Index

Back Top Print

[AR - BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya utume wa walei

Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

 

UTANGULIZI

1. HARAKATI ZA KITUME (Apostolicam Actuositatem) za watu wa Mungu[1] na usitawi wa nguvu zake vimewekwa kama lengo muhimu mojawapo la Mtaguso Mkuu. Hivyo, huo Mtaguso unawaelekea hima waamini walei, baada ya kuwa umeshakumbusha katika hati nyinginezo[2] sehemu yao halisi na ya muhimu sana katika utume wa Kanisa. Kwa kweli, utume wa walei, unaotokana na wito wenyewe wa kikristo, hauwezi kutoweka kamwe katika Kanisa. Maandiko Matakatifu yenyewe yanaonyesha wazi (taz. Mdo 11:19-21; 18:26; Rum 16:1-16; Flp 4:3) jinsi harakati hizo zilivyochipua na kuleta matunda katika Kanisa tangu awali.

Nyakati zetu pia zinadai bidii zisizopungua kutoka kwa walei; tena zaidi, mazingira ya siku hizi yanadai utume wao uwe umekua kweli katika nguvu na upana. Ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya kisayansi na ya kiteknolojia, mahusiano yanayokuwa ya jirani zaidi kati ya watu, yamepanua kwa utele nyanja za utume wa walei, nyanja ambazo mara nyingi walei tu wanaziweza, lakini pia yamezusha matatizo mapya yenye kudai bidii na hamasa zao. Utume huo ni wa lazima zaidi kutokana na kukua sana kwa kujitawala kwa sekta nyingi za maisha ya wanadamu, nako ni haki, ingawa mara nyingine kunaleta pia kutengana na utaratibu wa kimaadili na wa kidini; nalo laweza kuhatarisha sana maisha ya kikristo. Zaidi ya hayo, katika tarafa nyingi, ambamo mapadre ni wachache sana, au pengine wamezuiliwa uhuru wa kutoa huduma yao, Kanisa, bila utendaji wa walei, kwa shida tu lingeweza kudumu na kutenda kazi.

Ishara wazi ya kuwepo hitaji hilo la namna nyingi na la muhimu ni kazi inayofanywa na Roho Mtakatifu, ambaye leo anawajulisha zaidi na zaidi walei kuhusu wajibu wao, na anawahimiza popote wajiweke katika utumishi wa Kristo na wa Kanisa[3].

Katika hati hii Mtaguso unadhamiria kueleza kawaida na tabia yenye [utajiri wa] utofauti ya utume wa walei, na tena kuagiza misingi na kutoa miongozo ya kichungaji kwa ajili ya utekelezaji wake wenye mafanikio. Hayo yote yatakuwa mfano wa kanuni utakaosaidia katika marekebisho ya sheria za Kanisa kwa madhumuni ya utume wa walei.

Sura ya Kwanza

WITO WA WALEI KWA KAZI YA KITUME

Ushirikiano wa Walei katika utume wa Kanisa

2. Kanisa limeanzishwa kwa lengo la kuwashirikisha watu wote ukombozi wa wokovu, ambao hupatikana kwa kuenezwa ufalme wa Kristo duniani pote kwa utukufu wa Mungu[4]; na kwa njia ya wanadamu ulimwengu mzima unaelekezwa kweli kwa Kristo. Utendaji wote wa Mwili wa Fumbo unaoelekea shabaha hii unaitwa kazi ya kitume, nao Kanisa linautimiza kwa njia ya viungo vyake vyote, hata kama kwa namna mbalimbali; kwa vile wito wa kikristo ni pia, kwa tabia yake, wito kwa kazi ya kitume. Kama vile katika mwunganisho wa mwili hai kiungo chochote hakimo bila kuwa na kazi yake maalum, bali kinashiriki pamoja na uhai wa mwili pia utendaji wake, hali kadhalika katika Mwili wa Kristo, ulio Kanisa, mwili wote “kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe” (Efe 4:16). Vivyo, katika mwili huo, ushikamanisho na uungamanisho ni mkubwa (taz. Efe 4:16), kiasi kwamba kiungo kile ambacho kisingetenda kazi kwa ajili ya kuukuza mwili kadiri ya utendaji wake, kingeitwa hakina faida wala kwa Kanisa wala kwa chenyewe.

Katika Kanisa kuna tofauti za huduma, lakini utume ni mmoja. Mitume na waandamizi wao walikabidhiwa na Kristo majukumu ya kufundisha, kutakatifuza na kuongoza kwa jina lake na katika mamlaka yake. Lakini walei, hali wameshirikishwa huduma za Kristo za kikuhani, kinabii na kifalme, katika utume wa watu wa Mungu kwa ujumla wanatimiza wajibu kadiri ya hali yao katika Kanisa na katika ulimwengu [5]. Kwa kweli wanatimiza kazi za kitume kwa utendaji wao kwa ajili ya uinjilishaji na utakatifuzaji wa watu, na kwa kukuza na kukamilisha mpango wa malimwengu kwa roho ya Injili, na hivyo, katika kuyashughulikia malimwengu, humshuhudia Kristo kwa wazi na kusaidia wokovu wa watu. Kwa vile hali ya kawaida ya walei ni kuishi ulimwenguni kati ya shughuli za kidunia, wao huitwa na Mungu ili, hali wamejaa roho ya kikristo, watekeleze utume wao ulimwenguni kwa mfano wa chachu.

Misingi ya utume wa walei

3. Haki na wajibu wa utume wa walei hutokana moja kwa moja na muungano wao na Kristo aliye Kichwa. Kwa sababu, hali wameingizwa katika Mwili wa Fumbo wa Kristo kwa njia ya Ubatizo, wakapewa nguvu kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwa njia ya Kipaimara, hapo wanaagizwa kwa utume na Bwana mwenyewe. Wao wanawekwa wakfu ili kufanywa ukuhani wa kifalme na taifa takatifu (taz. 1Pet 2:4-10) ili watoe dhabihu za kiroho kwa njia ya utendaji wote, na kumshuhudia Kristo katika mahali pote. Aidha, kwa njia ya masakramenti, hasa Ekaristi, mapendo, ambayo ni kama mtima wa utume wote, yameshirikishwa kwao na kulishwa [6].

Utume unatekelezwa katika imani, tumaini na mapendo, ambavyo Roho Mtakatifu hueneza mioyoni mwa wanakanisa wote. Na ni katika amri ya upendo, iliyo amri kuu ya Bwana, kwamba wakristo wote wahimizwa kutafuta utukufu wa Mungu kwa ujio wa ufalme wake, na uzima wa milele kwa watu wote, ili wamjue Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo aliyemtuma (taz. Yn 17:3).

Waamini wote wametwishwa mzigo wenye heshima wa kutenda kazi ili ujumbe wa wokovu wa kimungu ujulikane na kupokelewa na wanadamu wote, popote duniani.

Kwa ajili ya kutekeleza utume huo Roho Mtakatifu, ambaye hutenda utakatifu wa watu wa Mungu kwa njia ya huduma takatifu na ya masakramenti anawagawia waamini karama za pekee (taz. 1Kor 12:7), “akimgawia kila mtu kama apendavyo yeye” (1Kor 12:11), ili “kila mmoja, kwa kadiri alivyoipokea karama, aitumie kwa kuhudumiana”, na hivyo pia wao “kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu” (1Pet 4:10) wanasaidia ili “mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo” (taz. Efe 4:16). Katika kupokea karama hizo, hata zile za kawaida zaidi (simpliciorum), hutokana kwa kila mwamini, haki na wajibu wa kuitumia kwa ajili ya manufaa ya wanadamu na ya ujengaji wa Kanisa, katika Kanisa na katika ulimwengu, kwa ule uhuru wa Roho Mtakatifu, ambaye “huvuma apendako” (Yn 3:8), na wakati huohuo katika ushirika na ndugu katika Kristo, hasa na wachungaji wao, wenye madaraka ya kufanya hukumu ya tabia yao halisi, pia ya matumizi yake yenye utaratibu; pasipo lengo la kumzimisha Roho, bali la kujaribu mambo yote na kulishika lililo jema (taz. 1The 5:12,19,21)[7].

Maisha ya kiroho ya walei na utume

4. Kwa kuwa chemchemi na asili za utume wote wa Kanisa ni Kristo aliyetumwa na Baba, ni wazi kwamba uzaaji wa utume wa walei hutegemea sana muungano wao wenye uhai na Kristo, kwa sababu Bwana asema: “Akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yn 15:5). Maisha haya ya muungano wa walei na Kristo hulishwa katika Kanisa kwa misaada ya kiroho, ambayo ni ya waamini wote kwa pamoja, hasa kwa njia ya mahudhurio ya dhati kwenye Liturujia takatifu[8]. Walei watumie misaada hiyo kwa namna ambayo, wakati wanatimiza kwa unyofu shughuli za ulimwengu katika hali ya kawaida ya maisha, wasitengane katika maisha yao na muungano na Kristo, bali wakue ndani yake, katika kutimiza matendo yao kulingana na mapenzi ya Mungu. Kwa njia hiyo, lazima walei waendelee katika utakatifu kwa moyo ulio tayari na mchangamfu, huku wakijaribu kumudu magumu kwa busara na subira[9]. Wala mahangaiko kwa ajili ya familia, wala majukumu mengine ya kiulimwengu, havitakiwi kuwa mbali na mwelekeo wa kiroho wa maisha, kadiri ya maneno ya Mtume: “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu Kristo, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye” (Kol 3:17).

Maisha haya yadai mazoezi yasiyokoma ya imani, tumaini na mapendo.

Kwa mwanga wa imani tu, na katika kutafakari Neno la Mungu huwezekana daima na popote kumtambua Mungu ambaye “ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda na kuwa na uhai wetu” (Mdo 17:28), kutafuta mapenzi yake katika tukio lolote, kumwona Kristo ndani ya kila mtu, wa jirani au wa mbali, kuamua hukumu iliyo sahihi kuhusu maana na thamani halisi za malimwengu, kwa yenyewe na kwa mtazamo wa kikomo cha mwanadamu.

Wenye imani hiyo huishi katika tumaini la kufunuliwa kwa wana wa Mungu, wakikumbuka msalaba na ufufuko wa Yesu.

Katika hija ya maisha haya, hao hali wamefichwa pamoja na Kristo kwa Mungu, na wakiwa huru kutoka katika utumwa wa mali, wakati wanatazamia mema yadumuyo milele, kwa moyo mkarimu wanajitoa kabisa kueneza ufalme wa Mungu, na kupenyeza na kukamilisha kwa roho ya kikristo mpango wa malimwengu. Kati ya taabu za maisha haya, wanapata nguvu katika tumaini, wakihesabu “mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu” (Rum 8:18).

Wakisukumwa na pendo litokalo kwa Mungu, [walei] huwatendea watu wote mema, na hasa jamaa waaminio (taz. Gal 6:10). Hivyo wakiweka mbali “uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote” (1Pet 2:1), wanawavuta watu kwa Kristo. Pendo la Mungu “lililokwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rum 5:5), linawawezesha walei kuonyesha kweli roho ya heri nane katika maisha yao. Wakimfuata Yesu maskini hawafishi moyo kwa sababu ya utovu wa mali zisizodumu, wala hawapandi kiburi endapo zinakuwa nyingi; wakimfuasa Yesu mnyenyekevu hawajigambi (taz. Gal 5:26), bali wanafanya bidii kumpenda Mungu kuliko kuwapenda wanadamu, wakiwa tayari kila wakati kuacha vyote kwa ajili ya Kristo (taz. Lk 14:26) na kuudhiwa kwa ajili ya haki (taz. Mt 5:10), wakikumbuka neno la Bwana: “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate” (Mt 16:24). Kwa kusitawisha urafiki wa kikristo kati yao wanapeana msaada katika kila hitaji.

Maisha ya kiroho ya walei ya namna hiyo, inatakiwa kuwa na sura ya pekee kutokana na hadhi ya ndoa na ya familia, ya useja au ya ujane, na hali ya ugonjwa wa kudumu, na harakati za kikazi au za kijamii. Hivyo wasiache kusitawisha kwa bidii sifa na vipawa walivyopewa na vinavyolingana na hali zao hizo, wala kuvitumia vipaji vyao walivyopatiwa na Roho Mtakatifu.

Aidha walei ambao, kwa kuufuata wito wao wamejiunga na shirika au chama kimojawapo kati ya vilivyokubaliwa na Kanisa, wajitahidi vilevile kujifunza kwa ndani tabia ya pekee ya maisha ya kiroho yake chenyewe.

Pia, watathmini sana ustadi wa kazi, maana ya familia na maana ya jamii, na fadhila zile zenye ubora katika mahusiano ya kijamii, yaani unyofu, roho ya haki, kusema ukweli, ukarimu, moyo imara, ambazo bila hizo haiwezekani tu maisha ya kweli ya kikristo yawepo.

Mfano kamili wa maisha haya ya kiroho na ya kitume ni Bikira Maria mtakatifu, Malkia wa Mitume, ambaye alipokuwa akiishi hapa duniani maisha ya kawaida sawa na wote, yenye kujaa bidii kwa ajili ya familia na kazi, alikuwa daima na moyo mmoja na Mwanae, akashiriki kwa namna ya pekee sana katika kazi ya Mwokozi. Tena sasa, baada ya kupalizwa mbinguni “kwa mapendo yake ya kimama, huwaangalia ndugu wa Mwanawe wanaohiji bado na kuishi katika hatari na taabu, mpaka watakapofikishwa kwenye makao yenye furaha”[10]. Wote wamtukuze kwa heshima kuu na kukabidhi kwa uongozi wake wa kimama maisha yao na utume wao.

Sura ya Pili

MADHUMUNI YA UTUME WA WALEI

Utangulizi

5. Kazi ya ukombozi wa Kristo, yenye kwa msingi wake lengo la kuwaokoa wanadamu, inahusiana pia na kuweka utaratibu wa mpango wa malimwengu. Kwa hiyo utume wa Kanisa sio tu kupeleka ujumbe wa Kristo na neema yake kwa watu wote, lakini pia kupenya na kuenea na kukamilisha mpango wa malimwengu kwa roho ya kiinjili. Kwa hiyo walei, huku wakitekeleza utume huo wa Kanisa, wanatimiza kazi za kitume katika Kanisa na katika ulimwengu, katika mpango wa mambo ya kiroho na mpango wa malimwengu. Mipango hiyo miwili, ingawa inatofautiana, katika azimio la Mungu lililo moja imeunganika sana, kiasi kwamba Mungu mwenyewe hutaka kuunganisha, katika Kristo, ulimwengu wote kuwa kiumbe kipya, [kilicho] kichanga hapa duniani na [kitakachokuwa] kikamilifu katika siku ya mwisho. Katika mipango hiyo miwili mlei, aliye mwamini na raia kwa wakati mmoja, anatakiwa kuongozwa daima na dhamiri ya kikristo iliyo moja.

Utume wa kuinjilisha na wa kutakatifuza

6. Lengo la utume wa Kanisa ni wokovu wa wanadamu unaopatikana kwa imani kwa Kristo na neema yake. Kwa hiyo, utume wa Kanisa, na wa kila mwanakanisa, unaelekea kabla ya yote kudhihirisha kwa maneno na matendo mbele ya ulimwengu ujumbe wa Kristo na kushirikisha neema yake. Utume huo hutekelezwa hasa kwa huduma ya neno na ya sakramenti, huduma iliyowekwa kwa namna mahsusi kwa wakleri, na ambayo pia walei wanayo sehemu yao muhimu sana ya kutekeleza, ili wapate kuwa “watenda kazi pamoja na kweli” (3Yoh 8). Hasa katika hayo utume wa walei na huduma ya kichungaji zinatimilizana.

Walei Wanapata fursa nyingi sana za kuweza kuutimiza utume wa uinjilishaji na wa utakatifuzaji. Ushuhuda wenyewe wa maisha ya kikristo na ya matendo mema yaliyotimizwa kwa roho ya kimungu vina nguvu ya kuwavutia watu kwenye imani na kwa Mungu, kama anavyosema Bwana: “Hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mt 5:16).

Lakini utume huo sio tu ushuhuda wa maisha; mtume wa kweli hutafuta nafasi ili apate kumtangaza Kristo kwa njia ya maneno kwa wasioamini, apate kuwaongoza kwenye imani; na kwa waaminio, apate kuwafundisha, kuthibitisha na kuongoza kwenye maisha yenye ari zaidi; “maana upendo wa Kristo watubidisha” (2Kor 5:14), na moyoni mwa kila mwamini yasikike maneno ya Mtume: “Ole wangu nisipoihubiri Injili” (1Kor 9:16)[11].

Maadamu wakati wetu huu matatizo mapya yanazuka na makosa mazito yanaenea ambayo yanajaribu kuangamiza dini toka misingi yake, na maadili na jamii yenyewe ya wanadamu, Mtaguso Mkuu huu unawasihi kwa moyo walei ili, kulingana na vipawa vya akili na mafundisho ya kila mmoja, kwa kufuata nia ya Kanisa, watimize kwa bidii zaidi sehemu yao katika kuchanganua, kulinda, na kutimiza kanuni za kikristo katika kukabili matatizo ya wakati huu.

Bidii ya kupenyeza roho ya kikristo katika mpango wa malimwengu

7. Azimio la Mungu kuhusu ulimwengu ni kwamba wanadamu waanzishe na kukamilisha zaidi na zaidi, kwa moyo mmoja, mpango wa malimwengu.

Mambo yote ambayo kwa jumla yanafanya mpango wa malimwengu, yaani mema ya maisha na ya familia, utamaduni, uchumi, sanaa na amali, taasisi za jamii mintarafu siasa, mahusiano ya kimataifa na mengine kama haya, pamoja na mabadiliko na maendeleo yake, siyo tu vyombo kwa ajili ya lengo la kikomo cha binadamu, lakini pia yana thamani yake ambayo Mungu aliweka ndani yake, yakitazamwa kwa yenyewe au kama sehemu za mpango mzima wa malimwengu: “Na Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana” (Mwa 1:31). Wema huu wa kutoka kuumbwa unapata hadhi mahsusi kutokana na uhusiano wake na binadamu, ambaye vyote viliumbwa ili kumtumikia yeye. Kisha, ilimpendeza Mungu kuweka umoja wa vitu vyote katika Kristo, vilivyo duniani na mbinguni, “ili kwamba awe mtangulizi katika yote” (Kol 1:18). Kikomo hicho, lakini, siyo kwamba kinayaondolea malimwengu uhuru wake, shabaha, sheria, vyombo vyake yenyewe, wala umuhimu wake kwa manufaa ya wanadamu, bali kinayakamilisha katika umbile na ubora wake, pamoja na kuyalinganisha na wito kamili wa binadamu hapa duniani.

Katika mfululizo wa historia, matumizi ya malimwengu yametiwa dosari na makasoro makubwa kwa sababu wanadamu, waliodhoofika kwa dhambi ya asili, mara nyingi walianguka katika makosa mengi kuhusu Mungu wa kweli, tabia ya binadamu na kanuni za msingi za maadili. Na kutokana na hayo, desturi na asasi za kibinadamu zimechafuka na ubinadamu wenyewe mara nyingi hugandamizwa. Siku hizi pia, watu wasio wachache, wakiwa na imani ya kupita kiasi kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia, wanaelekea kwenye namna ya uabudio wa vilimwengu, hali wamejifanya watumwa kwao badala ya kuwa mabwana wao.

Ni wajibu wa Kanisa zima kufanya kazi ili wanadamu wawezeshwe kuunda vema mpango mzima wa malimwengu na kuuelekeza kwa Mungu katika Kristo. Ni juu ya Wachungaji kutamka wazi kanuni za msingi kuhusu kikomo cha huluka na cha matumizi ya ulimwengu, kutoa misaada ya kimaadili na ya kiroho ili mpango wa malimwengu uundwe katika Kristo.

Lazima walei kuweka uundaji wa mpango wa malimwengu kama wajibu wao pekee, na wakiongozwa na mwanga wa Injili na nia ya Kanisa, pia wakisukumwa na upendo wa kikristo, wafanye kazi moja kwa moja ndani yake na kwa utendaji rasmi. Tena walei wanatakiwa kufanya kazi pamoja, kama raia pamoja na raia wenzao, kadiri ya ustadi wa kila mmoja kwa dhima yao wenyewe; kutafuta popote na katika mambo yote haki ya ufalme wa Mungu. Mpango wa malimwengu unatakiwa kuundwa kwa namna ambayo, pamoja na kuhifadhi sheria zake halisi, uafikiane zaidi na zaidi na kanuni za maisha ya kikristo, na kulingana na mazingira mbalimbali ya mahali, nyakati na mataifa. Kati ya kazi hizi za kitume, ina umuhimu wa pekee utendaji wa wakristo katika nyanja za kijamii, ambao Mtaguso hupenda uenee katika malimwengu yote, pia katika utamaduni[12].

Matendo ya huruma

8. Kila utendaji wa kitume unachota chanzo na nguvu katika mapendo. Lakini kuna matendo ambayo kwa tabia yake, kwa vile Kristo Bwana alitaka ziwe ishara za utume wake wa kimasiya (taz. Mt 11:4-5), yanaweza kuwa sura halisi ya mapendo.

Amri kuu katika Sheria ni kumpenda Mungu kwa moyo wote, na kumpenda jirani kama nafsi yako (taz. Mt 22:37-40). Lakini amri hii ya mapendo kwa jirani, Kristo aliifanya upya katika yeye na kuitajirisha kwa maana mpya pale alipoeleza kuwepo yeye mwenyewe katika ndugu zake wanapotendewa mapendo, akisema, “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mt 25:40). Maana yeye, alipochukua ubinadamu amewafunganisha naye kama familia yake, kwa mshikamano usio wa ulimwengu huu, wanadamu wote, na ameweka upendo kuwa alama ya wafuasi wake, akisema, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yn 13:35).

Kanisa takatifu katika asili yake lilikuwa linajidhihirisha kuwa kitu kimoja katika kifungo cha upendo pamoja na Kristo, kwa kuunganisha upendo (agape) na karamu ya Ekaristi. Hali kadhalika, wakati wowote latambulikana kwa alama hiyo ya mapendo, na pamoja na kuufurahia utendaji mwema wa wengine, linadai kuwa matendo ya huruma ni wajibu na haki zake zisizoondoleka. Kwa hiyo, huruma kwa maskini na wagonjwa, vilevile matendo ya huruma na ya ujima (mutui auxilii), yenye lengo la kupunguza kila aina ya dhiki za wanadamu, yanaheshimiwa na Kanisa kwa namna ya pekee[13].

Wakati huu, ambapo vyombo vya mawasiliano vimekuwa vyepesi zaidi, umbali kati ya wanadamu ni kama umeondolewa, na wakazi wa dunia nzima wamekuwa kama viungo vya familia moja, utendaji na matendo yamekuwa ya lazima kwa maeneo yote. Utendaji wa huruma leo waweza kuwaelekea watu wote kabisa na mahitaji yote, na lazima uwe wa namna hiyo. Popote wapo wenye kukosa chakula na kinywaji, mavazi, makao, madawa, kazi na elimu, na vifaa vinavyohitajika ili kuweza kuishi maisha yaliyo kweli ya kiutu; wapo wanaohangaika katika dhiki au kwa sababu ya kukosa afya, wanaoteseka mbali na makwao au kifungoni, na hapo mapendo ya kikristo lazima yawatafute na kuwapata, kuwaliwaza kwa uangalizi mkarimu, na kuwainua kwa kuwapatia msaada. Faradhi hiyo inawakalia, kabla ya wengine wowote, mtu binafsi na taifa moja moja wenye kuishi katika utajiri[14].

Kusudi utendaji wa huruma uweze kuwa usiotiliwa mashaka na kuonekana wa tabia hiyo, inabidi kutambua katika kila jirani sura ya Mungu, ambaye kwa mfano wake alimwumba, na Kristo Bwana, ambaye kwake kimetolewa kweli kila kitolewacho kwa wahitaji. Uheshimiwe, kwa adabu ya kujali, uhuru na hadhi vya mwanadamu apokeaye msaada; nia njema isitiliwe dosari ya kutafuta maslahi yoyote ya binafsi wala ya tamaa ya kutawala [15]; matakwa ya haki lazima yatimilizwe kwanza: kile ambacho tayari cha haki, hakitolewi kama zawadi ya mapendo; matokeo na sababu za maovu ziondolewe; misaada ipangwe kwa namna ambayo wale wanaoipokea wapate kuondokana polepole na kifungo cha kuwategemea wengine, bali waweze kujitegemea.

Kwa hiyo walei watilie maanani na kutegemeza, kwa kadiri ya uwezo wao, matendo ya huruma na miradi ya msaada wa kijamii, ya kutoka watu binafsi au ya kiserikali, pia ya kimataifa, ambayo kwa njia yake msaada wa kimatendo hutolewa kwa mtu mmoja mmoja au kwa mataifa wanaopambana na umaskini. [Nao wafanya hivyo] wakishikamana na watu wote wenye mapenzi mema[16].

Sura ya Tatu

NYANJA MBALIMBALI ZA UTUME

Utangulizi

9. Walei wanatimiza utume wao ulio wa namna nyingi, katika Kanisa na vilevile katika dunia. Katika pande mbili hizo, nyanja mbalimbali za kazi za kitume zafunguliwa kwao, ambazo twapenda hapa kuzikumbuka zile zilizo kuu. Zenyewe ni kama zifuatavyo: jumuiya za Kanisa, familia, vijana, mazingira ya kijamii, mpango wa kitaifa na wa kimataifa. Na kwa vile wanawake siku hizi wanashiriki zaidi na zaidi katika sehemu zote za maisha ya kijamii, ushirikiano wao mpana ni muhimu sana pia katika nyanja za utume wa Kanisa.

Jumuiya za Kanisa

10. Walei, kama washiriki wa huduma ya Kristo kuhani, nabii na mfalme, wanayo nafasi hai katika maisha ya Kanisa na katika utendaji wake. Ndani ya jumuiya za Kanisa matendo yao yanahitajika sana, kiasi kwamba pasipo haya hata utume wenyewe wa wachungaji huwa hauwezi kufikia mafanikio kamili. Maana walei wenye roho halisi ya kitume, kama wale wanaume na wanawake waliokuwa wakimsaidia Paulo katika kueneza Injili (taz. Mdo 18:18.26; Rum 16:3), wanawakirimia ndugu zao yale waliyopungukiwa, na wanaburudisha roho za wachungaji na za waamini wengine wa taifa la Mungu (taz. 1Kor 16:17-18). Huku wakilishwa na mahudhurio hai katika maisha ya kiliturujia ya jumuiya yao, wanashiriki kwa bidii katika kazi zake za kitume; wanawaongoza watu ambao labda wako mbali na Kanisa, wapate kuliingia; wanasaidia kwa moyo katika kupasha Neno la Mungu, hasa kwa njia ya kufundisha katekisimu; wakichangia ubingwa wao wanaleta ufanisi zaidi katika uangalizi wa roho na usimamizi wa mali ya Kanisa.

Parokia ni mfano mwangavu wa utume wa kijumuiya; kwa kuunganisha pamoja tofauti za watu ambao wanaishi katika eneo lake na kwa kuziingiza katika upopote (universalitati) wa Kanisa[17]. Walei wazoee kufanya kazi parokiani bega kwa bega na mapadre wao[18], kuieleza jumuiya ya Kanisa matatizo yao wenyewe na ya ulimwengu, na masuala yanayohusu wokovu wa wanadamu, ili yachunguzwe na kutatuliwa kwa mchango wa wote; wazoee pia kujitoa kwa bidii, kulingana na uwezo wa kila mmoja, kwa tendo lolote la kitume na la kimisioni la jamaa yao ya kikanisa.

Wazidi kufahamu maana ya jimbo, ambalo parokia ni kama chembechembe yake, tayari sikuzote, kwa mwaliko wa Mchungaji wao, kuweka nguvu zao katika shughuli za kijimbo. Aidha, ili wapate kukidhi haja za mjini na za maeneo ya mashambani[19], wasifunge ushirikiano wao ndani ya mipaka ya parokia au ya jimbo, bali wakubali kuupanua hadi eneo la kimaparokia, kimajimbo, kitaifa na kimataifa, seuze siku hizi ambapo uhamahamaji wa watu unavyozidi, mahusiano ya aina nyingi yanaongezeka na mawasiliano yamekuwa rahisi, hivyo vikiathiri sehemu zote za jamii zisiweze kujitosheleza. Kwa namna hiyo wazingatie mahitaji ya watu wa Mungu waliotawanyika popote duniani. Kabla ya yote, wajihusishe na utendaji wa kimisioni wakitoa misaada ya mali au wakijitolea wenyewe. Maana ni wajibu na heshima ya wakristo kumrudishia Mungu sehemu ya mali wanazojaliwa naye.

Familia

11. Kwa vile Muumba wa vitu vyote aliunda jumuiya ya ndoa kama chanzo na msingi wa jamii ya kibinadamu, na kwa neema yake aliifanya iwe fumbo kubwa katika Kristo na Kanisa (taz. Efe 5:32), hivyo utume wa wanyumba ( coniuges) na wa familia umepata umuhimu wa pekee kwa ajili ya Kanisa na kwa umma pia.

Wanyumba wa kikristo ni washiriki wa neema na mashahidi wa imani kila moja kwa mwenzake na mbele ya wana wao na jamaa wengine. Wao wenyewe ni kwa ajili ya watoto wao wajumbe wa kwanza wa imani na walezi; huwalea katika maisha ya kikristo na ya kitume kwa maneno na mifano, huwasaidia kwa busara katika kufuatilia wito wao na hutegemeza kwa bidii zote mwito mtakatifu ambao pengine unaonekana mwao.

Ilikuwa daima wajibu wa wanyumba, lakini leo hata zaidi ni sehemu kubwa wa utume wao: kuonyesha na kushuhudia kwa maisha yao hali ya kutokutanguka (indissolubilitatem) na ya utakatifu ya muungano wa ndoa; kuthibitisha kwa nguvu haki na wajibu, ulio wa wazazi na walezi, wa kuwalea kikristo watoto wao; kulinda hadhi na uhuru halali wa familia. Kwa hiyo wenyewe na waamini wengine washiriki pamoja na watu wa mapenzi mema, ili katika vifungu vya sheria haki hizi zitunzwe kikamilifu; katika uongozi wa jamii yazingatiwe madai ya familia kwa habari ya makazi, malezi ya watoto, hali ya kazi, usalama katika jamii na uzito wa kodi; katika kuratibu uhamaji, umoja wa nyumba ulindwe kwa makini[20].

Familia yenyewe inapokea toka kwa Mungu utume huo ili iwe chembechembe hai ya kwanza katika jamii. Itatimiza utume huo ikiwa, kwa kupendana wanafamilia na kusali sala za pamoja kwa Mungu, itakuwa kama patakatifu pa kinyumbani pa Kanisa; kama familia nzima inajiunga na ibada za kiliturujia za Kanisa; hatimaye, kama familia ni wakaribisha wageni kwa matendo kweli, kama inakuza haki na matendo mema mengine kwa ajili ya ndugu wote wenye matatizo. Kati ya kazi mbalimbali za kitume ambazo familia zatarajiwa kutekeleza, zinaweza kuhesabiwa hizi zifuatazo: kupokea (adoptare) kama wana watoto walioachwa, kukaribisha kwa wema wageni, kusaidia katika uongozi wa shule mbalimbali, kuwashauri vijana wabaleghe kwa nasaha na mali, kuwasaidia wenye kuchumbiana ili wajiandae vizuri kwa ndoa yao, kushiriki katika kufundisha katekisimu, kuwasimamia majozi na familia zikiwepo kwenye magumu ya kimwili au ya kiroho, kuwasaidia wazee siyo tu kwa mahitaji ya lazima, bali kuwashirikisha kwa haki matunda ya maendeleo ya kiuchumi.

Familia za kikristo ambazo katika maisha yao yote zinajilinganisha na Injili na zaonyesha mfano wa ndoa ya kikristo, daima na popote zinatoa ushuhuda muhimu sana wa Kristo mbele ya ulimwengu, hasa katika nchi zile ambazo mbegu za Injili zinaanza tu kumwagwa, au ambapo Kanisa linaanzishwa hapohapo, au pengine lipo katika hatari kubwa[21].

Ili familia ziweze kutekeleza utume wao kwa utimilifu mkubwa na rahisi zaidi, pengine itafaa ziweze kuunganika katika vyama[22].

Vijana

12. Vijana wanaathiri kwa nguvu sana jamii ya siku hizi [23]. Mazingira ya maisha yao, fikra na mahusiano na familia zao yamebadilika siyo kidogo. Mara nyingi wanaingia upesi mno mazingira mapya ya kiuchumi na ya kijamii. Lakini, wakati umuhimu wao kwa habari ya kijamii na ya kisiasa pia unakua siku kwa siku, wanaonekana kama hawamudu kuukabili inavyotakiwa wajibu huo mpya.

Uzito wao katika jamii uliokua unawadai utendaji wa kitume unaolingana nao, ambao hulka yao vilevile inawaweka tayari kwao. Kulingana na kukomaa kwa kujifahamu, wakisukumwa na hari ya maisha na ya uchangamfu wa nguvu zao, washike dhima yao, watamani kushika na kutimiza sehemu zao katika maisha ya kijamii na ya kitamaduni: juhudi hii ikipenyewa na roho ya Kristo na kusitawishwa na utii na upendo kwa wachungaji wa Kanisa, inaleta tumaini ya matunda tele. Wao wanatakiwa kuwa mitume wa kwanza na wa jirani sana kwa vijana, wakitimiza wenyewe utume kati yao, wakizingatia mazingira ya kijamii wanamoishi[24].

Watu wazima wajitahidi kuanzisha mazungumzo ya kirafiki na vijana, nayo yatasaidia kuwe rahisi kule kufahamiana na kushirikishana tunu za ndani za kila mmoja, kwa kushinda tofauti ya umri. Watu wazima wahimize vijana kujishughulisha katika utume, kwanza kabisa kwa njia ya mfano, na panapowezekana, kwa ushauri nasaha na msaada thabiti. Aidha vijana wawaheshimu na kuwaamini watu wazima; hata kama wanaelekea kwa tabia yao kwenye mambo mapya, waheshimu inavyofaa mapokeo yaliyo mazuri.

Watoto pia wana kazi zao za kitume. Kulingana na nguvu zao ni mashahidi walio hai wa Kristo kati ya wenzao.

Mazingira ya kijamii

13. Utume katika mazingira ya kijamii, yaani juhudi ya kupenyeza roho ya kikristo ndani ya fikra na desturi, sheria na miundo ya jumuiya wanamoishi ni jukumu na faradhi ya walei, kiasi kwamba haliwezi kutekelezwa na wengine kwa namna ya kuridhisha. Katika uwanja huo walei waweza kutimiza utume wa mtu kwa mwenzake aliye sawa na yeye. Hapa wanatimiliza ushuhuda wa maisha kwa kutoa pia ushuhuda wa maneno[25]. Hapa, katika mazingira ya kazi zao, au wa amali, au uwanja wa masomo, au eneo la makazi, au nafasi za kiburudisho, au katika vyama, walei ni wa kufaa kuliko wote kuwasaidia ndugu zao.

Walei wanatimiza utume huu wa Kanisa katika ulimwengu kwanza kabisa kwa mwambatano wa mwenendo na imani, ambao kwa njia yake wanakuwa mwanga wa ulimwengu; kwa kushughulikia lolote kwa unyofu, wao wanawavuta watu wote wapende ukweli na wema, na hatimaye kumpenda Kristo na Kanisa; kwa mapendo yale ya kidugu ambayo yanawawezesha washiriki hali ya maisha, ya kazi, mateso na matumaini ya ndugu zao, waandae polepole mioyo ya wote iwe tayari kutendewa kwa neema inayoweza kuokoa; kwa kuzingatia fika wajibu wao katika usitawi wa jamii unaowasukuma kuishika juhudi nyumbani, kazini na katika jamii, kwa ukarimu wa kikristo. Hivyo namna yao ya kutenda inapenya polepole mazingira wanamoishi na kufanya kazi.

Utume huo unatakiwa uwafikie wote wanaopatikana hapo, bila kuwa-nyima wema wowote wa kiroho au wa kimwili ambao unawezekana kuwapatia. Lakini walio mitume kwelikweli, hawaridhiki na matendo hayo peke yake, ila watamani kumtangaza Kristo kwa wenzao pia kwa njia ya maneno. Maana watu wengi hawapati kusikia Injili na kumjua Kristo, isipokuwa kwa njia ya walei walio jirani nao.

Mpango wa kitaifa na wa kimataifa

14. Uwanja wa utume unakuwa mpana mno tukiingia kwenye mipango ya kitaifa na ya kimataifa, ndipo wanapokuwa walei hasa wahudumu wa hekima ya kikristo. Katika kupenda nchi asili na kwa kutimiza kiaminifu wajibu wa kiraia, wakatoliki wajisikie wana faradhi ya kusitawisha mema ya wote, na uzani wa maoni yao uweze kuathiri kwa namna nzuri mamlaka ya kiserikali, nayo itawale kulingana na haki, na sheria zilingane na masharti ya kimaadili na mema ya wote. Wakatoliki waliofunzwa katika masuala ya siasa, na yakini, walio thabiti katika imani na mafundisho ya kikristo, wasikatae kushika nafasi katika uongozi; kwa sababu kwa njia ya cheo cha wadhifa wao, wakikishika kwa unyofu, wataweza kutoa msaada mkubwa kwa ajili ya mema ya wote, na wakati huohuo kuiandalia Injili njia.

Wakatoliki wajitahidi kushirikiana na watu wote wa mapenzi mema ili kusitawisha mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo matakatifu, yoyote yenye kupendeza (taz. Flp 4:8). Wakubali kuanzisha dialogia nao, wakiwawahi kwa busara na ukarimu; wachochee ili ufanyike utafiti na uchunguzi kuhusu taasisi za kijamii ili zipate kukamilishwa kwa kuafikiana na roho ya Injili.

Kati ya ishara za nyakati zetu yastahili kukumbukwa hisia ya mshikamano uliopo na unaokua siku kwa siku kati ya watu wa mataifa yote; nao pia ni wajibu wa utume wa walei kuikuza kwa juhudi na kuufanya ukawe upendo wa kweli na wa haki wa kidugu. Aidha, walei wanatakiwa kutambua mpango wa kimataifa na hoja na mielekeo, viwe vya kinadharia au vya kiutendaji, vinavyojitokeza ndani yake, hasa vile vinavyohusu mataifa yanayoendelea[26].

Wote wenye kufanya kazi kwenye nchi za nje, au kutoa msaada kwa ajili ya nchi hizo, wazingatie kwamba mahusiano kati ya mataifa yatakiwa kuwa badilishano la kidugu kweli, ambamo pande zote mbili hutoa na kupokea kwa wakati mmoja. Tena, wale wenye kusafiri kwa mujibu wa shughuli za kimataifa, au kwa biashara, au kitalii, wakumbuke ya kuwa wenyewe ni popote wajumbe wasafiri wa Kristo, na waenende kulingana kweli na tabia hii.

Sura ya Nne

AINA MBALIMBALI ZA UTUME

Utangulizi

15. Walei waweza kutimiza kazi zao za kitume ama kama mtu mmoja mmoja ama wakiwa wamejiunga katika jumuiya au umoja wa aina mbalimbali.

Umuhimu wa utume wa mtu mmoja mmoja, na tabia yake ya kuwa wa aina nyingi

16. Utume ambao kila mlei atakiwa kutimiza peke yake, kwa vile hububujika na chemchemi ya maisha yaliyo kweli ya kikristo (taz. Yn 4:14), ni chanzo na msingi wa kila aina ya utume wa walei, pia wa utume ule wa pamoja, na hakipo kiwezacho kuchukua nafasi yake.

Kwa utume wa aina hiyo, ambao daima na popote inafaa na ambao katika mazingira mengine ni ule pekee unaowezekana na wa kufaa, walei wowote wanalikwa na kudaiwa, wa kila hali, hata ikiwa wanakosa nafasi au uwezekano ya kushiriki katika umoja mbalimbali.

Kazi za kitume ambazo kwazo walei wajenga Kanisa, watakatifuza ulimwengu na kuuhuisha katika Kristo ni nyingi.

Namna ya pekee ya utume wa mtu mmoja mmoja na ishara inayofaa kwa nyakati zetu ili kuonyesha Kristo aliye hai katika waamini wote, ni ule ushuhuda wa maisha ya kilei yote, yatokanayo na imani, matumaini na mapendo. Halafu, kwa njia ya utume wa neno, ambao mara nyingine ni wa lazima kabisa, walei wamtangaza Kristo, wanafafanua mafundisho yake, wanayaeneza kadiri ya hali na uwezo wao na kuyakiri kiaminifu.

Hali wakishiriki pia, kama raia za dunia hii, katika yale yahusuyo kujenga na kustawisha mpango wa malimwengu, walei watazamiwa kutafuta katika nuru ya imani, kwenye maisha ya nyumbani, ya kazini, ya kitamaduni na ya kijamii, visa vya juu zaidi vya utendaji wao na, kila ikiwepo nafasi, kuvijulisha kwa wengine, wakizingatia kuwa wanapofanya hivyo wanakuwa washiriki wa Mungu muumbaji, mkombozi, mwenye kutakatifuza, na wanamtukuza.

Hatimaye, walei wajazie maisha yao uhai wa upendo, na wauonyeshe kwa matendo kadiri ya uwezo wao.

Wote wazingatie kuwa, kwa ibada za pamoja na sala, kwa toba na kuvumilia kwa hiari magumu na matatizo ya maisha, njia ambazo zinawafananisha na Kristo mteswa (taz. 2Kor 4:10; Kol 1:24), wao waweza kuwafikia watu wote na kusaidia ili ulimwengu mzima upate wokovu.

Utume wa mtu mmoja mmoja katika mazingira ya pekee

17. Utume huo wa mtu mmoja mmoja ni wa lazima sana katika nchi zile ambapo uhuru wa Kanisa hugandamizwa sana. Katika hali hiyo ngumu sana, walei, badala ya mapadre, kwa yote yawezekanayo, wakichukua nafasi yao, wakihatarisha uhuru wao na pengine hata uhai wao, wanafundisha mafundisho ya kikristo kwa majirani wao, wawazoesha kupokea mara nyingi sakramenti, na kusitawisha ibada, hasa ibada ya kiekaristi[27]. Mtaguso Mkuu, pamoja na kumshukuru Mungu kwa moyo wote, ambaye, hata katika nyakati zetu, hakosi kuinua walei mashujaa kati ya dhuluma, basi anawakumbatia kwa upendo wa kibaba na kwa moyo wa shukrani.

Utume wa mtu mmoja upo hasa katika nchi zile ambapo wakatoliki ni wachache na wametawanyika. Hapo walei, wenye kutimiza utume binafsi tu, ama kwa sababu zilizoelezwa hapo juu, ama kwa sababu nyinginezo maalum zitokanazo na kazi zao, wakusanyike kwa mijadala vikundi vikundi, hata pasipo kusimikwa rasmi wala pasipo mpangilio wa pekee, ili kukutana kwao kuonekane daima, mbele ya wengine, kama alama ya jumuiya za kikanisa na ushuhuda wa upendo. Kwa njia hii, katika urafiki na kwa kuchangiana mang’amuzi, kwa kusaidiana kiroho, wanaimarika ili kuweza kushinda matatizo ya maisha na ya harakati vilivyo vya upweke mno, na ili kuzaa zaidi na zaidi matunda katika utume wao.

Umuhimu wa utume wa pamoja

18. Waamini wanaitwa kutimiza utume wa mtu mmoja mmoja katika hali mbalimbali za maisha; lakini wanatakiwa kukumbuka kuwa mwanadamu, kwa asili yake, ameumbwa ili aishi katika jamii, na kwamba ilimpendeza Mungu kukusanya waamini katika Kristo katika taifa moja la Mungu (taz. 1Pet 2:5-10) na katika mwili mmoja (taz. 1Kor 12:12). Ndiyo sababu utume wa pamoja huendana vema na madai ya ubinadamu na ya ukristo ya waamini na vilevile hutolea alama ya ushirika na umoja wa Kanisa katika Kristo, aliyesema: “Walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” (Mt 18:20).

Kwa hiyo waamini watimize utume wao katika roho ya umoja[28]. Wawe mitume katika jumuiya ya familia yao, vilevile katika parokia na jimbo, [jumuiya] ambazo kwa tabia yake tayari huonyesha roho ya kijumuiya ya utume, na pia katika taasisi huru ambamo watapendelea kujiunga.

Utume wa umoja ni wa umuhimu mkubwa pia kwa sababu katika jumuiya za kikanisa au katika mazingira mbalimbali, mara nyingi utume unadai utekelezwe kwa utendaji wa pamoja. Ndiyo maana aina mbalimbali za umoja zianzishwazo kwa ajili ya kazi maalum za kitume za pamoja zinasaidia wanaumoja wake na kuwaandaa kwa utume, huratibu vema na kuongoza kazi zao za kitume, ili zitoe matunda mengi zaidi kuliko kama kila mmoja angalifanya kazi peke yake.

Katika hali ya siku hizi, lakini, ni ya lazima kabisa kwamba katika mazingira wanamofanya kazi walei, ile namna ya utume wa umoja na wenye mpangilio iimarike; maana kwa kushikamanisha nguvu za wengi tu inawezekana kuyafikia kikamilifu malengo yote ya utume wa siku hizi, na kuhifadhi mema yake[29]. Katika uwanja huo hasa, ni ya maana kwamba utume uweze kuwafikia watu katika fikra zao za kawaida na hali yao ya kijamii; kinyume chake watakuwa wanashindwa kukabili mbano wa maoni ya umma (opinionis publicae) na ya taasisi [za kiserikali].

Aina nyingi za utume wa pamoja

19. Kuna tofauti nyingi kati ya vyama mbalimbali vya kitume [30]; vingine vinadhamiria shabaha ya kitume ya kawaida ya Kanisa; vingine hasa madhumuni ya kuinjilisha na kutakatifuza; vingine vinalenga shabaha ya kupenyeza roho ya kikristo katika mpango wa malimwengu; vingine vinamshuhudia kwa namna ya pekee Kristo kwa matendo ya huruma na ya mapendo.

Kati ya vyama hivyo vinaheshimiwa kwanza vile ambavyo vinahimiza na kukuza umoja wa ndani kati ya maisha ya kila siku ya wanachama wake na imani yao. Hivi vyama havina shabaha katika vyenyewe, bali vinatakiwa kusaidia ili utendeke ule utume wa Kanisa kwa ajili ya ulimwengu; nguvu zake za kitume zinategemea ulinganifu wake na malengo ya Kanisa, na ushuhuda wa kikristo, na roho ya kiinjili ya kila mwanachama na ya chama kwa pamoja.

Kutokana na mabadiliko ya taasisi za kijamii na maendeleo ya haraka ya jamii mamboleo, jukumu la utume wa Kanisa la kuwa wa watu wote, ladai kwamba asasi za kitume za wakatoliki zikamilishe zaidi na zaidi ushirikiano katika vyama vyenye tabia ya kimataifa. Vyama vya kimataifa vya kikatoliki vinafikia lengo lake kwa namna ya kufaa ikiwa makundi yanayoviunda na wanaumoja wake wameunganika navyo kwa dhati.

Pamoja na kuhifadhi uhusiano ulio wa lazima na mamlaka ya Kanisa[31], walei wanayo haki ya kuunda na kuongoza vyama mbalimbali[32], na kuvipa majina vile vilivyoanzishwa. Hata hivyo, lakini, yafaa kuepukana na mgawanyiko wa nguvu uliopo wakati vimeanzishwa vyama vipya na asasi pasipo sababu zenye msingi, au vinadumishwa zaidi kuliko inavyotakiwa vyama au mtindo vilivyo vya zamani; wala pengine hakutakuwa na mafaa kupeleka popote mbinu zinazotumiwa katika nchi moja, bila kufikiri kama kweli zinafaa pia katika nchi nyingine[33].

Aksio Katoliki

20. Tangu kipindi cha miongo ( decennia), katika nchi nyingi walei, hali wamejiwajibisha zaidi na zaidi kwa utume, wamekusanyika katika makundi ya utendaji na ya umoja ambayo, kwa kuhusiana kwa undani na Hierarkia, yalilenga na yanaendelea kulenga shabaha za kitume halisi. Kati ya asasi hizi, au za aina kama hii za tangu zamani, zastahili kukumbukwa zile ambazo, ingawa utendaji wake ulikuwa na utofauti, hata hivyo zilitoa matunda tele kwa ajili ya ufalme wa Kristo na, zikiisha kuhimizwa na kupendwa na Mababa Watakatifu, pia na Maaskofu wengi, zimepewa nao jina la Aksio Katoliki ( Actionis Catholicae), na mara nyingi zilitambulishwa kama chombo cha ushirikiano wa walei na utume wa kihierarkia [34].

Namna hizo za utume, ziitwe Aksio Katoliki au vinginevyo, ambazo leo zinatimiza utume wenye thamani kubwa, zinaundwa kwa kufuata sifa hizi, zote kwa pamoja:

a) Lengo la kwanza la vyama hivyo ni lengo la kitume la Kanisa, yaani uinjilishaji na utakatifuzaji wa watu, na pia malezi ya kikristo ya dhamiri yao, kusudi waweze kupenyeza roho ya kiinjili katika jumuiya mbalimbali na mazingira mbalimbali.

b) Walei, wakishirikiana na Hierarkia kadiri ya hadhi yao, wanachangia ustadi wao na wanashika dhima za kuongoza vyama hivyo, za kuitathmini hali na namna unavyotakiwa kutimiza utendaji wa kichungaji wa Kanisa, na za kubuni na kutekeleza mpango wa utendaji.

c) Walei wanatenda umoja mithili ya mwili uliofungamana ili kuimaanisha kwa namna ya kufaa jumuiya ya kikanisa, na utume upate kuwa na mafanikio zaidi.

d) Walei, ama kwa kujitolea kwa hiari ama kwa kualikwa kufanya kazi na kushirikiana moja kwa moja na utume wa kihierarkia, wanatenda kazi chini ya uongozi mkuu wa Hierarkia yenyewe, ambayo yaweza kuidhinisha ushirikiano huo pia kwa njia ya agizo (mandatum) rasmi.

Vyama ambavyo, kwa shauri la Hierarkia, vina sifa hizi zote, vitazamwe kama Aksio Katoliki, hata kama kulingana na mahali na watu mbalimbali vinaweza kuchukua majina au maumbo tofauti.

Mtaguso Mkuu unavisifu sana vyama hivyo, ambavyo hakika katika nchi nyingi vinaendana na mahitaji ya utume wa Kanisa: unawaalika mapadre na walei ambao wanafanya kazi katika vyama hivyo wazingatie sifa hizo zilizotajwa hapo juu ili kuzitekeleza zaidi na zaidi, vilevile washirikiane daima na aina zozote nyingine za utume, kwa moyo wa kidugu katika Kanisa.

Taadhima ya vyama vya kitume

21. Vyama vyote vya kitume vinatakiwa kupewa heshima ya haki; vile ambavyo Hierarkia ilivisifu au kuvihimiza au iliamua kuvianzisha kwa sababu ni vya lazima zaidi, kulingana na mahitaji ya nyakati na ya mahali, lazima vithaminiwe sana na mapadre, watawa na walei, na kuchochewa kulingana na tabia ya kila kimoja. Kati ya hivyo, leo vyaweza kuhesabiwa hasa vyama na vikundi vya kimataifa vya wakatoliki.

Walei wanaolihudumia Kanisa kwa namna za pekee

22. Katika Kanisa wanastahili heshima na sifa pekee walei, waseja kwa waliofunga ndoa, ambao, kwa maisha yote au kwa muda, wanajifunga wenyewe na ustadi wao wa kikazi, kwa huduma ya taasisi [za Kanisa] na ya utendaji wake. Ni sababu ya furaha kubwa kwa Kanisa kuwa idadi ya walei wanaotoa huduma yao katika vyama na katika matendo ya kitume inakua siku kwa siku, ndani ya mipaka ya taifa lao, na vilevile katika nya-nja za kimataifa, hasa katika jumuiya za kikatoliki katika misheni na katika makanisa machanga.

Wachungaji wa Kanisa wawakubali kwa dhati na kwa shukrani hao walei, waangalie kwamba hali yao ilingane sawasawa iwezekanavyo na matakwa ya haki, na ya usawa na ya mapendo, hasa kuhusu suala la posho ya walei hao na ya familia zao; pia waangalie wasikose mafunzo wanayohitaji, wala faraja ya kiroho, wala kutiwa moyo.

Sura ya Tano

UTARATIBU WA KUFUATA KWA UTUME

Utangulizi

23. Utume wa walei, unaotekelezwa na mtu mmoja mmoja au na waamini kwa pamoja, inabidi uingie kwa utaratibu unaotakiwa katika utume wa Kanisa zima. Muungano na wale ambao Roho Mtakatifu amewaweka waangalizi wa Kanisa la Mungu (taz. Mdo 20:28) ni jambo la lazima katika utume wa kikristo. Hauna upungufu wa umuhimu ule ushirikiano kati ya vyama mbalimbali vya kitume na utendaji wake, ambao uratibishwe na Hierarkia kwa namna ya kufaa.

Kwa kweli, ili kusitawisha roho ya umoja, kusudi katika utume wote wa Kanisa mapendo ya kidugu yang’ae, malengo ya pamoja yatekelezwe, na ushindani wenye kuharibu uepukwe, inatakiwa kuwepo na kuheshimiana kati ya aina zote za utume katika Kanisa, na uratibu wa kufaa, lakini pamoja na kuhifadhi tabia pekee ya kila moja[35].

Hayo ni ya kufaa hasa pale ambapo utendaji maalum katika Kanisa unadai ulingano na ushirikiano na utume wa wakleri wa aina zote mbili [wa jimbo na wa mashirika ya kitawa], wa watawa na wa walei.

Mahusiano na Hierarkia

24. Ni wajibu wa Hierarkia kuhamasisha utume wa walei, kutoa miongozo na misaada ya kiroho, kuratibisha utendaji wa utume wenyewe kwa ajili ya mema ya wote katika Kanisa, kuangalia ili mafundisho na taratibu zilindwe.

Utume wa walei unakubali mahusiano ya namna mbalimbali na Hierarkia kulingana na aina na kusudi la utume huo wenyewe.

Maana, katika Kanisa asasi za kitume ni nyingi ambazo zinaundwa na chaguo la hiari la walei na kuongozwa na uamuzi wao wa busara. Kwa njia ya asasi hizo, katika mazingira fulani utume wa Kanisa unatimizwa kwa mafanikio makubwa; hivyo Hierarkia mara nyingi yazisifu na kuzihimiza[36]. Lakini asasi yoyote isiitwe ya kikatoliki isipokuwa imepewa idhini ya mamlaka ya kikanisa.

Aina kadhaa za utume wa walei zatambuliwa wazi na Hierarkia kwa namna mbalimbali.

Mamlaka ya kikanisa, kwa kuzingatia madai ya mema ya wote katika Kanisa, kati ya vyama na shughuli zao za kitume zenye kulenga moja kwa moja mambo ya kiroho, yaweza kuzichagua nyingine au vingine kwa uteuzi wa pekee, na kuvihamasisha vingine ambavyo dhima mahsusi inajichukulia juu yake. Kwa hiyo Hierarkia, kwa kuratibu kwa njia mbalimbali utume huu, kulingana na mazingira, yauunganisha na huduma yake ya kitume namna fulani za huo utume. Lakini itafanya hivyo kwa kuheshimu tabia na upekee wa tume zote mbili [ya Hierarkia na ya walei], bila kuwanyima walei haki ya kutenda kwa uhuru. Tendo hilo la Hierarkia, katika hati mbalimbali za kikanisa, laitwa ‘agizo’ (mandatum).

Hatimaye, Hierarkia inawakabidhi walei majukumu fulani, ambayo yanalingana sana na wajibu wa wachungaji, kama vile katika kufundisha mafundisho ya kikristo, katika vitendo kadhaa vya kiliturujia, katika uangalizi wa roho. Kwa mujibu wa utume huo, walei katika kutimiza jukumu lao, wako chini ya uongozi wa wakuu wa Kanisa.

Kwa habari ya matendo na taasisi za mfumo wa kidunia, jukumu la Hierarkia ya kikanisa ni kufundisha na kufafanua kihalisi kanuni za kimaadili zinazotakiwa kufuatwa katika mambo ya kidunia. Vilevile ni mamlaka yake kuamua – baada ya kutathmini yote, pia kwa kusaidiwa na mabingwa – ulinganifu wa matendo na taasisi hizo na kanuni za msingi za maadili na kuainisha ni mambo gani yanayotakiwa ili kulinda na kusitawisha mema ya mfumo wa kimungu.

Misaada ya wakleri kwa ajili ya utume wa walei

25. Maaskofu, maparoko na mapadre wengine wa aina zote mbili [wa jimbo na wa mashirika ya kitawa], wakumbuke kuwa haki na wajibu wa kutimiza utume ni wa waamini wote wakleri kwa walei, na kwamba walei wanazo sehemu zilizo zao wenyewe katika kujenga Kanisa [37]. Kwa sababu hiyo, wafanye kazi kidugu pamoja na walei katika Kanisa na kwa ajili ya Kanisa, na wawe na uangalizi mahsusi kwa walei katika shughuli zao za kitume [38].

Mapadre wanaofaa wateuliwe kwa uangalifu na wafunzwe inavyotakiwa ili wapate kusaidia katika fani mbalimbali za utume wa walei[39]. Wenye kushiriki katika huduma hiyo, baada ya kupewa utume na Hierarkia, wanaiwakilisha katika utendaji wao wa kitume. Wasaidie ili iwe rahisi kwa walei kuhusiana na Hierarkia, wakiwa wanaambatana daima na roho na mafundisho ya Kanisa; wajitolee katika kukuza maisha ya kiroho na hisia za kitume katika vyama vya kikatoliki vinavyokabidhiwa kwao; wavisaidie kwa njia ya nasaha zao zenye hekima katika kazi zao za kitume, na wahimize utendaji wao. Waanzishe mawasiliano ya kudumu na walei na watafute kwa makini njia zile ziwezazo kuleta matunda mengi katika kazi ya kitume; wastawishe roho ya umoja katika chama chenyewe, na vilevile kati yake na vyama vingine.

Aidha watawa, wa kiume na wa kike, wastahi matendo ya kitume ya walei; kulingana na tabia na katiba za mashirika yao, wasaidie kwa moyo kukuza matendo ya walei[40]; wasimamie, wasaidie na kushirikiana na huduma za mapadre.

Vyombo mbalimbali kwa ajili ya ushirikiano

26. Katika majimbo, kadiri iwezekanavyo, ziwepo kamati ( consilia) zenye lengo la kusaidia kazi ya kitume ya Kanisa, katika uwanja wa uinjilishaji na pia ya utakatifuzaji; pia katika nyanja za matendo ya huruma, za kijamii na nyinginezo, ambamo wanashirikiana kwa manufaa wakleri na watawa na walei. Kamati hizo zitasaidia kuratibisha kwa hali ya umoja vyama mbalimbali na shughuli za walei, bila kudhuru tabia pekee na uhuru wa kujiongoza wa kila kimoja [41].

Kamati za aina hii ziwepo pia, ikiwezekana, katika maparokia au muungano wa maparokia, kati ya majimbo, na vilevile ziwepo zenye tabia ya kitaifa au ya kimataifa[42].

Iundwe kwa Kiti Kitakatifu tume (secretariatus) mahsusi kwa ajili ya huduma na himizo ya utume wa walei, iwe kituo ambacho kwa mbinu za kufaa kinaweza kusambaza habari za utendaji wa kitume wa walei wa aina mbalimbali, kuandaa uchunguzi kuhusu masuala yanayojitokeza katika uwanja huo, na kusaidia kwa maoni yake Hierarkia na walei katika kazi zao za kitume. Katika tume hiyo zipewe nafasi matapo (movements) na asasi za utume wa walei zilizopo duniani pote, na washirikiane humo, pamoja na walei, pia wakleri na watawa.

Ushirikiano na wakristo waliojitenga na wasio wakristo

27. Hazina ya kiinjili, iliyo ya wote, na wajibu, nao wa wote, wa kutoa ushuhuda wa kikristo utokao humo, zinafanya utamaniwe, na mara nyingi uwe wa lazima, ushirikiano kati ya wakatoliki na wakristo wengine, wa kutekelezwa na kila mmoja na pia na jumuiya za kikanisa, katika miradi, katika vyama, kwa kiwango cha kitaifa na cha kimataifa[43].

Tunu za kikristo za wote zinahitaji mara nyingi ushirikiano wa namna hii wa wakristo, wenye kufuatilia malengo ya kitume, na watu wasiokiri ukristo, lakini wanatambua tunu hizo.

Kwa njia ya ushirikiano huu wenye nguvu na busara[44], ulio wa umuhimu mkubwa katika shughuli za kidunia, walei wanatoa ushuhuda kwa Kristo, Mwokozi wa ulimwengu, na kwa umoja wa familia ya wanadamu.

Sura ya Sita

MAFUNZO KWA AJILI YA UTUME

Haja ya mafunzo kwa ajili ya utume

28. Utume unaweza kuwa na mafanikio makuu kama tu ukiandaliwa na mafunzo mbalimbali na matimilifu. Hayo mafunzo hayatakiwi tu kutokana na maendeleo ya siku kwa siku ya kiroho na ya kimafundisho ya walei, lakini pia na mambo mbalimbali, kama vitu, watu na majukumu ambavyo utendaji wake lazima ujilinganishe navyo. Malezi hayo ya utume yatakiwa kuwekwa juu ya misingi ile ambayo Mtaguso Mkuu umetangaza na kueleza katika hati nyinginezo[45]. Licha ya malezi yaliyo ya wakristo wote, kutokana na tofauti za watu na za mazingira, aina za utume zinazodai mafunzo maalum na mahsusi si chache.

Kanuni za msingi kwa ajili ya kuwafunza walei utume

29. Kwa vile walei wanashiriki kwa namna yao pekee katika utume wa Kanisa, mafunzo yao ya kitume yana sura maalum kutokana na tabia ya kidunia iliyo halisi ya walei, na ya roho yake ya ibada, ambayo nayo ni ya pekee.

Mafunzo ya kitume huhitaji malezi ya kiutu matimilifu, yajuzuyo tabia na hali ya kila mmoja. Maana, kila mlei, hali akifahamu vizuri ulimwengu mamboleo, anatakiwa kuwa kiungo cha jamii yake na mwenye kustaarabu kulingana na kiwango chake.

Kwanza, mlei anatakiwa kujifunza utume wa Kristo na wa Kanisa, akiishi na imani katika fumbo la kimungu la uumbaji na la wokovu, hali akisukumwa na Roho Mtakatifu, mwenye kuhuisha watu wa Mungu, na mwenye kusukuma watu wote wampende Mungu Baba na, katika Yeye, ulimwengu na wanadamu. Mafunzo hayo lazima yatazamwe kama msingi na sharti la utume wa aina yoyote, unaotazamia kuleta matunda.

Pamoja na malezi ya kiroho, yanatakiwa mafunzo ya msingi katika mafundisho, yaani ya kiteolojia, ya kimaadili, ya kifalsafa, kuendana na tofauti za umri, hali na uwezo wa kila mmoja. Wala isiachwe kutilia maana elimu ya jumla, pamoja na mafunzo ya ufundi na ya kiteknolojia.

Ili kusitawisha mahusiano mema na wanadamu, tunu zilizo kweli za kiutu lazima zihamasishwe, kuanzia uadilifu katika kuishi pamoja, na ushirikiano wa kidugu, na ufanisi katika kuanzisha mawasiliano.

Lakini, kwa vile mafunzo ya utume hayatoshi yakiwa ya kinadharia tu, kwa hatua na kwa busara, walei wajifunze tangu mafunzo yao ya awali, kutazama kila jambo, na kukata shauri na kutenda katika mwanga wa imani, kujijenga na kujikamilisha wenyewe pamoja na wengine kwa njia ya matendo, na hivyo kupata nafasi katika huduma hai ya Kanisa[46]. Mafunzo hayo, ambayo yatakiwa kukamilishwa daima kutokana na ukomavu wa siku kwa siku wa utu wa watu na kwa mageuzi ya masuala mbalimbali, yadai ufahamu wa ndani zaidi na marekebisho yasiyokoma ya utendaji. Katika kutekeleza mahitaji yote ya mafunzo uzingatiwe daima umoja na ukamilifu wa hadhi ya mwanadamu, kusudi mlingano na utimamu wake utunzwe na kuimarishwa.

Kwa namna hii mlei anaingia kwa vitendo mpaka ndani katika mambo ya mpango ya malimwengu, na anashika sehemu yake kwa mafanikio katika utendaji, na pamoja na hayo, kama kiungo kilicho hai na shahidi wa Kanisa, analiwakilisha likifanya kazi ndani ya mpango wa ulimwengu[47].

Nani anafunza kwa ajili ya utume?

30. Mafunzo kwa ajili ya utume yanatakiwa kuanza tangu malezi ya awali ya watoto. Kwa namna ya pekee wafunzwe utume wabaleghe na vijana, na wapenyezwe na roho hii. Malezi hayo yakamilishwe katika maisha yote kulingana na wajibu mpya ambao mara kwa mara itawabidi kuushika. Ni dhahiri kwamba wale wenye kushika jukumu la kulea kikristo wanao pia wajibu wa kufunza utume.

Ni juu ya wazazi katika familia kufanya juhudi ili wazao wao tangu utoto watambue upendo wa Mungu kwa ajili ya wanadamu wote, na kuwafundisha hatua kwa hatua, hasa kwa njia ya mifano, kujali mahitaji ya kimwili na ya kiroho ya majirani. Familia nzima na maisha yake ya pamoja iwe kwa hiyo kama uanagenzi ( tirocinium) wa utume.

Aidha, watoto lazima walelewe kwa mtindo ambao unawaweka moyo wazi kwa ajili ya jumuiya ya kikanisa na ya kidunia, yaani kwa kupanua mipaka ya kifamilia. Wapokelewe katika jumuiya ya kiparokia ya mahali kwa namna ambayo watapata ndani yake hisia ya kuwa viungo hai na tendaji vya taifa la Mungu. Mapadre, kwa upande wao, katika katekesi na katika huduma ya neno, katika kuongoza roho za watu, na vilevile katika huduma nyinginezo za kichungaji wazingatie malezi kwa ajili ya utume.

Shule, vyuo vyenye bweni na taasisi nyinginezo za kikatoliki za mafunzo zatakiwa kuhamasisha katika vijana hisia za kikatoliki na utendaji wa kitume. Ikiwa mafunzo hayo hayapatikani, ama kwa sababu vijana hawahudhurii shule hizo, ama kwa sababu nyingine, hapo wazazi wajitahidi hata zaidi kushika wajibu huo, pamoja na wachungaji wa roho na vyama vya kitume. Na walimu na walezi, ambao kwa wito wao na kwa wadhifa wao watekeleza utume bora wa walei, wapatiwe elimu ya kufaa na umahiri wa ufundishaji (arte paedagogica), ambao kwao watafaulu kwa mafanikio zaidi kutoa mafunzo hayo.

Hali kadhalika, vikundi na vyama vya walei, vyenye lengo la kitume au malengo mengine yasiyo ya ulimwengu huu, kulingana na shabaha yao na uwezo, vinatakiwa kuchochea kwa makini na kwa bidii malezi kwa ajili ya utume[48]. Vyenyewe mara nyingi ni njia ya kawaida ya mafunzo ya utume. Maana, katika vikundi hivyo yanapatikana malezi ya kimafundisho (doctrinalis), ya kiroho na ya kimatendo. Wanavyama hao, pamoja na wenzao na marafiki, vikundi vikundi, watatathmini mbinu na mapato ya kazi zao za kitume, na kupima kwa Injili mwenendo wao wa kila siku.

Malezi hayo yatakiwa kuratibishwa kwa kuzingatia utume wote wa walei, ambao utatekelezwa sio tu ndani ya vyama au vikundi vyenyewe, bali katika mazingira yoyote na kwa maisha yote, hasa ya kikazi na ya kijamii. Tena, kila mmoja ni vema ajiandae kwa makini kwa utume, inavyotakiwa hasa kwa watu wazima. Maana, kwa kukua, roho hufunguka zaidi, na kila mmoja hutambua kwa usahihi zaidi vipaji ambavyo Mungu aliujalia moyo wake, na kuzitendea kazi kwa mafanikio zaidi karama zile alizojaliwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ndugu zake.

Kulinganisha mafunzo na aina mbalimbali za utume

31. Aina tofauti za utume zahitaji mafunzo maalum yanayolingana nazo.

a) Kuhusu utume kwa uinjilishaji na utakatifuzaji wa watu, walei watakiwa kuelimishwa hasa kuanzisha mawasiliano na wengine, waamini na wasio waamini, ili kuwatangazia wote ujumbe wa Kristo[49].

Na kwa vile nyakati hizi uyakinifu (materialismus) wa aina mbalimbali unaenea upesi popote, hata kati ya wakatoliki, walei wajifunze kwa uangalifu sana mafundisho ya kikatoliki, hasa mada ambazo zinapingwa [nao]. Zaidi ya hayo, lakini, dhidi ya aina yoyote ya uyakinifu watoe ushuhuda wa maisha ya kiinjili.

b) Kuhusu uratibu wa kikristo wa mpango wa malimwengu, walei wafunzwe juu ya maana na thamani halisi ya malimwengu, kwa yenyewe na kwa malengo ya utu wa watu; wazoee kutumia kwa unyofu vitu na kuratibisha asasi, wakiwa wanalenga daima manufaa ya wote kadiri ya kanuni za msingi za mafundisho ya Kanisa kuhusu maadili na jamii. Wajifunze hasa kanuni za msingi za mafundisho kuhusu jamii na maamuzi (conclusiones) yake, ili waweze, kwa kadiri ya sehemu zao, kushiriki katika maendeleo ya mafundisho, na kuyahusisha kwa manufaa na suala moja moja[50].

c) Kwa kuwa matendo ya mapendo na huruma yanakuwa ushuhuda mwangavu wa maisha ya kikristo, malezi kwa utume yatakiwa kufunza pia utekelezaji wa hayo, kusudi waamini wajifunze tangu utoto kusikitikia mateso ya ndugu na kuwasaidia kwa ukarimu wakiwepo kwenye shida[51].

Misaada

32. Walei wajifungao kwa utume wanayo kwa ajili yao misaada mingi, yaani: vikao, semina, mifungo, mazoezi ya kiroho, mikutano ya mara kwa mara, mihadhara, vitabu, magazeti, ili kufaulu kujipatia ujuzi wa ndani zaidi wa Maandiko Matakatifu na wa mafundisho ya kikatoliki, ili kulisha maisha yao ya kiroho, ili kufahamu hali mbalimbali za ulimwengu, na kubuni na kutimiza mbinu zinazofaa [52].

Misaada hiyo ya mafunzo inazingatia aina tofauti za utume katika mazingira unamotekelezwa.

Kwa lengo hilo vituo au taasisi za juu zimefunguliwa; nazo zimetoa tayari matokeo bora.

Mtaguso Mkuu huu unazifurahia asasi za aina hii zilizositawi mahali mahali, na unapendekeza kwamba zianzishwe pia katika sehemu nyinginezo, panapohitajika.

Aidha, visimikwe vituo vya hifadhi ya hati (Centra documentationis) na vya uchunguzi sio tu katika uwanja wa teolojia, lakini pia wa anthropolojia, saikolojia, elimujamii, methodolojia kwa manufaa ya nyanja zote za utume. Madhumuni ya vituo hivyo ni kuleta nafasi za kukuza vipaji vya maarifa vya walei, wanaume kwa wanawake, vijana kwa watu wazima.

MAWAIDHA

33. Mtaguso Mkuu unawasihi kwa ari katika Bwana walei wote, ili waitikie kwa hiari, na kwa moyo radhi na mkunjufu, sauti ya Kristo, ambaye katika saa hizi anawaalika kwa himizo kuu, na waitikie pia msukumo wa Roho Mtakatifu. Kwa namna ya pekee vijana wasikie mwaliko huo kama unaowaelekea wenyewe, na waupokee kwa hamu na kwa moyo mpana. Maana, ni Bwana mwenyewe ambaye tena, kwa njia ya Mtaguso huu, anawaalika walei wote waunganike zaidi na zaidi kwa undani naye, na wakawe ndani yao na nia ileile iliyokuwamo pia ndani ya Kristo (taz. Flp 2:5), na washiriki utume wake wa wokovu. Ni yeye ambaye tena anawatuma katika kila mji na kila mahali anapokusudia kuja mwenyewe (taz. Lk 10:1). [Yeye anawatuma] ili washiriki katika utume wa Kanisa, ambao ni mmoja hata kama una njia na mbinu mbalimbali, na unatakiwa kujirekebisha daima kulingana na mahitaji mapya ya nyakati, wakitenda kazi ya Bwana sikuzote kwa moyo, kwa kuwa wajua ya kwamba taabu yao siyo bure katika Bwana (taz. 1Kor 15:58).

 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 18 Novemba 1965

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)


   

[1] Taz. Ioannes XXIII, Const. Apost. Humanae salutis, 25 des. 1961: AAS 45 (1962) uk. 7-10.
[2] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, nn. 33nk.: AAS 57 (1965) uk. 36nk; taz. pia Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, nn. 26-40: AAS 56 (1964) uk. 107-111; taz. Decr. de instrumentis communicationis socialis, Inter Mirifica: AAS 56 (1964) uk.145-153; taz. Decr. de Oecumenismo, Unitatis redintegratio: AAS 57 (1965) uk. 90-107; taz. Decr. de pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, nn. 16, 17, 18: AAS 58 (1966) uk. 680- 682; taz. Declaratio de educatione christiana, Gravissimum educationis, nn. 3, 5, 7: AAS 58 (1966) uk. 731-734.
[3] Taz. Pius XII, Alloc. Ad Cardinales, 18 feb. 1946: AAS 38 (1946) uk. 101-102; Idem, Sermo ad Iuvenes Operarios Catholicos, 25 ago. 1957: AAS 49 (1957) uk. 843.
[4] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Rerum Ecclesiae: AAS 18 (1926) uk. 65.
[5] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 31: AAS 57 (1965) uk. 37.
[6] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 33: AAS 57 (1965) uk. 39; taz. pia n. 10, uk. 14.
[7] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 12: AAS 57 (1965) uk. 16.
[8] Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, sura ya I, n. 11: AAS 56 (1964) uk. 102-103.
[9] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 32: AAS 57 (1965) uk. 38; taz. pia nn. 40-41, uk. 45-47.
[10] Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 62: AAS 57 (1965) uk. 63; taz. pia n. 65, uk. 64-65.
[11] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Ubi arcano, 23 des. 1922: AAS 14 (1922) uk. 659; Pius XII, Litt. Encycl. Summi Puntificatus 20 okt. 1939: AAS 31 (1939) uk. 442-443.
[12] Taz. Leo XIII, Litt. Encycl. Rerum novarum: AAS 23 (1890-91) uk. 647; Pius XI, Litt. Encycl. Quadragesimo anno: AAS 23 (1931) uk. 190; Pius XII, Nuntius radiophonicus, 1 juni 1941: AAS 33 (1941) uk. 207.
[13] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra: AAS 53 (1961) uk. 402.
[14] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra: AAS 53 (1961) uk. 440-441.
[15] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra: AAS 53 (1961) uk. 442-443.
[16] Taz. Pius XII, Alloc. ad «Pax Romana M.I.I.C.», 25 apr. 1957: AAS 49 (1957) uk. 298-299; et praesertim Ioannes XXIII, Alloc. ad Conventum Consilii «Food and Agricolture Organization» ( F.A.O.), 10 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 856, 866.
[17] Taz. Pius X, Litt. Apost. Creationis duarum novarum paroeciarum, 1 juni 1905: AAS 3 (1905) uk. 65-67; Pius XII, Alloc. ad fideles paroeciae S. Saba, 11 jan. 1953: Dicorsi e Radiomessaggi di S. S. Pio XII, XIV, 1952-1953, uk. 449-454; Ioannes XXIII, Alloc. Clero et christifidelibus e diocesi suburbicaria Albanensi, ad Arcem Gandulfi habita, 26 ago. 1962: AAS 54 (1962) uk. 656-660.
[18] Taz. Leo XIII, Alloc., 28 jen. 1894: Acta 14 (1894) uk. 424-25.
[19] Taz. Pius XII, Alloc. ad Parochos, etc., 6 feb. 1951: Discorsi e Radiomessaggi di S.S. Pio XII, XII (1950-1951) uk. 437-443; 8 machi 1952: ibid., XIV (1952-1953) uk. 5-10; 27 machi 1953: ibid., XV (1953-1954) uk. 27-35
[20] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Casti connubii: AAS 22 (1930) uk. 554; Pius XII, Nuntius Radiophonicus, 1 iuni 1941: AAS 33 (1941) uk. 203; Idem, Delegatis ad Conventum Unionis Internationalis sodalitatum ad iura familiae tuenda, 20 sep. 1949: AAS 41 (1949) uk. 552; Idem, Ad patresfamilias e Gallia Romam peregrinantes, 18 sep. 1951: AAS 43 (1951) uk. 731; Idem, Nuntius Radiophonicus in Natali Domini 1952. AAS 45 (1953) uk. 41; Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 429, 439.
[21] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 514.
[22] Taz. Pius XII, Delegatis ad Conventum Unionis Internationalis sodalitatum ad iura familiae tuenda, 20 sep. 1949: AAS 41 (1949) uk. 552.
[23] Taz. S. Pius X, Alloc. ad Catholicam Associationem Iuventutis Gallicae de pietate, scientia et actione, 25 sep. 1904: AAS 37 (1904-1905) uk. 296-300.
[24] Taz. Pius XII, Epist. Dans quelques semaines, ad Archiepiscopum Marianopolitanum: de conventibus a iuvenibus operariis christianis Canadiensibus indictis, 24 mei 1947: AAS 39 (1947) uk. 257; Nuntius Radiophonicus ad J. O. C. Bruxell., 3 sep. 1950: AAS 42 (1950) uk. 640-641.
[25] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Quadragesimo anno, 15 mei 1931: AAS 23 (1931) uk. 225-226.
[26] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 448-450.
[27] Taz. Pius XII, Alloc. ad I Conventum ex omnibus Gentibus Laicorum apostolatui provehendo, 15 okt. 1951: AAS 43 (1951) uk. 788.
[28] Taz. ibid.: AAS 43 (1951) uk. 787-788.
[29] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Le pélerinage de Lourdes, 2 jul. 1957: AAS 49 (1957) uk. 615.
[30] Taz. Pius XII, Alloc. ad Consilium Foederationis internationalis virorum catholicorum, 8 des. 1956: AAS 49 (1957) uk. 26-27.
[31] Taz. infra sura ya V, n. 24
[32] Taz. S. C. Concilii, Resolutio Corrienten., 13 nov. 1920: AAS 13 (1921) uk. 139.
[33] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 10 des. 1959: AAS 51 (1959) uk. 856.
[34] Taz. Pius XI, Epist. Quae nobis, ad Card. Bertram, 13 nov. 1928: AAS 20 (1928) uk. 385. Taz. pia Pius XII, Alloc. ad A. C. Italicam, 4 sep. 1940: AAS 32 (1940) uk. 362.
[35] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Quamvis Nostra, 30 apr. 1936: AAS 28 (1936) uk. 160-161.
[36] Taz. S.C.Concilii, Resolutio Corrienten., 13 nov. 1920: AAS 13 (1921) uk. 137-140.
[37] Taz. Pius XII, Alloc. ad II Conventum ex omnibus Gentibus Laicorum apostolatui provehendo, 5 okt. 1957: AAS 49 (1957) uk. 927.
[38] Taz. Conc: Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 37: AAS 57 (1965) uk. 42-43.
[39] Taz. Pius XII, Adhort. Apost. Menti Nostrae, 23 sep. 1950: AAS 42 (1950), uk. 660.
[40] Taz. Conc. Vat. II, Decr. de accomodata renovatione vitae religiosae, Perfecte caritatis, n. 8: AAS 58 (1966) uk. 706.
[41] Taz. Benedictus XIV, De Synodo Diocesana, l. III, c. IX, n. VII-VIII: Opera omnia in tomos XVII distributa, tom. XI (Prati, 1844), uk. 76-77.
[42] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Quamvis Nostra, 30 apr. 1936: AAS 28 (1936) uk. 160-161.
[43] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 456-457. Taz. Conc. Vat. II, Decr. de Oecumenismo, Unitatis redintegratio, n. 12: AAS 57 (1965) uk. 99-100.
[44] Taz. Conc. Vat. II, Decr. de Oecumenismo, Unitatis redintegratio, n. 12: AAS 57 (1965) uk. 100. Taz. pia Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 15: AAS 57 (1965) uk. 19-20.
[45] Taz. Conc. Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, sura za II, IV, V: AAS 57 (1965) uk. 12-21, 37-49; taz. pia Decr. de Oecumenismo, Unitatis Redintegratio, n. 4, 6, 7, 12: AAS 57 (1965) uk. 94, 96, 97, 99, 100; taz. pia juu, n. 4.
[46] Taz. Pius XII, Alloc. ad IV Conferentiam internationalem “boy-scouts” 6 juni 1952: AAS 44 (1952) uk. 579-580; Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 456.
[47] Taz. Conc: Vat. II, Const. Dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 33: AAS 57 (1965) uk. 39.
[48] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 455.
[49] Taz. Pius XII, Epist. Encycl. Sertum laetitiae, 1 nov. 1939: AAS 31 (1939) uk. 635-644; taz. Idem, ad “Laureati” Act. Cath. It., 24 mei 1953.
[50] Taz. Pius XII, Alloc. ad Congressum universalem Foederationis mundialis Iuventutis Femineae Catholicae, 18 apr. 1952: AAS 44 (1952) uk. 414-419. Taz. Idem, Alloc. ad Associationem Christianam Operariorum Italiae ( A.C.L.I.), 1 mei 1955: AAS 47 (1955) uk. 403-404.
[51] Taz. Pius XII, ad Delegatos Conventus Sodalitatum Caritatis, 27 apr. 1952: AAS 44 (1952) uk. 470-471.
[52] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra, 15 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 454.