Kiti Kitakatifu
WARAKA WA KITUME
Ishara ya kustaajabisha
WA BABA MTAKATIFU FRANSISKO
KUHUSU MAANA NA UMUHIMU WA PANGO LA NOELI (PRESEPI)
1. Ishara ya kustaajabisha ya pango la Noeli, ya kuwapendeza sana watu wakristo, inaleta daima mshangao na ajabu. Kuigiza tukio la kuzaliwa kwake Yesu ni sawa na kutangaza fumbo la Umwilisho wa Mwana wa Mungu kwa upole na furaha. Maana, pango la Noeli ni sawa na Injili iliyo hai, inayobubujika kutoka kurasa za Maandiko Matakatifu. Tunapotazama ishara ya Noeli, tunaalikwa kufunga safari ya kiroho, tukiwa tunavutwa na unyenyekevu wa Yule ambaye alijifanya mtu ili kukutana na kila mtu. Na sisi twagundua kuwa Yeye anatupenda kiasi hicho, hadi kuungana nasi, kusudi pia sisi tuweze kuungana naye. Kwa Waraka huu ningependa kuwahimiza katika mapokeo mazuri ya familia zetu, ambazo katika siku zinazotangulia Noeli waandaa presepi, pango la Bethlehemu. Hali kadhalika, napenda kuwatia moyo katika desturi ya kuliandaa mahali pa kazi, shuleni, hospitalini, kwenye magereza, kwenye viwanja na njia kuu za mjini... Hili ndilo zoezi la ubunifu wa kisanaa, unaotumia vitu vya aina mbalimbali kabisa ili kutayarisha zile kazi bora za uzuri. Twajifunza tukiwa bado watoto wadogo: pale ambapo baba na mama, pamoja na kina bibi na babu, wataturithisha desturi hii yenye furaha, ambayo inabeba utajiri mkubwa wa uchaji na ibada za watu. Ninatumaini sana kwamba desturi hii isipotee kamwe; kinyume chake, ninategemea kwamba, pale ambapo kidogo imefifia, basi, desturi hiyo ifufuliwe na kusitawishwa tena.
2. Asili ya msingi ipo katika mambo madogo machache yaliyotajwa na Injili ya kuzaliwa kwake Yesu huko Bethlehemu. Mwinjili Luka anasema tu kwamba Maria “alimzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Lk 2:7). Yesu alilazwa katika hori ya kulia ng’ombe, ambayo kwa lugha ya Kilatini huitwa “presepium”, asili ya neno letu (jipya) “presepi”.
Alipokuja ulimwenguni humu, Mwana wa Mungu alipata nafasi pale mahali pa kuwalishia mifugo. Manyasi yanakuwa kilalio cha kwanza cha Yule ambaye atajidhihirisha kuwa “chakula kilichoshuka kutoka mbinguni” (Yn 6:41). Nayo ndiyo ishara ambayo tayari Mt. Augustino, pamoja na Mababa wengine wa Kanisa, aligundua, akaifafanua kwa kuandika: “Aliyelala katika hori ya kulia ng’ombe, akawa chakula chetu” (Hotuba 189, 4). Kwa kweli, presepi, yaani pango la Noeli, inasheheni mafumbo mbalimbali ya maisha ya Yesu na inayaweka karibu na maisha yetu ya kila siku.
Lakini tuje mara moja kwenye asili ya presepi kama sisi tunavyoielewa. Tunaelekeza mawazo yetu kule Greccio, katika bonde la Rieti, Mkoa wa Lazio, Italia, ambako Mt. Fransisko wa Asizi siku moja alisimama. Labda alikuwa anarudi kutoka Roma, ambapo mnamo tarehe 29 Novemba 1223 alikuwa amepokea idhini ya Papa Onorio wa Tatu kwa Kanuni yake. Baada ya safari yake katika Nchi Takatifu, mapango yale ya Greccio yalikuwa yakimkumbusha kwa karibu sana mazingira ya Bethlehemu. Pia inawezekana kwamba Mt. Fransisko, Fukara wa Mungu, aliguswa sana, huko Roma, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mtakatifu, na picha za mozaiki ambazo zilionyesha kuzaliwa kwake Yesu, karibu sana na mahali ambapo zinahifadhiwa mbao za hori ya Noeli, yanavyoeleza mapokeo ya zamani.
Kitabu cha Machimbuko ya Kifransisko kinasimulia kinaganaga kilichotokea huko Greccio. Siku kumi na tano kabla ya Noeli, Fransisko alimwita mwenyeji wa mahali pale, jina lake Yohane, akamwomba amsaidie kutekeleza nia yake. “Ningepenga kuigiza tukio la Mtoto aliyezaliwa Bethlehemu, na kwa namna fulani kuona kwa macho yangu ya mwili taabu alizopata kwa kukosa mahitaji muhimu kwa mtoto mchanga, namna alivyolazwa katika hori, na jinsi alivyolala manyasini kati ya ng’ombe na punda”.[1] Mara tu alipomsikiliza, yule rafiki mwaminifu akaenda kuandaa kila kilichohitajika pale mahali palipopendekezwa, kadiri ya maelekezo ya Mt. Fransisko. Tarehe 25 Desemba 1223 walifika huko Greccio watawa Wafransiskani wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, na walifika pia wanaume kwa wanawake kutoka nyumba za jirani, wakileta maua na mienge ili kumulika usiku ule mtakatifu. Alipofika Mt. Fransisko, alikuta hori limejaa manyasi, na ng’ombe na punda walikuwepo karibu. Umati wa watu walionyesha furaha isiyosemeka, ambayo walikuwa hawajaionja hapo kabla, mbele ya taswira ya Noeli. Kisha padri aliadhimisha kwa fahari Ekaristi juu ya hori, akionyesha muungano kati ya Umwilisho wa Mwana wa Mungu na Ekaristi. Siku ile huko Greccio hazikuwepo sanamu: Pango la Bethlehemu liliandaliwa na wale watu hai waliokuwepo.[2]
Ndivyo yalivyoanza mapokeo yetu: kwa kuzunguka wote pango la Noeli, kwa kujaa furaha, pasipo utengano wala umbali baina ya tukio linalotokea huko na wale ambao wanakuwa washiriki wa fumbo hilo.
Mwandishi wa kwanza kuandika historia ya maisha yake Mt. Fransisko, yaani Tomaso wa Chelano, anakumbuka kwamba usiku ule, kukawepo pia zawadi ya maono ya ajabu: mmoja wa waliohudhuria aliona kwamba katika hori amelala Mtoto Yesu mwenyewe! Toka pango la Noeli ya mwaka 1223, “kila mmoja alirudi nyumbani mwake akiwa amejaa furaha kubwa sana”.[3]
3. Mt. Fransisko, kwa njia ya ishara ile ndogo, alitenda tendo kubwa la uinjilishaji. Mafundisho yake yamepenya mioyo ya wakristo na kudumu hadi siku hizi zetu kama namna halisi na rahisi ya kuonyesha uzuri wa imani yetu. Mahali penyewe ambapo iliandaliwa presepi ya kwanza imejaa na kuibua hisia hizi. Greccio imekuwa ni kimbilio la watu wanaotaka kufichama katika milima na miamba na kuzungukwa na kimya kikuu.
Mbona presepi inatustaajabisha hivi na kutugusa moyoni? Kwanza kabisa ni kwa sababu inadhihirisha upendo wa Mungu. Yeye, aliye Muumba wa ulimwengu, anajishusha hadi kuufikia udogo wetu. Zawadi ya uhai, ambayo kila mara ni ya kimafumbo kwetu, inatuvutia hata zaidi kwa kuona kwamba Yule aliyezaliwa na Maria ndiye asili na tegemeo la kila kilicho hai. Katika Yesu, Mungu Baba ametupatia kaka ambaye anakuja kututafuta tunapoyumba na kutangatanga; rafiki mwaminifu ambaye yupo daima karibu nasi; ametupatia Mwanae anayetusamehe na kutuinua tena na tena kutoka dhambi.
Kuandaa presepi katika nyumba zetu kunatusaidia kuishi tena historia waliyoishi huko Bethlehemu. Bila shaka, Injili zinaendelea kuwa ndiyo chemchemi inayotuwezesha kujua na kutafakari Tukio kuu lile; hata hivyo, kuigiza pango la Noeli katika presepi kunatusaidia kutazama taswira zile, kukuza utamu wa upendo, kualikwa kujihusisha katika historia ya wokovu, katika muktadha wa tukio ambalo ni hai na kweli katika mazingira mbalimbali ya maisha na utamaduni vya watu.
Kwa namna ya pekee, tangu asili yake ya kifransisko, presepi ni mwaliko ili “tusikie” na “kugusa” umaskini ambao Mwana wa Mungu alichagua kwa ajili yake katika Umwilisho wake. Na hivyo, bila kelele, ni mwaliko wa kumfuata katika njia ya unyenyekevu, ya umaskini, ya kuachana na mali, njia ambayo kutoka hori ya Bethlehemu inaongoza hadi Kalvario, kwenye Msalaba. Ni mwito wa kumkuta na kumtumikia kwa huruma katika ndugu, kaka kwa dada, wenye uhitaji mkubwa zaidi (taz. Mt 25:31-46).
4. Ninapenda sasa kutazama moja moja zile ishara na sanamu mbalimbali zilizopo katika presepi, ili kutambua ile maana inayobebwa na kila moja. Kwanza kabisa, tunaweka alama ya uwingu pamoja na nyota zake, zinazong’aa katika ukimya na giza la usiku. Si tu kwa kuwa waaminifu na simulizi la Injili kwamba tunafanya hivyo, lakini pia kwa sababu ya maana inayotuletea. Tufikiri, ni mara ngapi giza linakumba maisha yetu. Basi, hata katika nafasi hizo, Mungu hatuachi peke yetu, bali anajitokeza ili kujibu maswali makuu yanayohusu maana ya maisha yetu: Mimi ni nani? Ninatoka wapi? Kwa nini nimezaliwa wakati huu? Kwa nini ninapenda? Kwa nini ninateseka? Kwa nini nitakufa? Ili kutoa majibu kwa maswali haya Mungu alijifanya mwanadamu. Ukaribu wake unaleta mwanga panapo giza na unaangaza walio katika uvuli wa mateso (taz. Lk 1:79). Neno moja yanastahili pia mandhari ambayo tunayatengeneza katika presepi, ambayo mara nyingi yanaonyesha kama magofu ya nyumba na ngome za zamani, na ambayo mara nyingine yanakuwa makao ya Familia Takatifu badala ya pango la Bethlehemu. Inawezekana kwamba wazo la kuweka magofu haya, asili yake ipo katika maandiko la Ngano ya Dhahabu ya mtawa Mdominiko Yakobo wa Varazze (karne ya 13), tunamosoma juu ya fununu ya kipagani isemayo kwamba hekalu la Amani huko Roma lingebomoka siku ambapo Bikira mmoja atakapozaa. Magofu yale ni hasa ishara wazi ya ubinadamu ulioanguka, ya vitu vyote viharibikavyo, vilivyopotoka na kuhuzunika. Hayo yote yasema kwamba Yesu ndiye kilicho kipya katika ulimwengu ulio kuukuu, naye alikuja kuponya na kutengeneza upya, kurudisha maisha yetu na ulimwengu wote kwenye mng’ao wake asilia.
5. Moyo wetu ungetakiwa kukunjuka tunapoziweka katika presepi sanamu za milima, mito, kondoo na wachungaji. Kwa namna hiyo tunakumbuka, kama walivyotabiri manabii, kwamba viumbe vyote vinashiriki furaha na shangwe za ujio wa Masiya. Malaika na nyota angavu ni ishara ya kwamba sisi pia twaalikwa kufunga safari ili kufika hadi kwenye pango ambamo twaweza kumwabudu Bwana.
“Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana” (Lk 2:15): ndivyo walivyosema wachungaji baada ya kupashwa habari na Malaika. Ni mafundisho mazuri sana yale tunayoyapata katika simulizi rahisi ya Injili. Tofauti na umati wa watu wenye shughuli nyingi mno, wachungaji wamekuwa mashahidi wa kwanza wa kile kilicho cha lazima, yaani zawadi ya wokovu. Hao ndio walio wanyenyekevu na maskini zaidi, nao waweza kirahisi kupokea tukio la Umwilisho. Wachungaji wanamjibu Mungu, anayekuja kwao katika Mtoto Yesu, kwa kufunga safari kuelekea kwake, ili kukutana kwa upendo na mshangao wenye shukrani. Na kweli, ndio mkutano huu wa Mungu na watoto wake, kwa njia ya Yesu, ambao unaunda dini yetu, unasababisha uzuri wake wa pekee, unaoonekana kwa namna mahsusi katika presepi.
6. Katika presepi zetu huwa tunaweka sanamu nyingi zenye maana fulani. Kwanza kabisa, sanamu za maskini na fukara ambao hawajui ufahari na utajiri, isipokuwa ule wa moyoni. Pia wao wako karibu na Mtoto Yesu kwa haki, wala hakuna awezaye kuwafukuza au kuwaweka mbali na ile hori iliyoandaliwa haraka haraka, ambapo watu maskini wajisikia vizuri kuikaribia. Tena zaidi: maskini ndio waliopendelewa mbele ya fumbo hili na, mara nyingi, ndio wale wanaoweza kutambua kirahisi uwepo wa Mungu kati yetu.
Nao maskini na wanyenyekevu waliopo kwenye presepi wanatukumbusha kwamba Mungu anajifanya mwanadamu kwa ajili ya wale ambao wanahitaji zaidi upendo wake na wanaomba awe karibu nao. Yesu, aliye “mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt 11:29), alizaliwa maskini, akaishi maisha ya kawaida ili kutufundisha kushika kilicho cha maana na kuishi kwa ajili yake. Presepi inaleta ujumbe wazi kwamba hatuwezi kudanganywa na utajiri na mali, wala na vishawishi vingi vya furaha batili. Ngome ya Herode ipo pale pembeni, imefungwa, na kushindwa kupokea tangazo la furaha. Akizaliwa kwenye presepi, Mungu mwenyewe anaanza mapinduzi pekee ya kweli yenye kuleta tumaini na heshima kwa wasio na kitu, kwa waliotengwa katika jamii: ni mapinduzi wa upendo, mapinduzi wa utamu wa mapendo. Kutoka katika presepi Yesu anatangaza, kwa uwezo wa unyenyekevu, mwito wa kushirikiana na walio wa mwisho, maskini na wahitaji, nako ndiyo njia kuelekea ulimwengu bora zaidi, unaoheshimu utu na udugu wa kibinadamu, ambamo hakuna mtu anayetengwa wala kusukumizwa pembezoni mwa jamii.
Mara nyingi watoto – lakini hata watu wazima, pia! – wapenda kuongeza kwenye presepi sanamu nyinginezo ambazo haziendani na masimulizi ya Injili. Hata hivyo, ubunifu huo unataka kuonyesha kwamba katika ulimwengu huu mpya aliouanzisha Yesu kuna nafasi kwa kila kilicho cha kibinadamu na kwa kila kiumbe. Iwe ni mchungaji au mhunzi, mwokaji wa mkate au mpiga ngoma, kina mama waliojitwisha ndoo ya maji au watoto wachezao... hizo zote ni picha za utakatifu wa siku kwa siku, ni furaha ya kutimiza kwa namna ya pekee yale yaliyo ya kawaida ya kila siku, Yesu anaposhiriki pamoja nasi maisha yake ya kimungu.
7. Polepole presepi inatuelekeza kwenye pango, ambapo twaziona sanamu za Maria na Yosefu. Maria ni mama anayemtazama mwanae na kumwonyesha kwa wote wanaokuja kumwamkia. Sanamu yake Maria inatufikirisha fumbo lile kuu lililomshika huyo msichana, pale ambapo Mungu alipopiga hodi kwenye mlango wa moyo wake safi. Malaika alipomtangazia ujumbe wa Mungu na kumwomba akubali kuwa mama wa Mungu, Maria alimjibu kwa utii wote na mkamilifu. Maneno yake: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38), ni ushuhuda kwetu wa jinsi ya kujiaminisha kwa mapenzi yake Mungu. Kwa ile “ndiyo”, Maria akawa mama wa Mwana wa Mungu bila kupoteza ubikira wake, bali akauweka wakfu kwa njia yake Yesu. Tunamwona kuwa Mama wa Mungu, ambaye hakumshika Mwanae kwa manufaa yake tu, bali anatuita wote kutii neno lake na kulitenda (taz. Yn 2:5).
Kando yake Maria, kwa namna ya kumlinda Mtoto na Mamaye, yupo mtakatifu Yosefu. Kwa kawaida sanamu yake inamwonyesha akishika bakora mkononi, mara nyingine anashika pia koroboi. Mtakatifu Yosefu ana jukumu muhimu sana katika maisha ya Yesu na Maria. Yeye ndiye mlinzi asiyechoka kamwe kuilinda familia yake. Mungu anapomtaarifu kuhusu mpango mwovu wa Herode, Yosefu hatasita kufunga safari na kuelekea ugenini Misri (taz. Mt 2:13-15). Na mara tu hatari imepita, Yosefu atairudisha familia yake mpaka Nazarethi, na huko yeye atakuwa mlezi wa kwanza wa mtoto Yesu hadi ujana wake. Yosefu alitunza moyoni lile fumbo kuu kuhusu Yesu na Maria mchumba wake, na akiwa mwenye haki alipokea daima mapenzi ya Mungu na kuyafanya.
8. Moyo wa presepi unaanza kudunda kwa furaha tunapofikia Noeli, na tunaweka humo sanamu ya Mtoto Yesu. Mungu anajitokeza hivi, katika mtoto mdogo, kusudi tumpokee mikononi mwetu. Yeye anauficha, katika udhaifu na unyonge, uwezo wake wenye kuumba na kutengeneza kila kitu upya. Inaonekana kana kwamba haiwezekani, lakini ndivyo ilivyo: katika Yesu, Mungu alikuwa mtoto, na katika hali hiyo alipenda kufunua ukuu wa upendo wake, unaodhihirika katika kutabasamu na katika kuwakunjulia watu mikono yake.
Kuzaliwa kwa mtoto kila mara kunaleta furaha na ushangao, kwa sababu kunatuweka mbele ya fumbo kuu ya maisha mapya. Tunapoona macho ya wanandoa vijana kung’aa machozi mbele ya mwanao aliyezaliwa hapohapo, twaelewa hisia za Maria na Yosefu, ambao kwa kumwangalia mtoto Yesu walihisi uwepo wa Mungu katika maisha yao.
“Na uzima ulidhihirika” (1Yoh 1:2): kwa maneno haya machache mtume Yohane anadokeza fumbo la Umwilisho. Presepi inatuonyesha na kugusisha tukio hilo la pekee na la ajabu lililogeuza mkondo wa historia, na kutokana nalo huhesabika mfululizo wa miaka, kabla na baada ya kuzaliwa kwake Kristo.
Namna ya kutenda ya Mungu karibu inatubabaisha, kwa sababu tunaona haiwezekani kwamba Yeye aachane na utukufu wake ili kujifanya mwanadamu sawa na sisi. Twashangaa kumwona Mungu kutenda vitendo vyetu vya kawaida: kulala, kunyonya maziwa ya mamaye, kulia na kucheza kama watoto wengine wote. Kama kawaida yake, lakini, Mungu anatushangaza, kwa vile alivyo na mawazo tofauti na tunavyoyategemea, mbali na taswira tuliyojifanya kuhusu yeye. Hivyo basi, presepi, pamoja na kutuonyesha jinsi Mungu alivyopenda kuingia ulimwenguni, pia inatusukuma kufikiri juu ya maisha yetu, yanavyounganika na yale ya Mungu; inatualika pia kujifanya wafuasi wake kama tunataka kufikia kikomo che kweli cha maisha.
9. Inapokaribia sikukuu ya Tokeo la Bwana (Epifania), twaweka katika presepi sanamu tatu za Mamajusi.
Kwa kutazama ile nyota, wale mabwana wenye hekima, matajiri wa Mashariki, walifunga safari kuelekea Bethlehemu ili kumfahamu Yesu, na kumtolea zawadi ya dhahabu, uvumba na manemane. Pia katika zawadi hizi imefichwa maana muhimu: dhahabu inatoa heshima kwa Yesu kama mfalme; uvumba unadokeza umungu wake; manemane inaashiria ubinadamu wake mtakatifu utakaoonja kifo na kuzikwa.
Kwa kutazama taswira hizo katika presepi twaalikwa kutafakari juu ya wajibu ambao kila mwamini mkristo anao wa kuwa mwinjilishaji. Kila mmoja wetu anakuwa mleta Habari Njema kwa wale wote anaokutana nao, kwa kutoa ushuhuda wa furaha ya kukutana na Yesu na wa upendo wake kwa kutenda matendo ya huruma.
Mamajusi wanafundisha kwamba mtu aweza kutoka mbali sana na kufika kwa Kristo. Hao ni matajiri, wageni wenye hekima, wanaotamani mambo ya kimungu, wenye kufunga safari, itakayokuwa ndefu na yenye hatari, kuelekea Bethlehemu (taz. Mt 2:1-12). Mbele ya huyo Mtoto aliye Mfalme wanajazwa na furaha kubwa. Hawakwazwi na umaskini wa mazingira yale; hawasiti kupiga magoti na kumwabudu. Mbele yake wanatambua kuwa Mungu, kama ambavyo anaratibu kwa hekima mizunguko ya sayari, vilevile anaongoza mkondo wa historia, akiwaangusha wakuu na kuwakweza wanyonge. Nao Mamajusi, bila shaka, waliporudi pao, watakuwa wametoa simulizi juu ya mkutano huo wa ajabu na Masiya, wakizindua hivyo safari ya Injili katika mataifa.
10. Mbele ya presepi, mawazo yetu yanarudi kwa furaha kukumbuka tulipokuwa watoto na kwa hamu sana tulikuwa tunatazamia wakati wa kuanza kuiandaa. Kukumbuka hivyo kunatufanya tujitahidi kuelewa kwa undani zaidi zawadi kubwa tuliyopata kwa kurithishwa imani; na wakati huohuo kunatuhimiza kuwajibika na kufurahi katika kuwashirikisha watoto na wajukuu mang’amuzi hayohayo. Si muhimu sana ni kwa jinsi gani tunavyoandaa presepi: inaweza kuwa ileile miaka yote, au kuwa tofauti kila mwaka; kilicho muhimu ni kwamba iweze kugusa maisha yetu. Kila mahali na kwa kila namna, presepi inasimulia upendo wa Mungu, yule Mungu aliyejifanya mtoto ili kutuambia wazi jinsi alivyo karibu na kila mwanadamu, wa kila hali aliyo nayo.
Ndugu zangu wapendwa, kaka na dada, presepi ni sehemu tamu na muhimu ya mchakato wa kurithisha imani. Tangu utotoni, na halafu katika kila kipindi cha maisha yetu, inatulea tuje kumtazama Yesu, kuonja upendo anaotupenda Mungu, kuona na kuamini kwamba Mungu yupo pamoja nasi, nasi tupo pamoja naye, wote tukiwa watoto wake na ndugu kati yetu, kwa neema aliyotujalia yule Mtoto Mwana wa Mungu na wa Bikira Maria. Na kuona kwamba hayo yote ndiyo furaha ya kweli. Kwenye shule ya mt. Fransisko, tufungue mioyo yetu kupokea neema hii tulivu, na turuhusu kwamba katika kushangazwa iinuliwe sala nyenyekevu: yaani, shukrani zetu kwa Mungu aliyependa kushiriki nasi kila kitu ili asituache kamwe peke yetu.
Ilitolewa Greccio, katika Sanktuari ya Presepe, tarehe 1 Desemba 2019, ya saba ya upapa wetu.
FRANSISKO
[1] Tomaso wa Celano, Maisha ya Kwanza, 84: Machimbuko ya Kifransisko, na. 468.
[2] Taz. sana kama iliyotangulia, 85: FF, n. 469.
[2] Taz. sana kama iliyotangulia, 85: FF, n. 470.
Matini: ©Copyright - Libreria Editrice Vaticana
Tafsiri: ©Copyright – Familia za Maamkio –Iringa na Libreria Editrice Vaticana
Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana