisema kwamba hatukutenda dhambi twamfanya yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:10). Maneno hayo ni kweli pia kuhusu dhambi dhidi ya umoja. Ndiyo maana katika unyenyekevu tunaomba msamaha kwa Mungu na kwa ndugu waliotengana nasi, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.

Waamini wote wakumbuke kwamba, kwa kadiri watakavyojitahidi kuishi maisha matakatifu kufuatana na Injili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha, na watatekeleza, umoja wa wakristo. Kwa maana waamini kwa kadiri wanavyokua katika ushirika na Mungu Baba, Neno na Roho, ndivyo watakavyoweza kukuza udugu kati yao kwa undani na kwa urahisi zaidi.

Ushirikiano katika sala

8. Uongofu huo wa moyo na utakatifu wa maisha, pamoja na sala za kibinafsi na za kijumuiya kwa ajili ya umoja wa wakristo lazima vitazamwe kama roho ya harakati zote za kiekumeni na vinastahili kuitwa “ekumeni ya kiroho”.

Kwa kweli ni kawaida kwa wakatoliki kukusanyika mara kwa mara ili kuuombea umoja wa Kanisa, ambao Mwokozi wetu mwenyewe siku iliyotangulia kufa kwake aliomba kidhati kwa Baba: “Ili wote wawe na umoja” (Yn 17:21).

Katika mazingira maalum, kwa mfano katika mikutano “ya kuuombea umoja”, kama vile katika makongamano ya kiekumeni, ni halali, tena ni ya kutamanika, Wakatoliki washiriki katika sala pamoja na ndugu zao waliojitenga. Bila shaka hizo sala za pamoja ni njia inayofaa ili kuomba fadhila ya umoja, pia ni ishara halisi ya vifungo ambavyo kwavyo Wakatoliki bado wameunganika na ndugu zao waliojitenga: “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao”. (Mt 18:20).

Walakini kushiriki pamoja katika matakatifu (communicatio in sacris) kusitazamwe kuwa kama mbinu ya kutumika ovyoovyo ili kurejesha umoja kati ya wakristo. Na kushirikiana huko kunazitegemea hasa kanuni hizi mbili zifuatazo: alama ya umoja wa Kanisa, na ushirika katika vyombo vya neema. [Kanuni ya] alama ya umoja kwa kawaida huzuia ushirika huo katika matakatifu. Kinyume chake, [kanuni ya] ushirika katika neema pengine unautakia. Askofu wa mahali aamue kwa busara jinsi gani hayo yote yapasavyo kutekelezwa, kufuatana na mazingira ya nyakati na ya mahali na ya wahusika; isipokuwa imekwisha kuamuliwa tofauti na Baraza la Maaskofu, kufuatana na kanuni zake, au na Baba Mtakatifu.

Kufahamiana

9. Inatupasa kufahamu mandhari ya ndani (animum) ya ndugu zetu waliojitenga. Hapa lazima mafunzo yafuatiliwe katika ukweli na kwa moyo mweupe. Wakatoliki waliokwisha kufundishwa vizuri inafaa wapate ujuzi wa ndani zaidi wa mafundisho na historia, wa maisha yao ya kiroho na ya kiliturujia, wa saikolojia ya kidini na wa utamaduni wa ndugu hao. Faida nyingi zinapatikana katika makongamano mbalimbali, yenye mahudhurio ya waamini wa pande zote mbili, wanaoheshimiana na kuchukuliana kuwa wako sawa, kwa kusudi la kujadiliana hasa masuala ya kiteolojia. Inawapasa wale wahudhuriao chini ya uangalizi wa maaskofu kweli wawe na uwezo. Kutokana na mazungumzo hayo itaonekana kidhahiri zaidi, hali halisi ya Kanisa Katoliki ilivyo. Pamoja na hayo zitatambulikana vizuri zaidi fikra za ndugu zetu waliojitenga, nasi tutapata kuwaelezea kwa undani zaidi imani yetu.

Kufundisha kwa kuizingatia ekumeni

10. Somo la teolojia takatifu na masomo mengine, hasa ya kihistoria, lazima yafundishwe kwa mtazamo wa kiekumeni; ili yaweze kuendana zaidi na zaidi na ukweli wa matukio ulivyo.

Ni jambo la muhimu sana kwamba wale wanaotarajia kuwa wachungaji na mapadre waelimishwe katika teolojia iliyoelezwa kwa uangalifu katika mwelekeo wa ekumeni na siyo katika malumbano (non polemice), hasa juu ya uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na ndugu waliojitenga.

Ikumbukwe kuwa mafundisho na malezi ya kiroho ya waamini na watawa hutegemea hasa malezi waliyopata mapadre.

Vilevile wale Wakatoliki wanaoshughulikia kazi za kimisionari katika nchi zilezile ambapo wanafanya kazi pia wakristo wa madhehebu mengine, lazima, hasa siku hizi, watambue katika utume wao masuala na mazao yanayoendana na ekumeni.

Njia na mbinu za kueleza imani katoliki

11. Njia na mbinu zitumikazo ili kuonyesha imani Katoliki lazima zisilete vikwazo kwa dialogia na ndugu zetu. Ni muhimu kupambanua waziwazi na kikamilifu mafundisho ya dini. Hakuna lililo kinyume cha ekumeni kuliko hali ile ya amanibandia (irenismus), iwezayo kudhuru usafi wa mafundisho Katoliki na kuleta kutoelewa maana yake halisi na kamili ilivyo.

Tena, imani ya kikatoliki huhitaji kuelezwa kinaganaga na kwa ufasaha zaidi kwa namna na kwa maneno ambayo ndugu zetu waliotengana nasi nao pia wataweza kuyaelewa sawasawa.

Aidha katika dialogia ya kiekumeni wanateolojia wakatoliki, huku wakishikamana na mafundisho ya Kanisa na wakichungulia mafumbo ya Mungu pamoja na ndugu waliojitenga, lazima waandamane kwa kuutamani ukweli, kwa upendo na unyenyekevu. Wanapolinganisha mafundisho ya dini wakumbuke kwamba upo mpango au “ngazi” (hierarchia) katika kweli za mafundisho ya kikatoliki, kutokana na utofauti wa uhusiano wa kila ukweli na misingi ya imani ya Kikristo. Hivyo itakuwa imefunguliwa njia, ambayo kwa kuelekezana kidugu namna hiyo, wote watasukumwa kwenye ufahamu mpana zaidi na kwenye ufunuo wazi zaidi wa utajiri wa Kristo usiopimika[25].

Ushirikiano wa wakristo katika nyanja mbalimbali

12. Wakristo wote wakiri mbele ya mataifa yote imani yao kwa Mungu mmoja mwenye nafsi tatu, kwa Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili, ndiye Mkombozi na Bwana wetu, na tena walishuhudie lile tumaini letu lisilotahayarisha kwa juhudi ya pamoja na wakiheshimiana wao kwa wao. Maadamu nyakati hizi ushirikiano mpana sana umeundwa katika uwanja wa kijamii, basi watu wote pasipo ubaguzi wanaitwa kwa ajili ya kazi hii ya pamoja, ila wanaohusika zaidi ndio wamwaminio Mungu, na kwa namna ya pekee Wakristo, maana hao wamepewa heshima ya kuitwa kwa jina la Kristo. Ushirikiano baina ya Wakristo kwa wazi unaonyesha kile kiungo ambacho tayari kinawaunganisha na kinaweka wazi sura ya Kristo mtumishi. Na ushirikiano huo uliokwisha undwa katika mataifa mengi, hauna budi kukamilishwa siku kwa siku, hasa katika mataifa ambamo maendeleo ya kijamii na ya kiteknolojia hutokea. Nao ushirikiano lazima utimilizwe kwa kuuheshimu ipasavyo utu wa binadamu, tena kwa kuhamasisha baraka ya amani, kutekeleza maazimio ya kijamii ya Injili na hatimaye kwa kuzisitawisha sayansi na sanaa kwa roho ya kikristo. Vilevile ushirikiano huo hauna budi kukamilishwa siku kwa siku kwa kutumia njia za kila namna dhidi ya taabu za nyakati zetu, kama vile njaa na balaa mbalimbali, kutoweza kusoma na kuandika, umaskini, ukosefu wa nyumba, na mgawanyo wa mali usio sawa. Basi, kutokana na ushirikiano huo wanaomwamini Kristo huweza kujifunza kwa urahisi jinsi ya kufahamiana na kuheshimiana zaidi na wengine na hatimaye jinsi ya kuinyosha njia inayouelekea umoja wa wakristo.

Sura ya Tatu

MAKANISA NA JUMUIYA ZA KIKANISA ZILIZOJITENGA NA KITI CHA ROMA

Mitengano mbalimbali katika historia ya Kanisa

13. Sasa tunaichunguza mitengano mikubwa ya namna mbili iliyoharibu kanzu isiyoshonwa ya Yesu.

Mitengano ya kwanza ilitokea Mashariki. Kwa sababu ya kutokubaliana juu ya kanuni za kidogma za Mitaguso ya Efeso na Kalkedonia, na baadaye kwa sababu ya kuvunjika kwa ushirika wa kikanisa kati ya Mapatriarka wa majimbo ya Mashariki na Kiti cha Roma.

Baada ya karne nne hivi, palitokea mitengano mingine katika nchi za Magharibi, ambayo ilisababishwa na matukio mbalimbali yajulikanayo kwa jina la “Reformatio” (maana yake “Matengenezo” au marekebisho). Tangu zama zile Jumuiya nyingi za kitaifa ama za kimadhehebu zilijitenga na Kiti cha Roma. Kati yao Usharika wa Kiangalikana unashika nafasi ya pekee, ambao ndani yake bado zinapatikana sehemu za mapokeo na miundo ya kikatoliki.

Walakini mitengano hiyo mbalimbali inatofautiana sana kati yao, si tu kutokana na chanzo, mahali na wakati [wa kusimikwa kwake], bali hasa kwa sababu ya umbo na uzito wa masuala yake juu ya imani na juu ya muundo wa Kanisa.

Kwa sababu hiyo Mtaguso huu Mtakatifu, bila kukanusha tofauti zilizopo kati ya madhehebu mbalimbali ya kikristo na bila kutojali vifungo vya umoja ambavyo bado vinapatikana kati yao ingawaje kuna utengano; ili jitihada za ekumeni zifanywe kwa busara, unaamua kupendekeza mawazo yafuatayo.

I - HESHIMA MAHSUSI KWA MAKANISA YA MASHARIKI

Tabia na historia ya Makanisa ya Mashariki

14. Kwa muda wa karne nyingi, Makanisa ya Mashariki na ya Magharibi yalifuata kila moja njia yake, ingawa yaliungana kama ndugu kwa ushirika wa imani na wa sakramenti. Palikuwa na maafikiano kwamba ikitokea mizozo juu ya mambo ya imani au nidhamu Kiti cha Roma kikate shauri la mwisho. Mtaguso unafurahia, kati ya mengine mengi, kuwakumbushia wote kuwa huko Mashariki yanasitawi Makanisa faridi au mahalia mengi, ambayo kati yake yale makubwa ni Makanisa ya kipatriarka, na mengi kati yake huona fahari ya kuwa yalianzishwa na Mitume wenyewe. Hivyo kwa upande wa Makanisa ya Mashariki juhudi na bidii kubwa zilifanyika, na bado zipo, za kuhifadhi katika ushirika wa imani na wa mapendo, ule uhusiano wa kidugu unaopaswa kuwepo, mithili ya maumbu wawili (ut inter sorores), kati ya Makanisa ya mahali.

Vilevile isisahaulike kwamba Makanisa ya Mashariki yanahifadhi tangu mwanzo hazina, ambamo kutoka mle Kanisa la Magharibi limepokea mambo mengi ya liturujia, ya mapokeo ya kiroho na ya kisheria. Wala isipunguzwe uzito kwamba dogma zilizo za msingi kwa imani ya kikristo, kama vile ile ya Utatu Mtakatifu na ile ya Neno wa Mungu aliyechukua mwili kwa Bikira Maria ziliainishwa katika Mitaguso ya kiekumeni iliyofanyika huko Mashariki. Kwa madhumuni ya kulinda imani hiyo, yale Makanisa ya Mashariki yaliteswa sana na bado yanateswa.

Tangu mwanzo wa Kanisa urithi wa mafundisho ya Mitume ulipokelewa kwa mitindo na namna nyingi, na kufunuliwa huko na huko kitofauti, kutokana na fikra na hali za maisha zilivyo tofauti. Hayo yote, licha ya sababu nyingine zisizo za kidini, yalisababisha utengano, kwa sababu pia ya kasoro za uelewano na za mapendano.

Ndiyo maana Mtaguso Mkuu unawasihi watu wote, hasa wale walio na nia ya kujishughulisha kwa kurudisha ule ushirika kamili unaotarajiwa kati ya Makanisa ya Mashariki na Kanisa Katoliki, ili wakubali kuiheshimu inavyostahili hali hiyo ya pekee ya uanzishaji na ustawishaji wa Makanisa ya Mashariki, na hali ya mahusiano yaliyokuwepo kati yao na kati ya Kiti cha Roma kabla hayajatengana, na wajipatie picha ya kweli ya mambo hayo yote. Kuyafuatilia hayo kwa bidii kutaleta faida nyingi kwa dialogia inayoandaliwa.

Mapokeo ya kiliturujia na ya kiroho katika Makanisa ya Mashariki

15. Inajulikana kwa wote jinsi wakristo wa Makanisa ya Mashariki wanavyoadhimisha ibada takatifu kwa upendo mkuu, hasa lile adhimisho la Ekaristi takatifu, chemchemi ya maisha ya Kanisa na amana ya utukufu ujao. Kwa njia ya ibada hiyo waamini wote, hali wameunganika na Askofu, wanapata njia ya kumwelekea Mungu Baba kwa njia ya Mwana, Neno aliyechukua mwili, aliyeteseka na kutukuzwa, katika miminiko la Roho Mtakatifu. Hapa waamini, hali wamepata “kuwa washirika wa tabia ya umungu” (2Pet 1:4), wanaingia katika ushirika wa Utatu Mtakatifu. Hivyo, kwa njia ya maadhimisho ya Ekaristi ya Bwana, Kanisa la Mungu linajengwa na kukuzwa katika Makanisa hayo mbalimbali[26], na kwa njia ya konselebrasio ushirika kati yao hujidhihirisha.

Katika ibada hizo za kiliturujia wakristo wa Mashariki wana heshima ya juu kwa Bikira Maria kwa tenzi tukufu, yeye ambaye katika Mtaguso Mkuu wa kiekumeni wa Efeso, alitangazwa kwa fahari kuwa Mama Mtakatifu wa Mungu (Deipara), kusudi Kristo atambulikane kuwa kweli Mwana halisi wa Mungu na Mwana wa Adamu, kulingana na Maandiko Matakatifu. Aidha, hao wakristo wanawaheshimu watakatifu wengi ambao miongoni mwao wamo Mababa wa Kanisa lote zima.

Makanisa hayo ingawa yametengana nasi yana sakramenti za kweli, hasa Upadre na Ekaristi, kutokana na uandamizi wa kitume (successionis apostolicae); na kwa njia ya sakramenti hizo, bado yameunganika nasi kwa vifungo vya karibu sana; ndiyo maana “kushiriki pamoja katika matakatifu” (communicatio in sacris), kwa fursa maalum na kwa idhini ya mamlaka ya Kanisa, sio tu kwamba kunawezekana bali pia kunahimizwa kufanyika.

Aidha, Kanisa la Mashariki linatunza pia hazina ya mapokeo ya kiroho, ambayo hasa yamepatikana katika maisha ya kimonaki. Huko, tangu zama zile tukufu za Mababa Watakatifu wa Kanisa, imesitawi ile roho ya kimonaki na kuenea baadaye katika Kanisa la Magharibi, na kutokana na roho hiyo, kama toka kwa chemchemi, kanuni za kitawa za waroma zikapata asili yake, na, katika karne zilizofuata, zikazidishiwa mara nyingi nguvu mpya. Kwa sababu hiyo wakatoliki wanahimizwa kutumia kwa wingi zaidi hazina za kiroho za Mababa wa Kanisa la Mashariki ambazo zinamwinua mtu mzima apate kuyatafakari mafumbo ya Mungu.

Waamini wote wapate kuelewa kwamba kujua, kuheshimu, kulinda na kuchochea urithi wa kiliturujia na wa kiroho ulio mwingi ajabu wa Kanisa la Mashariki, ina maana kubwa sana ili kuhifadhi kiaminifu mapokeo yote ya kikristo, pamoja na kutimiliza upatanisho kati ya wakristo wa Mashariki na wa Magharibi.

Kanuni na taratibu za Makanisa ya Mashariki

16. Tangu mwanzo Makanisa ya Mashariki yalifuata kanuni zao yenyewe zilizokuwa zimeidhinishwa au na Mababa Watakatifu au na Sinodi au na Mitaguso Mikuu (Oecumenicis). Hivi sasa, kiasi hiki cha utofauti wa mila na desturi uliozungumzwa hapo juu, haupingani hata kidogo na umoja wa Kanisa, bali huliongezea fahari pamoja na kusaidia kutimiza utume wake. Ndiyo sababu Mtaguso Mkuu, ili kuondoa kila shaka, unakiri kwamba Makanisa ya Mashariki, wakati yanazingatia akilini umuhimu wa umoja wa Kanisa zima, yanayo mamlaka ya kujitawala yenyewe kwa mujibu wa sheria zao, kwa vile sheria hizo zimewekwa kulingana na tabia za waamini wake na zinafaa zaidi kwa mafaa ya roho zao. Kufuata kiaminifu hiyo kanuni ya asili ya mapokeo ambayo kwa kweli mara nyingi imeshindikana kuishika, ni suala mojawapo kati ya yale ya lazima ili kuanza kufanya jitihada ya kurudisha umoja.

Maelezo mbalimbali ya kiteolojia yanayotimilizana

17. Yaliyosemwa hapo juu kuhusu uhalali wa utofauti [uliopo kati ya Makanisa], tunapenda kuyatamka pia kuhusu tofauti zinazokuwepo katika maelezo ya kiteolojia ya mafundisho [ya kikristo]. Maana, katika kuchambua ukweli uliofunuliwa Kanisa la Mashariki kwa upande mmoja na Kanisa la Magharibi kwa upande mwingine, ili kufahamu na kukiri mambo ya Mungu, yalitumia mitindo na mitazamo inayotofautiana. Hivyo haishangazi ikiwa mara kwa mara vipengele fulani vya fumbo lililofunuliwa vinahisiwa kwa usawa zaidi na kubainishwa waziwazi na Kanisa moja kuliko jingine. Hapo, mara nyingi inaonekana kwamba hizo formula za kiteolojia hazina mashindano, bali zinatimilizana. Kuhusu mapokeo halisi ya kiteolojia ya [wakristo wa] Mashariki, lazima itambulike kwamba yamesimikwa kwa namna bora ya pekee katika Maandiko Matakatifu, yamesitawishwa na kudhihirishwa pia na maisha ya kiliturujia, yanayolishwa na mapokeo ya Mitume yaliyo hai, na maandishi ya Mababa na watunzi wa kiroho wa Mashariki. Hayo yanaelekea kuwa mwongozo sahihi wa maisha, na hasa kuwa mtazamo mkamilifu wa ukweli wa kikristo.

Mtaguso huu Mkuu unamtolea Mungu shukrani kwa sababu ya waana wengi wa Kanisa Katoliki wenye asili ya Mashariki, ambao wanatunza hazina hiyo na wanayo hamu ya kuiishi kwa uaminifu na kwa usahihi zaidi katika maisha yao, na tayari wanaishi katika ushirika kamili na ndugu wanaofuata mapokeo ya [Kanisa la] Magharibi. Pamoja na hayo Mtaguso huu unatangaza kwamba urithi huo wote wa kiroho na wa kiliturujia, wa nidhamu na wa teolojia, katika mapokeo yake mbalimbali unahusiana na hali halisi ya kikatoliki na ya kitume ya Kanisa.

Hitimisho

18. Baada ya kuchunguza hayo yote, Mtaguso Mkuu huu unasisitiza neno lile lililotangazwa na Mitaguso ya hapo nyuma kama vile na Mababa Watakatifu, ya kwamba ili kupata tena au kulinda ushirikiano na umoja inabidi “tusiwatwike [wenzetu] mzigo, ila hayo yaliyo lazima” (Mdo 15:28). Tena unatamani sana kwamba, tangu sasa, taasisi na mitindo ya maisha ya Kanisa vilenge katika jitihada zote za kufikia hatua kwa hatua, ushirikiano na umoja, hasa kwa njia ya sala na ya dialogia ya kidugu kuhusu mafundisho na mahitaji ya lazima zaidi ya wajibu wa uchungaji wa nyakati zetu. Vivyo hivyo Mtaguso unawasihi wachungaji na waamini wa Kanisa Katoliki watunze uhusiano na wale waamini ambao hawaishi tena huko Mashariki, bali wako ugenini, ili kwamba katika roho ya upendo ule ushirikiano wa kidugu uliopo, nao ukue na iachwe hali ile ya mabishano au ugomvi. Iwapo juhudi hiyo itachukuliwa kwa moyo mweupe, Mtaguso unatumaini kwamba, baada ya kuubomoa ule ukuta wa utengano kati ya Kanisa la Magharibi na la Mashariki, patakuwepo makao ya pamoja imara katika jiwe kuu la pembeni, yaani Kristo Yesu, afanyaye yale yaliyokuwa mawili kuwa moja[27].

II - MAKANISA NA JUMUIYA ZA KIKANISA ZILIZOJITENGA HUKO MAGHARIBI

Hali ya Jumuiya hizo

19. Makanisa na Jumuiya za kikanisa, ambazo zimejitenga na Kiti cha Kitume cha Roma, wakati wa vurugu kuu iliyoanzishwa huko Magharibi mwishoni mwa Karne za Kati (karne XVI) ama baadaye, zinaunganika na Kanisa Katoliki kwa njia ya uhusiano na ujamaa maalum, kutokana na muda mrefu ambao wakristo wote katika karne za kwanza walikuwa wanaishi katika ushirika wa kikanisa.

Walakini kwa kuwa hayo Makanisa na hizo Jumuiya za Kikanisa, kutokana na asili yake, mafundisho na maisha ya kiroho, zinatofautiana sana siyo nasi tu, bali pia kati yao zenyewe, ni vigumu sana kuzifafanua sawasawa, nako hatukusudii kufanya hapa.

Ingawa harakati za kiekumeni na hamu ya amani na Kanisa Katoliki bado hazijathibitika pote, ni tumaini letu kwamba polepole moyo wa kiekumeni na wa kuheshimiana utasitawi kati ya [waamini] wote.

Hatima, inabidi kutambua kwamba kati ya Makanisa hayo na Jumuiya hizo kwa upande mmoja na Kanisa Katoliki kwa upande mwingine kuna tofauti kubwa sana, siyo tu za kihistoria, au za kisosiolojia, au kisaikolojia na za kiutamaduni tu, bali hasa katika ufafanuzi wa ukweli uliofunuliwa. Ili kurahisisha kuingia katika dialogia ya kiekumeni licha ya tofauti hizo, tunapenda kusisitiza hapa mada kadha wa kadha, zinazoweza na kupaswa kuwekwa, kama misingi na kichocheo cha dialogia hiyo.

Imani kwa Yesu Kristo aliye Mungu

20. Kwanza kabisa mawazo yetu yawaelekee wale wakristo wanaomkiri waziwazi Yesu Kristo kuwa ndiye Mungu na Bwana na mpatanishi pekee kati ya Mungu na wanadamu, kwa utukufu wa Mungu mmoja, Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Twafahamu kwamba kuna tofauti kubwa kulingana na mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu Kristo Neno wa Mungu aliyechukua mwili na kuhusu kazi ya ukombozi, na vilevile juu ya fumbo na huduma ya Kanisa na kuhusu nafasi ya Bikira Maria katika kazi ya ukombozi. Lakini tunafurahi tukiwaona ndugu zetu waliojitenga wanamwelekea Kristo kama chimbuko na kiini cha ushirika wa kikanisa. Hali hii ya kutamani sana kuunganika na Kristo inawahimiza kutafuta zaidi na zaidi umoja, na pia kuishuhudia imani yao popote kwa mataifa.

Sifa kwa Maandiko Matakatifu

21. Upendo na heshima nusu kuabudu Maandiko Matakatifu vinawasukuma ndugu zetu kusoma kwa bidii na kwa uthabiti Vitabu Vitakatifu. Kwa kweli Injili “ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia” (Rum 1:16).

Kwa kumwomba Roho Mtakatifu, katika Maandiko Matakatifu yenyewe, hao wanamtafuta Mungu anayeongea nao katika Kristo aliyetabiriwa na Manabii, Neno wa Mungu aliyechukua mwili kwa ajili yetu. Katika Maandiko wanatafakari maisha ya Kristo na yale yote ambayo yeye Mwalimu wa kimungu amefundisha na kutenda, kwa ajili ya wokovu wa wanadamu, huku wakitazama hasa fumbo la kufa na kufufuka kwake.

Lakini, wakati wakristo hawa waliojitenga nasi wanapoikubali mamlaka ya kimungu ya Maandiko Matakatifu, hapohapo wana mawazo tofauti na sisi na pia wao kwa wao juu ya uhusiano kati ya Maandiko Matakatifu na Kanisa ambalo ndani yake, kufuatana na imani katoliki, mamlaka-fundishi (magisterium) yanashika nafasi maalum ya kulieleza na kulihubiri Neno la Mungu lililoandikwa.

Hata hivyo, katika dialogia yenyewe, Maandiko Matakatifu ni chombo kilicho bora katika mkono wa kuume wa Mungu ili kuufikilia ule umoja ambao Mwokozi hutaka kuwapa watu wote.

Imani kwa Ubatizo na Sakramenti nyinginezo

22. Kwa njia ya sakramenti ya ubatizo, ikiwa inatolewa kwa utaratibu unaokubalika na kupokelewa kwa moyo unaodaiwa, kufuatana na maagizo ya Bwana wetu, mwanadamu anaunganishwa kwelikweli na mwili wa Kristo msulubiwa na mtukuzwa, na anazaliwa upya kwa kushiriki maisha ya kimungu, kama anavyosema Mtume Paulo, “mlizikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu” (Kol 2:12)[28].

Kwa hiyo ubatizo ndio kifungo cha kisakramenti cha umoja uliopo kati ya wale wote waliozaliwa upya kwa njia yake. Walakini, ubatizo kwa wenyewe ni chanzo na awali tu, kwa sababu ndio tukio lile maalum ambalo linaelekea lote kujipatia utimilifu wa maisha katika Kristo. Ndiyo maana ubatizo hukusudia kulenga katika kukiri imani kikamilifu, na kuingizwa kikamilifu katika mpango wa wokovu kwa jinsi Kristo mwenyewe alivyotaka, na hatimaye kuunganishwa kikamilifu katika ushirika wa kiekaristi.

Jumuiya za kikanisa zilizojitenga nasi, ingawa zinakosa ule umoja kamili nasi unaotokana na ubatizo, na ingawa twaamini kwamba hazikulinda maana kamili na halisi ya fumbo la Ekaristi, hasa kwa kuikosa sakramenti ya Daraja takatifu, hata hivyo, wanapokumbuka katika Karamu Takatifu kufa na kufufuka kwake Bwana, wanakiri kwamba katika ushirika wa Kristo uzima unamaanishwa na wanangoja ujio wake mtukufu. Hivyo, inabidi mafundisho mintarafu Karamu ya Bwana, sakramenti nyinginezo, ibada na huduma za Kanisa yawe mada za dialogia.

Maisha ya kikristo katika imani na matokeo yake

23. Maisha ya kikristo ya hao ndugu hulishwa na imani katika Kristo, na yanatiwa nguvu na neema ya ubatizo na katika kusikiliza neno la Mungu. Nayo yanajidhihirisha katika sala za binafsi, katika kutafakari Biblia, katika maisha ya familia ya kikristo na katika ibada za Jumuiya inayokusanyika kwa kumsifu Mungu. Aidha, pengine ibada yao huhifadhi sehemu mashuhuri za liturujia iliyokuwa imeadhimishwa zamani na wakristo wote.

Imani kwa Kristo huleta matunda ya sifa na shukrani kwa mema yaliyojaliwa na Mungu; tena huongeza hamu halisi ya haki na upendo mnyofu kwa jirani. Pamoja na hayo, imani hii ya kimatendo imekuwa chanzo cha taasisi nyingi za kusaidia kuondoa umaskini wa kiroho na wa kimwili, kuboresha malezi ya vijana, kufanya hali ya jamii ilingane na heshima ya kila binadamu, na kuimarisha amani ulimwenguni.

Na ikiwa katika suala la kimaadili wapo wakristo wengi wasioielewa Injili sawasawa na wakatoliki, wala hawakubali majibu yaleyale kwa masuala magumu zaidi ya jamii ya kisasa, hata hivyo wanataka, kama vile sisi, kuambatana na neno lake Kristo, kama chimbuko la fadhila za kikristo, na kulitii agizo la Mtume: “Na kila mfanyalo kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye” (Kol 3:17). Kutokana na hayo itakuwa inawezekana kuanzisha dialogia ya kiekumeni kuhusu utekelezaji wa kimaadili wa Injili.

Hitimisho

24. Hivi, baada ya kueleza kwa ufupi masharti, ambayo kwayo inafanyika juhudi ya ekumeni, pamoja na misingi yenye kuisimamisha, tunaelekeza macho ya tumaini kwa mambo ya mbeleni. Mtaguso huu Mkuu unawasihi waamini waepukane na ujinga wa kila aina au bidii zisizo na tahadhari ambazo zinaweza kudhuru maendeleo halisi ya kurudisha umoja. Kwa kweli juhudi yao ya kiekumeni haina budi kuwa yote katoliki kwelikweli, yaani lazima ifuate kwa uaminifu ile kweli tuliyopokea kwa Mitume na kwa Mababa wa Kanisa. Tena juhudi hiyo lazima ilingane na imani ambayo Kanisa Katoliki daima limeikiri, pamoja na kuuendea utimilifu ule, ambao kwao Bwana ataka Mwili wake uongezeke katika mfululizo wa nyakati.

Mtaguso huu Mkuu unatamani sana kwamba juhudi za utendaji za waana wa Kanisa Katoliki ziendelezwe pamoja na zile za ndugu waliojitenga, pasipo kuweka kikwazo chochote katika maongozi ya Mungu na bila kuiharibu misukumo ijayo ya Roho Mtakatifu. Aidha Mtaguso unatangaza kwamba unatambua ya kuwa azimio hilo takatifu la kuwapatanisha wakristo wote katika umoja wa Kanisa la Kristo, lililo moja na pekee, lazidi uwezo na nguvu za kibinadamu. Ndiyo sababu unaweka tumaini lake lote katika sala ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, katika upendo wa Mungu Baba kwetu, na katika nguvu ya Roho Mtakatifu. “Na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rum 5:5). 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila mmoja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunayaamuru yawekwe kwa utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 21 Novemba 1964.

 

Mimi mwenyewe Paolo, Askofu wa Kanisa Katoliki.

(zinafuata sahihi za Mababa)

  


[1] Taz. 1Kor 1:13.
[2] Taz. 1Yoh 4:9; Kol 1:18-20; Yn 11:52.
[3] Taz. Yn 13:34.
[4] Taz. Yn 16:7.
[5] Taz. 1Kor 12:4-11.
[6] Taz. Mt 28:18-20; na Yn 20:21-23.
[7] Taz. Mt 16:19; na Mt 18:18.
[8] Taz. Lk 22:32.
[9] Taz. Yn 21:15-17.
[10] Taz. Efe 2:20.
[11] Taz. 1Pet 2:25; Conc.Vatic. I, Const. Pastor Aeternus: Coll. Lac. 7, 82a.
[12] Taz. Isa 12:10-12.
[13] Taz. Efe 2:17-18; na Mk 16:15.
[14] Taz. 1Pet 1:3-9.
[15] Taz. 1Kor 11:18-19; Gal 1:6-9; 1Yoh 2:18-19.
[16] Taz. 1Kor 1:11nk; na 11:22.
[17] Taz. Conc. Florent., Sess.VIII (1439), Decretum Exultate Deo: Mansi 31, 1055 A.
[18] Taz. Mt. Augustino, In Ps. 32, Enarr. II, 29: PL 36, 299.
[19] Taz. Conc.Lateranense IV (1215), Konstitutio IV: Mansi 22, 990; Conc. Lugdunense II (wa Lyon) (1274), Professio fidei Michaelis Paleologi: Mansi 24, 71, E; Conc. Florentinum, Sess. VI (1439), Definitio Laetentur Caeli: Mansi 31, 1026 E.
[20] Taz. Yak 1:4; Rum 12:1-2.
[21] Taz. 2Kor 4:10; Flp 2:5-8.
[22] Taz. Efe 5:27.
[23] Taz. Conc. Lateranense V, Sess. XII (1517), Constit. Constituti: Mansi 32, 988, B-C.
[24] Taz. Efe 4:23.
[25] Taz. Efe 3:8.
[26] Taz. Mt. Ioannes Chrysostomus, In Ioannem Homilia XLVI, PG 59, 260-262.
[27] Taz. Conc.Florent., Sess. VI (1439), Definitio Laetentur Caeli: Mansi 31, 1026 E.
[28] Taz. Rum 6:4.