IBADA YA KUWEKWA WAKFU KWA MOYO SAFI WA BIKIRA MARIA
Ee Bikira Maria, Mama wa Mungu na Mama yetu, sisi, katika saa hii ya dhiki, tunakukimbilia. Wewe ni Mama, unatupenda na unatujua: hakuna kitu kilichofichwa kwako kutoka nyoyoni mwetu. Mama wa huruma, mara nyingi tumeonja huruma yako ya upendo, uwepo wako unaoturejeshea amani, ili utuongoze daima kwa Yesu, Mfalme wa amani.
Lakini tumepoteza njia ya amani. Tumesahau somo la majanga ya karne iliyopita, dhabihu ya mamilioni ya watu walioanguka katika Vita Kuu ya Dunia. Tumepuuza ahadi zilizotolewa kama Jumuiya ya Kimataifa na tunasaliti ndoto za amani za watu na matumaini ya vijana. Tumeugua kwa tabia ya uchoyo, tumejifungia kwa maslahi ya utaifa, tumejiruhusu kulemazwa na hali ya kutojali na kudhohofishwa na ubinafsi. Tulipendelea kumpuuza Mwenyezi Mungu, kuishi na uwongo wetu, kuchochea uchokozi, kukandamiza uhai na kulimbikiza silaha, tukisahau kwamba sisi ni walinzi wa jirani yetu na mazingira nyumba ya wote. Tumeirarua bustani ya dunia vipande vipande kwa vita, tumeujeruhi moyo wa Baba yetu kwa dhambi, ambaye anataka tuwe ndugu na dada. Tumekuwa watu wasiojali kila mtu na kila kitu isipokuwa sisi wenyewe. Na kwa aibu tunasema: utusamehe, Bwana!
Katika taabu ya dhambi, katika juhudi na udhaifu wetu, katika fumbo la uovu na vita, wewe, Mama Mtakatifu, unatukumbusha kwamba Mwenyezi Mungu hatutupi, bali anaendelea kututazama kwa upendo, akitamani kutusamehe na kuamka tena. Yeye ndiye aliyetupatia wewe na ameweka katika Moyo wako Safi kimbilio kwa Kanisa na kwa wanadamu. Kwa wema wa kimungu uko pamoja nasi na hata katika mikunjo finyu ya historia unatuongoza kwa upole.
Basi na tunakimbilia kwako, tuubishe mlango wa Moyo wako Safi, watoto wako wapendwa ambao hawachoki kutembelea na kuwaalika kwenye wongofu. Kanisa katika saa hii ya giza, njoo utusaidie na kutufariji. Rudia kwa kila mmoja wetu: "Je, mimi si niko hapa, Mama yako ni nani?" Wewe unajua jinsi ya kufungua kinzani ya mioyo na mafundo ya nyakati zetu. Tunaweka imani yetu kwako. Tuna hakika kwamba wewe, haswa wakati wa majaribio, hatadharau maombi yetu na uje hima kutusaidia.
Hivi ndivyo mlivyofanya kule Kana ya Galilaya, mlipoharakisha saa ya Yesu kuingilia kati na kufanya ishara yake ya kwanza ulimwenguni. Sikukuu ilipogeuka kuwa huzuni ulimwambia: "Hawana divai" (Yn 2: 3). Rudia tena kwa Mwenyezi Mungu, Ee Mama, kwa sababu leo tumetindikiwa na divai ya matumaini, furaha imetoweka, udugu umemwagika. Tumepoteza ubinadamu, tumepoteza amani. Tumekuwa na uwezo wa vurugu na uharibifu wote. Tunahitaji uingiliaji wako wa kina mama haraka.
Kwa hivyo, Mama, tunaomba ukubali ombi letu.
Wewe, nyota ya bahari, usituruhusu tuvunjike katika dhoruba ya vita.
Wewe, Sanduku la Agano Jipya, himiza miradi na njia za upatanisho.
Wewe, "Nchi ya Mbinguni", unaleta upatanisho wa Mungu duniani.
Zima chuki, ondoa tabia ya kulipiza kisasi, utufundishe kusamehe.
Tukomboe kutoka kwenye vita, linda ulimwengu kutokana na tishio la Vita ya Nyuklia.
Malkia wa Rozari Takatifu, uamshe ndani yetu haja ya kusali na kupenda.
Malkia wa familia ya wanadamu, anawaonesha watu njia ya udugu.
Malkia wa Amani, ombea amani kwa ulimwengu.
Machozi yako, Ee Mama, yasogeze mioyo yetu migumu. Machozi uliyotutolea yafanye yachipushe bonde hili ambalo chuki yetu imelikausha. Na wakati kelele za silaha hazikomi, sala yako inatuweka kwenye amani. Mikono yako ya kimama inawajali wale wanaoteseka na kukimbia chini ya uzito wa mabomu. Kumbatio lako la kina mama hiwafariji wale wanaolazimika kukimbia nyumba zao na nchi yao. Moyo wako wa huzuni utusogeze kwenye huruma na utusukume kufungua milango na kuwatunza wanadamu waliojeruhiwa na kukataliwa.
Mzazi Mtakatifu wa Mungu, ulipokuwa chini ya Msalaba, Yesu, alipomwona mfuasi kando yako, alikuambia: “Tazama mwanao” (Yn 19:26): ndivyo alivyokukabidhi kila mmoja wetu kwako. Kisha kwa mwanafunzi, kwa kila mmoja wetu, alisema: "Tazama mama yako" (Yn:19: 27). Mama, sasa tunataka kukukaribisha katika maisha yetu na historia yetu. Katika saa hii, ubinadamu, umechoka na kufadhaika, uko chini ya uzito wa Msalaba pamoja nawe. Na tunahitaji kujikabidhi kwako, kujiweka wakfu kwa Kristo kupitia kwako. Watu wa Ukraine na Warussi, wanaokuheshimu kwa upendo, wanakukimbilia, wakati Moyo wako unadunda kwa ajili yao na kwa watu wote waliouawa kutokana na vita, njaa, ukosefu wa haki na taabu.
Kwa hivyo, sisi, Mama wa Mungu na Mama Yetu, tunajikabidhi kwa dhati na kujiweka wakfu, Kanisa na wanadamu wote, haswa Urussi na Ukraine kwa Moyo wako Safi. Kubali Ibada hii tunayofanya kwa uaminifu na upendo, vita vikome, tujalie amani ulimwenguni. Ndiyo iliyochipuka kutoka kwenye Moyo wako Safi ili kufungua malango ya historia kwa Mfalme wa Amani; tunatumaini kwamba tena, kupitia Moyo wako, amani itatufikia. Kwa hiyo, tunaweka wakfu wakati ujao wa familia nzima ya binadamu, mahitaji na matarajio ya watu, mahangaiko na matumaini ya ulimwengu.
Kupitia kwako Rehema ya kimungu imiminike Duniani na mapigo matamu ya amani yanarudi kuangaza nyakati zetu. Bikira Maria Mwanamke wa ndiyo, ambaye Roho Mtakatifu alikushukia turejeshee maelewano ya Kimungu. Zima ukavu wa mioyo yetu, wewe uliye “chemchemi hai ya matumaini.” Umesuka ubinadamu Yesu, utufanye tuwe wasanii wa ushirika. Ulitembea katika njia zetu, utuongoze katika njia za amani. Amina.
Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana