[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH] Dikrii juu ya Makanisa katoliki ya Mashariki Paulo Askofu Mtumishi wa Watumishi wa Mungu pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu ataka haya yakumbukwe daima UTANGULIZI 1. Kanisa Katoliki huheshimu sana taasisi (institutions), madhehebu ya kiliturujia*, mapokeo ya kikanisa na nidhamu ya maisha ya kikristo ya Makanisa ya Mashariki (Orientalium Ecclesiarum). Maana ndani yake, maadamu ni maarufu kwa ukale wake mstahiki, hung’ara mapokeo yatokanayo na Mitume kwa njia ya Mababa[1]; na mapokeo hayo ni sehemu ya hazina iliyofunuliwa na Mungu na isiyogawanyika ya Kanisa lote zima. Kwa hiyo Mtaguso huo Mkuu na Mtakatifu, ukijibidisha kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki yaliyo mashahidi hai ya mapokeo hayo, unatamani haya yachanue na kuutekeleza kwa nguvu mpya utume yaliokabidhiwa; na hivyo Mtaguso, pamoja na yale yalihusuyo Kanisa zima, umeamua kuweka vichwa kadhaa na kuviacha vingine kwa uangalizi wa Sinodi za Mashariki na wa Baba Mtakatifu. KUHUSU MAKANISA MAALUM AMA RITI** Umbalimbali wa riti haudhuru umoja 2. Kanisa takatifu na katoliki, ambalo ni Mwili wa fumbo wa Kristo, umetengenezwa kwa waamini wanaounganishwa kiundani katika Roho Mtakatifu na imani ileile, na sakramenti zilezile na pia na uongozi uleule; nao waamini, wakifungamanishwa na hierarkia, wanaunda Makanisa maalum ama riti. Na kati ya Makanisa haya kuna ushirika wa ajabu, hivi kwamba umbalimbali katika Kanisa haudhuru umoja wake, bali zaidi unaudhihirisha; maana ni azimio la Kanisa Katoliki kuwa mapokeo ya kila Kanisa maalum ama riti yadumu na kutunzwa yalivyo; na vilevile Kanisa linataka kulinganisha mfumo wa maisha yake na mahitaji mbalimbali ya nyakati na mahali[2]. Riti mbalimbali zina heshima ileile 3. Makanisa haya maalum, ya Mashariki kama vile ya Magharibi, hutofautiana kwa sehemu fulani kwa sababu ya yale yaitwayo riti; yaani liturujia, nidhamu ya kikanisa na urithi wake wa kiroho; lakini hata hivyo yamekabidhiwa vilevile kwa uongozi wa kichungaji wa Baba Mtakatifu wa Roma ambaye kwa mapenzi ya Mungu yu halifa wa Mtakatifu Petro katika mamlaka kuu juu ya Kanisa lote ulimwenguni. Hivyo Makanisa haya yana heshima ileile, hivi kwamba hakuna kati yao linaloyashinda mengine kutokana na riti; tena yana haki zilezile na yanapaswa masharti yaleyale hata mintarafu utangazaji wa Injili duniani pote (taz. Mk 16:15), chini ya usimamizi wa Baba Mtakatifu wa Roma. Riti mbalimbali zifahamike kwa makini 4. Hivyo, popote duniani Makanisa maalum yote yalindwe na kukuzwa; na kwa lengo hilo maparokia yawekwe, na viongozi (hierarchia) wake, pale ambapo hudaiwa na manufaa ya kiroho ya waamini. Aidha, hierarkia za Makanisa maalum mbalimbali zilizo na mamlaka ya kisheria juu ya eneo lilelile moja wajibidishe kuhamasisha umoja wa utendaji kwa kupeana mawaidha mbalimbali wao kwa wao katika mikutano ya kufanyika kila baada ya muda fulani; tena wajibidishe, kwa kuunganisha nguvu zao, ili kusaidia kazi za pamoja kwa minajili ya kuendeleza haraka zaidi manufaa ya dini na kulinda kwa mafanikio zaidi nidhamu ya makleri[3]. Makleri wote na wale wanaopanda madaraka matakatifu waelimishwe vizuri juu ya riti na hasa mintarafu kanuni za kiutendaji zihusuzo mahusiano baina ya riti mbalimbali; na zaidi hata walei waelimishwe katika mafundisho ya kikatekesi juu ya riti na kanuni zake. Na hatimaye wakatoliki wote na kila mmoja wao pamoja na wabatizwa wa Kanisa lolote lile au jumuiya isiyo ya kikatoliki wanaoujia utimilifu wa ushirika wa kikatoliki, watunze riti yao popote walipo na kuyaheshimu na kuyashika kadiri ya nguvu zao[4]; ila katika nafasi za pekee ihifadhiwe haki ya watu, jumuiya au kanda kukata rufaa kwa Baba Mtakatifu ambaye, kama mwamuzi mkuu wa mahusiano kati ya Makanisa atayashughulikia mwenyewe mahitaji hayo kadiri ya roho ya kiekumeni au atayakabidhi kwa wengine wenye mamlaka kwa njia ya dikrii, hati au amri. ULAZIMA WA KUTUNZA HAZINA YA KIROHO YA MAKANISA YA MASHARIKI Tunu za Makanisa ya Mashariki 5. Historia, mapokeo na taasisi nyingi sana za kikanisa hudhihirisha kinagaubaga kiasi Makanisa ya Mashariki yalivyo na tunu katika Kanisa zima[5]. Kwa sababu hii Mtaguso huo Mkuu unatoa heshima ipasayo na sifa iliyo ya haki kwa urithi huu wa kikanisa na wa kiroho; lakini pia unauhesabu kwa uthabiti kama hazina ya Kanisa zima. Hivyo unatangaza rasmi kuwa Makanisa ya Mashariki kama vile yale ya Magharibi yana haki na wajibu wa kujiongoza kadiri ya nidhamu zake maalumu, kwa maana yanadhaminiwa kwa ukale wake mstahivu, tena yanalingana zaidi na desturi za waamini wake na kufaa zaidi ili kuyashughulikia mema ya roho zao. Badiliko lolote lisiingizwe bila idhini 6. Waamini wote wa Mashariki wajue na wawe na hakika kwamba waweza sikuzote na wapaswa kutunza madhehebu yao ya kiliturujia yaliyo halali na pia nidhamu yao; wala mabadiliko hayawezi kuingizwa, isipokuwa kwa sababu ya maendeleo yake yenyewe. Hivyo, mambo hayo yote lazima yashikwe kwa uaminifu kamili na waamini wa Mashariki wenyewe, ambao hupaswa kupata ujuzi uzidio kuwa na kina na pia matumizi yaliyo kamili zaidi; na ikiwa waamini wameyaacha isivyopasa kwa sababu zitokanazo na nyakati ama watu, basi wajibidishe kuyarudia mapokeo ya mababa. Wale ambao, kutokana na madaraka waliyopewa au huduma ya kitume, wanahusiana mara kwa mara na Makanisa ya Mashariki ama na waamini wake, kadiri ya umuhimu wa wadhifa wanaoshika waelimishwe kwa makini katika ujuzi na utekelezaji wa madhehebu, nidhamu, mafundisho, historia na tabia ya waamini wa Mashariki[6]. Mashirika ya kitawa na vyama vyenye madhehebu ya kilatini vinavyofanya kazi katika nchi za Mashariki ama kati ya waamini wa Mashariki vinahimizwa kwa bidii viweke nyumba au pia provinsi zenye madhehebu ya Mashariki kadiri iwezekanavyo kwa minajili ya kuzidisha manufaa ya utume[7]. MAPATRIARKA WA MASHARIKI Asasi ya Upatriarka 7. Tangu nyakati za kale katika Kanisa iliwekwa asasi ya Upatriarka ambayo ilikwisha tambuliwa na Mitaguso Mikuu ya kwanza[8]. Kwa jina la Patriarka wa Mashariki anamaanishwa Askofu mwenye mamlaka ya kisheria juu ya Maaskofu wote, wakiwemo miongoni mwao Mametropolita, Makleri na waamini wa eneo au riti yake, kadiri ya kanuni za sheria na ikihifadhiwa mamlaka kuu ya Baba Mtakatifu wa Roma[9]. Popote pale anaposimikwa mwenyedaraja wa riti fulani nje ya mipaka ya eneo lililo chini ya Patriarka, kadiri ya sheria huyo anaendelea kuunganika na wenyedaraja wa upatriarka wa riti ileile. 8. Mapatriarka wa Makanisa ya Mashariki, ijapo wengine wamesimikwa baada ya wenzao, wote wako sawa katika cheo cha upatriarka, ila uhifadhiwe kati yao utangulizi wa heshima uliowekwa kihalali[10]. Heshima ya pekee kwa Mapatriarka wa Mashariki 9. Kwa mujibu wa mapokeo ya kale ya Kanisa, Mapatriarka wa Makanisa ya Mashariki hutazamwa kwa heshima ya pekee, maadamu kila mmoja anasimamia upatriarkati wake kama baba na kiongozi. Hivyo Mtaguso huo Mkuu unaamua kwamba haki na mapendeleo yao yarudishwe tena, kadiri ya mapokeo ya kale ya kila Kanisa na ya dikrii za Mitaguso Mikuu[11]. Haki na mapendeleo hayo ni yale yaliyokuwepo wakati wa [kuwepo] umoja baina ya [Makanisa ya] Mashariki na Magharibi, ingawa hayana budi kulinganishwa na hali ya siku hizi. Mapatriarka pamoja na sinodi zao wana uwezo mkuu juu ya shughuli zote zihusuzo upatriarka, ikiwemo haki pia ya kuunda maeparkia [yaani majimbo] (eparchias) mapya na kuteua maaskofu wa riti yao ndani ya mipaka ya eneo lililo la patriarkati; isipokuwa tu ihifadhiwe haki isiyofutika ya Baba Mtakatifu wa Roma kuingia katika suala lolote maalum. Uundaji wa patriarkati mpya 10. Kwa mujibu wa sheria, yaliyosemwa juu ya Mapatriarka yana nguvu pia kwa Maaskofu Wakuu wanaolisimamia Kanisa maalum zima ama riti[12]. 11. Maadamu katika Makanisa ya Mashariki asasi ya upatriarka ni mtindo wa uongozi wa kimapokeo, Mtaguso huo Mkuu na Mtakatifu unapendelea kwamba, palipo na lazima, patriarkati mpya zianzishwe; na uundaji wake ni juu ya Mtaguso Mkuu au Baba Mtakatifu[13]. UTARATIBU WA SAKRAMENTI Kurudisha tena utaratibu wa kale wa Sakramenti 12. Mtaguso Mkuu unathibitisha na kusifu na, ikihitajika, unapendekeza urudishwe tena utaratibu wa kale wa Sakramenti uliokuwepo katika Makanisa ya Mashariki, kama vile pia mwongozo uhusuo adhimisho na utoaji wake. Utoaji wa Kipaimara 13. Utaratibu kuhusu mhudumu wa Krisma [au Kipaimara] (S. Chrismatis) uliokuwepo tangu kale katika Makanisa ya Mashariki urudishwe tena kikamilifu. Kwa hiyo mapadre wanao uwezo wa kutoa sakramenti hii kwa [mafuta ya] Krisma yaliyobarikiwa na Patriarka ama na Askofu[14]. 14. Mapadre wote wa Mashariki wana uwezo wa kutoa kihalali sakramenti hii pamoja na Ubatizo au peke yake kwa waamini wote wa riti yoyote ile, hata ya kilatini; na kusudi iwe halali wafuate maagizo ya sheria ya kawaida na ya pekee[15]. Na hata mapadre wa riti ya kilatini, kadiri ya idhini waliyo nayo ya kutoa sakramenti hii, waweza kuitoa pia kwa waamini wa Makanisa ya Mashariki bila kuathiri riti ile; na kusudi iwe halali wafuate maagizo ya sheria ya kawaida na ya pekee[16]. Amri ya kusali Jumapili na siku za sikukuu 15. Jumapili na siku za sikukuu waamini wapaswa kushiriki Liturujia takatifu (divina liturgia) ama adhimisho la masifu ya kimungu (divinarum laudum), kadiri ya maagizo au desturi za riti yao[17]. Kwa minajili ya waamini kuitimiza kwa urahisi zaidi amri hii huamuliwa kuwa muda ufaao kwa kulitimiza hilo agizo uendelee tangu jioni ya vijilia (vesperis vigiliae) hadi mwisho wa Jumapili au siku ya sikukuu[18]. Na waamini huhimizwa kwa nguvu ili katika siku hizo wapokee Ekaristi takatifu, na pengine waipokee mara nyingi zaidi au hata kila siku[19]. Kuhusu Kitubio 16. Madhali kuna mchanganyiko wa kila siku wa waamini wa Makanisa maalum mbalimbali katika ukanda au eneo lilelile la Mashariki, basi mapadre wa riti yoyote ile wana idhini ya kupokea kitubio katika eneo lote, ikiwa wameruhusiwa kwa halali na pasipo kizuio na viongozi wao; tena wana idhini hiyo pia mahali pote na kwa waamini wa riti yoyote katika eneo lile moja; isipokuwa kama Mkuu wa mahali pale amekataa wazi ruhusa kwa eneo la riti yake[20]. Sakramenti ya Daraja takatifu 17. Ili kusudi katika Makanisa ya Mashariki utaratibu wa kale wa sakramenti ya Daraja takatifu upate nguvu mpya, Mtaguso huo Mkuu unapendelea iwekwe tena asasi ya Ushemasi wa kudumu pale ilipoachwa[21]. Na mintarafu Ushemasi mdogo na Daraja ndogo nyinginezo na haki na wajibu zao wenye mamlaka kisheria wa kila Kanisa maalum wajihusishe navyo[22]. Adhimisho la ndoa za mseto 18. Inabidi kuzuia ndoa batili wakati mkatoliki wa Mashariki anapofunga ndoa na asiye mkatoliki wa Mashariki aliyebatizwa; tena inapasa kushughulikia udumifu na utakatifu wa ndoa na pia amani katika nyumba; kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu unaamua kuwa utaratibu wa kisheria (formam canonicam) wa uadhimishaji ni wa lazima kwa habari ya uhalali (ad liceitatem) [wa ndoa]; na kwa habari ya uthabiti (ad validitatem) [wake] inatosha kuwepo kwa mhudumu (presentiam ministri sacri), hali vimefuatwa vipengere vingine vinavyodaiwa na sheria [za Kanisa][23]. IBADA TAKATIFU Sikukuu 19. Tangu sasa ni juu ya Mtaguso Mkuu tu au Kiti Kitakatifu kuamua, kusogeza au kufuta siku za sikukuu zilizo za Makanisa yote ya Mashariki. Lakini kuamua, kusogeza au kufuta sikukuu zielekeazo kila Kanisa maalum ni wajibu wa sinodi za Mapatriarka au za Maaskofu Wakuu, zaidi ya Kiti Kitakatifu; ila izingatiwe ipasavyo hali ya ukanda ule wote na ya Makanisa maalum mengine[24]. Adhimisho la Pasaka 20. Hadi wakristo wote watakapoyafikia maafikiano yanayotarajiwa kuhusu kuadhimisha kwa pamoja sikukuu ya Pasaka katika tarehe ileile, basi kwa sasa hivi, ili kuhamasisha umoja kati ya wakristo wanaoishi katika ukanda au nchi ileile, ni juu ya Mapatriarka au wenye mamlaka kuu ya kikanisa katika mahali pale kuafikiana kuhusu dominika ileile moja ambapo wapate kuadhimisha Pasaka. Hilo lifanyike kwa makubaliano ya wote, baada ya kusikia maoni ya wahusika[25]. Majira matakatifu 21. Mintarafu sheria ya majira matakatifu, kila mwamini anayejikuta kuishi nje ya nchi au eneo la riti yake aweza kufuata kikamilifu utaratibu uliopo mahali anapokaa. Na katika familia zenye mseto wa riti yaweza kufuatwa sheria hiyo kadiri ya riti mojawapo[26]. Masifu ya kimungu 22. Makleri na watawa wote wa Mashariki wayaadhimishe masifu ya kimungu kadiri ya maagizo na mapokeo ya utaratibu wao; na tangu nyakati za kale hayo Masifu yalizingatiwa kwa heshima kubwa katika Makanisa yote ya Mashariki[27]. Hivyo waamini nao, wakifuata mfano wa babu zao, wapaswa kujishirikisha katika Masifu ya kimungu kwa moyo wa ibada, kadiri ya kipimo cha nguvu zao. Lugha ya Liturujia 23. Ni wajibu wa Patriarka pamoja na Sinodi au wa mwenye mamlaka ya juu katika kila Kanisa pamoja na Halmashauri ya wakuu kupanga matumizi ya lugha katika madhehebu takatifu za kiliturujia na kuidhinisha tafsiri za matini katika lugha ya kienyeji, baada ya kukipelekea maelezo Kiti Kitakatifu[28]. MAHUSIANO NA NDUGU WA MAKANISA YALIYOJITENGA Kuhamasisha umoja wa Makanisa ya Mashariki yaliyojitenga 24. Ni wajibu maalum wa Makanisa ya Mashariki yaliyo katika ushirika na Kiti cha Kitume cha Roma kuhamasisha umoja wa wakristo wote, hasa wa Mashariki, kulingana na kanuni za dikrii “kuhusu Ekumeni” iliyotangazwa na Mtaguso huu Mkuu. Na kazi hii ifanyike kwanza kwa njia ya sala, mfano wa maisha, uaminifu mwangalifu kwa mapokeo ya kale ya Mashariki, ujuzi wenye kina zaidi wa wao kwa wao, ushirikiano na heshima ya kidugu kwa vitu na watu[29]. 25. Ndugu wa Mashariki waliojitenga ambao, wakisongwa na neema ya Roho Mtakatifu, wanakuja katika umoja wa kikatoliki, hawa wasidaiwe zaidi ya kile kinachodaiwa na ungamo tu la imani ya kikatoliki. Na madhali kati yao umehifadhiwa upadre ulio halali, makleri wa Mashariki wanaokuja katika umoja wa kikatoliki wanao uwezo wa kutumia Daraja yao, kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na mwenye mamlaka anayehusika[30]. Kanuni kuhusu “ushirika katika matakatifu” 26. Ushirika katika matakatifu, ambao unadhuru umoja wa Kanisa ama unaleta ukubali wazi wa kosa au tena hatari ya kukosa katika imani, kutoa kikwazo na kutojali, basi ushirika huo hukatazwa na sheria ya kimungu[31]. Lakini, kuhusu ndugu wa Mashariki, mang’amuzi ya kichungaji yanathibitisha kuwa zinaweza na zinapaswa kuzingatiwa mazingira mbalimbali yahusuyo watu mmoja mmoja, ambamo katika hayo umoja wa Kanisa haudhuriwi, wala hakuna hatari za kuepukana nazo, bali haja ya wokovu na manufaa ya kiroho ya nafsi yanasihi sana. Ndiyo maana kulingana na mazingira ya nyakati, mahali na watu, Kanisa Katoliki mara nyingi limeshika na linaendelea kushika tabia ya upole mkubwa zaidi, likiwatolea wote kati ya wakristo zana za wokovu na ushuhuda wa upendo, kwa njia ya kushiriki katika sakramenti na ibada nyinginezo, na katika mambo matakatifu mengine. Kwa kuyazingatia hayo, “ili tusiwe sisi kizuio kwa wale wanaokombolewa, kwa sababu ya ukali wa maamuzi yetu”[32]; tena ili kuhamasisha umoja na Makanisa ya Mashariki yaliyojitenga nasi, Mtaguso Mtakatifu unaamua mwongozo huu ufuatao. Matekelezo ya kichungaji ya “ushirika katika matakatifu” 27. Kisha kuwekwa kanuni zilizokumbushwa hapo juu, zaweza kutolewa sakramenti za Kitubio, Ekaristi na Mpako wa wagonjwa kwa ndugu wa Mashariki ambao, kwa dhamiri safi, wanajikuta wametengana na Kanisa Katoliki, ikiwa wanaziomba hizo sakramenti kwa hiari na kwa moyo mzuri. Na zaidi, hata wakatoliki nao wana ruhusa kuomba sakramenti hizi kutoka kwa wahudumu wasio wakatoliki, ambao katika Kanisa lao hutolewa sakramenti zilizo halali; na wafanye hivyo kila wanaposukumwa na haja au manufaa halisi ya kiroho wakati haiwezekani kumsogelea padre mkatoliki uso kwa uso au kwa sababu ya kimaadili[33]. 28. Vilevile, kisha kuwekwa kanuni zilezile, kwa sababu ya haki inaruhusiwa kushirikiana pamoja katika madhehebu, mambo matakatifu na mahali patakatifu kati ya wakatoliki na ndugu waliojitenga wa Mashariki[34]. 29. Tabia hii ya upole zaidi mintarafu ushirika katika matakatifu pamoja na ndugu wa Makanisa ya Mashariki yaliyojitenga inakabidhiwa kwa uangalifu na uongozi wa wenye mamlaka katika kila mahali ili, wakishauriana kati yao na, ikitakiwa, wakiisha kuwasikiliza pia wenye mamlaka wa Makanisa yaliyojitenga, waweze kuratibu mahusiano ya wakristo wao kwa wao kwa njia ya maagizo na kanuni zenye nguvu na za kufaa. HITIMISHO 30. Mtaguso Mtakatifu waufurahia sana ushirikiano wenye kuzaa na kutenda kazi baina ya Makanisa katoliki ya Mashariki na Magharibi na wakati huo watamka ifuatavyo: maagizo hayo yote ya kisheria yanawekwa kuelekea hali ya sasa, mpaka wakati Kanisa katoliki na Makanisa ya Mashariki yaliyojitenga yatakapoufikia ukamilifu wa ushirika. Lakini wakati huo wakristo wote, wa Mashariki na Magharibi, wanaalikwa kwa dhati kumwinulia Mungu maombi yenye juhudi na yasiyokoma, na zaidi yatolewe kila siku, ili, kwa msaada wa Mama Mtakatifu sana wa Mungu (Deipara), wote wapate kuwa kitu kimoja. Vilevile waombe ili wakristo walio wengi wa Kanisa lolote lile, ambao wanalikiri kwa ushujaa jina la Kristo na wanateswa na kudhulumiwa, uwamiminikie utimilifu wa tulizo na faraja ya Roho Mtakatifu Mfariji. Kwa upendo wa kidugu tupendane wote sisi kwa sisi, kwa heshima tukiwatanguliza wenzetu[35]. Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 21 Novemba 1964 Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki (zinafuata sahihi za Mababa)
UTANGULIZI (1) KUHUSU MAKANISA MAALUM AMA RITI (2-4) Umbalimbali wa riti haudhuru umoja (2) Riti mbalimbali zina heshima ileile (3) Riti mbalimbali zifahamike kwa makini (4) ULAZIMA WA KUTUNZA HAZINA YA KIROHO YA MAKANISA YA MASHARIKI (5-6) Tunu za Makanisa ya Mashariki (5) Badiliko lolote lisiingizwe bila idhini (6) MAPATRIARKA WA MASHARIKI (7-11) Asasi ya Upatriarka (7-8) Heshima ya pekee kwa Mapatriarka wa Mashariki (9) Uundaji wa patriarkati mpya (10-11) UTARATIBU WA SAKRAMENTI (12-18) Kurudisha tena utaratibu wa kale wa Sakramenti (12) Utoaji wa Kipaimara (13-14) Amri ya kusali Jumapili na siku za sikukuu (15) Kuhusu Kitubio (16) Sakramenti ya Daraja takatifu (17) Adhimisho la ndoa za mseto (18) IBADA TAKATIFU (19-23) Sikukuu (19) Adhimisho la Pasaka (20) Majira matakatifu (21) Masifu ya kimungu (22) Lugha ya Liturujia (23) MAHUSIANO NA NUGU WA MAKANISA YALIYOJITENGA (24-29) Kuhamasisha umoja wa Makanisa ya Mashariki yaliyojitenga (24-25) Kanuni kuhusu “ushirika katika matakatifu” (26) Matekelezo ya kichungaji ya “ushirika katika matakatifu” (27-29) HITIMISHO (30)
*Kwa usemi
Madhehebu ya kiliturujia (au
ya ibada) zinamaanishwa katika hati hii dhana hizi mbili: 1. Ujumla wa utaratibu wa ibada unaofuatwa na Kanisa maalum lolote la Mashariki; au 2.Sala kuu ya Ekaristi, au “Anafora”.
[1]Taz. Leo XIII, Litt. Ap.
Orientalium dignitas, 30 novemba 1894, katika Leonis XIII Acta, Vol. XIV, uk. 201-202.
** Neno
Riti ambalo limetumika sana katika hati hii lieleweke hivi: Jamii ya waamini (au Kanisa maalum) yenye kufuata jumla ya mapokeo ya kiliturujia inayoeleweka. Riti zinaainishwa kwa 1. Kanisa maalum linalilofuata; 2. Mafundisho ya pekee ya kikristo; 3. Lugha ya kiliturujia; na 4. Ujumla wa madhehebu ya ibada.
[2]Taz. Mt. Leo IX,
In terra pax, ann. 1053: “Ut enim”:
PL 143, 744-769. – Innocentius III, Synodus Lateranensis IV, ann. 1215, cap.IV: “Licet Graecos”:
Conc. Oec.Decr., uk. 211-212. – Id., Litt.
Inter
quatuor, 2 agosti 1206: “Postulasti postmodum”:
PL 215, 964. – Innocentius IV, Ep.
Cum de cetero, 27 agosti 1247. – Id., Ep.
Sub catholicae, 6 machi 1254, prooem.:
Magnum Bullarium Romanum III, uk. 340. – Nicolaus III, Instructio
Istud est memoriale, 9 oktoba 1278. – Leo X, Litt. Ap.
Accepimus nuper, 18 mei 1521. – Paulus III, Litt. Ap.
Dudum, 23 desemba 1534. – Pius IV, Const.
Romanus Pontifex, 16 februari 1564, § 5. – Clemens VIII, Const.
Magnus Dominus, 23 desemba 1595, § 10:
Magnum Bull. Rom. V, 2, uk. 87-92. – Paulus V, Const.
Solet circumspecta, 10 desemba 1615, § 3:
Magnum Bull. Rom. V, 4, uk. 199. – Benedictus XIV, Ep. Enc.
Demandatam, 24 desemba 1743, § 3. – Id., Ep. Enc.
Allatae sunt, 26 juni 1755, §§ 3, 6-19, 32. – Pius VI, Litt. Enc.
Catholicae communionis, 24 mei 1787. – Pius IX, Litt.
In suprema, 6 jenuari 1848, § 3. – Id., Litt. Ap.
Ecclesiam Christi, 26 novemba 1853. – Id., Const.
Romani Pontificis, 6 jenuari 1862. – Leo XIII, Litt. Ap.
Praeclara, 20 juni 1894, n. 7. – Id., Litt. Ap.
Orientalium dignitas, 30 novemba 1894, prooem. – n. k.
[3] Taz. Pius XII, Motu proprio
Cleri sanctitati, 2 juni 1957, can. 4:
AAS 49 (1957), uk. 437.
[4]
Ibid., can. 8: “sine licentia Sedis Apostolicae” (= bila idhini ya Kiti cha Kitume), kufuatana na utaratibu wa karne zilizotangulia; hali kadhalika, kuhusu waliobatizwa wasio katoliki husomwa katika can. 11: “ritum quem maluerint amplecti possunt” (= waweza kufuata riti wanayoipendelea):
AAS 49 (1957), uk. 438-439. Katika fasuli ilivyotolewa hapo juu hushauriwa wazi kwamba, wote na mahali pote, washike riti, yaani madhehebu za ibada, waliyo nayo.
[5]Taz. Leo XIII, Litt. Ap.
Orientalium dignitas, 30 novemba 1894. – Id., Ep. Ap.
Praeclara gratulationis, 20 juni 1894. – Taz. pia hati nyingine kama katika dondoo n. 2 hapo juu.
[6]Taz. Benedictus XV, Motu proprio
Orientis catholicis, 15 oktoba 1917:
AAS 9 (1917), uk. 531-533. – Pius XI, Litt. Enc.
Rerum orientalium, 8 septemba 1928:
AAS 20 (1928), uk. 277-288. – n.k.
[7] Utaratibu wa Kanisa Katoliki wakati wa Pius XI, Pius XII na Ioannes XXIII huonyesha kwa vikubwa mwelekeo huu.
[8]Taz. Synodum Nicaenam I, can. 6:
COD, uk. 8; Constantinopolitanam I, can. 2 na 3: l.c., uk. 27-28; Chalcedonensem, can. 28: l.c., uk. 75-76; id., can. 9: l.c., uk. 67; Constantinopolitanam IV, can. 17: l.c., uk. 155-156; id., can. 21: l.c., uk. 158; Lateranensem IV, can. 5: l.c., uk. 212; id., can. 30, l.c., uk. 225; Florentinam,
Decr. pro Graecis, 6 julai 1439: l.c., uk. 504; n.k.
[9]Taz. Synodum Nicaenam I, can. 6:
COD, uk. 8; Constantinopolitanam I, can. 3: l.c., uk. 28; Constantinopolitanam IV, can. 17: l.c., uk. 155-156. – Pius XII, Motu proprio
Cleri sanctitati, can. 216, §§ 2, 11:
AAS 49 (1957), uk. 497.
[10] Katika Mitaguso ya kiekumeni kama ifuatavyo: Synodum Nicaenam I, can. 6:
COD, uk. 8; Constantinopolitanam I, can. 3: l.c., uk. 28; Constantinopolitanam IV, can. 21: l.c., uk. 158; Lateranensem IV, can. 5: l.c., uk. 212; Florentinam,
Decr. pro Graecis, 6 julai 1439, § 9: l.c., uk. 504. – Pius XII, Motu proprio
Cleri sanctitati, can. 219:
AAS 49 (1957), uk. 498. – n.k.
[11]Taz. dondoo n. 8 hapo juu.
[12]Taz. Synodum Ephesinam, can. 8:
COD, uk. 55-56. – Clemens VII,
Decet Romanum Pontificem, 23 februari 1596:
Magnum Bull. Rom. V, 2, uk. 94-96. – Pius VII, Litt. Ap.
In universalis Ecclesiae, 22 februari 1807:
Magnum Bull. Rom. Cont. XIII, uk. 97-101. – Pius XII, Motu proprio
Cleri sanctitati, 2 juni 1957, can. 324-339:
AAS 49 (1957), uk. 530-534. – Syn. Carthaginen., ann. 419, can. 17: Mansi 4, 485.
[13]Syn. Carthaginen., ann. 419, can. 17 na 57: Mansi 4, 485 na 496-497; Chalcedonensem, ann. 451, can. 12:
COD, uk. 69. – Mt. Innocentius I, Litt.
Et onus et honos, a. c. 415: “Nam quid sciscitaris”:
PL 20, 548-549. – Mt. Nicolaus I, Litt.
Ad consulta vestra, 13 novemba 866: “A quo autem”:
PL 119, 1007. – Innocentius III, Litt.
Rea regum, 25 februari 1204:
PL 215, 277-280. – Leo XII, Const. Ap.
Petrus Apostolorum Princeps, 15 agosti 1824:
Magnum Bull. Rom. - Cont. XVI, uk. 82-84. – Leo XIII, Litt. Ap.
Christi Domini, ann. 1895. – Pius XII, Motu proprio
Cleri sanctitati, 2 juni 1957, can. 159:
AAS 49 (1957), uk. 478.
[14] Taz. Innocentius IV, Ep.
Sub catholicae, 6 machi 1254, § 3, n.4:
Magnum Bullarium Romanum III, uk. 340-342. – Syn. Lugdunensis (Lyons) II, ann. 1274 (Ungamo la imani la Mikaeli Palaelogus mbele ya Gregori X). – Eugenius IV, katika Syn. Florentina, Const.
Exultate Deo, 22 novemba 1439, § 11:
COD, uk. 520. – Clemens VIII, Instr.
Sanctissimus, 31 agosti 1595:
Magnum Bull. Rom. V, 2, uk. 72-73. – Benedictus XIV, Const.
Etsi pastoralis, 26 mei 1742, § II, n. 1, § III, n. 1, n.k. – Synodus Laodicena, ann. 347/381, can. 48: Mansi 2, 571-572 (taz. pia
Codificazione Canonica Orientale, fonti IX, uk. 183); Syn. Sisen. Armenorum, ann. 1342: Mansi 25, 1240-1241; Syn.Libanen. Maronitarum, ann. 1736, P. II, cap. III, n. 2: Mansi 38, 48; na Sinodi nyinginezo faridi.
[15]Taz. S.S.C.S. Officii, Instr. (kwa Askofu wa Spis), ann. 1783. – S.C. de Prop. Fide (pro Coptis), 15 machi 1790, n. XIII. – Id., Decr. 6 oktoba 1863, C. a. – S.C. pro Eccl. Orient., 1 mei 1948. – S.S.C.S. Officii, resp., 22 aprili 1896, kwa waraka wa 19 mei 1896.
[16]
CIC, can. 782 § 4. – S.C. pro Eccl. Orient., Decr.
De Sacramento Confirmationis administrando etiam fidelibus orientalibus a presbyteris latini ritus, qui hoc indulto gaudent pro fidelibus sui ritus, 1 mei 1948:
AAS 40 (1948) uk. 422-423.
[17]Taz. Synodus Laodicena, ann. 347/381, can. 29: Mansi 2, 569-570. – Mt. Nicephorus Constant., cap. 14:
PG 111, 749-760. – Syn. Duinen. Armenorum, ann. 719, can. 31. – Mt. Theodorus Studita, sermo 21:
PG 99, 536-538. – Mt. Nicolaus I, Litt.
Ad consulta vestra, 13 novemba 866: “In quorum Apostolorum”, “Nosse capitis”, “Quod interrogatis”, “Praeterea consulitis”, “Si die Dominico”:
PL 119, 984-985, 993-994. – Taz. pia Sinodi nyinginezo faridi.
[18] Kanuni hii ni – kwa namna fulani – mpya, walau pale panapo ulazima wa kushiriki Liturujia Takatifu. Lakini inaendana na desturi ya wakristo wa Mashariki wanavyotambua siku za kiliturujia.
[19] Taz.
Canones Apostolorum, 8 na 9: Mansi 1, 29-32. – Syn. Antiochena, ann. 341, can. 2: Mansi 2, 1309-1310. – Timotheus Alex., interog. 3. – Innocentius III, Const.
Quia divinae, 4 jenuari 1215. – Taz. pia sinodi faridi nyingi za Makanisa ya Mashariki za hivi karibuni.
[20] Pamoja na kuhifadhi umahalia (
territorialitate) wa mamlaka ya kisheria, kanuni hii ina lengo ya kusaidia mema ya roho, kati ya wingi wa mamlaka ya kisheria katika eneo moja lilelile.
[21]Taz. Synodum Nicaenam I, can. 18:
COD, uk. 13-14; Syn. Neocaesarien., ann. 314/325, can. 12: Mansi 2, 543-546; Syn. Sardicen., ann. 343, can. 8: Mansi 3, 11-12; Syn. Chalcedonensem, can. 6:
COD, uk. 66; Constantinopolitanam IV, can. 23:
COD, uk. 159; id., can. 26: l.c., uk. 161; n.k. – Mt. Leo M., Litt.
Omnium quidem, 13 jenuari 444:
PL 54, 616-620.
[22] Ushemasi mdogo katika Makanisa mengi ya Mashariki unahesabiwa kama Daraja ya chini, lakini kwa Motu proprio ya Pius XII,
Cleri sanctitati, 2 juni 1957, cann. 70 na 76:
AAS 49 (1957), uk. 457-458, hupewa faradhi kama za Daraja za za juu. Kanuni hii inashauri kuwa ni vema kurudia kwenye utaratibu wa zamani wa kila Kanisa pekee mintarafu masharti ya wenye ushemasi mdogo, kwa kengeuko la sheria ya kawaida ilivyotolewa na
Cleri sanctitati.
[23]Taz. Pius XII, Motu proprio
Crebrae allatae, 22 februari 1949, can. 32, § 2, n. 5 (uwezo wa Mapatriarka wa kuruhusu kuhusu utaratibu “
forma”):
AAS 41 (1949), uk. 96; Pius XII, Motu proprio
Cleri sanctitati, 2 juni 1957, can. 267 (uwezo wa Mapatriarkawa kusahihisha tangu mwanzoni “
sanandi in radice”):
AAS 49 (1957), uk. 514; S.S.C.S. Officii na S.C. pro Eccl. Orient., an. 1957 hutoa idhini na kuruhusu kuhusu utaratibu na kusahihisha “kwa hitilafu wa utaratibu” (kwa miaka mitano): “nje ya eneo la Upatriarkati, kwa Mametropolita na Wakuu wengine wa mahali... wasio na mkuu yeyote mwingine baada ya Kiti Kitakatifu”.
[24]Taz. Mt. Leo M., Litt.
Quod saepissime, 15 aprili 454: “Petitionem autem”:
PL 54, 1094-1096. – Mt. Nicephorus Constant., cap. 13. – Syn. Sergii Patriarchae, 18 septemba 1596, can. 17. – Pius VI, Litt. Ap.
Assueto paterne, 8 aprili 1775:
Magnum Bull. Rom. - Cont. V, uk. 35-37. –n.k
[25]Taz. Conc.Vat. II, Const. de Sacra Liturgia,
Sacrosanctum Concilium, 4 desemba 1963:
AAS 56 (1964), uk. 133 (nyongeza).
[26]Taz. Clemens VIII, Instr.
Sanctissimus, 31 agosti 1595, § 6: “Si ipsi graeci”:
Magnum Bull. Rom. V, 2, uk. 73. – S.S.C.S. Officii, 7 juni 1673, ad 1 na 3. – Id., 13 machi 1727, ad 1. – S.C. de Prop. Fide, Decr. 18 agosti 1913, art. 33:
AAS 5 (1913) uk. 398. – Id., Decr. 14 agosti 1914, art. 27:
AAS 6 (1914) uk. 462-463. – Id., Decr. 27 machi 1916, art. 14:
AAS 8 (1916) uk. 107. – S.C. pro Eccl. Orient., Decr. 1 machi 1929, art. 36:
AAS 21 (1929) uk. 158. – Id., Decr. 4 mei 1930, art. 41:
AAS 22 (1930) uk. 352-353.
[27]Taz. Synodus Laodicena, ann. 347/381, can. 18: Mansi 2, 567-568. – Syn. Mar Issaachi Chaldaeorum, ann. 410, can. 15. – Mt. Nerses Glaien. Armenorum, ann. 1166. – Innocentius IV, Ep.
Sub catholicae, 6 machi 1254, § 8:
Magnum Bullarium Romanum III, uk. 341. – Benedictus XIV, Const.
Etsi pastoralis, 26 mei 1742, § 7, n. 5. – Id., Instr.
Eo quamvis tempore, 4 mei 1745, §§ 42 ss. – Taz. pia Sinodi faridi za hivi karibuni, agh.Armenorum (1911), Coptorum (1898), Maronitarum (1736), Rumenorum (1872), Ruthenorum (1891), Syrorum (1888).
[28] Kadiri ya mapokeo ya Mashariki.
[29] Kulingana na maumbile ya Bulla za umoja za Makanisa katoliki ya Mashariki moja moja.
[30] Ni sharti la Mtaguso mintarafu ndugu waliojitenga wa Mashariki wa Daraja yoyote na wa kiwango chochote, ya amri ya kimungu na ya kikanisa.
[31] Fundisho hili lina nguvu pia katika Makanisa yaliyojitenga.
[32] Mt. Basilius M.,
Epistula canonica ad Amphilochium,
PG 32, 669B.
[33] Misingi ya mpunguzo huu iko katika: 1. Uthabiti wa masakramenti; 2. Nia njema na mwelekeo mwema; 3. Haja ya wokovu wa milele; 4. Kutokuwepo padre wake pekee; 5. Utovu wa hatari za kuepukana nazo na wa ukubali wa wazi wa kosa.
[34] Inaongelewa hapa ule “ushirika katika matakatifu nje ya masakramenti”. Ni Mtaguso unaotoa ruhusa hii, ila yafuatwe yaliyoagizwa.
|