SALA KWA HESHIMA YA BIKIRA MARIA IMAKULATA, KWENYE PIAZZA DI SPAGNA
ILIYOTUNGWA NA BABA MTAKATIFU FRANSISKO
Tarehe 8 Desemba 2015, Jumanne
Ee Bikira Maria,
katika sikukuu hii ya kutungwa wewe mimba bila doa la dhambi,
ninakuja kukuletea heshima za imani na upendo
kwa niaba ya taifa takatifu la Mungu linalokaa katika Mji huu na Jimbo hili.
Ninakuja kwa niaba ya familia nyingi, pamoja na furaha zao na shida zao;
kwa niaba ya watoto na vijana, wanaotarajia kuishi vyema;
kwa niaba ya wazee, waliosukuma miaka na kujaa maarifa;
ha hasa ninakuja kwako
kwa upande wa wagonjwa, wa wafungwa,
na wa wote wanaosikia zaidi ugumu wa maisha.
Kama Mchungaji, ninakuja pia kwa niaba ya wote
waliofika kwetu kutoka nchi za mbali kutafuta amani na kazi.
Chini ya joho lako kuna nafasi kwa wote,
kwa sababu wewe ni Mama wa Huruma.
Moyo wako umejaa upendo kwa watoto wako wote:
ndio upendo wa Mungu, ambaye kwako alitwaa mwili, akawa ndugu yetu, Yesu,
Mwokozi wa kila mwanamume na wa kila mwanamke.
Tukikutazama wewe, Mama yetu uliyekingiwa kila doa la dhambi,
tunatambua ushindi wa Huruma ya Mungu
juu ya dhambi na juu ya matunda yote ya dhambi;
na tunapata tena tumaini la kuishi maisha mazuri,
yaliyo huru na kila utumwa, chuki na hofu.
Leo, huku, kwenye kiini cha jiji la Roma, tunasikia sauti yako ya kimama
inayotuita sote tufunge safari
kuelekea ule Mlango, ulio ishara ya Kristo.
Wewe unatuambia sisi sote: “Njooni, mjongee kwa tumaini,
ingieni na kupokea zawadi ya Rehema;
msiwe na hofu, msione aibu:
Mungu Baba anawasubiri kwa mikono miwili
ili awape msamaha wake na kuwapokea nyumbani mwake.
Njooni wote kwenye chemchemi ya amani na furaha”.
Tunakushukuru, ee Mama Maria Imakulata,
kwani katika safari hii ya upatanisho
hukutuacha peke yetu, bali unatusindikiza,
upo karibu nasi na kututegemeza katika magumu yote.
Na ubarikiwe, sasa na sikuzote, ee Mama! Amina.
Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana