Kiti Kitakatifu
WARAKA WA KITUME KWA JINSI YA “MOTU PROPRIO”
WA BABA MTAKATIFU FRANSISKO
“ALIWAFUNULIA AKILI ZAO”
AMBAO KWA NJIA YAKE INAANZISHWA DOMINIKA YA NENO LA MUNGU
1. “Aliwafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” (Lk 24:45). Kitendo hicho ni kati ya vitendo vya mwisho alivyovitenda Bwana mfufuka, kabla ya kupaa kwake mbinguni. Alionekana kwa wanafunzi wake walipokuwa wamekusanyika pamoja, akamega mkate pamoja nao, akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko Matakatifu. Kwa watu wale waliokuwa wameshikwa na hofu na kukata tamaa, alifunua maana ya fumbo la Pasaka: yaani kwamba, kadiri ya mpango wa milele wa Mungu Baba, Yesu alipaswa kuteswa na kufufuka kutoka katika wafu ili awajalie watu wote uongofu na msamaha wa dhambi (taz. Lk. 24:26.46-47); pia aliahidi kumpeleka Roho Mtakatifu atakayewapa nguvu ya kuwa mashahidi wa Fumbo hili la wokovu (taz. Lk 24:49). Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee katika uhusiano wa dhati kati ya Bwana Yesu Mfufuka, jumuiya ya waamini na Maandiko Matakatifu. Bila ya Bwana Yesu anayetuangaza, haiwezekani kabisa tuelewe kwa kina Maandiko Matakatifu; lakini pia ni kweli kinyume chake: yaani, bila ya Maandiko Matakatifu haiwezekani kuelewa matukio ya utume wake Yesu na wa Kanisa lake ulimwenguni. Ndiyo maana Mt. Hieronimo aliweza kuandika: “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo” (In Is., Utangulizi: PL 24,17).
2. Mwishoni mwa Jubilei ya pekee ya huruma niliomba ifikiriwe juu ya “dominika ya kuwekwa moja kwa moja kwa ajili ya Neno la Mungu, ili kutambua utajiri usio na kikomo unaotokana na mazungumzano ya daima ya Mungu na watu wake" (Waraka ya kitume Misericordia et misera, 7). Kuweka kwa namna ya pekee Dominika moja ya Mwaka wa kiliturujia kwa ajili ya Neno la Mungu kunaleta nafasi, hasa, ya kurudia katika Kanisa tendo lile la Bwana Mfufuka anayetufunulia sisi pia hazina ya Neno lake ili tuweze kuwa ulimwenguni watangazaji wa utajiri huo usio na mwisho. Kuhusu jambo hilo, tunakumbuka mafundisho ya Mt. Efrem: “Nani anaweza kufahamu, ee Bwana, utajiri wote wa mojawapo la maneno yako? Ni zaidi sana wingi wa tunayokosa kushika, kuliko tunaloweza kulifahamu. Sisi ndio watu wenye kiu, tunaokinywea chemchemi. Neno lako linatujalia maana nyingi mbalimbali, kama ilivyo mingi mitazamo ya wenye kulisoma na kutafakari. Bwana alitilia neno lake uzuri wa rangi mbalimbali, kusudi wale wanaolichunguza waweze kugundua ndani yake kile wanachokipendelea. Alificha hazina zote katika neno lake, kusudi kila mmoja wetu apate utajiri wake ndani ya lile analolitazama” (Maelezo juu ya Diatessaron, 1, 18).
Kwa njia ya Waraka huu, basi, ninataka kuitikia maombi mengi yaliyonijia kutoka kwa watu wa Mungu, ili katika Kanisa zima ianze kuadhimishwa kwa nia moja Dominika ya Neno la Mungu. Imekuwa tayari utaratibu wa kawaida kuishi kipindi maalumu ambapo jumuiya ya kikristo inatafakari kwa makini thamani kubwa ya Neno la Mungu kwa ajili ya maisha yake ya kila siku. Katika Makanisa mahalia kuna utajiri mkubwa wa miradi mbalimbali ya kuwezesha waamini kuzoea zaidi na zaidi kusoma Maandiko Matakatifu, hadi kuwafikisha kwenye hatua ya kushukuru sana kwa kipaji kikubwa namna hiyo walichokipokea, na kujibidisha kukiishi katika maisha yao ya kila siku na kuwajibika kukishuhudia kwa ukweli.
Mtaguso Mkuu wa Vatikano II ulilihimiza sana Kanisa litambue tena umuhimu wa Neno la Mungu, kwa njia ya Konstitusyo ya kidogma Dei Verbum. Katika hati hiyo, ambayo daima tunapaswa kuitafakari na kuiishi, hufafanuliwa kidhahiri maumbile na maana ya Maandiko Matakatifu, urithishaji wa ufunuo wa kimungu kizazi hata kizazi (sura ya 2), uvuvio wa kimungu wa Maandiko Matakatifu (sura ya 3) yanayofumbata Agano la Kale na Agano Jipya (sura za 4 na 5), na umuhimu wake kwa maisha ya Kanisa (sura ya 6). Kwa lengo la kusisitiza mafundisho hayo, Papa Benedikto wa 16 aliitisha mnamo mwaka 2008 Mkutano wa Sinodi ya Maaskofu wenye dhamira hii: “Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa”, na, kutokana na huo, alitolea Wosia wa Kitume “Verbum Domini” (“Neno la Bwana”), ambayo imekuwa mafundisho ya lazima kwa jumuiya zetu. [1] Katika Hati hiyo, kwa namna ya pekee, inachunguzwa tabia ya kiutendaji wa Neno la Mungu, hasa katika tendo la kiliturujia ambapo tabia yake ya kisakramenti hudhihirika zaidi. [2]
Ni vema, basi, kwamba usikosekane kamwe katika maisha ya watu wetu uhusiano halisi na Neno lililo hai ambalo Bwana hachoki kulisema kwa Bibi harusi wake, ili aweze kukua katika upendo na katika kushuhudia imani.
3. Kwa sababu hiyo, ninaagiza kwamba Dominika ya 3 ya Kipindi cha Kawaida cha Mwaka wa kiliturujia iwekwe rasmi kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu. Kwa namna hii, Dominika hiyo ya Neno la Mungu itaangukia katika wakati muafaka wa duru ya mwaka wa kiliturujia, yaani tunapoalikwa kuimarisha uhusiano wetu na ndugu Waebrania na kusali kwa ajili ya umoja wa Wakristo. Si tu suala la upatanifu wa majira: kuadhimisha Dominika ya Neno la Mungu kuna thamani ya kiekumeni, kwani Maandiko Matakatifu yanawaonyesha wote wenye kuyasikiliza njia inayoelekeza kwenye umoja kamili na thabiti. Jumuiya zote zitapanga namna ya kuisherehekea vyema Dominika hii. Itakuwa muhimu, kwa vyovyote, kwamba katika adhimisho la Ekaristi kitabu cha Biblia kitawazwe, kusudi ionekane wazi kwa wote waliokusanyika kwamba Neno la Mungu lina uwezo wa kutuamuru. Katika Dominika hiyo, kwa namna ya pekee, itafaa sana kusisitiza usomaji bora wa Neno la Mungu, na kutengeneza homilia kwa kusudi la kuheshimu huduma inayotolewa kwa ajili ya Neno la Bwana. Maaskofu wataweza kuadhimisha katika Dominika hii ibada ya kuwaweka rasmi Wasomaji au kukabidhi huduma inayofanana nayo, ili kukumbusha umuhimu wa kutangaza vyema Neno la Mungu katika liturujia. Maana, ni muhimu sana kwamba juhudi zizidi kufanyika ili kuwaandaa waamini kadha wa kadha wawe watangazaji hodari wa Neno kwa kupitia maandalizi maalumu, jinsi inavyotokea tayari kwa waakoliti na wahudumu wa dharura wa Ekaristi takatifu. Hali kadhalika, maparoko watatafuta njia za kukabidhi Biblia, au kitabu chake kimojawapo, kwa wote waliohudhuria, kusudi watambue wazi umuhimu wa kuendelea kuisoma katika maisha ya kila siku, kuitafakari na kusali na Maandiko Matakatifu, kwa namna ya pekee kwa kutumia utaratibu wa somo la kimungu, yaani lectio divina.
4. Kurudi kwa watu Waisraeli kwenye nchi takatifu, baada ya uhamisho wa Babeli, kulisindikizwa kwa namna ya pekee na usomaji wa kitabu cha Torati. Biblia inatupatia simulizi la kuvutia la tukio lile, katika kitabu cha Nehemia. Watu walikuwa wamekusanyika huko Yerusalemu, kwenye uwanja uliokuwa mbele ya lango la Maji, kuisikiliza Torati. Watu wale walikuwa wametawanyika uhamishoni, lakini sasa wamekusanyika tena mbele ya Maandiko Matakatifu kama “mtu mmoja” tu (Neh 8:1). “Masikio ya watu wote yalisikiliza” (Neh 8:3) yale yaliyokuwa yakisomwa katika kitabu kitakatifu, watu wakijua kwamba watapata katika maneno yale maana halisi ya matukio yaliyowapata. Wakauitikia utangazaji wa maneno yale kwa kuguswa moyoni na kulia: “Nao [Walawi] wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa. Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote: ‘Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie.’ Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. [...] ‘Wala msihuzunike, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.’" (Neh 8:8-10). Maneno haya yana mafundisho makuu ndani yake. Biblia haiwezi kuhesabiwa kuwa urithi wa wengine tu, wala mkusanyo wa vitabu kwa ajili ya wachache waliobahatika. Awali ya yote, Biblia ni kitabu cha watu waliokusanyika ili kuisikiza na kujitambua katika Neno lile. Mara nyingi, vinatokea vikundi vinavyojaribu kuhodhi kitabu kitakatifu na kukifanya mali ya wachache au ya kikundi kiteule tu. La! Sivyo! Biblia ni kitabu cha watu wa Mungu, ambao kwa kukisikiliza wanatoka mgawanyiko na utengano wakielekea umoja. Neno la Mungu linawaunganisha waamini na kuwafanya kuwa taifa moja.
5. Katika umoja huu, uliotengenezwa kwa kusikiliza, Wachungaji kwanza wana wajibu mkuu wa kueleza Maandiko Matakatifu na kuwasaidia wote kuyaelewa. Kwa vile yenyewe ni kitabu cha taifa la Mungu, wote wenye wito wa kuwa wahudumu wa Neno wanapaswa kujisikia kwamba wana wajibu mkubwa wa kusaidia yawafikie waamini wote wa jumuiya yao.
Homilia hasa inakuwa msaada mahususi, kwa sababu ina “tabia inayoelekea kuwa ya kisakramenti” (Wosia wa kitume Evangelii gaudium, 142). Kuwaingiza waamini katika Neno la Mungu kwa kina, kwa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka kwa wasikilizaji, inamruhusu padre kufunua pia “uzuri wa mifano ambayo Bwana Yesu alitumia ili kuwachochea watu kutenda mema” (taz. hapohapo kama kabla). Hiyo ni fursa ya kichungaji ambayo lazima tusiikose!
Maana, kwa waamini wetu walio wengi, hii ni nafasi pekee waliyo nayo ya kushika uzuri wa Neno la Mungu na kuona jinsi linavyohusiana na maisha yao ya kila siku. Kwa hiyo, ni lazima kutumia muda wa kutosha ili kuandaa homilia. Haiwezekani kubuni hapohapo maelezo ya masomo matakatifu. Kinyume chake, sisi wahubiri tunatakiwa kufanya bidii tusitoe hotuba ndefu kupita kiasi, za kisomi au zenye masuala mengine yasiyoendana na Masomo. Tukitulia kutafakari masomo matakatifu, hapo basi tutaweza kusema kwa moyo ili kuifikia mioyo ya watu wanaotusikiliza, kusudi tusisitize lililo muhimu la kulishikilia na litoalo tunda. Tusichoke kamwe kujipatia muda wa kusali na Maandiko Matakatifu, ili yapokelewe “si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli” (1The 2:13).
Pia makatekista, kwa ajili ya huduma waliyo nayo ya kuwasaidia wengine kukua katika imani, wanapaswa kufanyika wapya daima na daima kwa njia ya kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, na kwa njia hii wataweza kuwachochea wanaowasikiliza kuwa na uhusiano wa kweli na Neno la Mungu pia wao wenyewe.
6. Kabla ya kufika kwa wanafunzi, waliokuwa wamejifungia nyumbani, na kuwafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko Matakatifu (taz. Lk 24:44-45), Yesu Mfufuka aliwatokea wawili miongoni mwao kwenye njia ambayo kutoka Yerusalemu inaelekea Emau (taz. Lk 24:13-35). Luka katika simulizi lake linaonyesha kuwa mkutano huo ulitokea siku ileile ya Ufufuko, yaani Dominika. Wanafunzi hao wawili walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo yote yaliyohusu mateso na kifo chake Yesu. Walikuwa wakisafiri kwa huzuni kubwa na kukata tamaa kwa sababu ya kifo cha ukatili cha Yesu. Walikuwa wakimtumaini kwamba Yeye ndiye Masiya mkombozi, na wanakabiliana sasa na kikwazo cha Msulibiwa. Polepole, Yesu Mfufuka mwenyewe alikaribia, akaandamana nao, lakini wale hawakumtambua (taz. a. 16). Walipokuwa njiani, Bwana Yesu aliwauliza maswali, akagundua kwamba wao hawakuielewa maana ya mateso na kifo chake; akawaambia: “Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito” (a. 25) na “akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika Maandiko yote yaliyomhusu Yeye mwenyewe" (a. 27). Kristo ndiye mfafanuzi wa kwanza! Siyo tu kwamba Maandiko ya zamani yalitangulia kusema nini atakachotenda, lakini Yeye mwenyewe alitaka kuwa mwaminifu kwa Neno lile, kusudi aonyeshe kwamba historia ya wokovu iliyo moja inatimizwa ndani yake Kristo.
7. Kwa hiyo, Biblia, iliyo Maandiko Matakatifu, inasema ya Yesu Kristo na kumtangaza kuwa yeye ndiye aliyepaswa kupitia mateso ili kuingia kwenye utukufu (taz. a. 26). Maandiko yote yanasema habari zake, si tu sehemu fulani za Maandiko. Haiwezekani kuelewa maana ya kifo chake na ufufuko wake mbali na Maandiko Matakatifu. Ndiyo sababu ungamo la imani la kale linasisitiza kwamba Yesu Kristo “alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo Maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo Maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa” (1Kor 15:3-5). Kwa vile Maandiko Matakatifu yanasema habari za Yesu Kristo, yanatuwezesha kuamini kwamba kifo na ufufuko wake si mambo yanayohusu visasili, bali ni matukio ya kihistoria ambayo yaunda kiini cha imani ya wanafunzi wake. Kuna uhusiano wa pekee baina ya Maandiko Matakatifu na imani ya waamini. Kwa vile imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo (taz. Rum 10:17), mwito muhimu tunaopata ni kwamba sisi waamini tupokee upesi Neno la Bwana, kwa kulisikiliza katika tendo la kiliturujia, katika sala na katika kutafakari binafsi.
8. “Safari” ya Yesu Mfufuka pamoja na wanafunzi wa Emau inatimia kwa kula pamoja jioni. Msafiri yule asiyefahamika anakubali ombi la wale wawili: “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha" (Lk 24:29). Waliketi chakulani, na Yesu alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua (taz. a. 31).
Tokeo hilo linadhihirisha ulivyo wa ndani uhusiano baina ya Maandiko Matakatifu na Ekaristi Takatifu. Mtaguso Mkuu wa Vatikano II unatufundisha kuwa “Kanisa limekuwa linayaheshimu Maandiko wakati wote kama linavyouheshimu Mwili wa Bwana. Haliachi kamwe, hasa katika Liturujia ya kimungu, kujilisha na kuwapa waamini mkate wa uzima, unaochukuliwa kutoka meza ya Neno la Mungu na meza ya Mwili wa Kristo” (Dei Verbum, 21).
Kudumu katika kusoma Maandiko Matakatifu na kuadhimisha Ekaristi Takatifu kunawasaidia watu wa Mungu kuzidi kutambuana. Kama wakristo sisi ni taifa moja linalosafiri katika historia, tukitegemezwa na Bwana Yesu ambaye yupo kati yetu na kusema nasi na kutulisha. Siku iliyowekwa kwa ajili ya Biblia inataka iwe siyo “mara moja tu kila mwaka”, bali mara moja kwa ajili ya mwaka mzima, kwani tunahitaji sana tukawe wazoefu na wapenzi wa Maandiko Matakatifu na wa Bwana Mfufuka, ambaye hakomi kumega Neno na Mkate kwa ajili ya jumuiya ya waamini. Ndiyo sababu tunahitaji kukuza uhusiano wetu na Maandiko Matakatifu, vinginevyo moyo wetu unabaki baridi na macho yanabaki yamefungwa, kutokana na aina mbalimbali za upofu.
Maandiko Matakatifu na Sakramenti hazitenganikani. Kila mara Sakramenti zinapotanguliwa na kuangaziwa na Neno la Mungu, zinadhihirika wazi kuwa kituo cha safari ambapo Kristo mwenyewe anatufungulia akili na mioyo tupate kutambua tendo lake la wokovu. Katika muktadha huu, ni muhimu tusisahau mafundisho yanayopatikana katika kitabu cha Ufunuo. Hapo tunafundishwa kwamba Bwana anasimama mlangoni, na kubisha hodi. Mtu akiisikia sauti yake na kuufungua mlango, Yeye ataingia kwake, na atakula pamoja naye (taz. Ufu 3:20). Yesu Kristo anabisha mlangoni petu kwa njia ya Maandiko Matakatifu; nasi tukisikiliza na kuufungua mlango wa akili na moyo, Yeye ataingia katika maisha yetu na kubaki pamoja nasi.
9. Katika Waraka wa Pili kwa Timotheo, ambayo kwa namna fulani ni kama wosia wake, Mtakatifu Paulo anamsihi huyo mshiriki wake mwaminifu azidi kusoma Maandiko Matakatifu. Mtume Paulo ana imani kwamba “kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza na kwa kuwaadibisha katika haki” (2Tim 3:16). Himizo hilo la Paulo kwa Timotheo limekuwa msingi mmojawapo ambao juu yake Konstitusyo ya Mtaguso Mkuu Dei Verbum inajadili dhamira kuu la uvuvio wa Maandiko Matakatifu, msingi inayodokeza wazi tabia yake, yaani hasa lengo la wokovu, hali ya kiroho na msingi wa umwilisho.
Kwa kunukulu kwanza agizo la Paulo kwa Timotheo, hati ya Dei Verbum inasisitiza kwamba “vitabu vya Maandiko Matakatifu vinafundisha kwa nguvu, kwa uaminifu thabiti na bila hitilafu ukweli ambao Mungu alitaka ukabidhiwe kwa Maandiko Matakatifu” (na. 11). Kwa vile hayo yanatufundisha kwa ajili ya wokovu unaokuja kwa imani katika Kristo (taz. 2Tim 3:15), kweli zilizomo ndani yake zinafaa kwa wokovu wetu. Biblia si mkusanyo wa vitabu vya historia, wala vya taarifa za habari, bali ni moja kwa moja chombo cha wokovu halisi ya binadamu. Kwamba vitabu vya Biblia vina misingi yake katika historia halisi isiwe sababu ya kutufanya tusahau lengo hili la awali: yaani, wokovu wetu. Yote yanaelekea lengo hilo ambalo limo mwenye tabia yenyewe ya Biblia, iliyotungwa kama historia ya wokovu ambamo Mungu anasema na kutenda ili kuwaendea watu wote na kuwaokoa kutoka katika uovu na mauti.
Ili kufikia hatima hiyo ya wokovu, Maandiko Matakatifu chini ya utendaji wa Roho Mtakatifu yanageuza maneno ya wanadamu yaliyoandikwa kibinadamu hadi kuwa Neno la Mungu (taz. Dei Verbum, 12). Kazi ya Roho Mtakatifu katika Maandiko Matakatifu ni ya msingi kabisa. Pasipo utendaji wake, kuna hatari ya kufungwa katika mipaka finyu ya maneno yaliyoandikwa tu, na kuhalalisha ufafanuzi wa kifondamentalisti, ambao ni muhimu kuepukana nao ili kutokusaliti hali ya uvuvio, ya kukua na ya kiroho ya maneno ya kitabu kitakatifu. Kama Mtume Paulo anavyokumbusha: “Andiko huua, bali roho huhuisha” (2Kor 3:6). Kwa hiyo, Roho Mtakatifu anayafanya Maandiko Matakatifu kuwa Neno lililo hai la Mungu, ambalo watu wake watakatifu wanaliishi na kurithisha katika imani yao.
10. Utendaji wa Roho Mtakatifu hauhusu tu uundaji wa Maandiko Matakatifu, bali anatenda kazi pia ndani ya wale wanaojiweka kulisikia Neno la Mungu. Ni muhimu tamko hili la Mababa wa Mtaguso lisemalo kwamba “Maandiko Matakatifu lazima yasomwe na kufunuliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu mwenyewe ambaye kwa njia yake yaliandikwa” (Dei Verbum, 12). Ufunuo wa Mungu unatimilika na kukamilika kwa njia ya Yesu Kristo; hata hivyo, Roho Mtakatifu anaendeleza kazi yake. Maana, tungepunguza hadhi ya kazi ya Roho Mtakatifu tukifikiri kwamba inahusu tu hali ya uvuvio wa kimungu wa Maandiko Matakatifu na waandishi wake mbalimbali tu. Ni muhimu kuwa na imani katika utendaji wa Roho Mtakatifu ambaye anaendelea kutimiza aina yake pekee ya uvuvio pale ambapo Kanisa linafundisha Maandiko Matakatifu, pale ambapo Majisterio inayafafanua kihalisi (taz. Dei Verbum, 10) na ambapo kila mwamini anayafanya kuwa kanuni yake ya kiroho. Kwa maana hii twaweza kuelewa maneno ya Yesu alipowaambia wanafunzi wake, ambao walikuwa wakishuhudia kuwa wameelewa maana ya mifano yake, akisema: “Kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale” (Mt 13:52).
11. Hatimaye, hati ya Dei Verbum inaeleza kwamba “maneno ya Mungu yaliyotamkwa kwa lugha za kibinadamu yameingia katika maneno ya wanadamu, kama vile Neno wa Baba wa milele alivyojifanya mtu, akichukua udhaifu wa maumbile ya kibinadamu” (na. 13). Ni sawa na kusema kwamba umwilisho wa Neno wa Mungu ni kielelezo na maana ya uhusiano baina Neno la Mungu na maneno ya wanadamu, yakiwa pamoja na maumbile yake ya kihistoria na kitamaduni. Ni katika tukio hili ambamo huundwa Mapokeo, ambayo pia ni Neno la Mungu (taz. Dei Verbum, 9). Mara nyingi tupo kwenye hatari ya kutenganisha Maandiko Matakatifu na Mapokeo, bila kugundua kwamba yenyewe, kwa pamoja, ndiyo chimbuko pekee ya Ufunuo. Tabia ya Maandiko Matakatifu ya kuwekwa kimaandishi haidhuru hali yake ya kuwa kihalisi neno lililo hai; hali kadhalika Mapokeo yaliyo hai ya Kanisa, lenye kuyarithisha kwa mfululizo karne baada ya karne na kizazi baada ya kizazi, yanahifadhi kile kitabu kitakatifu kama “kanuni kuu kuliko zote ya maisha yake ya imani" (Dei Verbum, 21). Na kwa kweli, kabla ya kuwa matini zilizoandikwa, Neno la Mungu lilirithishwa kisimulizi na kuhifadhiwa katika imani ya watu ambao walilitambua kama historia yake na utambulisho wake halisi kati ya mataifa mengine mengi. Kwa hiyo, imani ya kibiblia ina misingi yake katika Neno lililo hai, si juu ya kitabu.
12. Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Roho yuleyule ambaye kwake yaliandikwa, yanadumu daima kuwa mapya. Agano la Kale si kamwe kuukuu, likiwa ni sehemu ya Agano Jipya, kwa sababu yote yanageuzwa na yule Roho mmoja anayeyavuvia. Ujumla wa matini takatifu una tabia ya kinabii: nayo haihusu mambo yajayo, bali ya leo ya kila anayejilisha Neno hili. Yesu mwenyewe anasisitiza kwa wazi ukweli huu mwanzoni mwa kuhubiri kwake: “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu” (Lk 4:21). Mtu anayejilisha kila siku Neno la Mungu anakuwa, kama Yesu, jirani wa watu anaokutana nao; hashawishiki kutamani mambo yasiyozaa ya zamani, wala kutegemea matazamio yasiyowezekana kwa siku za mbele.
Maandiko Matakatifu yatenda unabii wake kwanza juu ya yule ayasikilizaye. Yenyewe yasababisha utamu na uchungu. Tunayakumbuka maneno ya nabii Ezekieli alipoalikwa na Bwana Mungu kula gombo la kitabu, akasema: “Kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali” (Eze 3:3). Mwinjili Yohane pia, akiwa kwenye kisiwa kiitwacho Patmo, anaishi yaleyale aliyoyang’amua nabii Ezekieli alipokula kitabu, lakini anaongeza maelezo ya hisia ya wazi zaidi: “Nacho kitabu kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu” (Ufu 10:10).
Utamu wa Neno la Mungu unatusukuma kulishiriki na wale tunaokutana nao katika maisha yetu ili kuonyesha uhakika wa tumaini lililo ndani yake (taz. 1Pet 3:15-16). Uchungu, kwa upande wake, unatokana mara nyingi na kuhakikisha jinsi ilivyo vigumu kwetu sisi kuliishi kiaminifu, au kung’amua jinsi linavyodharauliwa kwa sababu hatulioni kuwa na uwezo wa kutia maana kwa maisha yetu. Kwa hiyo, ni muhimu tusiwe na uzoefu mbaya na Neno la Mungu, bali tujilishe nalo ili kutambua na kuishi kwa kina uhusiano wetu na Mungu na ndugu.
13. Changamoto nyingine inayoletwa kwetu na Maandiko Matakatifu inahusu mapendo. Neno la Mungu linatuita daima kwenye upendo wa Mungu Baba uliojaa huruma na kutudai sisi wanae tuishi katika mapendo. Maisha ya Yesu ni kielelezo bora na kikamilifu cha upendo huu wa Mungu, asiyebakiza chochote kwa ajili yake, bali anajitolea kwa wote bila ubaguzi. Katika mfano wa Lazaro, yule mtu maskini, tunapata maelezo yaliyo muhimu. Hapo Lazaro na mtu tajiri walipokufa, yule tajiri, akimwona aliyekuwa maskini amepokelewa kifuani mwa Ibrahimu, anaomba ili Lazaro apelekwe kwa ndugu zake na kuwaonya waishi kwa kuwapenda majirani, wasije wao pia wakafika mahali pale pa mateso alipofika yule tajiri. Jibu la Ibrahimu ni kali: “Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao" (Lk 16:29). Kusikiliza Maandiko Matakatifu ili kujifunza kutenda huruma: hii ni changamoto kubwa kwa maisha yetu. Neno la Mungu linaweza kuyafumbua macho yetu na kutuwezesha tuachane na ubinafsi unaotufunga katika utasa, na kutufungulia njia ya ushirikiano na mshikamano.
14. Kugeuka sura Bwana Yesu ni tukio lenye maana katika uhusiano wa Yesu na wanafunzi wake. Yesu alipanda mlimani ili kuomba, pamoja na Petro na Yakobo na Yohane. Wainjili wamekumbuka kwamba uso na mavazi ya Yesu yaling’aa, na watu wawili walikuwa wakiongea naye. Musa na Eliya, ambao ni mfano wa Torati na Manabii, yaani Maandiko Matakatifu. Jibu la Petro, alipoona hivyo, lilikuwa la furaha na ushangao. “Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya” (Lk 9:33). Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, na wanafunzi wakaogopa walipoingia katika wingu hilo.
Tukio hilo la kugeuka sura Bwana Yesu linakumbusha Sikukuu ya Vibanda, ambapo Ezra na Nehemia walisoma kitabu kitakatifu mbele ya watu, baada ya kurudi kutoka uhamishoni. Lakini pia, linaonyesha kabla utukufu wa Yesu, kama maandalizi ya kikwazo cha mateso, utukufu wa kimungu ambao unadokezwa na wingu linalowafunika wanafunzi, likiwa ishara ya uwepo wa Bwana Mungu. Kugeuka sura kwa Yesu kunafanana na kugeuka sura kwa Maandiko Matakatifu, ambalo linakuwa tukufu linapolisha maisha ya waamini. Kama inavyokumbusha Waraka wa Verbum Domini: “Katika kuzingatia muungano kati ya maana mbalimbali za Maandiko Matakatifu, inakuwa muhimu kugundua namna ya kutoka kwenye ‘andiko’ na kufika kwenye ‘roho’ yake. Si hatua inayofikiwa kwa yenyewe, pasipo kufanya juhudi; bali inatakiwa kuwepo tukio la ‘kugeuza sura’ kwa andiko” (na. 38).
15. Katika safari yetu ya kupokea Neno la Mungu anatusindikiza Maria, Mama wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunayemheshimu mtakatifu kwa sababu aliamini kuwa yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana (taz. Lk 1:45). Heri ya Maria inatangulia heri zote alizotamka Yesu juu ya maskini, walioteseka, wapole, wapatanishi na wale wanaodhulumiwa, kwa sababu ndiyo kigezo cha lazima kwa ajili ya kila heri nyingine. Hakuna maskini aliye mwenye heri kwa sababu ni maskini; ila, anakuwa ana heri ikiwa, sawa na Maria, anaamini kwamba Neno la Mungu linatimia. Anatukumbusha jambo hilo mtakatifu mmoja, aliyekuwa mwanafunzi mkuu na mwalimu wa Maandiko Matakatifu: Augustino. “Mwanamke mmoja katika mkutano, akishikwa na mshangao mkubwa, alipaza sauti na kusema: ‘Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya’. Lakini Yesu alisema, ‘Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.’ Sawa na kusema: Pia mama yangu, unayemwita heri, ndiye mwenye heri kwa vile anavyolishika neno la Mungu, si kwa sababu katika tumbo lake Neno wa Mungu alifanyika mwili na akakaa kwetu, ila kwa sababu yeye analishika neno lenyewe la Mungu ambalo kwa njia yake Maria alifanywa, na ambaye ndani mwake lilichukua mwili” (Hotuba juu ya Injili ya Yohane, 10, 3).
Dominika kwa ajili ya Neno iweze kukuza katika watu wa Mungu hamu na uzoefu wa kushinda na Maandiko Matakatifu, jinsi mwandishi mtakatifu alivyokuwa akifundisha tayari hapo zamani: “Neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya” (Kum 30:14).
Imetolewa huku Roma, kwenye Kanisa la Mt. Yohane katika Laterani, tarehe 30 Septemba 2019
Kumbukumbu ya kiliturujia ya Mt. Hieronimo, katika uzinduzi wa mwaka wa 1600 tangu kifo chake.
FRANSISKO
[1] Taz. AAS 102 (2010), 692-787.
[2] “Tabia ya kisakramenti ya Neno la Mungu inaweza kueleweka kwa kuilinganisha na uwepo halisi wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai yaliyowekwa wakfu. Kwa kujongea altare na kushiriki meza ya Ekaristi sisi tunapokea na kushiriki kwelikweli mwili na damu vya Kristo. Kutangazwa kwa Neno la Mungu katika adhimisho la kiliturujia ni kitu kimoja na kutambua kuwa Kristo mwenyewe ndiye aliyepo mbele yetu na kusema nasi ili sisi tumpokee” (Verbum Domini, 56).
Matini: ©Copyright - Libreria Editrice Vaticana
Tafsiri: ©Copyright – Familia za Maamkio –Iringa na Libreria Editrice Vaticana
Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana