Index

Back Top Print

[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya kazi za kimisioni za Kanisa

Ad Gentes

Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

 

UTANGULIZI

1. Kanisa limetumwa na Mungu KWA MATAIFA YOTE (Ad Gentes), ili liwe “sakramenti ya wokovu kwa wote”[1]; na kwa kudaiwa na wajibu wa ndani wa ukatoliki wake, na kwa kulitii agizo la Mwanzilishi wake[2], lafanya bidii kuitangaza Injili kwa watu wote. Maana Mitume wenyewe ambao Kanisa lilijengwa juu yao, hali wakifuata nyayo zake Kristo, “walihubiri neno la kweli na kuanzisha Makanisa”[3]. Kwa hiyo ni wajibu wa waandamizi wao kuendeleza kazi hiyo, ili “Neno la Mungu liendelee na kutukuzwa” (2The 3:1) na Ufalme wa Mungu utangazwe na kusimikwa duniani kote.

Lakini, kwa majira ya siku hizi, ambayo hali mpya ya ubinadamu inaonekana, Kanisa, lililo chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu[4], linaitwa kwa lazima zaidi kuviokoa na kuvifanya upya viumbe vyote, ili vyote vijumlishwe katika Kristo, na katika yeye wanadamu wapate kuunganika kama familia moja na taifa moja la Mungu.

Kwa hiyo Mtaguso Mkuu, pamoja na kumtolea Mungu shukrani kwa matendo matukufu yaliyotimizwa kwa njia ya ukarimu wa jitihada za Kanisa zima, hutaka kufafanua kanuni za msingi za kazi za kimisioni na kuziunganisha pamoja juhudi za waamini wote, ili Taifa la Mungu, likiiendea ile njia nyembamba ya msalaba, liueneze popote Ufalme wake Kristo, Bwana na mwangalizi (conspectoris) wa milele[5], na hivyo kumtayarishia njia Yeye anayekuja.

Sura ya Kwanza

KANUNI ZA MSINGI ZA MAFUNDISHO

Azimio la Mungu Baba

2. Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa kwa Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na azimio la Mungu Baba[6].

Azimio hilo labubujika kutokana na “upendo-mfano-wa-chemchemi“, yaani mapendo ya Mungu Baba, ambaye ndiye asili asiye na asili, kutoka kwake Mwana huzaliwa, na Roho Mtakatifu hutoka kwa njia ya Mwana. Kutokana na wema wake wenye huruma na usio na mipaka, alituumba kwa hiari na pia alituita bila gharama kushiriki katika uzima na utukufu, tena alimimina kwa wingi neema yake, wala hakomi kuimimina, ili kwamba yeye aliye Muumba wa wote, apate pia kuwa “yote katika wote” (1Kor 15:28), hivyo kufanyiza utukufu wake na heri yetu sawia. Na ilimpendeza Mungu kuwaita wanadamu kwenye ushirika wa uzima wake sio mmoja mmoja, kana kwamba hawana muungano kati yao, bali ilimpendeza kuwaunda kama taifa moja, ambalo ndani yake watoto wake Mungu waliotawanyika wapate kuwa wamoja[7].

Utume wa Mwana wa Mungu

3. Azimio hilo la Mungu kwa ajili ya wokovu wa wanadamu wote halitimizwi kisirisiri tu katika akili za wanadamu au kwa njia ya juhudi, za kidini pia, ambazo kwazo watu wamtafuta Mungu kwa namna nyingi “kama wataweza kumpapasa au kumkuta, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu” (Mdo 17:27). Maana juhudi hizo lazima zitiwe nuru na kusahihishwa hata kama – kwa azimio jema la Mungu mfadhili – zinaweza pengine zikaongoza kwa Mungu wa kweli, au zikawa maandalio kwa Injili[8]. Mungu, ili kuweka amani, au ushirika naye, na pia kuunda jamii ya kidugu kati ya wanadamu, walio wenye dhambi, aliazimu kuingia historia ya wanadamu kwa namna mpya na ya mwisho, akimtuma Mwanae katika mwili sawa na mwili wetu, ili kwa njia yake apate kuwanyang’anya watu kutoka kwa nguvu za giza na za shetani[9] na kuupatanisha naye ulimwengu katika huyu Mwana[10]. Huyo ndiye ambaye Mungu aliufanya ulimwengu kwa njia yake[11], akamfanya kuwa mrithi wa vitu vyote, ili kuvijumlisha vitu vyote katika yeye[12].

Maana Kristo Yesu alitumwa ulimwenguni kama mshenga halisi kati ya Mungu na wanadamu. Kwa kuwa ni Mungu, “katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili” (Kol 2:9); na kadiri ya tabia ya ubinadamu [wake, yeye ndiye] Adamu mpya, “amejaa neema na kweli” (Yn 1:14), amesimikwa kuwa kiongozi wa watu waliofanywa upya. Kwa hiyo, Mwana wa Mungu amekubali kuchukua mwili kweli ili kuwafanya watu wote washiriki wa tabia ya kimungu; ingawa alikuwa tajiri alijifanya maskini kwa ajili yetu sisi, ili kwamba sisi nasi tupate kuwa matajiri kwa umaskini wake[13]. Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi, yaani ya wote[14]. Mababa wa Kanisa husisitiza mara nyingi kwamba kila kisichotwaliwa na Kristo hakikuponywa[15].Yeye alitwaa kweli ubinadamu kikamilifu, ulivyo kwetu sisi tulio wadhaifu na maskini, isipokuwa hakuwa na dhambi[16]. Maana Kristo “ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni” (Yn 10:36), alisema kuhusu yeye mwenyewe: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta, amenituma kuwahubiria maskini habari njema, kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena” (Lk 4:18); na tena: “Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea” (Lk 19:10).

Sasa, mambo yote ambayo Bwana alihubiri, au yaliyotendeka katika yeye kwa ajili ya wokovu wa wanadamu wote, hayana budi kutangazwa na kuenezwa mpaka miisho ya dunia[17],kuanza tangu Yerusalemu[18]; hivyo yale yaliyotimizwa mara moja tu na kwa daima kwa ajili ya wokovu wa wote, yataweza kuleta manufaa kamili kwa wote, katika mfululizo wa nyakati.

Utume wa Roho Mtakatifu

4. Ili kutekeleza hayo yote Kristo alimtuma Roho Mtakatifu kutoka kwa Baba ili atimize kwa ndani kazi yake ya wokovu, na alisisimue Kanisa lijieneze. Bila shaka Roho Mtakatifu alitenda kazi ulimwenguni hata kabla ya Kristo kutukuzwa[19]. Walakini katika siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu aliwashukia wanafunzi ili kukaa nao milele[20], likaonekana wazi Kanisa mbele ya umati wa watu, uenezaji wa Injili kati ya mataifa yote ukaanza kwa njia ya mahubiri. Hatima, katika siku ile ilitabiriwa kuunganika kwa mataifa yote katika ukatoliki wa imani kwa njia ya Kanisa la Agano Jipya, Kanisa ambalo hunena kwa lugha zote, na ambalo huelewa na kujumuisha lugha zote katika upendo, na hivyo kuushinda mtawanyo wa Babeli[21]. Maana siku hiyo ya Pentekoste yalianzishwa “Matendo ya Mitume”, kama vile kwa uwezo wa Roho Mtakatifu juu ya Bikira Maria Kristo alivyojimwilisha, na tena kwa kushuka kwake Roho Mtakatifu juu yake Kristo alipokuwa akisali, ameongozwa kutimiza utume wake[22]. Na Bwana Yesu mwenyewe, kabla ya kutoa uhai wake kwa hiari kwa ajili ya ulimwengu, aliratibisha huduma ya kitume na alitoa ahadi ya kwamba atamtuma Roho Mtakatifu, ili wote wawili wafanye kazi pamoja daima na popote na kutimiza tendo la wokovu[23]. Roho Mtakatifu katika nyakati zote “hulifanya Kanisa kuwa moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili vipawa mbalimbali vya kihierarkia na vya kikarama”[24]. Tena, huzitilia uhai taasisi za kikanisa[25], akiwa ni mtima wake, na akimimina katika nyoyo za waamini roho ya kimisioni, ambayo Yesu mwenyewe alisukumwa nayo. Na huyu Roho pengine hutangulia waziwazi utendaji wa kimisioni[26], kama vile kwa namna mbalimbali huandamana nao, na kuuongoza bila kukoma[27].

Utume wa Kanisa

5. Tangu mwanzo wa utume wake, Bwana Yesu “aliwaita aliowataka mwenyewe... akawaweka watu kumi na wawili wapate kuwa pamoja naye na kwamba awatume kuhubiri (Mk 3:13)[28]. Hivyo mitume wakawa chipukizi la Israeli mpya na papo hapo mwanzo wa hierarkia takatifu. Halafu, baada ya kuyatimiza ndani yake mafumbo ya wokovu wetu na ya kuvifanya upya vitu vyote kwa njia ya kufa na kufufuka kwake, Bwana Yesu, hali amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani[29], kabla hajapaa kwenda mbinguni[30],alilisimika Kanisa lake kama sakramenti ya wokovu, na aliwatuma mitume waende ulimwenguni kote, kama vile yeye alivyokuwa ametumwa na Baba[31], akawaagiza hivi: “Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Robo Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Mt 28:19-20); “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa” (Mk 16:15). Kwa hiyo Kanisa limewajibika kueneza imani na wokovu wa Kristo kwa nguvu za agizo la waziwazi ambalo Daraja ya Maaskofu, likisaidiwa na Mapadre, na kwa kuunganika na Halifa wa Petro, aliye Mchungaji mkuu wa Kanisa, limerithi kutoka kwa Mitume. Tena, [linaieneza] kwa nguvu za uhai ambao Kristo hushirikisha viungo vyake: “Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikamanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, hukuza mwili upate kujijengea wenyewe katika upendo” (Efe 4:16). Utume wa Kanisa hutekelezwa kwa njia ya tendo lile ambalo, kwa kulitii agizo la Kristo na kusukumwa na neema na upendo wa Roho Mtakatifu, hujifanya liwepo kikamilifu (pleno actu) kati ya watu wote na mataifa yote, ili, kwa kielelezo cha maisha yake na kwa mahubiri, kwa sakramenti na vyombo vingine vya neema, lipate kuwaongoza kufikia imani, uhuru na amani ya Kristo, na hivyo liwaandalie njia nyeupe na thabiti ifikishayo kwenye kushiriki kikamilifu fumbo la Kristo.

Maadam utume huo hufuliza na kufunua katika mfululizo wa historia utume wa Kristo mwenyewe, aliyetumwa kuwahubiria maskini Injili, Kanisa – kwa nguvu ya Roho wa Kristo – halina budi kuifuata njia ileile aliyoifuata Kristo, yaani njia ya umaskini, ya utii, ya huduma na ya kujitoa mhanga mwenyewe mpaka mauti, ambamo alitoka mshindi kwa ufufuko wake. Maana hivyo ndivyo walivyoenenda katika tumaini Mitume wote, ambao walipata taabu na mateso mengi, na hivyo walitimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani Kanisa lake[32].Na mara nyingi damu ya Wakristo ikawa mbegu[33].

Kazi ya kimisioni

6. Wajibu huu, ambao Daraja ya Maaskofu, chini ya uongozi wa Halifa wa Petro, hupaswa kutimilizwa kwa njia ya sala na ushirikiano wa Kanisa zima; ni mmoja na uleule popote na katika hali yoyote ile, hata kama utekelezaji wake unategemea mazingira. Kwa hiyo, tofauti ambazo lazima zitambulikane katika shughuli hizi za Kanisa, hazitokani na mtima wenyewe wa utume wake, bali na mazingira ambapo utume huo hutekelezwa.

Mazingira hayo yanategemea Kanisa, kama vile na mataifa, jumuiya, ama watu, ambao ujumbe huo huwaelekea. Maana Kanisa, ingawa lina ukamilifu wa vyombo vyote vya wokovu, halitendi wala haliwezi kutenda kila mara, na moja kwa moja kwa namna iliyokwisha kukamilika. Katika utendaji wake, unaoelekea kutimiza mpango wa Mungu, Kanisa huwa linaanzisha shughuli au linazitekeleza hatua kwa hatua, na pengine, baada ya uanzishaji wenye mafanikio mazuri, lapaswa kusikitika kurudi nyuma, au kukawia likifanikiwa nusu au kuwa na upungufu fulani. Mintarafu watu, jumuiya na mataifa, Kanisa linawagusa na kuwapenya hatua kwa hatua, na hivyo huwakusanya katika utimilifu wa kikatoliki. Kulingana na hali au mazingira yalivyo tofauti, basi mtindo maalum na vyombo vifaavyo lazima vitumiwe.

Shughuli za pekee, ambazo zinafanywa na watu wenye kutangaza Injili waliotumwa na Kanisa, wakienda ulimwenguni kote ili kutimiza wajibu wa kuhubiri Injili na kupandikiza Kanisa lenyewe kati ya Mataifa na ya makundi ambayo bado hayajamwamini Kristo, zaitwa kwa kawaida “Misioni”. Hizo zinatimilika kwa matendo ya kimisioni na aghalabu zinashughulikiwa katika maeneo maalum, yaliyoidhinishwa na Kiti Kitakatifu. Lengo la kazi hizo za kimisioni ni uenezi wa Injili na uanzishaji wa Kanisa kati ya mataifa na kati ya makundi ya watu ambapo bado halijaweka mizizi[34].Hivyo kutokana na mbegu ya Neno la Mungu yapate kustawi Makanisa faridi ya wazalendo, yaliyosimikwa popote duniani kwa idadi ya kufaa. Makanisa hayo, yakipata nguvu zake na ubivu wake, na yenye hierarkia yake iliyounganika na waamini, na pia yenye vile vyote vinavyohitajika ili kuishi vema maisha ya kikristo, yaweze kutoa mchango wao kwa ajili ya Kanisa zima. Chombo cha msingi cha juhudi hiyo ya kuanzisha Makanisa ni tendo la kuihubiri Injili ya Yesu Kristo. Kwa kusudi la kuitangaza Injili, Bwana Yesu aliwatuma wafuasi wake ulimwenguni mwote, ili wanadamu, wakizaliwa upya kwa Neno la Mungu[35],wapate kuunganishwa kwa Ubatizo katika Kanisa, ambalo, kwa vile ni mwili wake Neno aliyejimwilisha, hulishwa na kupata uzima kwa njia ya Neno lake Mungu na ya mkate wa Ekaristi[36].

Katika utendaji huo wa kimisioni wa Kanisa, zinaonekana hatua ambazo zatofautiana, na pengine zachanganyikana: mwanzoni hali ya uanzishaji au ya upandikizaji, baadaye, hali ya upya au uchanga. Walakini, shughuli za kimisioni za Kanisa, hazikomi wakati hatua hizo zimetimia; bali ni wajibu wa Makanisa faridi yaliyokwisha simamishwa kuziendeleza, na kuihubiri Injili kwa kila mmoja ambaye bado yuko nje nayo.

Tena makundi, ambayo kati yao Kanisa limewekewa misingi, yanaweza kubadilika sana kwa sababu mbalimbali, hata mazingira yao yageuke kuwa mapya kabisa. Papo hapo Kanisa linapaswa kukadiria kama mazingira hayo yanahitaji tena kazi zake za kimisioni. Aidha, mara nyingine jinsi mambo yalivyo, huuzuia kwa muda utangazaji wazi na mpenyevu wa ujumbe wa kiinjili. Hapo wamisionari, kwa subira na busara, pamoja na imani kubwa, wanaweza na kupaswa kutoa walau ushuhuda wa mapendo na wema wa Kristo, na hivyo kumtayarishia Bwana njia, na kwa namna fulani kusimika uwepo wake.

Hivyo inaonekana wazi kwamba kazi za kimisioni kwa asili hububujika kutoka katika maumbile yenyewe ya Kanisa, huieneza imani yenye kuokoa, huukamilisha umoja wake wa kikatoliki pamoja na kuupanua, huwa na misingi yake katika hali yake, ya kuwa la Mitume, hutimiza juhudi ya baraza zima la Hierarkia yake, hushuhudia kuueneza na kusisimua utakatifu wake. Vilevile, kazi za kimisioni kati ya mataifa hutofautiana na kazi za kichungaji zifanyikazo kwa manufaa ya waamini, na jitihada za kurudisha umoja wa Wakristo. Walakini shughuli za namna hizo mbili zinafungamana mno na jitihada za umisioni za Kanisa[37]: maana utengano kati ya Wakristo ni kikwazo kibaya sana kwa tendo takatifu la kuhubiri Injili kwa watu wote[38], na huwafungia wengi mlango wa imani. Kwa vile kazi za kimisioni ni za lazima, Wakristo wote huitwa kukusanyika katika zizi moja, na hivyo, wakiwa na moyo mmoja, waweze kutoa ushuhuda kwa Kristo, Bwana wao, mbele ya mataifa yote. Maana wasipoweza bado kuungama imani moja kikamilifu, wanapaswa kujawa na moyo wa kuheshimiana na kupendana wao kwa wao.

Sababu zinazodai kazi za kimisioni

7. Kazi hizo za kimisioni zinapata sababu na asili zake katika mapenzi ya Mungu, ambaye “hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, mwanadamu Kristo Yesu, ambaye alijitoa mwenyewe kwa ajili ya ukombozi wa wote” (1 Tim 2:4-6), “wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote” (Mdo 4:12). Ndiyo sababu wote wanapaswa kumwongokea Yeye, ambaye hujulikana kwa njia ya mahubiri ya Kanisa, na kwa njia ya Ubatizo kuunganishwa naye na pia na Kanisa, yaani Mwili wake, hata kuwa mwili mmoja. Maana, Kristo mwenyewe “alisisitiza kwa maneno wazi ulazima wa imani na ubatizo[39], na papo hapo akathibitisha ulazima pia wa Kanisa, ambamo watu wanaingia kwa njia ya ubatizo kama kwa mlango. Kwa sababu hiyo, hawawezi kuokoka watu wale ambao, ingawa wanajua ya kwamba Kanisa katoliki limeasisiwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo kama la lazima, wanakataa au kuingia ndani ya Kanisa au kudumu ndani yake”[40]. Hata kama Mungu, kwa njia anazozijua yeye, anaweza kufanya watu, ambao pasipo kosa lao hawajajua Injili, wakubali imani, ambayo ikikosekana haiwezekani kumpendeza[41],hata hivyo kueneza Injili ni sharti lisiloepukika la Kanisa[42],na pia ni haki yake tukufu. Kwa hiyo kazi za kimisioni hata siku hizi, kama siku zote, bado zinashika umuhimu na ulazima wake.

Kwa sababu ya kazi hizo Mwili wa fumbo wa Kristo unazikusanya na kuzielekeza bila kukoma nguvu zake ili upate kujijenga wenyewe[43].Viungo vya Kanisa vinahimizwa kuzitimiza kazi hizo kwa upendo, ambao kwao [wenyewe wakristo] wanampenda Mungu na wanatamani kuwashirikisha watu wote katika mema ya rohoni ya maisha ya hapa duniani na ya yale yajayo.

Hatimaye, kwa sababu ya kazi hizo za kimisioni, Mungu hutukuzwa kikamilifu, wakati wanadamu wanapokubali kwa akili na moyo wote tendo lake la wokovu, alilolitimiza katika Kristo. Hivyo, kwa tendo hilo unatimizwa mpango wa Mungu, ambao Kristo alijiweka wakfu kwa moyo wa utii na wa upendo, kwa ajili ya utukufu wa Mungu Baba aliyemtuma[44].Mpango huo ni kuwafanya wanadamu wote wawe taifa moja na la Mungu, wakusanyike katika mwili mmoja wa Kristo, wajengwe katika hekalu moja la Roho Mtakatifu. Hayo yote, pamoja na kuhusiana na maafikiano ya kidugu, hujibu shauku ya moyoni ya kila mtu. Kwa hiyo linatimizwa kwelikweli azimio la Muumba wetu, aliyemwumba mtu kwa mfano na sura yake, pale ambapo wote wanaoshiriki huluka ya kibinadamu, wakiisha kuzaliwa upya katika Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu, wanapoweza kusema, wakiutazama kwa moyo mmoja utukufu wa Mungu: “Baba yetu”[45].

Kazi za kimisioni katika maisha na historia ya wanadamu

8. Kazi za kimisioni zinahusiana sana na huluka ya kibinadamu na matarajio yake pia. Kwa maana, katika kumtangaza Kristo, Kanisa linawafunulia watu ukweli halisi kuhusu hali yao na wito wao kamili, kwa sababu Kristo ndiye chanzo na kielelezo cha utu huu uliofanywa mpya, uliopenywa na upendo wa kidugu, na unyofu wa moyo, na roho ya amani, [utu mpya] ambao wote wautamani sana. Kristo na Kanisa, ambalo linamshuhudia yeye kwa njia ya kuhubiri Injili, hupita upeo wa ukabila au wa utaifa, na hivyo hawawezi kuonekana kama wageni kwa yeyote wala popote[46]. Kristo mwenyewe ni ukweli na njia anayedhihirishwa kwa wote kwa njia ya mahubiri ya Injili, hasa wanapoambiwa maneno ya Kristo mwenyewe: “Tubuni na kuiamini Injili” (Mk 1:15). Na kwa vile asiyeamini amekwisha kuhukumiwa[47],maneno ya Kristo ni maneno ya hukumu na ya neema, ya kifo na uzima sawia. Maana, kwa kuyafisha tu yale yote yaliyo kuukuu, tunaweza kuingia katika upya wa maisha: hilo nalo ni la kweli kwanza kwa watu, lakini pia kwa mali zozote za ulimwengu huu, ambazo zimetiwa chapa ya dhambi ya binadamu, na pia ya baraka ya Mungu: “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Rum 3:23). Mtu awaye yote hawezi kwa nguvu zake binafsi kujikomboa na dhambi, na kuinuka, wala kujiokoa na udhaifu wake, na upweke wake, wala na utumwa wake[48], lakini wote wamhitaji Kristo, aliye kielelezo, mwalimu, mkombozi, mwokozi, na mwenye kutia uzima. Kwa kweli katika historia – hata ya kidunia – ya wanadamu, Injili ilikuwa kama chachu kwa ajili ya uhuru na maendeleo, na daima huendelea kuwa chachu kwa ajili ya udugu, umoja na amani. Hivyo basi, kwa haki Kristo huheshimiwa na waamini kama “matumaini ya Mataifa na Mkombozi wao”[49].

Maana ya kieskatolojia ya kazi za kimisioni

9. Kipindi cha kutenda kazi za kimisioni ni kati ya ujio wa kwanza na wa pili wa [Kristo] Bwana, ambapo Kanisa, mithili ya mavuno, litakusanyika toka pepo nne katika ufalme wa Mungu[50]. Maana kabla ya ujio wa pili wa Kristo, sharti Injili ihubiriwe katika mataifa yote[51].

Kazi za kimisioni si kitu kingine au zaidi ya kufunua, yaani kudhihirisha na kuutimiliza mpango wa Mungu katika ulimwengu na katika historia yake; hapo ambapo Mungu, kwa njia ya misioni, hutimiza waziwazi historia ya wokovu. Kwa njia ya kuhubiri neno na kuadhimisha sakramenti ambazo kiini na kilele chake ni Ekaristi Takatifu, utendaji huo unaleta uwepo wa Kristo mwenye kutenda wokovu. Hizo kazi zinasafisha matope ya uovu katika yale yote ya kweli na ya neema yapatikanayo katika mataifa, mfano wa kuwepo kisiri kwa Mungu, na kuyarudisha kwa Kristo, muumba wake, yeye anayepindua utawala wa shetani na kufukuza maovu ya dhambi yaliyo ya namna nyingi. Kwa hiyo “mbegu za mema yote yaliyomo moyoni na rohoni mwa wanadamu, desturi na tamaduni za mataifa mbalimbali zisipotee, bali ziponywe, ziinuliwe, na kukamilishwa kwa utukufu wa Mungu kwa kumwaibisha shetani na kwa kuwapatia watu heri yao”[52]. Hivyo, kazi za kimisioni zinaelekea utimilifu wa wakati wa mwisho (plenitudinem eschatologicam)[53]. Maana kwa njia yake, kufuatana na nyakati na majira Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe[54],Taifa la Mungu laongezeka, hilo taifa ambalo nabii alitabiria: “Panua mahali pa hema yako, wayatandaze mapazia ya maskani yake; usiwakataze” (Isa 54:2)[55]; tena Mwili wa fumbo hujengwa hata kufika kwenye cheo cha kimo cha ukamilifu wa Kristo[56],na Hekalu la kiroho, ambamo Mungu huabudiwa katika roho na kweli[57],linakua na kujengwa “juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni” (Efe 2:20).

Sura ya Pili

KAZI ZENYEWE ZA KIMISIONI

Utangulizi

10. Kanisa, ambalo limetumwa na Kristo ili kuwaonyesha na kuwashirikisha watu wote na mataifa yote upendo wa Mungu, linatambua kwamba kazi ya kimisioni ambayo inalibakia ya kufanya ni kubwa mno. Maana bilioni mbili za watu – na idadi yao huzidi kukua siku hadi siku – hawajasikia kamwe habari za Injili ama wamezisikia kidogo tu. Hawa wameunganika katika makundi makubwa mbalimbali kulingana na viungo imara vya kiutamaduni au na mapokeo ya dini za jadi au na mahusiano thabiti ya kijamii. Miongoni mwao, wapo wengine ambao wanafuata mojawapo ya dini kuu, na wengine ambao hawana habari yoyote juu ya Mungu, wengine ambao wanakanusha waziwazi uwepo wake, na mara nyingine hata wanaupinga. Ili kuweza kuwatolea watu wote fumbo la wokovu na uzima ulioletwa na Mungu, Kanisa linapaswa kujiingiza katika makundi hayo yote vilevile kama Kristo mwenyewe kwa umwilisho wake alivyoungana na hali za kijamii na za kiutamaduni za watu alioishi nao.

Ibara ya kwanza

USHUHUDA WA KIKRISTO

Ushuhuda wa maisha na dialogia

11. Kanisa hupaswa kuwepo katika makundi hayo ya watu kwa njia ya wanawe, waishio kati yao ama wanaotumwa kwao. Maana Wakristo wote, popote waishipo, wanapaswa kuonyesha kwa mfano wa maisha na kwa ushuhuda wa neno ule utu mpya ambao wameuvaa katika ubatizo, na ule uwezo wa Roho Mtakatifu, ambaye katika kipaimara wameimarishwa kwake, na hivyo watu wengine, waonapo matendo yao mema, wamtukuze Baba[58], na watambue kwa ukamilifu zaidi maana halisi ya maisha ya kibinadamu, na ya kifungo cha ushirikiano kati ya wanadamu wote.

Ili kutoa ushuhuda wa Kristo uletao matunda, wana wa Kanisa wahusiane na watu wote kwa heshima na upendo, na wajitambue kuwa viungo vya jamii ile ambamo wanaishi; na, kwa njia za shughuli na mambo ya maisha ya kibinadamu, washiriki katika maisha ya kiutamaduni na ya kijamii. Tena wazijue vizuri mila zao za kitaifa na za kidini; wazipekuepekue ili kuzigundua kwa furaha na heshima zile mbegu za Neno [la Mungu] zilizofichama ndani yake. Inawapasa pia kutazama kwa makini mabadiliko makubwa yanayotukia kati ya mataifa, na wafanye bidii ili wanadamu, ambao siku hizi mara nyingi wanashikwa mno na mambo ya kisayansi na ya kiteknolojia ya ulimwengu wa leo, wasiwekwe mbali na mambo ya kimungu, bali waamshwe kwa hamu motomoto ya ukweli na ya upendo uliofunuliwa na Mungu. Kama vile Kristo alivyochunguza mioyo ya watu, akawaongoza mpaka nuru ya kimungu, kwa njia ya mazungumzo ya kibinadamu kwelikweli, vivyo hivyo wafuasi wake, hali wamejazwa ndani yake na Roho wa Kristo, lazima wawafahamu watu ambao wanaishi kati yao na kuwa na uhusiano nao, ili kwa njia ya dialogia ya kweli na yenye subira wapate kujua utajiri gani Mungu mkarimu aliwajalia mataifa. Wakati huohuo inawapasa waamini kujaribu kuumulika utajiri huo kwa nuru ya kiinjili, na pia kuuokoa na kuurejesha kwa utawala wa Mungu Mwokozi.

Maana ya upendo wa kikristo

12. Uwepo wa wakristo katika makundi ya kibinadamu unabidi utiliwe moyo na upendo ule ambao Mungu alitupenda, Yeye ambaye ataka sisi nasi tupendane kwa upendo huohuo[59]. Kwa kweli upendo wa kikristo unaenea kuwafikia watu wote bila ubaguzi wowote wa ukabila, cheo, au dini: haungojei faida wala shukrani. Kama vile Mungu alivyotupenda kwa upendo wa bure, vivyo hivyo waamini kwa upande wao wajishughulishe kwa ajili ya binadamu, huku wakimpenda kwa moyo uleule ambao Mungu alimtafuta binadamu. Kama vile Kristo alivyokuwa anazunguka miji yote na vijiji akiponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina, kielelezo cha kwamba Ufalme wa Mungu umefika[60], vivyo hivyo Kanisa kwa njia ya wanawe huungana na watu wa cheo chochote, lakini hasa na maskini na wanaoteseka na kujishughulisha kwa furaha kwa ajili yao[61].Maana, Kanisa lenyewe hushiriki furaha zao na mateso yao, hufahamu matarajio na mafumbo ya maisha, huteseka pamoja nao katika uchungu wa mauti. Kwa wale watafutao amani, Kanisa linatamani kuwaitikia kwa dialogia ya kidugu, na kuwapelekea amani na mwanga wa Injili.

Wakristo wafanye bidii na washirikiane na wengine wote katika kuratibisha kwa haki mambo ya kiuchumi na ya kijamii. Wajitie kwa juhudi mahususi katika malezi ya watoto na vijana katika shule za aina mbalimbali, ambazo lazima zisitazamwe tu kama chombo bora cha kumlea na kumkuza kijana mkristo, lakini zitambulike pia kama huduma yenye maana kubwa sana kwa watu wote, hasa katika nchi zinazoendelea, kwa ajili ya kukuza hadhi ya binadamu na kutayarisha mazingira yanayolingana zaidi na heshima ya binadamu. Aidha, washike nafasi yao katika jitihada za watu wale, ambao kwa kupiga vita dhidi ya njaa, ujinga na maradhi wanajitahidi kubuni hali za maisha zilizo bora, na kusimika amani ulimwenguni. Waamini watamani kushiriki kwa busara katika shughuli hizo zianzishwazo na taasisi za kibinafsi au za kiserikali, na serikali yenyewe, na vyama vya kimataifa, na jumuiya mbalimbali za kikristo au pia na dini nyinginezo.

Walakini Kanisa halitaki hata kidogo kujipenyeza katika uongozi wa jamii ya kidunia. Lenyewe ladai kwake mamlaka ile tu ya kuwatumikia watu wote katika upendo na uaminifu, kwa msaada wa Mungu[62].

Wafuasi wa Kristo, hali wanashirikiana na watu wote kwa njia ya maisha na ya kazi watumaini kuwatolea ushuhuda halisi wa Kristo na kufanya kazi kwa ajili ya wokovu wao, hata pale wasipoweza kumhubiri waziwazi Kristo. Maana hawatafuti maendeleo na ustawi wa kugusika tu, bali wasisimua heshima ya watu na muungano wa kidugu kati yao. Na hivyo kwa kuzifundisha kweli za kidini na za kimaadili, ambazo Kristo alizifafanua kwa nuru yake, waendelea kufungua hatua kwa hatua njia ya kumkaribia Mungu kikamilifu zaidi. Hivyo wanadamu husaidiwa kuufikiria wokovu kwa njia ya upendo kwa Mungu na kwa jirani, na linaanza kung’ara fumbo la Kristo, ambalo ndani yake utu mpya umeonekana, ulioumbwa kwa namna ya Mungu[63],na ambamo upendo wa Mungu hufumbuka.

Ibara ya pili

KUHUBIRIWA KWA INJILI NA KUKUSANYIKA KWA 

TAIFA LA MUNGU

Uenezaji wa Injili na toba

13. Popote pale Mungu anapofungua mlango kwa neno ili kutangaza fumbo la Kristo[64], [papo hapo] anapaswa kuhubiriwa[65] kwa ujasiri na ushujaa[66]mbele ya watu wote[67], Mungu aliye hai na yule aliyemtuma kwa ajili ya wokovu wa wote, yaani Yesu Kristo[68]. [Nalo lafanyika] ili wasio Wakristo, ambao mioyo yao itafunguliwa na Roho Mtakatifu[69],wapate kuamini na hivyo wamwongokee kwa hiari Bwana na waambatane naye kwa unyofu, ambaye, kwa vile ni “njia na kweli na uzima” (Yn 14:6), hushibisha taraja zote za rohoni, naam, huzipita upeo.

Bila shaka wongofu huo ndio chanzo tu; hata hivyo hutosha kwa kufanya mwanadamu atambue kwamba kwa kunyakuliwa kutoka kwenye dhambi, anaingizwa katika fumbo la upendo wa Mungu, ambaye humwalika kufunga uhusiano naye katika Kristo. Kwa maana, kutokana na neema ya Mungu, kila mwongofu mpya hufunga safari ya kiroho, na papo hapo, kwa kushiriki tayari kwa imani fumbo la Kifo na Ufufuko, hugeuka kutoka utu wa zamani katika utu mpya unaopata ukamilifu wake katika Kristo[70].Geuko hilo, linalosababisha mabadiliko ya fikara na ya mwenendo zaidi na zaidi, halina budi kujidhihirisha katika matokeo ya kijamii na kuendelea hatua kwa hatua katika kipindi cha ukatekumeni. Na kwa vile Bwana tunayemwamini ni ishara itakayonenewa[71],mara nyingi inatokea kwamba aliyeongoka hupatwa na taabu na utengano, lakini pia na furaha ambazo Mungu hutolea bila kipimo[72].

Kanisa linakataza vikali mtu yeyote asishurutishwe wala asishawishiwe au kuvutwa kwa hila zisizofaa kukumbatia imani. Vivyo hivyo linadai kwa nguvu haki ya kwamba asiwepo yeyote anayeweza kuzuiliwa kwa udhalimu asifuate dini[73]

Kulingana na desturi za Kanisa zilivyo tangu zamani, sababu za wongofu zichunguzwe, na ikiwa lazima, zisahihishwe.

Ukatekumeni na uingizaji katika ukristo

14. Wale ambao kwa njia ya Kanisa wamepokea kutoka kwa Mungu imani katika Kristo[74]wanaruhusiwa kuingia hali ya ukatekumeni kwa njia ya ibada za kiliturujia. Ukatekumeni sio tu kuelezwa mafundisho makuu (dogma) na amri, bali ni kulelewa katika maisha yote ya kikristo, na ni kipindi kirefu cha kutosha cha uanafunzi, ambacho wanafunzi wanajiunga na Kristo Mwalimu wao. Kwa hiyo, wakatekumeni lazima waelezwe na kufunzwa – kwa jinsi ya kufaa – fumbo la wokovu na wazoeshwe maadili ya kiinjili. Kwa ibada takatifu zitakazoadhimishwa kwa kufuatana na vipindi mbalimbali[75],waingizwe katika maisha ya imani, ya liturujia na ya upendo ya Taifa la Mungu.

Baadaye, hali wameopolewa kutoka katika nguvu za giza[76] kwa njia ya sakramenti za unyago wa kikristo (initiationis christianae sacramenta), [yaani] wamekufa na kuzikwa na kufufuliwa pamoja na Kristo[77], hupokea Roho[78]wa kufanywa wana, na kuadhimisha ukumbusho wa kifo na ufufuko wake Bwana pamoja na Taifa zima la Mungu.

Marekebisho ya liturujia ya vipindi vya Kwaresima na Pasaka yanatazamiwa sana, ili mioyo ya wakatekumeni ipate kuandaliwa kwa adhimisho la Fumbo la Pasaka, ambapo wenyewe hupata kuzaliwa kwa mara ya pili katika Kristo kwa njia ya ubatizo, katika sikukuu hizo.

Kuingizwa kwa watu katika ukristo kipindi cha ukatekumeni si jambo linalowahusu makatekista na mapadre tu, bali jumuiya nzima ya waamini, na kwa namna ya pekee wasimamizi, kiasi kwamba tokea mwanzo kabisa wakatekumeni wajisikie kuwa katika Taifa la Mungu. Kwa kuwa maisha ya Kanisa ni maisha ya kitume, wakatekumeni yawapasa pia wajifunze kushiriki kwa ari katika kueneza Injili kwa kulijenga Kanisa kwa ushuhuda wa maisha yao na kwa kuungama imani yao.

Kisha, hadhi ya kisheria ya wakatekumeni ifafanuliwe waziwazi katika sheriakanuni (Codice) mpya ya Kanisa. Maana wenyewe wamekwisha unganika na Kanisa[79],tayari ni watu wa jamaa ya Kristo[80],na mara nyingi wanaishi tayari maisha ya imani, matumaini na mapendo.

Ibara ya tatu

KUJENGWA KWA JUMUIYA YA KIKRISTO

Utangulizi

15. Roho Mtakatifu ambaye, kwa mbegu ya Neno na mahubiri ya Injili, anawaita watu wote kwa Kristo na kuamsha katika mioyo yao utii wa imani, anapowazalisha tumboni mwa kisima cha Ubatizo wanaomwamini Kristo ili waanze maisha mapya, anawakusanya katika taifa pekee la Mungu, ambalo ndilo “mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu” (1Pet 2:9)[81].

Kwa hiyo, wamisionari, wafanya kazi pamoja na Mungu[82], wastawishe jumuiya za waamini, ambazo, kwa kuenenda kama unavyostahili wito wao walioitiwa[83], zitimilize huduma za kikuhani, kinabii na kifalme walizokabidhiwa na Mungu. Hivyo, jumuiya ya kikristo inakuwa ishara ya uwepo wake Mungu ulimwenguni, kwa maana, katika [maadhimisho ya] sadaka ya Ekaristi hujitolea kwa Baba daima pamoja na Kristo[84],hujilisha kwa makini na Neno la Mungu[85]na kumshuhudia Kristo[86], huenenda katika upendo na kujaa moyo wa kitume[87].

Aidha, jumuiya ya kikristo lazima iundwe tangu mwanzo wake namna hii, yaani iweze kujitegemea katika mahitaji yake, kadiri iwezekanavyo.

Kundi la waamini la namna hiyo, litunzalo urithi wa utamaduni wa taifa lake, lapaswa kujipenyeza sana kati ya watu: familia zenye roho ya kiinjili[88] zichipuke, na zipate kuimarishwa na shule zinazofaa; viundwe vyama na taasisi ambavyo kwavyo utume wa walei upate kupenyeza roho ya kiinjili katika jamii nzima. Mwisho, upendo ung’ae kati ya wakatoliki wa ibada mbalimbali[89].

Pia roho ya kiekumeni ikuzwe kati ya waamini wapya: hao watambue kwa haki kwamba ndugu wanaomwamini Kristo ni wafuasi wa Kristo, waliozaliwa upya katika ubatizo na washirika pamoja nao katika mema mengi ya Taifa la Mungu. Kulingana na hali ya kidini zinavyoruhusu, jitihada ya ekumeni ihamasishwe, kusudi wakatoliki, huku wakiondoa kila aina ya kutojali na ya vurugu, na pia kila mashindano yasiyo na busara, wapate kufanya kazi kidugu pamoja na ndugu waliojitenga, kufuatana na kanuni za hati juu ya Ekumeni. Hilo litatimizwa kiasi kiwezekanacho, kwa kukiri imani moja kwa Mungu na kwa Yesu Kristo mbele ya mataifa, na kwa kushirikiana katika nyanja za kiufundi na kijamii, kidini, na kitamaduni. Hasa wafanye kazi pamoja kwa ajili ya Kristo, Bwana wa hao wote: Jina lake liwaunganishe! Ushirikiano huo uwepo sio kati ya watu binafsi tu, bali kati ya Makanisa ama jumuiya za kikanisa na matendo yao, kufuatana na uamuzi wa Askofu wa mahali.

Waamini, hali wamekusanyika katika Kanisa kutoka kwa mataifa yote, “hawatengani na wanadamu wengine wala kwa dola, kwa lugha, wala kwa taasisi za kisiasa”[90];kwa hiyo inawapasa kuishi kwa Mungu na kwa Kristo, wakifuata desturi zilizo safi za umma wao. Kama raia wema, inawapasa kushika kweli kwa vitendo pendo kwa nchi yao; walakini wajiepushe na kila namna ya ubaguzi na ya utaifa upitao kiasi, hivyo wachochee upendo kati ya watu wote ulimwenguni.

Ili kufuatilia malengo hayo, walei, yaani waamini ambao, hali wameunganika na Kristo kwa ubatizo, huishi katika ulimwengu, wanashika nafasi muhimu sana na wanastahili mitazamo mahususi. Maana, ni juu yao waliopenywa na Roho wa Kristo, mfano wa chachu, kutia moyo kwa ndani na kuyaelekeza mambo ya kidunia ili daima yalenge mapenzi ya Kristo[91].

Walakini haitoshi watu wa wakristo wawepo na kupata nafasi miongoni mwa taifa fulani, wala haitoshi watende kazi ya kitume kwa njia ya vielelezo; hao wakristo wapo na husimikwa ili wamtangaze Kristo kwa njia ya maneno na matendo mbele ya raia wenzao wasio wakristo, na pia ili wawasaidie kumpokea kikamilifu Kristo.

Kwa kusudi la kupandikiza Kanisa na kustawisha jumuiya ya kikristo, basi, zinahitajika huduma za aina mbalimbali, ambazo, mara tu zinapooteshwa na wito wa Mungu katika mkusanyiko wa waamini, wote wapaswa kuzikuza na kuzisitawisha. Kati ya huduma hizo zipo nyadhifa za upadre, ushemasi na ukatekista, na chama cha Aksio Katoliki. Kadhalika watawa wa kiume na wa kike wanashika nafasi ya lazima kwa kupandikiza na kuimarisha Ufalme wa Kristo katika mioyo ya watu, na pia kuueneza zaidi kwa njia ya sala na juhudi za kimatendo.

Wakleri wazalendo

16. Kwa furaha kubwa Kanisa hutoa shukrani kwa ajili ya karama isiyokadirika ya wito wa upadre, ambao Mungu aliwajalia vijana wengi miongoni mwa mataifa yaliyomwongokea Kristo hivi karibuni. Maana Kanisa linatia mizizi imara zaidi katika kundi liwalo lote la kibinadamu pale ambapo jumuiya za waamini hutwaa kati ya wanajumuiya wake wahudumu wa wokovu katika Daraja ya Maaskofu, ya Mapadre na ya Mashemasi, wanaowatumikia wenzao, ili kusudi Makanisa machanga yajipatie kwa utaratibu muundo wa jimbo lenye wakleri wake wenyewe.

Yale yote yaliyothibitishwa na Mtaguso Mkuu kuhusu wito na malezi ya upadre, yafuatiliwe kwa heshima popote pale Kanisa linapopandwa kwa mara ya kwanza na katika Makanisa machanga. Yatunzwe kwa bidii sana yaliyotamkwa juu ya malezi ya kiroho yanayopaswa kuunganika sana na yale ya kimafundisho na ya kichungaji, pia juu ya mwenendo wa maisha yanayoongozana na Injili pasipo kutafuta faida ya ubinafsi au ya kifamilia; na hatima, juu ya kutambua maana ya ndani ya fumbo la Kanisa. Kutokana na hayo yote mapadre watajifunza kwa namna tukufu, kujitolea kabisa kwa kuhudumia mwili wa Kristo, na kwa kazi ya kiinjili; na pia kuambatana na askofu wao kama washirika waaminifu, na kuwasaidia mapadre wenzao[92]

Ili kufikia lengo hilo kubwa, malezi yote ya waseminari, lazima yapangwe katika nuru ya fumbo la wokovu, lilivyodhihirishwa katika Maandiko Matakatifu. Hao wenyewe wagundue na kuliishi fumbo hilo la Kristo na la wokovu kwa wanadamu lililomo katika liturujia[93].

Hayo madai ya msingi ya malezi ya kipadre, pia ya kichungaji na ya kimatendo, kadiri ya kanuni za Mtaguso[94],inabidi yaendane na hamu ya kufuatilia tabia pekee ya kufikiri na ya kutenda ya wazawa wenzao (propriae gentis). Kwa hiyo, akili za waseminari zifunuliwe na kuerevushwa, wapate kutambua vizuri na kuthamini utamaduni wa nchi yao. Katika masomo ya kifalsafa na ya kiteolojia wachunguze mahusiano yawezayo kuwemo kati ya utamaduni na dini za kitaifa na dini ya kikristo[95].Hali kadhalika katika malezi ya kipadre yakumbukwe mahitaji ya kichungaji ya eneo lile: waseminari wajifunze historia, malengo na mitindo ya kazi za kimisioni za Kanisa, na tena mazingira mahususi ya kijamii, ya kiuchumi na ya kitamaduni ya taifa lao. Aidha, wafundishwe katika roho ya kiekumeni na waandaliwe kwa dialogia ya kidugu na wale wasio wakristo[96]. Hayo yote yanadai kwamba mafunzo kwa ajili ya upadre yatimizwe iwezekanavyo wakiendelea kuishi katika mazingira yao ya kawaida ya taifa lao, na kati ya jamaa zao[97].Bidii zifanyike kuwafundisha katika uendeshaji sahihi wa Kanisa, hata kwa mambo ya uchumi.

Aidha, wachaguliwe mapadre wenye uwezo ambao, baada ya kutoa kwa muda huduma ya kichungaji, watimilize masomo ya juu katika vyuo vikuu hata vikiwa vya nchi nyingine, hasa huko Roma, na katika taasisi nyinginezo za kitaaluma, kusudi, kwa njia ya elimu na ustadi wao, wapate kusaidia Makanisa machanga kama wakleri wa mahali wanaoshika hata nyadhifa za juu za Kanisa.

Baraza la Maaskofu linapoona inafaa lirudishe Daraja takatifu ya ushemasi wa kudumu, kufuatana na mwongozo wa “Hati juu ya Kanisa”[98].Maana ni bora wanaume wanaofanya kazi ya huduma kweli ya kishemasi, ama kwa kuwa makatekista wanahubiri Neno la Mungu, ama kwa sababu wanaongoza kwa niaba ya paroko au ya askofu jumuiya za kikristo zilizo mbali, ama kwa kuwa wanajishughulisha kwa upendo katika kazi za maendeleo ya kijamii au za hisani, wapate kuimarishwa kwa njia ya kuwekewa mikono, kwa mfululizo wa urithi wa kitume, na hivyo wakihusiana kwa nguvu kubwa zaidi na altare, waweze kutekeleza kwa faida zaidi huduma zao kwa nguvu ya neema ya kisakramenti ya ushemasi.

Malezi ya makatekista

17. Makatekista waume kwa wake, hustahili sifa kweli kwa kazi ya kimisioni kati ya mataifa. Kwani wakiongozwa na roho ya kitume, wanasaidia kwa namna ya pekee na ya lazima katika uenezaji wa imani na wa Kanisa, kwa jitihada zao kubwa.

Katika nyakati zetu, ambapo makleri ni wachache sana wa kuhubiri Injili kwa watu wengi hivi, na kuzitenda kazi za kichungaji, wajibu wa makatekista ni wa maana kubwa sana. Kwa hiyo malezi yao lazima yawe kamili, tena yapatane na maendeleo ya elimu, ili waweze kutimiza shughuli zao kama wasaidizi wa mapadre vema iwezekanavyo, hata ikiwa wajibu wao umeongezewa na mizigo mipya.

Inafaa iongezwe idadi ya vyuo vya kijimbo na vya kimajimbo, ambamo wanaotarajia kuwa makatekista wajifunze mafundisho ya kikatoliki, hasa juu ya Biblia na ya Liturujia, na pia mitindo ya katekesi na utendaji wa kichungaji, tena wapate malezi ya kimaadili ya kikristo[99],pamoja na kujitahidi bila kukoma kusitawisha utauwa na utakatifu wa maisha. Semina na kozi zifanyike katika nafasi maalum ili kuwaweka kisasa makatekista katika masomo na taaluma zinazofaa kwa huduma watoayo, na tena ili kulisha na kuimarisha maisha yao ya kiroho. Aidha, wale waliojitolea kabisa kwa kazi hiyo lazima wadhaminiwe namna ya kuishi kwa heshima, pamoja na usalama katika jamii kwa ujira wa haki[100].

Ni vema kwamba, kwa upande wa malezi na posho ya makatekista, shughuli zifanyike kwa misaada hususa ya Idara ya Kipapa ya kueneza imani (Propaganda Fide). Ikiwa inaonekana kuwa jambo la lazima, basi iundwe taasisi kwa ajili ya makatekista.

Aidha Makanisa yatambue kwa moyo wa shukrani kazi njema inayotendwa na makatekista wasaidizi, ambao msaada wao yanauhitaji sana. Wao katika jumuiya zao wanaongoza sala na kufundisha dini. Malezi yao, ya kielimu na ya kiroho, yashughulikiwe ifaavyo. Tena inatarajiwa kwamba makatekista waliopata malezi mazuri, kila ionekanapo panafaa, wapewe rasmi utume wa kikanisa katika adhimisho la liturujia, ili wawe watumishi wa imani wenye madaraka makubwa zaidi kati ya jumuiya.

Kuhamasisha maisha ya kitawa

18. Maisha ya kitawa ni bora yahamasishwe tangu awali ya kuanzisha Kanisa jipya, kwa sababu hayatoi tu misaada yenye thamani na ya lazima, kwa kazi za kimisioni, bali, kwa njia ya kujiweka wakfu na moyo wote kwa Mungu, katika Kanisa, huonyesha na kueleza wazi hali halisi ya wito wa Kikristo[101].

Mashirika ya kitawa yanayofanya kazi kwa uanzishaji wa Kanisa, kwa vile yana hazina za kifumbo ndani yake, yaani utajiri wa mapokeo ya kidini ya Kanisa, yajitahidi kuzifunua na kuzitoa kufuatana na sanaa na tabia ya kila taifa. Aidha, wakadirie kwa makini jinsi gani mapokeo ya kiwalii na ya kitaamuli, ambayo Mungu, pengine hata kabla ya kuhubiriwa Injili, ameingiza katika tamaduni za awali, yanaweza kuchukuliwa kwa ajili ya maisha ya kitawa ya kikristo.

Katika makanisa machanga inabidi zisitawishwe aina mbalimbali za maisha ya kitawa, ili [mashirika] yaweze kutoa mifano mbalimbali ya utume wa Kristo na ya maisha ya Kanisa, kujitolea kwa kazi mbalimbali za kichungaji na kuwaandaa wanashirika wao watimize vema kazi zile. Lakini Maaskofu katika Baraza lao waangalie yasizidishwe mashirika yenye nia ileile ya kitume, ili yasilete hasara yoyote kwa maisha ya kitawa na kwa utume [wake].

Juhudi mbalimbali za kuanzisha maisha ya kitawa ya kitaamuli zinastahili sifa ya pekee. Kwa njia yake, kwa upande mmoja mapokeo yenye thamani kubwa ya shirika fulani yanapandikizwa, huku zikidumisha desturi za msingi za kanuni ya kimonaki; au, kwa upande mwingine, mitindo iliyo sahili (simpliciores) ya umonaki wa asili inarejewa. Kwa vyovyote mashirika yote yafanye bidii kutafuta utamadunisho wa kweli kulingana na mazingira ya mahali. Kwa kuwa maisha ya utawa wa kitaamuli yanahusu ukamilifu wa uwepo wa Kanisa, inabidi yaoteshwe popote katika Makanisa machanga.

Sura ya Tatu

MAKANISA FARIDI

Maendeleo ya Makanisa machanga

19. Kazi ya kupandikiza Kanisa kati ya jamii fulani ya watu hufikia kiwango cha kuridhisha, pale ambapo jumuiya ya waamini, ikijipenyeza tayari katika maisha ya kijamii na kulingana kwa namna fulani na utamaduni wa mahali, inapofurahia uthabiti na udumifu: yaani ilipo na kundi la makasisi, watawa na walei wake, hata kama ni wachache, na hivyo inaponufaika na huduma na taasisi zinazohitajika ili watu wa taifa la Mungu, chini ya uongozi wa Askofu wake mwenyewe, wapate kuongoza na kustawisha maisha yake.

Katika Makanisa hayo machanga, maisha ya Taifa la Mungu lazima yakomae katika nyanja zote za maisha ya kikristo yanayotakiwa kurekebishwa kufuatana na kanuni za Mtaguso huu. Mikusanyiko ya waamini yazidi kujitambua siku kwa siku kwamba inakuwa jumuiya hai katika imani, liturujia na mapendo; na walei kwa kazi zao za kijamii na za kitume, wanajitahidi kusimika katika nchi utaratibu wa haki na mapendo; vyombo vya upashanaji habari vyatumika inavyofaa na kwa busara; familia, kwa kuishi maisha thabiti ya kikristo zinakuwa mithili ya vitalu kwa utume wa walei na kwa miito ya upadre na utawa. Kisha imani hufundishwa kwa njia ya katekesi ya kufaa, huadhimishwa katika liturujia inayolingana na tabia ya taifa, na huingizwa kwa njia ya sheria maalum ya kikanisa katika taasisi na desturi zilizo bora za mahali.

Aidha Maaskofu, kila mmoja akiunganika na mapadre wa jimbo lake, wakipenywa moyoni nia ya Kristo na ya Kanisa, wanapaswa kuhisi na kuishi pamoja na Kanisa lote zima. Ushirika kati ya Makanisa machanga na Kanisa zima udumu kuwa wa ndani; nayo Makanisa yajitahidi kuunganisha vipengere kadhaa vya mapokeo ya Kanisa zima na utamaduni wake yenyewe, ili kuuongeza kwa njia ya kuhimizana, uzima wa Mwili wa Fumbo[102]. Kwa hiyo zichochewe sehemu zile za kiteolojia, na kisaikolojia, na za kiutu ambazo huonekana kuwa zinasaidia kukuza moyo huo wa ushirikiano na Kanisa zima.

Makanisa hayo, ambayo mengi yapo katika nchi zilizo maskini zaidi duniani, yanataabika bado na uhaba wa mapadre na wa zana za kidunia. Kwa sababu hiyo, sharti kazi za kimisioni za Kanisa zima ziendelee bila kukoma kuyatolea misaada ile inayohitajika kwa kusitawisha Kanisa mahalia na kwa maendeleo ya maisha ya kikristo. Hizo kazi za kimisioni ziyaelekee vilevile Makanisa ambayo, ingawa ni ya muda mrefu, yapo katika hali ya kurudi nyuma au ya udhaifu.

Hata hivyo, Makanisa hayo yanapaswa kukazana kupanga kazi za kichungaji za kawaida na pia vitendo ambavyo kwa njia yake miito katika upadre wa kijimbo na katika mashirika ya kitawa izidi kwa idadi, ikaguliwe kwa uhakikisho bora zaidi, na isitawishwe kwa mafanikio makubwa zaidi[103],ili Makanisa polepole yaweze kujitegemea na kuyasaidia mengine pia.

Kazi za kimisioni za Makanisa faridi

20. Kwa vile kila Kanisa faridi linapaswa kuwakilisha kikamilifu iwezekanavyo Kanisa lote zima, basi lizingatie kuwa limetumwa pia kwa wale wasiomwamini Kristo na wanaoishi katika eneo lake lilelile, ili lipate kuwa ishara inayowaonyesha Kristo, kwa ushuhuda wa maisha ya mwamini mmoja mmoja na ya jumuiya nzima.

Aidha, huduma ya neno haina budi kuwepo ili Injili iwafikie wote. Askofu apaswa kuwa kwanza kabisa mjumbe wa imani, ili kumletea Kristo wafuasi wapya[104].Na kwa kusudi la kutimiza vema wajibu huo bora sana, lazima afahamu kwa ndani hali za kondoo wake, na pia maoni ya moyo juu ya Mungu waliyo nayo watu wa jimbo lake, vilevile akikadiria barabara uzito wa mabadiliko yaliyoingizwa huko kwa njia ya uhamiaji, hasa uhamiaji mjini, na ya ubaridi kwa mambo ya dini.

Katika Makanisa machanga mapadre wazalendo washiriki kwa bidii katika kazi ya kuhubiri Injili. Wajiunge katika kazi hiyo na wamisionari wa ng’ambo, na hivyo wataunda pamoja nao baraza moja la mapadre (Presbyterium), linalokusanyika chini ya madaraka ya Askofu, siyo kwa ajili ya kuwachunga waamini na kuadhimisha ibada kwa Mungu tu, lakini pia kwa ajili ya kuhubiri Injili kwa wale walio nje. Wajionyeshe wako tayari, na – ikitokea fursa – wajitolee kwa moyo wote kwa Askofu wao, ili kuanzisha kazi za kimisioni katika sehemu za jimbo lao zilizo mbali zaidi na zilizo na ukiwa, na hata katika sehemu za majimbo mengine pia.

Watawa wa kiume na wa kike, pamoja na walei, wajawe na moyo huohuo kwa wananchi wao hasa kwa walio maskini zaidi.

Mabaraza ya Maaskofu mara kwa mara yaratibu kozi za usasaisho juu ya Biblia, na ya kiteolojia, na ya kiroho au ya kichungaji, kusudi makleri, mbele ya mfululizo wa mageuzi waweze kuchunguza ujuzi wa kiteolojia na ya mitindo ya kichungaji.

Kuhusu mengine, zifuatiliwe kwa makini kanuni zote zilizoidhinishwa na Mtaguso huu, hasa katika Dikrii juu ya Huduma na Maisha ya Mapadre.

Kusudi kazi hizi za kimisioni zipate kutimizwa na Kanisa faridi, wanahitajika wahudumu wa kufaa; hao lazima waandaliwe upesi na barabara kulingana na mahitaji ya kila Kanisa. Na kwa kuwa watu hupenda kuishi makundi makundi, inafaa sana Mabaraza ya Maaskofu kupanga maazimio ya pamoja, ili dialogia ianzishwe na makundi hayo. Walakini, kama mahali pengine yakipatikana makundi ya watu ambayo hukataa kushiriki imani katoliki, kwa sababu wanashindwa kulingana na umbile lile la pekee ambalo Kanisa faridi limeshika huko, bila shaka yatamanika kwamba katika hali hiyo, yote hayo yashughulikiwe kwa namna ya pekee[105],hata Wakristo wote wapate fursa ya kukusanyika katika jumuiya moja tu. Ikiwa Kiti cha Kitume kinao wamisionari wenye kufaa kwa kazi hizo, basi, kila Askofu awaite katika Jimbo lake ama awapokee kwa mikono miwili na pia ahamasishe shughuli zao.

Ili moyo huo wa kimisionari uchanue kati ya wananchi inabidi Makanisa machanga yashiriki mapema iwezekanavyo kimatendo katika utume wa Kanisa wa popote ulimwenguni. Nayo yatume wamisionari kuhubiri Injili pote, hata kama yenyewe yangali yana uhaba wa makleri. Ushirika wao wa Kanisa zima la ulimwengu utakuwa kwa namna fulani umekamilika wakati tu yanapokuwa yenyewe yanashiriki kwa vitendo katika juhudi ya kimisionari kwa kwenda katika nchi nyinginezo.

Kuhamasisha utume wa walei

21. Kanisa halijaimarika kweli, haliishi kikamilifu, wala kuwa alama kamili ya uwepo wa Kristo kati ya wanadamu iwapo halijawa na walei hodari waendao bega kwa bega na hierarkia katika shughuli mbalimbali. Maana Injili haiwezi kupenya mpaka ndani katika fikra, maisha na kazi za taifa lolote lile, wakikosekana walei watendaji. Ndiyo sababu, tangu wakati wa kuanzisha Kanisa jipya lazima kufanya bidii ili kuwaandaa walei waliokomaa katika ukristo.

Walei huhusiana kikamilifu na Taifa la Mungu sawia na jamii ya wanadamu. Kwanza ni wananchi wa mahali pale walipozaliwa; kwa njia ya elimu huanza kushiriki urithi wa utamaduni wake; huunganika na maisha yake kwa mahusiano mbalimbali ya kijamii; hutoa mchango wao kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao, kwa njia ya ufundi wao; husikia matatizo yake kama ni yao wenyewe, na kufanya bidii kuyatatua. [Haohao] huhusiana pia na Kristo, kwa vile walivyohuishwa mara ya pili katika Kanisa kwa imani na ubatizo, ili, hali wamefanywa wapya katika uzima na katika utendaji, wawe wa Kristo[106],na katika Kristo “vitu vyote vitiishwe chini yake Mungu, ili kwamba Mungu awe yote katika wote”[107].

Wajibu wao wa kwanza, waume kwa wake, ni kumshuhudia Kristo kwa maisha na maneno yao, katika familia, kati ya watu wa tabaka lao, na katika mazingira ya kazi wanayoifanya. Ndani yao inabidi uonekane ule “utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli[108]”. Haya maisha mapya lazima wayaonyeshe ndani ya jamii na utamaduni wa watu wao, kulingana na mapokeo ya kitaifa. Wenyewe wanapaswa kujua sana utamaduni huo, kuusahihisha na kuuhifadhi, kuusitawisha kulingana na hali mpya [ya kikanisa], na hatimaye kuukamilisha katika Kristo ili imani ya Kristo na maisha ya Kanisa yasiwe tena mambo ya kigeni kwa jamii ambamo wanaishi, bali yaanze kuipenya na kuigeuza. Walei washikamane na wananchi wenzao kwa upendo wa kweli ili katika mwenendo wao kiungo kipya cha umoja na cha mshikamano na watu wote kionekane wazi, kile wanachokichota katika fumbo la Kristo. Pia waeneze imani ya Kristo kati ya wale ambao viungo vya kimaisha au kikazi vimewaunganisha nao; na wajibu huo unakuwa wa lazima zaidi siku kwa siku, kwa sababu watu wengi sana hushindwa kusikia Injili wala kumjua Kristo isipokuwa kwa njia ya walei, wanaokuwa jirani kwao. Na zaidi, panapowezekana, walei wawe tayari – katika ushirikiano mkubwa na hierarkia – kutimiza utume maalum wa kutangaza Injili na kushirikisha mafundisho ya kikristo ili kuimarisha Kanisa changa.

Wahudumu wa Kanisa wathamini kazi za kitume zifanywazo na walei. Wawafunze ili wafahamu zaidi na zaidi wajibu na madaraka yao mbele ya watu wote, kwa vile ni viungo vya Kristo; tena, wawapatie ujuzi wa ndani wa fumbo la Kristo, wawafundishe taratibu za kimatendo, wawasaidie katika magumu, kufuatana na roho ya Konstitusio juu ya Kanisa (Lumen Gentium) na ya Dikrii juu ya Utume wa walei (Apostolicam Actuositatem).

Hapo, wakati wachungaji na walei wanaposhika wajibu na madaraka kila mmoja ya kwake, Kanisa lote changa litoe ushuhuda wa Kristo, ulio mmoja, hai, wenye nguvu, na hivyo liwe ishara ing’arayo ya wokovu unaotujia katika Kristo.

Utofauti katika umoja

22. Mbegu iliyo Neno la Mungu, ikiota katika udongo mzuri, ikimwagiliwa na umande wa kimungu, yanywa utomvu hata kuugeuza na kujilisha nao, kisha yazaa matunda mengi. Bila shaka, kama katika mpango wa kujimwilisha kwa Kristo, Makanisa hayo machanga, yaliyosimikwa katika Kristo na kujengwa juu ya misingi ya Mitume, yana uwezo unaoshangaza wa kupokea utajiri wa mataifa ambayo yametolewa kwa Kristo kuwa urithi wake[109]. Makanisa hayo huchota kutoka katika mila na desturi, katika elimu na tamaduni, katika sanaa na utaalamu wa mataifa yao, yale yote yanayofaa ili kumtukuza Muumba wetu, ili kuonyesha neema ya Mwokozi na kupanga vema maisha ya kikristo[110].

Ili kulifikia lengo hilo inabidi uhamasishwe uchunguzi wa kiteolojia katika kila jamii kubwa yenye utamaduni wake pekee. Katika mwanga wa mapokeo ya Kanisa zima matukio na maneno yaliyofunuliwa na Mungu, yaliyopokelewa katika Maandiko Matakatifu na kufafanuliwa na Mababa na Majisterio ya Kanisa, hayo yote yapate kuchunguzwa na kukaguliwa tena. Hivyo itafahamika vizuri zaidi kwa njia gani imani, bila kudharau falsafa na hekima za mataifa, inaweza kukutana na akili zao, na pia itafahamika vizuri kwa namna gani mila na desturi, mtazamo wa maisha na muundo wa jamii, hayo yote yanaweza kupatanishwa na mwenendo wa maisha unaodhihirishwa na ufunuo wa kimungu. Kwa hiyo, zitafunguliwa njia za kuyalinganisha kwa ndani na maisha ya kikristo kwa jumla. Kwa kufanya hivyo itaepwa kila namna ya mchanganyo-dini (syncretismus) na upekee usiofaa, na maisha ya kikristo yatalingana na hekima na tabia ya utamaduni uwao wote[111]. Tena mapokeo faridi pamoja na thamani za pekee za kila jamii ya wananchi, yakitiwa nuru na mwanga wa Injili yatapokelewa katika umoja wa kikatoliki. Kisha, Makanisa faridi machanga, huku yakitajirishwa na mapokeo yao, yatapata nafasi yanazostahili katika ushirika wa Kanisa, bila kudhuru urais wa Kiti cha Petro, kinachosimamia ushirika wote wa mapendo[112].

Hapo inatumainiwa, naam inafaa sana, kwamba Mabaraza ya Maaskofu, ndani ya mipaka ya kila provinsi yenye umoja wa kijamii na wa kiutamaduni, yakutane pamoja, ili kwa moyo mmoja na ushirika wa maamuzi, wapate kutekeleza mpango huo wa ulinganifu.

Sura ya Nne

WAMISIONARI

Wito wa kimisionari

23. Ingawa kila mfuasi wa Kristo[113] hupaswa kuipanda mbegu ya imani, kadiri ya nguvu zake, daima Kristo Bwana huwaita kutoka katika umati wa wafuasi wake wale anaowataka mwenyewe ili wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuwahubiria watu wote[114]. Ndiyo sababu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, agawaye karama zake apendavyo kwa kufaidiana[115],huwasha mioyoni mwa watu mmoja mmoja wito wa kimisionari, na kadhalika kuchochea uanzishaji wa Mashirika[116]ambayo huchukua ule wajibu wa uinjilishaji ulio wa Kanisa zima kama wajibu wao wenyewe.

Maana wameitwa kwa wito wa pekee wale ambao, wakipewa kipaji cha kimaumbile, na uwezo na akili, wako tayari kushika kazi za kimisioni[117], wawe ni wazalendo ama wa ng’ambo: nao huwa mapadre, watawa au walei. Wakiisha tumwa na mwenye mamlaka halali, huwaendea kwa imani na utii wale walio mbali na Kristo, na kujitenga kwa ajili ya kazi ile tu, ambayo kama wahudumu wa Injili, waliitiwa waifanye[118]“kusudi mataifa wawe sadaka yenye kibali ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu” (Rum 15:16).

Roho ya umisionari

24. Mungu anapoita, binadamu sharti amwitikie bila kufanya shauri na “watu wenye mwili na damu”[119],na kujitolea kwa moyo wote kwa kazi za Injili. Lakini haiwezekani kuitikia pasipo kuhimizwa na kupewa nguvu na Roho Mtakatifu. Maana, kila mtu anayetumwa huingia katika maisha ya utume wa yule ambaye “alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa” (Flp 2:7). Kwa hiyo lazima awe tayari kudumu kwa maisha yake yote katika wito wake, kujikana mwenyewe na kuacha vyote alivyokuwa navyo binafsi, na kujifanya hali zote kwa watu wote[120].

Mwenye kuhubiri Injili kati ya mataifa, atangaze kwa yakini fumbo la Kristo, kwamba yeye ni mjumbe wake, hivyo apate katika yeye, kila inapotakiwa, ujasiri wa kunena[121],bila kukionea aibu kikwazo cha msalaba. Akifuata mfano wa Mwalimu wake, aliye mpole na mnyenyekevu wa moyo, aonyeshe kuwa nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi[122]. Kwa kuiishi Injili kwelikweli[123], kwa uvumilivu, kwa saburi, kwa wema, na kwa upendo wa kweli[124]atoe ushuhuda kwa Bwana wake, mpaka kumwaga damu yake, ikihitajika. Yeye atamwomba Mungu amjalie wema na nguvu, kusudi atambue kwamba kwenye mang’amuzi ya mateso makali na umaskini mwingi, ndiko kwenye wingi wa furaha[125].Asadiki kuwa utii ndiyo fadhila mahususi ya mtumishi wa Kristo, ambaye kwa utii wake aliwaokoa wanadamu wote.

Wajumbe wa Injili, ili wasiache kuitumia karama iliyomo ndani yao, wafanywe upya katika roho na nia zao siku kwa siku[126]. Mara kwa mara Maaskofu na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa wawakutanishe wamisionari ili kuwatia nguvu katika tumaini la wito wao, wapate kujishughulisha kwa ari mpya katika kazi ya kitume, na nyumba maalum ziandaliwe kwa lengo hilo.

Malezi ya kiroho na ya kimaadili

25. Kila anayetarajia kuwa mmisionari atayarishwe kwa njia ya malezi ya pekee ya rohoni na ya kimaadili kwa ajili ya kazi hiyo maarufu sana[127].Lazima awe tayari kuanzisha shughuli yoyote, awe thabiti katika kuzitekeleza, mwenye kudumu katika magumu, mvumilivu na imara katika kustahimili upweke, uchovu, na kazi isiyozaa. Atawafuata watu kwa akili wazi na kwa moyo mpana; atakubali kwa hiari nyadhifa anazokabidhiwa, atajitahidi sana kujilinganisha na desturi zilizo tofauti za mataifa, na mazingira yanayobadilika; kwa itifaki ya moyo na upendano, atajitolea kushirikiana na ndugu pia na wote wanaohusika na kazi yake ileile, ili pamoja na waamini wote wawe moyo mmoja na roho moja[128], mithili ya jumuiya ya [wakati wa] kitume.

Hali ya roho ya namna hiyo isitawishwe na kuchochewa tangu wakati wa malezi, na kwa njia ya maisha ya rohoni, iinuliwe na kulishwa. Mmisionari halisi awe mtu wa sala, akisukumwa na imani hai na tumaini lisilotahayarika; awake roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi[129];ajifunze kuwa radhi na hali yoyote aliyo nayo[130];siku zote achukue katika mwili, kwa moyo wa kujihinisha, kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu ufanye kazi ndani yao aliotumwa kwao[131];katika juhudi afanyazo kwa ajili ya roho zote akubali kutapanya vitu vyote alivyo navyo, hata yeye mwenyewe, kwa ajili ya wokovu wao[132],ili “wakue katika upendo wa Mungu na wa jirani kwa kutimiza wajibu wao kila siku”[133].Hivyo, akiunganika na Kristo katika kuyatii mapenzi ya Baba, atafuliza utume wake chini ya mamlaka ya kihierarkia ya Kanisa na atashirikiana katika fumbo la wokovu.

Malezi ya kimafundisho na ya kitume

26. Watakaotumwa katika mataifa mbalimbali, kama watumishi wema wa Kristo, walishwe na “maneno ya imani na mafundisho mazuri” (1Tim 4:6) watakayochota kwanza kabisa katika Maandiko Matakatifu, wakitafakari na kuchunguza Fumbo la Kristo, na watakuwa watangazaji na mashahidi wake Yeye.

Kwa sababu hiyo wamisionari wote – mapadre, watawa wa kike na wa kiume na walei – waandaliwe kila mmoja kulingana na hadhi yake ilivyo, ili waweze kufaulu kazi walizoitiwa wazifanye[134].Malezi yao juu ya mafundisho ya dini lazima yaratibishwe tangu mwanzo wake kwa kutazama hali ya Kanisa ya kuwa la watu wote, na papo hapo hali za tofauti zilizopo kati ya mataifa. Hayo yasemwa mintarafu masomo yote yanayowasaidia kujiandaa kwa huduma, hali kadhalika kwa sayansi nyinginezo, wanazonufaika kufundishwa ili wapate ujuzi wa juu wa mambo ya mataifa, ya tamaduni na ya dini mbalimbali, siyo mintarafu mambo ya kale tu, bali pia ya kisasa. Maana, yule anayetarajia kuondoka kwenda kati ya watu wa taifa jingine hana budi kustahi sana urithi wao, lugha na mila zao. Kwanza inafaa kabisa kwamba anayetarajia kuwa mmisionari ahudhurie mafunzo ya misiolojia, yaani mafundisho na kanuni za Kanisa zihusuzo kazi za kimisioni, kujua taratibu gani wajumbe wa Injili walifuata katika mkondo wa karne, hali kadhalika kujua hali ya misioni ya wakati huu na mitindo inayodhaniwa kuwa inafaa zaidi kwa siku hizi[135].

Hata ikiwa mafunzo hayo ya jumla huhamasishwa na juhudi za kichungaji, lazima malezi maalum ya kitume yatolewe kwa utaratibu wa kinadharia na pia wa mazoezi ya kimatendo[136].

Umati mkubwa iwezekanavyo wa watawa wa kiume na wa kike uelimishwe na kuandaliwa katika katekesi, kusudi waweze kushiriki zaidi na zaidi katika kazi ya kitume.

Hali kadhalika wale wanaojitolea kwa muda kwa kazi za kimisionari, wanapaswa kupata malezi yafaayo kulingana na wadhifa wao.

Malezi ya aina hizo [ilivyoelezwa hapo juu] yakamilishwe katika nchi za misioni, ili wamisionari wapate kufahamu vizuri sana historia, miundo ya kijamii na desturi za mataifa; aidha, wachunguze mpango wa kimaadili, kanuni za kidini na fikara kuu ambazo mataifa walitunga juu ya Mungu, ulimwengu na binadamu, kutokana na mapokeo yao matukufu[137]. Wajifunze barabara lugha zao ili waweze kuzitumia kwa ufasaha na usanifu, na hivyo wakaribie kwa urahisi nia na nyoyo za watu[138]. Tena wapate mafunzo ya kufaa juu ya mahitaji ya pekee ya kichungaji.

Wengine tena, wapate mafunzo mathubuti zaidi kwenye taasisi za elimu ya misioni (Instituta Missiologica) ama kwenye vitivo au vyuo vikuu vingine, kusudi waweze kushika kwa manufaa zaidi wadhifa maalum[139],pia kwa ajili ya elimu yao waweze kuwa msaada kwa wamisionari wengine katika utekelezaji wa kazi za kitume katika misioni, ambazo hasa siku hizi, zaonyesha magumu mengi pamoja na fursa zilizo za neema. Zaidi ya hayo, inatamanika kwamba Mabaraza ya Maaskofu ya kitaifa yaweze kulitegemea kundi fulani la mabingwa wa aina hiyo wenye kutumia elimu na mang’amuzi kwa faida yao, katika mahitaji ya huduma zao. Wasikosekane mabingwa wa kutumia kiufundi vyombo vya upashanaji habari, ambavyo umuhimu wake wote wanaitwa kuuthamini.

Mashirika yafanyayo kazi katika misioni

27. Hayo yote ingawa ni ya lazima kwa awaye yote anayetumwa katika mataifa, kwa kweli ni vigumu sana yatekelezwe na kila mmoja binafsi. Kwa kuwa kazi zenyewe za kimisioni – kama mang’amuzi yanavyoshuhudia – haiwezekani zitendeke kwa juhudi ya mmoja mmoja, wale wanaoshiriki mwito uleule wanakusanyika katika Mashirika ambamo, kwa kutoa mchango wa nguvu zao, wanapata malezi yanayofaa, ili kutekeleza kazi hizo kwa niaba ya Kanisa na kwa agizo la mwenye madaraka ya kihierarkia (Askofu). Kwa karne nyingi Mashirika hayo yamestahimili taabu na hari za mchana kutwa, iwe wanashiriki kazi hiyo ya kimisioni kwa muda wao wote, ama kwa vipindi tu. Mara nyingi Kiti Kitakatifu kiliwakabidhi maeneo makubwa sana ili wahubiri Injili, na humo wakamkusanyikie Mungu watu wapya, yaani Kanisa mahalia linaloambatana na wachungaji wake. Mashirika yatayahudumia kwa bidii na ustadi Makanisa yaliyoyaanzisha kwa jasho lao, naam, kwa damu yao hasa; yatashirikiana kidugu, ama katika uangalizi wa roho za watu ama kwa kushika wadhifa maalum kwa ajili ya wema wa jumuiya yote.

Mara nyingine yatajichukulia jukumu la lazima katika eneo lote la nchi fulani, kwa mfano kuhubiri Injili kwa tabaka la pekee la watu, ama kwa jamii fulani ambayo, kwa kisa cha pekee, labda haijapokea ujumbe wa Injili, au, mpaka sasa hupingana nao[140].

Ikihitajika, Mashirika yawe tayari kuwafunza na kuwasaidia kutokana na uzoefu yalio nao, wale wanaojitolea kwa muda tu kwa kazi za kimisioni.

Kwa sababu hizo zote, na pia kwa vile watu wa kuletwa kwa Kristo bado ni wengi, Mashirika yanaendelea kuwa ya lazima kabisa.

Sura ya Tano

UTARATIBU WA KUENDESHA KAZI ZA KIMISIONI

Utangulizi

28. Wakristo, kwa kuwa wana karama zilizo mbalimbali[141], sharti washiriki kazi katika Injili, kila mmoja kadiri ya nafasi, uwezo, karama na huduma yake[142].Wote basi, wenye kupanda mbegu kwa wenye kuvuna[143],wenye kuatika kwa wenye kutia maji, lazima wawe wamoja[144],kusudi “wakielekea shabaha ileile kwa hiari na kwa utaratibu”[145]wazielekeze kwa umoja nguvu zao kwa ajili ya kujenga Kanisa.

Kwa sababu hiyo kazi za wajumbe wa Injili na misaada ya wakristo wengine zipangwe na zishikamane kwa namna maalum ili “mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu” (1Kor 14:40) katika nyanja zote za utendaji na za ushirikiano wa kimisioni.

Utaratibu unaohusu Idara ya Uenezi wa Imani (Propaganda Fide)

29. Kwa vile jukumu la kuhubiri Injili ulimwenguni mwote lina hasa Umoja wa Maaskofu[146],Sinodi ya Maaskofu, yaani “Halmashauri ya kudumu ya Maaskofu kwa ajili ya Kanisa lote ulimwenguni”[147], kati ya mada zenye umuhimu kwa wote[148]ifuatilie kwa hamasa ya pekee utendaji wa kimisioni, ambao ni wajibu mkuu na mtakatifu wa Kanisa[149].

Minajili ya Misioni zote na kwa utendaji wa kimisioni kwa jumla lazima iwe inahusika Idara moja tu, yaani ile ya “Propaganda Fide” (Uenezi wa Imani), ambayo ina mamlaka ya kusimamia na kuratibu ulimwenguni pote kazi za kimisioni na pia ushirikiano wa kimisioni. [Hata hapo] lakini iheshimiwe haki ya Makanisa ya Mashariki[150].

Hata ikiwa Roho Mtakatifu husitawisha kwa namna nyingi moyo wa umisioni katika Kanisa, akitangulia mara nyingi hata matendo ya wale wanaoshika wajibu wa kuongoza maisha ya Kanisa, basi Idara hiyo kwa upande wake hupaswa kuhamasisha miito na roho ya kimisioni, hamasa na sala kwa ajili ya misioni, na kutolea habari za kweli na zifaazo juu ya kazi za kimisioni. Ni wajibu wake kuwalea na kuwatuma wamisionari, kulingana na mahitaji ya lazima zaidi ya mahali mbalimbali. Kadhalika ni juu yake kuandaa mpango maalum wa utendaji, kutoa miongozo na kanuni mahususi kwa ajili ya uinjilishaji, na kuuchochea. Vilevile ni wajibu wake kuitisha na kuratibisha kwa mafanikio ukusanyaji wa misaada, ambayo hapo baadaye itagawanywa kufuatana na mahitaji au na maafa yaliyopo, pia na ukubwa wa maeneo, na idadi ya waamini na wasioamini, na matendo na taasisi mbalimbali, na wahudumu pamoja na wamisionari.

Idara hiyo, kwa kushikamana na Sekreterieti ya Kukuza Umoja wa Wakristo, itafute njia na mbinu za kuletea na kuratibia ushirikiano wa kidugu na pia uhusiano na shughuli mbalimbali za kimisioni za madhehebu mengine ya kikristo, ili kuondoa, kadiri inavyowezekana, kikwazo cha utengano.

Kwa hiyo inabidi Idara hii iwe chombo cha uendeshaji na ofisi ya uongozi wa kimkikimkiki, itumie mbinu za kitaalamu pamoja na vyombo vinavyolingana na nyakati zetu, yaani inufaike na uchunguzi wa siku hizi katika teolojia, na wa elimu-mbinu (methodologicae) na wa uchungaji wa kimisioni.

Katika uongozi wa Idara hiyo wahusike wawakilishi wenye kura ya uamuzi walioteuliwa miongoni mwa makundi na vyama vinavyoshiriki katika utendaji wa kimisioni. Nao ni Maaskofu wa ulimwengu mzima walioteuliwa na Mabaraza ya Maaskofu, na wakurugenzi wa Taasisi na Mashirika ya kipapa, kulingana na utaratibu na kanuni zinavyothibitishwa na Baba Mtakatifu. Hao wote, watakaokongamanishwa kwa vipindi maalum, watasimamia chini ya madaraka ya Baba Mtakatifu mipangilio mikuu ya kazi zote za kimisioni.

Penye Idara hiyo patakuwa na Halmashauri ya kudumu ya wataalamu washauri, mabingwa kwa ualimu na mazoea. Wenyewe, pamoja na kushika nyadhifa nyinginezo, jukumu lao hasa litakuwa ni kukusanya habari zenye manufaa juu ya mazingira ya nchi mbalimbali na juu ya tabia ya pekee ya makundi yoyote ya watu, kadhalika kuhusu mitindo ya uenezaji Injili inayofuatika. Kisha wapendekeze maazimio yenye misingi ya maarifa kwa ajili ya utendaji na ushirikiano wa kimisioni.

Mashirika ya watawa wa kike, taasisi za kikanda kwa Misioni, vyama mbalimbali vya walei, hasa vya kimataifa, yawakilishwe kwa idadi inayoridhika.

Utaratibu wa kimisioni wa Kanisa mahalia

30. Kusudi katika utendaji wa kimisioni yafikiliwe malengo na mafanikio mazuri, lazima wale wote wafanyao kazi za kimisioni wawe “na moyo mmoja na roho moja” (Mdo 4:32).

Ni juu ya Askofu, aliye kiongozi wa kazi ya kitume jimboni na mtima wa umoja wake, kuhamasisha, kuongoza na kuratibisha utendaji wa kimisioni. Uhifadhiwe, lakini, na kuchochewa uanzishaji wa hiari wa wale wanaoshiriki katika shughuli hizo. Wamisionari wote, hata walioondolewa katika mamlaka ya wakuu wa jimbo (religiosi exempti), wako chini yake katika shughuli zote zinazohusu utendaji wa utume mtakatifu[151]. Ili kuratibisha vizuri zaidi uanzishaji wote, Askofu aunde mara iwezekanapo, Halmashauri ya Uchungaji, ambamo makleri, watawa na walei wawakilishwe na wajumbe wa kuchaguliwa. Ashughulikie pia ili harakati ya kitume isiwafikie walioongoka tu, bali atoe baadhi inayofaa ya wamisionari na ya misaada kwa ajili ya uenezaji wa Injili kati ya wasio Wakristo.

Uratibu wa kikanda

31. Katika Mabaraza ya Maaskofu, wenyewe wawasiliane na kushauriana juu ya masuala mazito zaidi na juu ya shida za lazima, pasipo kusahau utofauti wa kimazingira[152].Kwa kusudi la kutokutapanya mali na watu, ambao mara nyingi ni haba, na la kutokuzidisha uanzishaji pasipo lazima, inahimizwa kushirikisha nguvu ili kuanzisha miradi iletayo manufaa kwa wote, kwa mfano seminari, shule za sekondari na za ufundi, vituo vya uchungaji, katekesi, liturujia, na vituo vishughulikavyo na vyombo vya upashanaji habari.

Ushirikiano wa namna hiyo uwepo pia – kulingana na fursa – kati ya Mabaraza kadha wa kadha ya Maaskofu.

Utaratibu wa utendaji wa Mashirika mbalimbali

32. Inafaa kwamba pia shughuli zifanywazo na Mashirika au na Vyama vya kikanisa ziratibishwe. Nazo, za namna zozote zile, ziratibiwe na Askofu wa mahali hapo, kwa mambo yote yanayohusu kazi za kimisioni. Kwa madhumuni hayo, itakuwa ni bora kufanya mapatano ya kimaandishi (mkataba) halisi, kwa ajili ya kuthibitisha jinsi ulivyo uhusiano kati ya Askofu wa mahali na Kiongozi Mkuu wa Shirika.

Pindi Shirika fulani linapokabidhiwa sehemu ya nchi, itakuwa moyo wa Mkuu halisi wa Kanisa (Superior Ecclesiasticus) mahali pale, na wa Shirika lenyewe, kuelekeza nguvu zote kwa lengo la kukuza jumuiya mpya hadi kuwa Kanisa mahalia, ambalo, kwa wakati ufaao, litasimamiwa na mchungaji wake pekee pamoja na makleri wake.

Ukiisha malizika ukabidhi (commissione) juu ya sehemu fulani, mambo yanahitaji kubadilishwa. Hapo, Mabaraza ya Maaskofu wakifanya shauri na Mashirika, watoe amri zinazoratibisha mahusiano kati ya Maaskofu wa mahali na Mashirika[153].Lakini ni juu ya Kiti Kitakatifu kuagizia kanuni za msingi, ambazo zitafuatwa wakati wa kukubaliana mikataba ile ya kikanda kama vile ya kipekee.

Ijapo Mashirika yangekuwa tayari kuendeleza kazi walizozianzisha, yaani kushiriki katika huduma ya kawaida ya uangalizi wa roho, hata hivyo, kulingana na ukuaji wa [idadi ya] mapadre wazalendo, inafaa Mashirika – kwa mujibu wa lengo lao – waendelee kushikamana na jimbo lilelile, kwa kushika kwa moyo utume ulio mahususi au kufanya shughuli katika maeneo fulani [ya jimbo lilelile].

Uratibu kati ya Mashirika

33. Inafaa kweli kwamba Mashirika yanayohusika katika utendaji wa kimisioni kwenye eneo lilelile, yatafute na kupata njia na namna za kuratibu shughuli zao. Kwa lengo hilo Mabaraza ya Watawa wa kiume na Umoja wa Masista vyasaidia sana, ambamo bora washiriki Mashirika yote ya nchi ile au ya ukanda. Mabaraza hayo hutafuta yale yote yanayoweza kufanyika kwa juhudi za umoja, pamoja na kuambatana na Mabaraza ya Maaskofu.

Hali kadhalika inafaa Mashirika ya kimisionari yahusishe katika mambo hayo nyumba zao zilizopo katika nchi za asili, kusudi yatatuliwe kwa urahisi na bila kutumia gharama mno, masuala na uanzishaji wa pamoja kama vile yale yanayohusika na malezi ya kimafundisho kwa wale watakaokuwa wamisionari, na kazi za wamisionari, au na risala za kupelekwa kwa wakuu wa Serikali au kwa vyama na mashirika ya kimataifa.

Uratibu kati ya Taasisi za kitaaluma

34. Kutekeleza kwa unyofu na utaratibu utendaji wa kimisioni kunadai kwamba wanaofanya kazi za kiinjili waandaliwe kitaaluma kwa wajibu wao hasa kwa ajili ya mijadala na dini na tamaduni zisizo za kikristo; hali kadhalika kunadai wasaidiwe kwa namna ya kufaa katika utekelezaji wa huo wajibu wao. Ndiyo maana, inatamanika kwamba ushirikiano mkubwa wa kidugu uwepo kati ya Taasisi zote za kitaaluma, zinazochambua misiolojia, na mada au sanaa nyingine zinufaishazo misioni, kama vile ethnolojia na isimu, historia na taaluma ya dini mbalimbali, elimujamii, mitindo ya kichungaji, na kadhalika.

Sura ya Sita

USHIRIKIANO

Utangulizi

35. Kwa kuwa Kanisa zima ni la kimisionari na kwa kuwa uenezaji wa Injili ni jukumu la msingi kwa Taifa la Mungu, basi Mtaguso Mkuu huwaalika wote kujifanya upya moyoni, ili kwa kutambua waziwazi wajibu wao wa kueneza Injili una maana gani, watoe mchango wao katika kazi za kimisionari kwa mataifa yote.

Wajibu wa kimisioni wa waamini wote

36. Waamini wote wameunganika ndani ya Kristo, kama viungo vyake hai, na wamefanywa wafanane naye kwa njia ya Ubatizo, Kipaimara, na Ekaristi. Kwa hiyo, wote wamewajibika kushiriki katika kueneza na kukuza Mwili wake ili ufike upesi kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo[154].

Kwa hiyo wanakanisa wote watambue waziwazi wajibu wao mbele ya ulimwengu, wakuze ndani yao wenyewe roho ya kikatoliki kweli, na wajitolee kwa nguvu zao zote katika kazi za uinjilishaji. Lakini wote wajue kwamba wajibu wao wa kwanza na wa msingi kwa ajili ya kueneza imani ndio huu: kuishi maisha ya kikristo kwelikweli. Maana ari yao katika utumishi wa Mungu na upendo wao kwa ajili ya wengine vitaleta mithili ya uvuvio mpya wa kiroho katika Kanisa zima. Nalo litaonekana kuwa “ishara iliyoinuliwa kati ya Mataifa”[155], “nuru ya ulimwengu” (Mt 5:14), na “chumvi ya dunia” (Mt 5:13). Ushuhuda wa maisha wa namna hii, bila shaka, utakuwa na mafanikio, hasa kama utatolewa katika umoja na madhehebu mengine ya wakristo, kufuatana na kanuni za dikrii juu ya Ekumeni[156].

Tokea katika roho hiyo mpya zitatolewa kwa hiari sala na matendo ya toba kwa Mungu, ili arutubishe kwa neema yake kazi zinazofanywa na wamisionari. Hivyo kutasitawi miito ya kimisionari, pamoja na misaada inayohitajika katika misioni.

Lakini, kusudi waamini mmoja mmoja na wote kwa pamoja wajue kwa namna inayofaa hali ya Kanisa katika ulimwengu wa leo ilivyo, na wafikiwe na sauti ya umati wa watu wanaolia: “Utusaidie”[157], lazima kuwapatia, hata kwa njia ya vyombo vya upashanaji habari, taarifa juu ya misioni, ili, huku wakisikia kwamba kazi za kimisioni ni jambo lao wenyewe, wafungue mioyo yao mbele ya mahitaji mengi na makubwa ya wanadamu, wakawasaidie.

Vivyo hivyo inahitajika kuratibisha taarifa hizo, na kushirikiana na vyama vya kitaifa na vya kimataifa.

Wajibu wa kimisioni wa jumuiya za kikristo

37. Kwa kuwa watu wa Mungu huishi katika jumuiya, hasa za kijimbo na za kiparokia, na katika hizo Taifa la Mungu huonekana wazi, kwa namna fulani, ni juu ya jumuiya hizo nazo kumshuhudia Kristo mbele ya mataifa.

Neema ya kufanywa upya haiwezekani ikuzwe katika jumuiya, kama kila moja yao isipopanua nafasi ya mapendo mpaka kufikia miisho ya dunia, wala isipoonyesha kwa walio mbali uangalifu uleule ilio nao kwa wanajumuiya wake.

Hivyo jumuiya nzima husali, hushirikiana, hutenda kazi kati ya mataifa kwa njia ya wanajumuiya wale ambao Mungu huchagua kwa huduma hii bora.

Itakuwa inafaa sana, bila kuzisahau kazi za kimisioni katika ulimwengu wote, kutunza uhusiano na wamisionari waliotokea kwenye jumuiya yenyewe, ama na parokia au jimbo fulani la kimisioni, kusudi ushirika kati ya jumuiya mbalimbali uonekane kweli na ulete faida ya kujengana wao kwa wao.

Wajibu wa kimisioni wa Maaskofu

38. Maaskofu wote, kwa vile ni wanabaraza wa Umoja wa Maaskofu, na waandamizi wa Urika wa Mitume, wamewekwa wakfu si kwa ajili ya jimbo moja tu, lakini pia kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima. Agizo la Yesu la kuhubiri Injili kwa kila kiumbe[158],linawahusu kwanza kabisa hao wenyewe, pamoja na Petro na chini ya Petro. Napo ndipo unapotokea ule ushirika na ushirikiano kati ya Makanisa, ambao leo hivi huhitajika kweli ili kuendeleza kazi ya uinjilishaji. Kwa mujibu wa ushirika huo Makanisa faridi yanafadhaika kwa ajili ya Makanisa mengine, yanapeana taarifa juu ya mahitaji yaliyo nayo, yanasaidiana kwa kupelekeana vifaa na mali zao yenyewe, na hayo yote yatekelezwa kwa sababu ukuaji wa Mwili wa Kristo ni wajibu wa Umoja wa Maaskofu kwa pamoja[159].

Kwa njia ya kuchochea, kuhimiza na kuongoza kazi za kimisioni katika jimbo lake, lililo kitu kimoja naye mwenyewe, Askofu hufanya roho na ari za kimisioni za watu wa Mungu zionekane wazi, na hivyo jimbo zima linakuwa la kimisionari.

Ni wajibu wa Askofu kuziamsha katika watu wake, hasa miongoni mwa wagonjwa na wanaoteseka, roho ambazo kwa moyo mkuu wamtolee Mungu sala na matendo ya toba kwa manufaa ya uinjilishaji wa ulimwengu; kuwatia moyo konde vijana na makleri kwenye miito ya kimisionari, na kupokea kwa shukrani hiari ya Mungu anayechagua wengine ili kuwashirikisha katika shughuli za kimisioni za Kanisa. Askofu hupaswa pia kusukuma na kusimamia Mashirika ya kijimbo ili yashike sehemu inayoyaangukia katika misioni; vilevile kuhimiza matendo ya Mashirika ya kimisionari kati ya waamini wake, hasa Mashirika ya Kipapa ya Misioni (Opera Pontificalia Missionalia). Nayo hasa yastahili kupewa nafasi za kwanza, kwa sababu ni njia ya kuotesha katika wakatoliki, tangu utotoni, moyo wa umisioni unaoweza kutazama ulimwenguni kote, na pia kusukumiza ukusanyaji wa kufaa wa misaada kwa nafuu za misioni zote, kulingana na mahitaji ya kila moja[160].

Maadam haja ya kupata wafanyakazi katika shamba la Bwana inazidi kuwa ya lazima zaidi siku kwa siku, na mapadre wa jimbo wanatamani kupata nafasi kubwa zaidi katika uinjilishaji wa ulimwengu, Mtaguso Mkuu hutarajia kwamba Maaskofu, huku wakifikiria uhaba mkali wa mapadre, unaozuilia uinjilishaji katika sehemu nyingi za dunia, watume kutoka miongoni mwa mapadre wake, baada ya mafunzo ya kufaa, wengine walio bora zaidi, ili wajishughulishe na kazi za kimisioni kule kwenye majimbo yanayosongwa na uchache wa mapadre, nako watahusika, walau kwa muda fulani, na huduma ya kimisioni kwa roho ya utumishi[161].

Walakini, kusudi utendaji wa kimisioni wa Maaskofu ifaidi Kanisa lote, yafaa kwamba Mabaraza ya Maaskofu yaratibu masuala yote yanayohusu utaratibu wa ushirikiano katika eneo lake.

Katika Mabaraza yao Maaskofu wajadiliane kuhusu mada zifuatazo: juu ya mapadre wa jimbo wa kutumwa kueneza Injili kati ya Mataifa; juu ya kiwango cha mchango wa pesa ambacho kila jimbo, kulingana na mapato yake[162],huwajibika kutoa kila mwaka kwa ajili ya kazi za kimisioni; juu ya namna ya kusimamia na kuratibisha njia na mali ziletazo auni moja kwa moja kwa misioni; juu ya misaada ya kutolewa kwa Mashirika ya kimisionari na kwa seminari za kijimbo kwa ajili ya misioni, ama – ikiwa ni lazima – kwa kuyaunda hayo; juu ya namna ya kuhifadhi na kukazia uhusiano mzuri kati ya Mashirika hayo na majimbo.

Hali kadhalika inawapasa Mabaraza ya Maaskofu kuanzisha na kusimamia vituo, ambamo itakuwa inawezekana kuwapokea kwa moyo wa kidugu na kwa uangalifu wa kichungaji wale ambao, minajili ya kazi au mafunzo, wanatoka nchi za misioni. Kwa njia ya hao ndugu, watu wa mbali wanakuwa – kwa namna fulani – jirani, na hivyo jumuiya zilizo za kikristo tangu kale, zinapata fursa bora ya kuanzisha mawasiliano na mataifa ambayo bado hayajasikia Injili, na kuwaonyesha, katika huduma ya upendo na msaada, uso wa kweli wa Kristo ulivyo[163].

Wajibu wa kimisioni wa mapadre

39. Mapadre wanamwakilisha Kristo na kushirikiana na Maaskofu katika majukumu ya aina tatu ya utakatifu ambayo, kwa tabia yake yanahusu utume wa Kanisa[164]. Hivyo wasadiki kweli kuwa maisha yao yaliwekwa wakfu kwa huduma ya misioni pia. Na kwa vile kwa njia ya huduma yao – ambayo asili na kiini chake ni Ekaristi, ilileteayo Kanisa ukamilifu wake – wanaungana na Kristo, aliye kichwa, wanawaongoza wengine kwa ushirika huo naye, hawana budi kuhisi kiasi gani bado kinakosekana ili kuufikilia utimilifu wa mwili wake na kiasi gani bado kinahitajika kutenda ili ukuzwe zaidi na zaidi. Hapo, wenyewe wataratibisha shughuli za uchungaji kusudi zisaidie kueneza Injili kati ya wasio wakristo.

Mapadre katika shughuli za uchungaji wataamsha na kuhifadhi kati ya waamini hamu ya kueneza Injili ulimwenguni. Watatimiza hilo kwa njia ya kuwafundisha katekesi na kwa hotuba watoazo kuhusu wajibu wa Kanisa wa kumhubiri Kristo kati ya mataifa; kwa kuzielezea familia za kikristo haja na heshima ya kustawisha miito ya kimisionari kati ya wana na binti zao; kwa kukuza kati ya vijana wa shuleni na wa vyama vya kikatoliki ari ya kimisioni, ili wengine kati yao wafanywe wajumbe wa Injili. Aidha, mapadre wawafundishe waamini kusali kwa ajili ya misioni, wala wasione aibu kuwaomba sadaka, hivyo wakijifanya kama waombaji kwa ajili ya Kristo na ya wokovu wa watu[165].

Wahadhiri katika seminari na vyuo watawaelezea wanafunzi hali halisi ya ulimwengu na ya Kanisa, wapate kutambua waziwazi ulazima wa kufanya bidii sana katika uinjilishaji wa wasio wakristo, na zichochewe juhudi zao. Vilevile katika kufundisha masomo ya dogma, ya biblia, ya Maadili na ya historia watokeze mambo yote yanayohusu umisioni, ili kujenga tabia ya kimisioni ndani yao watakaokuwa mapadre.

Wajibu wa kimisioni wa Mashirika ya kitawa

40. Mashirika ya kitawa ya maisha ya kitaamuli (contemplativa) au yenye kufanya kazi ya kitume (activa), yalikuwa mpaka leo hivi, na yanaendelea kuwa na wadhifa maridhawa wa uenezaji wa Injili ulimwenguni. Mtaguso Mkuu hukiri kwa furaha mastahili yao na humshukuru Mungu kwa ajili ya matatizo mengi waliyoyamudu kwa utukufu wa Mungu na kwa huduma ya watu. Tena unawasihi wadumu bila kuchoka katika kazi waliyoianzisha, huku wakijua kwamba fadhila ya mapendo, wanayodaiwa kuihifadhi kwa ukamilifu zaidi kwa ajili ya wito wao, inawasukuma na kuwalazimisha kukuza roho na juhudi zilizo za kikatoliki kwelikweli[166].

Mashirika ya maisha ya kitaamuli, kwa njia ya sala zao, ya matendo ya toba na ya taabu, yanakuwa muhimu sana kwa ajili ya uongofu wa watu, kwa sababu ndiye Mungu ambaye, akiombwa, huwapeleka watenda kazi katika mavuno yake[167],hufungua roho ya wasio wakristo ili waisikie Injili[168],na hukuza katika mioyo yao Neno la wokovu[169]. Pamoja na hayo, Mashirika ya aina hiyo hualikwa kufungua nyumba nyingine katika nchi za kimisioni, jinsi mengineyo yalivyofanya tayari, ili, kwa kuishi pale kwa mitindo inayolingana na desturi zenye ibada halisi za watu, yatolee mbele ya wasio wakristo ushuhuda ulio bora wa fahari na wa mapendo ya Mungu, na vilevile wa umoja katika Kristo.

Mashirika ya maisha ya kitendaji, yakiwa yanahusika moja kwa moja na misioni ama sivyo, yajiulize mbele ya Mungu katika ukweli, kama yangeweza kupanua jitihada zao mpaka kushiriki kueneza Ufalme wa Mungu kati ya Mataifa; kama yangeweza kuwaachia wengine kazi nyinginezo za huduma yao ili kutia nguvu zao kwa ajili ya misioni; kama yangeweza kuanzisha shughuli fulani katika misioni, baada ya kurekebisha, iwapo inahitajika, sheria yao,lakini katika nia na roho ya mwanzilishi; kama washirika wake wakijitolea kulingana na nguvu zao kwa ajili ya utendaji wa kimisioni; kama mtindo wa maisha yao unakuwa ushuhuda wa Injili, unaofaa kwa tabia na hali ya watu.

Kisha, kwa vile chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu, yanastawi zaidi na zaidi katika Kanisa Mashirika yenye kuishi kati ya watu (Instituta saecularia), basi kazi zao chini ya mamlaka ya Askofu, zinaweza kuleta faida kubwa sana katika misioni na kuwa ishara ya kujitolea kwa moyo wote kwa ajili ya uinjilishaji wa ulimwengu.

Wajibu wa kimisioni wa walei

41. Walei hushirikiana katika kazi ya Kanisa ya kueneza Injili na kushika nafasi yao kama mashahidi na kama vyombo hai katika utume wake kwa wokovu[170], hasa iwapo baada ya kuitwa na Mungu, wanawekwa na Askofu kwa ajili ya kazi hiyo.

Katika nchi zilizo za kikristo tangu muda mrefu, walei watashiriki katika uenezaji wa Injili, wakikuza ndani yao wenyewe na ndani ya wengine ujuzi na upendo kwa misioni, wakichochea miito katika familia zao, katika vyama mbalimbali vya kikatoliki na katika shule, wakitoa misaada ya aina yoyote ile, ili kipaji cha imani walichokipata bure, kitolewe kwa wengine pia.

Kwa upande mwingine, katika nchi za misioni walei, wawe wageni au wazalendo, wajibu wao ni kufundisha shuleni, kusimamia mambo ya kidunia, kusaidia katika kazi mbalimbali za parokiani na jimboni, kuanzisha na kuhimiza kazi mbalimbali za utume wa walei, kusudi waamini wa Makanisa machanga wapate upesi kutimiza shughuli zilizo za haki yao katika maisha ya Kanisa[171].

Kisha, yafaa walei washiriki kwa hiari katika kuendeleza uchumi na maendeleo ya kijamii ili mataifa yaweze kusonga mbele. Ushirikiano huo unastahili kusifiwa, hasa unapohusu moja kwa moja uundaji wa taasisi zifanyazo kazi kwa ajili ya maisha ya kijamii, ama zinazosaidia kwa malezi ya wale ambao wanashika madaraka ya kuongoza umma.

Wanastahili sifa za pekee walei wale ambao katika vyuo vikuu au katika taasisi za taaluma, kwa njia ya chunguzi zao za kihistoria au za kitaaluma ya dini, wanasisimua kuwafahamu watu na dini zao, hivyo wakitoa msaada kwa wajumbe wa Injili na kuandaa dialogia na wasio wakristo.

[Walei] washiriki kidugu na wakristo wengine, na wasio wakristo, hasa na wanavyama wa kimataifa, huku ikikumbukwa kila mara kwamba “jengo la mji wa kidunia liwe daima na msingi katika Bwana na kumwelekea Yeye”[172].

Ili kutimiza wajibu hizo zote, walei wanahitaji mafunzo madhubuti ya kimaarifa na ya kiroho, ya kupewa katika vyuo maalum. Hapo, maisha yao yawe ushuhuda wa Kristo kati ya wasiomwamini, kulingana na neno la Mtume Paulo: “Msiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala Kanisa la Mungu, vilevile kama mimi niwapendavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa” (1Kor 10:32-33).

HITIMISHO

42. Mababa wa Mtaguso, pamoja na Baba Mtakatifu, wakihisi sana jukumu la kueneza popote Ufalme wa Mungu, wanatoa heko za upendo kwa wote wenye kutangaza Injili, hasa kwa wale wanaodhulumiwa kwa jina la Yesu Kristo[173],huku wakijiunga na mateso yao.

Nao wenyewe huwaka upendo uleule ambao Kristo alikuwa anawaka kwa ajili ya wanadamu. Lakini wanafahamu pia kuwa ni Mungu afanyaye Ufalme wake ufike hapa duniani. Ndiyo sababu wanatoa maombi pamoja na waamini wote, ili kwa maombezi ya Bikira Maria, Malkia wa Mitume, mataifa yote wapate kuelekezwa kujua yaliyo kweli[174],na utukufu wa Mungu, ung’aao katika uso wa Yesu Kristo, uangaze katika wote kwa nguvu ya Roho Mtakatifu[175].

  

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuriwa kwa pamoja katika Sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 7 Desemba 1965

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)

 

UTANGULIZI (1) 

I - KANUNI ZA MSINGI ZA MAFUNDISHO (2-9)
Azimio la Mungu Baba (2)
Utume wa Mwana wa Mungu (3)
Utume wa Roho Mtakatifu (4)
Utume wa Kanisa (5)
Kazi ya kimisioni (6)
Sababu zinazodai kazi za kimisioni (7)
Kazi za kimisioni katika maisha na historia ya wanadamu (8)
Maana ya kieskatolojia ya kazi za kimisioni (9) 

II - KAZI ZENYEWE ZA KIMISIONI (10-18)
Utangulizi (10)
I - USHUHUDA WA KIKRISTO (11-12)
Ushuhuda wa maisha na dialogia (11)
Maana ya upendo wa kikristo (12)
II - KUHUBIRIWA KWA INJILI NA KUKUSANYIKA KWA TAIFA LA MUNGU (13-14)
Uenezaji wa Injili na toba (13)
Ukatekumeni na uingizaji katika ukristo (14)
III - KUJENGWA KWA JUMUIYA YA KIKRISTO (15-18)
Utangulizi (15)
Wakleri wazalendo (16)
Malezi ya makatekista (17)
Kuhamasisha maisha ya kitawa (18)

III - MAKANISA FARIDI (19-22)
Maendeleo ya Makanisa machanga (19)
Kazi za kimisioni za Makanisa faridi (20)
Kuhamasisha utume wa walei (21)
Utofauti katika umoja (22) 

IV - WAMISIONARI (23-27)
Wito wa kimisionari (23)
Roho ya umisionari (24)
Malezi ya kiroho na ya kimaadili (25)
Malezi ya kimafundisho na ya kitume (26)
Mashirika yafanyayo kazi katika misioni (27) 

V - UTARATIBU WA KUENDESHA KAZI ZA KIMISIONI (28-34)
Utangulizi (28)
Utaratibu unaohusu Idara ya Uenezi wa Imani (Propaganda Fide) (29)
Utaratibu wa kimisioni wa Kanisa mahalia (30)
Uratibu wa kikanda (31)
Utaratibu wa utendaji wa Mashirika mbalimbali (32)
Uratibu kati ya Mashirika (33)
Uratibu kati ya Taasisi za kitaaluma (34) 

VI - USHIRIKIANO (35-42)
Utangulizi (35)
Wajibu wa kimisioni wa waamini wote (36)
Wajibu wa kimisioni wa jumuiya za kikristo (37)
Wajibu wa kimisioni wa Maaskofu (38)
Wajibu wa kimisioni wa mapadre (39)
Wajibu wa kimisioni wa Mashirika ya kitawa (40)
Wajibu wa kimisioni wa walei (41)
HITIMISHO (42)

    

[1] Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 48: AAS 57 (1965) uk. 53.
[2] Taz. Mk 16:15
[3] Mt Augustinus, Enarr. in Ps. 44, 23; PL 36, 508; Chr 38, 510.
[4] Taz. Mt 5:13-14.
[5] Taz. Ybs 36:19 Vulg.
[6] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 2: AAS 57 (1965) uk. 5-6
[7] Taz. Yn 11:52.
[8] Taz. Mt. Ireneus, Adv. Haer. III, 18,1: “Neno aliyekuwapo kwa Mungu, ambaye vitu vyote viliumbwa kwake, na ambaye alikuwa sikuzote pamoja na wanadamu...”: PG 7, 932; id. IV, 6,7: “Tangu awali Mwana wa Mungu aliyekuwapo kwa viumbe vyake, humdhihirisha Mungu Baba kwa wale wote anaowataka Yeye Baba, na kwa njia anazozipenda Yeye Baba...”: ib. 990; taz. IV, 20,6 na 7: ib. 1037; Demonstratio n. 34; Patr. Or. XII, 773; Sources Chrét. 62, Paris 1958, uk. 87; Clemens Alex., Protrept. 112,1: GCS Clemens I,79; Strom. VI, 6,44,1: GCS Clemens II,453; 13,106,3 na 4: ib. 485. Kuhusu mafundisho hayo, taz. Pius XII, Nuntius radiophon. 31 des. 1952; Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 16: AAS 57 (1965) uk. 20
[9] Taz. Kol 1:13; Mdo 10:38.
[10] Taz. 2Kor 5:19.
[11] Taz. Ebr 1:2; Yn 1:3,10; 1Kor 8:6; Kol 1:16.
[12] Taz. Efe 1:10.
[13] Taz. 2Kor 8:9.
[14] Taz. Mk 10:45.
[15] Taz. Mt. Athanasius, Ep. ad Epictetum, 7: PG 26, 1060; Mt. Cyrillus Hieros., Catech. 4, 9: PG 33, 465; Marius Victorinus, Adv. Arium, 3, 3: PL 8, 1101; Mt. Basilius, Epist. 261, 2: PG 32, 969; Mt. Gregorius Naz., Epist. 101: PG 37, 181; Mt. Gregorius Nyss., Antierheticus, Adv. Apollin., 17: PG 45, 1156; Mt. Ambrosius, Epist. 48, 5: PL 16, 1153; Mt. Augustinus, In Ioan. Ev. tr. XXIII, 6: PL 35, 1585; CChr. 36, 236; zaidi ya hayo huonyesha kwa namna hii kwamba Roho Mtakatifu hakutukomboa kwa vile hakutwaa mwili: De Agone Christ. 22, 24: PL 40, 302: Mt. Cyrillus Alex., Adv. Nestor. I, 1: PG 76, 20; Mt. Fulgentius, Epist. 17, 3, 5: PL 65, 454; Ad Trasimundum, III, 21: PL 65, 284: kuhusu huzuni na hofu.
[16] Taz. Ebr 4:15; 9:28.
[17] Taz. Mdo 1:8.
[18] Taz. Lk 24:47.
[19] Roho Mtakatifu ndiye aliyenena kwa vinywa vya Manabii: Symb. Constantinopol.: Denz. 150 (86); Mt. Leo Mkuu, Sermo 76: PL 54, 405-406: “Roho Mtakatifu alipowajazia wafuasi wa Bwana kwenye siku ya Pentekoste, tendo hilo halikuwa awali ya jukumu lake, bali upanuko wa ukarimu wake, kwa maana mababu, manabii, makuhani na watakatifu wote wa zamani zilizotangulia walikuwa wanalishwa na Roho mleta utakatifu huyohuyo.... ingawa kiasi cha kipawa kilikuwa tofauti”. Taz. pia Sermo 77, 1: PL 54, 412; Leo XIII, Litt. Encycl. Divinum illud, 9 mei 1897: AAS 29 (1897) uk. 650-651. Pia Mt. Ioannes Chrysostomus, ijapo husisitiza hali mpya ya utume wa Roho Mtakatifu katika siku ya Pentekoste: In Eph. c. 4, Hom. 10,1: PG 62,75.
[20] Taz. Yn 14:16.
[21] Mababa wa Kanisa mara nyingi hunena juu ya Babeli na Pentekoste: Origenes, in Genesim, c. 1: PG 12, 112; Mt. Gregorius Naz., Oratio 41, 16: PG 60, 44; Mt. Augustinus, Enarr. In Ps. 54, 11: PL 36, 636; CChr. 39, 664s.; Sermo 271: PL 38, 1245; Mt. Cyrillus Alex., Glaphyra in Genesim II: PG 69, 79; Mt. Gregorius Mkuu, Hom. In Evang., Lib. II, Hom. 30, 4: PL 76, 1222; Mt. Beda, In Exaem., Lib. III: PL 91, 125. Taz. pia picha katika ukumbi wa Basilika ya Mt. Marko, huko Venezia.

Kanisa hunena kwa lugha zote, na hivyo hukusanya watu wote katika ukatoliki wa imani: Mt. Augustinus, Sermones, 266, 267, 268, 269: PL 38, 1225-1237; Sermo 175, 3: PL 38, 946; Mt. Ioannes Crysost., In Ep. 1 ad Cor., Hom. 35: PG 61, 296; Mt. Cyrillus Alex., Fragm. In Act.: PG 74, 758; Mt. Fulgentius, Sermo 8, 2-3: PL 65, 743-744.

Kuhusu Pentekoste kama siku ya kuwekwa wakfu Mitume kwa ajili ya utume wao, taz. J. A. Cramer, Catena in Acta SS. Apostolorum, Oxford, 1838, uk. 24s.

[22] Taz. Lk 3:22; 4:1; Mdo 10:38.
[23] Taz. Yn sura ya 14 hadi 17; Paulus VI, Hotuba iliyotolewa kwenye Mtaguso, tarehe 14 septemba 1964: AAS 56 (1964) uk. 807.
[24] Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 4: AAS 57 (1965) uk. 7.
[25] Mt. Augustinus, Sermo 267, 4: PL 38, 1231: “Roho Mtakatifu hutenda katika Kanisa zima yale ambayo roho hutenda katika viungo vyote vya mwili”. Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 7 (na rejeo n.8): AAS 57 (1965) uk. 11.
[26] Taz. Mdo 10: 44-47; 11:15; 15:8.
[27] Taz. Mdo 4:8; 5:32; 8:26.29.39; 9:31; 10; 11:24-28; 13:2.4.9; 16:6-7; 20:22-23; 21:11 n.k.
[28] Taz. pia Mt 10:1-42.
[29] Taz. Mt 28:18.
[30] Taz.Mdo 1:4-8.
[31] Taz. Yn 20:21.
[32] Taz. Kol 1:24.
[33] Tertullianus, Apologeticum, 50, 13: PL 1, 534; CChr. 1, 171.
[34] Wajibu wa kitume wa kuanzisha (au kupandikiza) Kanisa unatajwa tayari na Mt. Tomaso Akw.: rej. Sent. Lib. I, dist. 16, q. 1, a.4, ad 2 et ad 4; a. 3 sol.; Summa Theol. I, q. 43, a. 7 ad 6; I-II, q. 106, a. 4 ad 4. Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 445 na 453; Pius XI, Litt. Encycl. Rerum Ecclesiae, 28 feb. 1926: AAS 18 (1926) uk. 74; Pius XII, 30 apr. 1939, kwa Wakurugenzi OO. PP. MM.: AAS 36 (1944) uk. 210; na tena katika AAS 42 (1950) uk. 727, na 43 (1951) uk. 508; Id., 29 jun. 1948 kwa Wakleri wazalendo: AAS 40 (1948) uk. 374; Id., Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 jun. 1951: AAS 43 (1951) uk. 507; Id., Litt. Encycl. Fidei Donum, 15 jen. 1957: AAS 49 (1957) uk. 236; Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 835; Paulus VI, Hotuba ya 18 okt. 1964: AAS 55 (1964) uk. 911.

Mapapa, Mababa na Maskolastisi hutaja mara nyingi “uenezaji” (dilatatione) wa Kanisa: Mt. Tomaso Akw., Comm. In Matth. 16, 28; Leo XIII, Litt. Encycl. Sancta Dei Civites, 3 des. 1880: ASS 13 (1880) uk. 241; Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 442; Pius XI, Litt. Encycl. Rerum Ecclesiae, 28 feb. 1926: AAS 18 (1926) uk. 65.

[35] Taz. 1Pet 1:23.
[36] Taz. Mdo 2:42.
[37] Ni dhahiri kuwa katika dhana hii ya “kazi (au harakati) za kimisioni” yanaingia, bila shaka, pia maeneo yale ya Marekani ya Kusini ambamo wala haimo hierarkia yake pekee, wala maisha ya kikristo hayajakomaa, wala Injili haijahubiriwa kwa namna ya kuridhisha. Kwamba sehemu hizo ziwe zimekubaliwa rasmi na Kiti Kitakatifu ama sivyo, siyo jambo la kujadiliwa na Mtaguso. Ndiyo maana panapoongelewa juu ya uwiano kati ya dhana hiyo ya kazi za kimisioni na maeneo maalum, basi inasemwa kwamba “aghalabu” ( plerumque) zinashughulikiwa katika maeneo maalum yaliyoidhinishwa na Baba Mtakatifu.
[38] Conc. Vat. II, De Oecumenismo, Unitatis Redintegratio, n. 1: AAS 57 (1965) uk. 90.
[39] Taz. Mk 16:16; Yn 3:5.
[40] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 14: AAS 57 (1965) uk. 18.
[41] Taz. Ebr 11:6.
[42] Taz. 1Kor 9:16.
[43] Taz. Efe 4:11-16.
[44] Taz. Yn 7:18; 8:30 na 44; 8:50; 17:1.
[45] Kuhusu dhana hiyo ya sanisi, tazama mafundisho ya Mt. Ireneo juu ya Recapitulatione. Taz. pia Mt. Ipoliti, De Antichristo 3: “Huku akiwataka wote na akipenda kuwaokoa wote, akitaka kuwafanya wote wana wa Mungu, na akiwaita watakatifu wote ili kuwa mtu mmoja mkamilifu...”; PG 10, 732; GCS Hippolyt. I, 2 uk. 6; Benedictiones Iacob, 7: T.U., 38-1 uk. 18, lin. 4nk.; Origenes, In Ioann. Tom. I, n. 16: “Kwa wale waliomjia Mungu, hali wakiongozwa na yule Neno aliye kwa Mungu lipo tendo moja tu la kumjua Mungu, yaani kulelewa kama wana katika kumjua Mungu, kama sasa Mwanae peke yake humjua Baba.”: PG 14, 49; GCS Orig. IV, 20; Mt. Augustino; De Sermone Domini in monte, I, 41: “Tupende basi yanayoweza kutuongoza kwenye falme zile ambamo hayumo asemaye: Baba yangu, bali wote husema kwa Mungu aliye mmoja: Baba yetu”: PL 34, 1250; Mt. Sirili wa Iskandaria, In Ioann. I: “Sisi tu katika Kristo, na maumbile yetu ya kibinadamu yanahuishwa katika Yeye. Ndiyo sababu Yeye huitwa Adam mpya... Yeye aliye kwa tabia yake Mwana wa Mungu, amekaa kwetu, na hivyo katika Roho wake twalia: Aba, Baba! Neno huishi katika wote katika hekalu moja, yaani katika hekalu lile ambalo Yeye alilichukua kwa ajili yetu na kutoka kwetu, kusudi la kuwa na watu wote ndani yake mwenyewe, ili kuwapatanisha watu wote, kama alivyosema Mt. Paulo, katika mwili mmoja”: PG 73, 161-164.
[46] Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 445: “Kwa vile Kanisa la Mungu lilivyo katoliki (= la popote ulimwenguni), halitakuwa kamwe la kigeni kwa kabila au taifa lolote...”. Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Mater et Magistra: “Kwa azimio la Mungu, Kanisa laenea kwa mataifa yote....kwa hiyo linaingiza nguvu zake kama katika mishipa, tuseme, ya taifa lolote lile, na hivyo halijifikirii lenyewe kama taasisi tu iliyotwikwa juu ya taifa hilo kutoka kwa nje....Ndiyo maana, yote yanayoonekana kwao kuwa ni mema na manyofu, basi wao [yaani waliozaliwa kwa mara ya pili katika Kristo] wanayapokea na kuyatimiliza”, 25 mei 1961: AAS 53 (1961) uk. 444.
[47] Taz. Yn 3:18.
[48] Taz. Mt. Ireneo, Adv. Haer. III, 15, n. 3: PG 7, 919: “Walikuwa wahubiri wa ukweli na mitume wa uhuru”.
[49] Breviarium romanum, Ant. “O” ad Vesperas diei 23 decembris.
[50] Taz. Mt 24:31; Didaké 10,5; Funk. I, uk. 32.
[51] Taz. Mk 13:10.
[52] Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 17: AAS 57 (1965) uk. 21-22; Mt. Augustino, De Civitate Dei, 19, 17: PL 41, 646; Instr. S. C. de Propaganda Fide: Collectanea, I, n. 135, uk. 42.
[53] Kama alivyofundisha Orijene, Injili haina budi kuhubiriwa kabla ya mwisho wa ulimwengu huu: Hom. in Lc. XXI: GCS Orig., IX, 136, 21nk; In Matth. Comm. ser .39: XI, 75, 25nk; 76, 4nk; Hom. in Ierem. III, 2: VIII, 308, 29nk; Mt. Tomaso Akw., Summa Theol. I-II, q. 106, a. 4, ad 4.
[54] Taz. Mdo 1:7.
[55] Hilarius Pict., In Ps. 14: PL 9, 301; Eusebio Caesariensis, In Isaiam 54, 2-3: PG 24, 462-463; Sirili Alex., In Isaiam V, cap. 54, 1-3: PG 70,1193.
[56] Taz. Efe 4:13.
[57] Taz. Yn 4:23.
[58] Taz. Mt 5:16.
[59] Taz. 1Yoh 4:11.
[60] Taz. Mt 9:35nk; Mdo 10:38.
[61] Taz. 2Kor 12:15.
[62] Taz. Mt 20:26; 23:11; Hotuba ya Paolo VI iliyotolewa kwenye Mtaguso, tarehe 21 nov. 1964: AAS 56 (1964) uk. 1013.
[63] Taz. Efe 4:24.
[64] Taz. Kol 4:3.
[65] Taz. 1Kor 9:16; Rum 10:14.
[66] Taz. Mdo 4:13. 29. 31; 9:27-28; 13:46; 14:3; 19:8; 26:26; 28:31; 1The 2:2; 2Kor 3:12; 7:4; Flp 1:20; Efe 3:12; 6:19-20.
[67] Taz. Mk 16:15.
[68] Taz. 1The 1:9-10; 1Kor 1:18-21; Gal 1:31; Mdo 14:15-17; 17:22-31.
[69] Taz. Mdo 16:14.
[70] Taz. Kol 3:5-10; Efe 4:20-24.
[71] Taz. Lk 2:34; Mt 10:34-39.
[72] Taz. 1The 1:6.
[73] Taz. Conc. Vat. II, Decl. De Libertate Religiosa, Dignitatis Humanae, nn. 2, 4, 10; Const. past. De Ecclesia in mundo huius temporis, Gaudium et Spes, n. 21.
[74] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 17: AAS 57 (1965) uk. 20-21.
[75] Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, nn. 64-65: AAS 56 (1964) uk. 117.
[76] Taz. Kol 1:13. Kwa habari ya wokovu huo kutoka kwa utumwa wa shetani na wa giza, katika Injili, taz. Mt 12:28; Yn 8:44; 12:31 (rej. 1Yoh 3:8; Efe 2:1-2). Katika Liturujia ya Ubatizo, taz. Rituale Romano.
[77] Taz. Rum 6:4-11; Kol 2:12-13; 1Pet 3:21-22; Mk 16:16.
[78] Taz. 1The 3:5-7; Mdo 8:14-17.
[79] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 14: AAS 57 (1965) uk. 19.
[80] Taz. Mt. Augustino, Tract. In Ioann. 11, 4: PL 35, 1476.
[81] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 9: AAS 57 (1965) uk. 13.
[82] Taz. 1Kor 3:9.
[83] Taz. Efe 4:1.
[84] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 10, 11, 34: AAS 57 (1965) uk. 14-17; 39-40.
[85] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Divina Revelatione, Dei Verbum, n. 21: AAS 58 (1966) uk. 827.
[86] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 12, 35: AAS 57 (1965) uk. 16; 40-41.
[87] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 23, 36: AAS 57 (1965) uk. 28; 41-42.
[88] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 11, 35, 41: AAS 57 (1965) uk. 15-16; 40-41, 47.
[89] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Ecclesiis Orientalibus Catholicis, Orientalium Ecclesiarum, n. 4: AAS 57 (1965) uk. 77-78.
[90] Epist. Ad Diognetum, 5: PG 2, 1173; taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 38: AAS 57 (1965) uk. 43.
[91] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 32: AAS 57 (1965) uk. 38; Decr. De Apostolatu Laicorum, Apostolicam Actuositatem, nn. 5-7: AAS 58 (1966) uk. 842-844.
[92] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Institutione Sacerdotali, Optatam totius, nn. 4, 8, 9: AAS 58 (1966) uk. 716, 718-719.
[93] Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, nn. 17: AAS 56 (1964) uk. 105.
[94] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Institutione Sacerdotali, Optatam totius, n. 1: AAS 58 (1966) uk. 713-714.
[95] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 843-844.
[96] Taz. Conc. Vat. II, De Oecumenismo, Unitatis Redintegratio, n. 4: AAS 57 (1965) uk. 94-96.
[97] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 842.
[98] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 29: AAS 57 (1965) uk. 36.
[99] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 855.
[100] Hapa panaongelewa juu ya – jinsi wanavyotajwa – “makatekista wa muda wote” (full time catechists).
[101] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 31, 44: AAS 57 (1965) uk. 37, 50-51.
[102] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 838.
[103] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Presbyterorum Ministerio et Vita, Presbyterorum Ordinis, n. 11: AAS 58 (1966) uk. 1008; Decr. De Institutione Sacerdotali, Optatam totius, n. 2: AAS 58 (1966) uk. 714-715.
[104] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 25: AAS 57 (1965) uk. 29.
[105] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Presbyterorum Ministerio et Vita, Presbyterorum Ordinis, n. 10, ambapo, ili kurahisisha kazi maalum za uchungaji kati ya watu wa tabaka mbalimbali, panakubalika kuidhinisha “Prelatura personalia”, iwapo unaihitaji kweli unafuu wa uchungaji: AAS 58 (1966) uk. 1007.
[106] Taz. 1Kor 15:23.
[107] Taz. 1Kor 15:28.
[108] Taz. Efe 4:24.
[109] Taz. Zab 2:8.
[110] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 13: AAS 57 (1965) uk. 17-18.
[111] Taz. Hotuba ya Paulo VI kwenye kuwatangaza Watakatifu Mashahidi wa Uganda, 18 okt. 1964: AAS 56 (1964) uk. 908.
[112] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 13: AAS 57 (1965) uk. 18.
[113] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 17: AAS 57 (1965) uk. 26.
[114] Taz. Mk 3:13nk.
[115] Taz. 1Kor 12:11.
[116] Kwa jina la “Mashirika” ( Institutorum) vinanuiwa: Ordines, Congregationes, Instituta na Associationes ambavyo vinafanya kazi katika Misioni.
[117] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Rerum Ecclesiae, 28 feb. 1926: AAS 18 (1926) uk.69-71; Pius XII, Litt. Encycl. Saeculo exeunte, 13 juni 1940: AAS 32 (1940) uk. 256; Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 506.
[118] Taz. Mdo 13:2.
[119] Taz. Gal 1:16.
[120] Taz. 1Kor 9:22.
[121] Taz. Efe 6:19nk; Mdo 4:31.
[122] Taz. Mt 11:29nk.
[123] Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 449-450.
[124] Taz. 2Kor 6:4nk.
[125] Taz. 2Kor 8:2.
[126] Taz. 1Tim 4:14; Efe 4:23; 2Kor 4:16.
[127] Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 448-449; Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 507. Kuhusu malezi ya Mapadre wamisionari yafuatiliwe pia yaliyonenwa katika Conc. Vat. II, Decr. De Institutione Sacerdotali, Optatam totius.
[128] Taz. Mdo 2:42; 4:32.
[129] Taz. 2Tim 1:7.
[130] Taz. Flp 4:11.
[131] Taz. 2Kor 4:10nk.
[132] Taz. 2Kor 12:15nk.
[133] Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 41: AAS 57 (1965) uk.46.
[134] Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 440; Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 507.
[135] Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 448; Decr. S.C. de Propaganda Fide, 20 mei 1923: AAS 15 (1923) uk. 369-370; Pius XII, Litt. Encycl. Saeculo exeunte, 13 juni 1940: AAS 32 (1940) uk. 256; Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 507; Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 843-844.
[136] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Institutione Sacerdotali, Optatam totius, nn. 19-21: AAS 58 (1966) uk. 725-726; taz. pia Const. Apost. Sedes Sapientiae cum Statutis generalibus, 31 mei 1956: AAS 48 (1956) uk. 354-365.
[137] Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 523-524.
[138] Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 448; Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 507.
[139] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Fidei Donum, 15 jen. 1957: AAS 49 (1957) uk. 243.
[140] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Presbyterorum Ministerio et Vita, Presbyterorum Ordinis, n. 10, ambapo zipo habari za Majimbo na za Maaskofu wasio na Jimbo ( = “Prelatura Personalis”) na mambo kama hayo: AAS 58 (1966) uk. 1007.
[141] Taz. Rum 12:6.
[142] Taz. 1Kor 3:10.
[143] Taz. Yn 4:37.
[144] Taz. 1Kor 3:8.
[145] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 18: AAS 57 (1965) uk. 22.
[146] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 23: AAS 57 (1965) uk. 28.
[147] Taz. Paulus VI, Motu Proprio Apostolica Sollicitudo, 15 sep. 1965: AAS 57 (1965) uk. 776.
[148] Taz. Paulus VI, Hotuba ya tarehe 21 nov. 1964 iliyotolewa kwenye Mtaguso: AAS 56 (1964) uk. 1011.
[149] Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 39-40.
[150] Ikiwa, kwa sababu maalum, Misioni kadha wa kadha kwa sasa ziko chini ya Idara nyinginezo, yafaa Idara hizo zihusiane sana na “Sacra Congregatione de Propaganda Fide”, kusudi uwepo mwongozo ulio mmoja na sawa kwa ajili ya kuratibisha na kuongoza Misioni zote.
[151] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, n. 35, 4: AAS 58 (1966) uk. 691-692.
[152] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, n. 36-38: AAS 58 (1966) uk. 692-694.
[153] Conc. Vat. II, Decr. De Pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, n. 35, 5-6: AAS 58 (1966) uk. 691-692.
[154] Taz. Efe 4:13.
[155] Taz. Isa 11:12.
[156] Taz. Conc. Vat. II, De Oecumenismo, Unitatis Redintegratio, n. 12: AAS 57 (1965) uk. 99.
[157] Taz. Mdo 16:9.
[158] Taz. Mk 16:15.
[159] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 23, 24: AAS 57 (1965) uk. 27-29.
[160] Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919) uk. 453-454; Pius XI, Litt. Encycl. Rerum Ecclesiae, 28 feb. 1926: AAS 18 (1926) uk. 71-73; Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 jun. 1951: AAS 43 (1951) uk. 525-526; Id., Litt. Encycl. Fidei Donum, 15 jen. 1957: AAS 49 (1957) uk. 241.
[161] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Fidei Donum, 15 jen. 1957: AAS 49 (1957) uk. 245-246.
[162] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus Dominus, n. 6: AAS 58 (1966) uk. 675-676.
[163] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Fidei Donum, 15 jen. 1957: AAS 49 (1957) uk. 245.
[164] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965) uk.34.
[165] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Rerum Ecclesiae, 28 feb. 1926: AAS 18 (1926) uk. 72.
[166] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 44: AAS 57 (1965) uk.50.
[167] Taz. Mt 9:38.
[168] Taz. Mdo 16:14.
[169] Taz. 1Kor 3:7.
[170] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 33, 35: AAS 57 (1965) uk.30, 40-41.
[171] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 510-514. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 851-852.
[172] Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 46: AAS 57 (1965) uk.52.
[173] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Evangelii Praecones, 2 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 527. Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Princeps Pastorum, 28 nov. 1959: AAS 51 (1959) uk. 846.
[174] Taz. 1Tim 2:4.
[175] Taz. 2Kor 4:6.