Index

Back Top Print

[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya utume wa kichungaji
wa Maaskofu katika Kanisa
 

Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

  

UTANGULIZI

 

1. KRISTO BWANA (Christus Dominus), Mwana wa Mungu aliye hai, aliyekuja ili kuokoa watu wake kutoka kwa dhambi[1], na kusudi watu wote watakatifuzwe, kama alivyotumwa Yeye na Baba, vivyo hivyo aliwatuma Mitume wake[2], ambao aliwatakatifuza akiwapelekea Roho Mtakatifu, kusudi wao nao wamtukuze Baba hapa duniani, na kuwaokoa watu “hata mwili wa Kristo ujengwe” (Efe 4:12), ambao ni Kanisa.

Baba Mtakatifu na Maaskofu wanadumisha kazi ya Kristo

2. Katika Kanisa hili la Kristo, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Petro, ambaye Kristo alimkabidhi kondoo na wanakondoo zake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili, inayojitegemea na ya jumla kwa uangalizi wa roho za watu (curam animarum). Hivyo yeye, kwa kuwa amewekwa kuwa mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote ya Kanisa zima, na pia ya Makanisa pekee, anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote.

Vilevile na Maaskofu, waliowekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu[3], na, pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya madaraka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo, Mchungaji wa milele[4], kwa sababu Kristo aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Kwa hiyo, kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambaye wao walipewa, Maaskofu ndio waliofanywa Walimu kweli na halisi wa imani, Makuhani na Wachungaji[5].

3. Maaskofu, wakishiriki katika kuyahangaikia Makanisa yote, wanatimiza huduma na majukumu yao ya kiaskofu waliyopokea kwa kuwekwa wakfu [6], katika ushirika na chini ya mamlaka ya Baba Mtakatifu, katika yote yahusuyo Ualimu na Uongozi wa kichungaji, wote wakiwa umoja katika urika au mwili, kwa ajili ya Kanisa zima.

Maaskofu, kila mmoja kati yao, wanatimiza huduma hiyo kwa ajili ya sehemu za kundi la Bwana zilizokabidhiwa kwao kwa kuwa waangalifu juu ya Kanisa faridi ambalo kila mmoja alikabidhiwa. Lakini inawezekana pia kwamba Maaskofu wengine wasaidie kwa pamoja mahitaji yahusuyo Makanisa mbalimbali.

Ndiyo sababu, Mtaguso Mkuu huu, kwa kutazama hali ya jamii ya binadamu, ambayo siku hizi huelekea muundo mpya wa utaratibu[7], kwa nia ya kuainisha kinaganaga wajibu wa kichungaji wa Maaskofu, unathibitisha haya yafuatayo.

Sura ya Kwanza

MAASKOFU NA KANISA ZIMA

I - NAFASI YA MAASKOFU KWA AJILI YA KANISA ZIMA

Madaraka ya Urika wa Maaskofu

4. Maaskofu, kwa nguvu ya uwakfu wa kisakramenti (vi sacramentalis consecrationis) na kwa ushirika wa kihierarkia (hierarchica communione) pamoja na Kichwa cha Urika (Collegii Capite) na viungo vyake, wanafa-nywa washiriki wa Umoja huo wa Maaskofu.[8]. “Urika wa Maaskofu (Ordo Episcoporum) ni urithi wa urika wa Mitume katika kufundisha na katika uongozi wa kichungaji; na ndani yake umoja wa Mitume huendelezwa katika nyakati. [Urika huo wa Maaskofu] pamoja na Kichwa chake aliye Baba Mtakatifu, na kamwe pasipo yeye, una mamlaka ya juu kabisa na kamili juu ya Kanisa lote. [Mamlaka hiyo] yaweza kutekelezwa tu kwa idhini ya Baba Mtakatifu”[9]. Kwa kweli mamlaka hii “hutekelezwa kwa jinsi iliyo rasmi katika Mitaguso Mikuu”[10]; hivyo sinodi hii takatifu huamua kwamba Maaskofu wote, walio wanachama wa Urika wa Maaskofu, wanayo haki ya kuhudhuria Mtaguso Mkuu.

“Mamlaka hiyohiyo ya Urika [wa Maaskofu] yaweza kutekelezwa na Maaskofu walioko pande zote za dunia wakishirikiana na Baba Mtakatifu, ilimradi mkuu wa Urika awe amewaita kutenda kiurika, au walau aidhinishe au kukubali kwa hiari tendo la pamoja la Maaskofu waliotawanyika, ili lipate kuwa kweli tendo la kiurika ( actus collegialis)” [11].

Sinodi (au Halmashauri kuu) ya Maaskofu

5. Maaskofu waliochaguliwa kutoka katika sehemu mbalimbali za dunia wataweza kutoa msaada wa kufaa kweli kwa Mchungaji Mkuu wa Kanisa, kulingana na utaratibu uliowekwa au utakaowekwa na Baba Mtakatifu mwenyewe, wakiwa wamekutanika katika Halmashauri ambayo jina lake halisi ni “Sinodi ya Maaskofu”[12]. Sinodi ambayo kwa kuwakilisha Uaskofu wote wa kikatoliki, inadhihirisha kwamba Maaskofu wote wanayashiriki, katika muungano wa kihierarkia, mahangaiko kwa ajili ya Kanisa zima[13].

Maaskofu wanashiriki mahangaiko ya Kanisa zima

6. Maaskofu, kwa kuwa ni waandamizi halali wa Mitume, na pia wanaumoja wa urika wa Maaskofu, wajue daima kuunganika kati yao, na kujihangaisha kwa ajili ya Makanisa yote. Wakumbuke pia kwamba, kwa agizo la kimungu, na amri ya huduma ya kitume, kila mmoja kati yao, pamoja na Maaskofu wengine, ni mdhamini wa Kanisa[14]. Kwa namna ya pekee wajiwajibishe katika sehemu zile za dunia ambapo Neno la Mungu halijatangazwa bado, au pale ambapo, kwa sababu ya uhaba wa mapadre, waamini wamo hatarini mwa kuacha matendo ya maisha ya kikristo, au zaidi kupoteza hata imani yenyewe.

Kwa hiyo, Maaskofu wajitahidi ili kwamba waamini wasimamie na kutegemeza kwa ari matendo ya uinjilishaji na ya kitume. Wafanye bidii pia katika kuandaa mapadre wastahivu, na wasaidizi watawa kwa walei, sio tu kwa ajili ya Misioni, lakini pia kwa kanda ambazo zina uhaba wa wakleri. Wajitahidi iwezekanavyo ili wengine miongoni mwa wakleri wao waende katika nchi za misioni au majimboni tulivyosema hapo juu, ili kutekeleza huduma takatifu [ya upadre], kwa maisha yao yote, au walau kwa muda maalum.

Maaskofu wakumbuke kwamba, katika matumizi ya mali za Kanisa, inatakiwa kutazama siyo mahitaji ya Jimbo lao tu, bali pia ya Makanisa faridi mengine, kwa sababu hayo nayo ni sehemu ya Kanisa la Kristo lililo moja. Kisha, watakiwa kuhudumia majimbo au kanda nyinginezo ambazo zakabiliwa na mahitaji na shida.

Mapendo hai kwa ajili ya Maaskofu wanaodhulumiwa

7. Maaskofu wawakumbatie kwa upendo wa kidugu na kwa matendo ya huruma hasa Maaskofu wale ambao, kwa sababu ya jina la Kristo, wanaudhiwa kwa masingizio na dhuluma, au wamefungwa gerezani, au wanazuiliwa kutekeleza huduma yao. Kwa kufanya hivyo, kwa njia ya sala na matendo, wadhamirie kutuliza na kupunguza mateso ya [Maaskofu] wenzao.

II - MAASKOFU NA KITI KITAKATIFU (CHA ROMA)

Mamlaka ya Maaskofu katika majimbo yao

8. a) Maaskofu, kama waandamizi wa Mitume, katika majimbo waliyokabidhiwa wanayo moja kwa moja mamlaka yote ya kawaida, halisi na inayojitegemea inayohitajika ili kutekeleza huduma yao ya kichungaji, isipokuwa inadumu katika nyanja zote mamlaka ya Baba Mtakatifu, kwa nguvu ya huduma yake, ya kukabidhi kwake yeye mwenyewe au kwa mamlaka nyingine, masuala fulani.

b) Kila Askofu wa jimbo, katika shida maalum, anapewa uwezo wa kuwaondolea (in casu particulari dispensandi) kutoka kwa sheria ya kawaida ya Kanisa, waamini ambao kwa mujibu wa sheria anayo madaraka juu yao. Hilo lifanyike kila wanapoona kuwa inafaa kwa manufaa yao ya kiroho; kama hakuna kipingamizi maalum kilichowekwa kuhusu hilo na Mamlaka kuu ya Kanisa.

Idara za Kuria ya Roma

9. Katika utekelezaji wa mamlaka yake ya juu kabisa, kamili na inayojitegemea juu ya Kanisa zima, Baba Mtakatifu anatumia Idara za Kuria ya Roma, ambazo, kwa hiyo, zinatimiza kazi zao kwa jina lake na kwa mamlaka yake, kwa manufaa ya Makanisa, na kwa utumishi wa Wachungaji watukufu.

Lakini Mababa wa Mtaguso Mkuu wanatoa pendekezo kwamba Idara hizo, ambazo bila shaka mpaka sasa zimetoa msaada mkubwa kwa Baba Mtakatifu na kwa Wachungaji wa Kanisa, zipewe utaratibu mpya, unaolingana zaidi na mahitaji ya nyakati zetu, ya kanda na ya Riti, hasa kwa mambo yahusuyo idadi yake, majina rasmi, wajibu, utaratibu wa utendaji, uratibu wa kazi zake[15]. Hali kadhalika wanatumaini kwamba, kutokana na majukumu ya kichungaji ya Maaskofu, wadhifa wa Mabalozi (Legatorum) wa Baba Mtakatifu udhihirishwe wazi zaidi.

Washiriki wa Idara za Roma

10. Zaidi ya hayo, kwa vile Idara hizo zimesimikwa kwa manufaa ya Kanisa zima, hutamanika pia kuwa washiriki wake, Maafisa na wasaidizi wake, hali kadhalika Mabalozi wa Baba Mtakatifu, kadiri iwezekanavyo, wazidi kuchaguliwa, kwa kiwango kikubwa, kutoka kwa kanda mbalimbali za Kanisa, ili maofisi, yaani taasisi (officia seu organa) kuu za Kanisa Katoliki ziwe kweli na tabia ya ulimwengu mzima.

Inasisitizwa pia kwamba miongoni mwa washiriki wa Idara hizo wateuliwe pia Maaskofu wengine, hasa wa majimbo; kusudi kwa namna ya ndani zaidi waweze kumtaarifu Baba Mtakatifu mawazo, matarajio na mahitaji ya Makanisa yote.

Hatimaye, Mababa wa Mtaguso wanathamini kuwa ya manufaa kweli kwamba Idara tukufu zitake ushauri – zaidi kuliko ilivyotokea katika vipindi vilivyopita – kutoka kwa walei, wanaotambulikana kwa utauwa, elimu na mang’amuzi; ili wao nao wawe na nafasi ya kufaa katika mambo ya Kanisa.

Sura ya Pili

MAASKOFU NA MAKANISA FARIDI

I - MAASKOFU WA MAJIMBO

Dhana ya jimbo na wajibu wa Maaskofu

11. Jimbo ni sehemu ya watu wa Mungu iliyokabidhiwa kwa uchungaji wa Askofu akishirikiana na mapresbiteri (presbyterii)[, yaani mapadre,] wake, ili kwamba likiambatana na mchungaji wake na likikusanywa naye kwa njia ya Injili na ya Ekaristi Takatifu katika Roho Mtakatifu liunde Kanisa faridi. Katika hilo, Kanisa la Kristo lililo Moja, Takatifu, Katoliki na la Kitume kweli lipo na hutenda.

Kila Askofu, ambaye amekabidhiwa uangalizi wa Kanisa faridi, chini ya mamlaka ya Baba Mtakatifu, kama mchungaji halisi, wa kawaida na anayejitegemea, anawachunga kondoo zake kwa jina la Bwana, na anatekeleza kwa manufaa yao majukumu ya kufundisha, kutakatifuza na kuo-ngoza. Lakini anatakiwa kutambua haki halali za Mapatriarka na pia za Viongozi wengine wa kihierarkia[16].

Maaskofu watakiwa kutekeleza majukumu yao ya kitume kama mashahidi wa Kristo mbele ya watu wote, wakishughulikia sio wale tu ambao tayari wanafuasa Mkuu wa Wachungaji, bali wakijitoa kwa moyo wote kwa ajili ya wale ambao kwa namna zozote zile walijitenga na njia ya ukweli, au bado hawajajua Injili ya Kristo na huruma yake yenye kuokoa; hadi wote watakapoendea njia ya “wema wote na haki na kweli” (Efe 5:9).

Jukumu la kufundisha

12. Katika kutekeleza jukumu lao la kufundisha, [Maaskofu] wawatangazie wote Injili ya Kristo, nalo ni kati ya majukumu muhimu zaidi ya Maaskofu[17]; na wafanye hivyo kwa kuwaalika watu kwenye imani katika nguvu ya Roho au kwa kuwathibitisha uhai wa imani yao. Wawafunulie fumbo zima la Kristo, yaani zile kweli ambazo kutozifahamu maana yake ni kutomfahamu Kristo mwenyewe; na pia wawaonyeshe njia iliyofunuliwa na Mungu, ambayo inaongoza kwenye kumtukuza Bwana, na papo hapo, kwenye heri ya milele[18].

Waonyeshe pia kwamba vitu vyenyewe vya dunia na asasi za wanadamu, katika mpango wa Mungu Muumbaji zimeamriwa kwa wokovu wa wanadamu; hivyo zaweza kusaidia siyo kidogo kwa ujenzi wa Mwili wa Kristo.

Kwa sababu hiyo wafundishe, kulingana na mafundisho ya Kanisa, thamani ya hadhi ya binadamu, ya uhuru wake, na ya uzima wenyewe wa mwili wake; thamani ya familia, ya umoja na uimara wake, ya kuzaa na kulea watoto; thamani ya jamii, pamoja na sheria zake na taaluma za kazi mbalimbali zilizomo ndani yake; thamani ya kazi na ya burudani, ya sanaa na ya teknolojia; thamani ya umaskini na ya wingi wa mali. Hatimaye watamke jinsi inavyopasa kutatua shida na matatizo makuu yahusuyo umilikaji wa mali, uzalishaji wake na ugawaji wake wa haki, ya amani na ya vita na ya kuishi kidugu kwa watu wote[19].

Jinsi inavyotakiwa kufundisha ukristo leo

13. [Maaskofu] watakiwa kutoa mafundisho ya kikristo kulingana na mahitaji ya wakati wanaoishi: yaani kwa namna inayofaa kulingana na magumu na matatizo ambayo watu wa siku hizi wanakabiliwa na kufadhaishwa nayo. Hiyo imani lazima pia waitunze sio wao tu, bali pia wawafundishe waamini kuitetea na kuieneza. Mafundisho hayo yatolewe kwa namna ya kuonyesha mahangaiko ya kimama ya Kanisa kwa ajili ya watu wote, waaminio na wasioamini; wakionyesha uangalifu wa pekee kwa maskini na wadhaifu zaidi, kwa kukumbuka kwamba walitumwa na Bwana kutangaza Injili kwao.

Na kwa vile Kanisa linatakiwa kuhusiana na jamii ya wanadamu [20], ambamo linaishi, ni juu ya Maaskofu kwanza ule wajibu wa kuwakaribia watu, na kuanzisha na kusitawisha mawasiliano nao. Halafu, ili katika mazungumzo hayo ya kufaa ukweli uendane daima na mapendo, na uelewano na upendo, basi inabidi hayo yaendelezwe kwa ufasaha wa lugha, kwa uvumilivu na upole, lakini pia kwamba busara inayotakiwa iendane na kuaminiana; ili, kwa kuaminiana, urafiki uzushwe na roho za watu ziunganike [21].

Kwa ajili ya uenezaji wa imani ya kikristo watumie njia zinazopatikana siku hizi; kwanza kabisa mahubiri na mafundisho ya katekesi, ambayo yana daima umuhimu wa pekee; lakini pia mafundisho ya imani katika shule, katika vyuo vikuu, katika semina na mikutano ya aina zote; hatimaye, pia kwa matamko ya hadharani, kwenye matukio maalum, ya kutolea kwa njia ya uchapishaji na vyombo mbalimbali vya upashanaji habari, ambavyo vyafaa vitumiwe kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo[22].

Mafundisho ya katekesi

14. [Maaskofu] wafanye bidii ili yatolewe kwa namna ya kufaa mafundisho ya katekesi, ambayo lengo lake ni kukuza imani katika watu, iwe hai, wazi na ya utendaji, kwa watoto na kwa vijana na kwa watu wazima, kwa njia ya mafundisho maangavu. Waangalie ili mafundisho hayo yatolewe kufuatana na utaratibu na mtindo unaolingana sio tu na mada yenyewe, bali pia na tabia, uwezo, umri na jinsi ya kuishi ya wasikilizaji. Yawe yana misingi katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo, juu ya Liturjia na Majisterio na maisha ya Kanisa.

Washughulike pia ili kuwaandaa makatekista kwa namna ifaayo kuitimiza huduma yao, hivi kwamba wafahamu kwa ndani mafundisho ya Kanisa, na wajifunze kinadharia na kwa matendo sheria za saikolojia na mambo ya kipedagojia.

Wazingatie kuanzisha upya, au kurekebisha kufuatana na nyakati zetu, taasisi ya ukatekumeni wa watu wazima.

Jukumu la kutakatifuza

15. Katika kutekeleza jukumu lao la kutakatifuza, Maaskofu wakumbuke kuwa wamechaguliwa miongoni mwa watu wote na kuwekwa kwa ajili ya watu wote, katika yote yaliyo ya Mungu, ili kutoa vipaji na sadaka kwa ajili ya dhambi. Maana Maaskofu wamejaliwa utimilifu wa Sakramenti ya Daraja Takatifu; pia, katika kutekeleza mamlaka yao, wanawategemea mapresbiteri (au mapadre) ambao pia waliwekwa wakfu kama makuhani wa kweli wa Agano Jipya ili wawe wasaidizi wakimu ( provvidi) wa daraja ya kiaskofu; na pia mashemasi, ambao walipewa Daraja kwa huduma, katika ushirikiano na Askofu na Mapresbiteri wake, ili kuwatumikia watu wa Mungu. Kutokana na hayo, Maaskofu ni mawakili wa kwanza wa siri za Mungu (1Kor 4:1), na vilevile viongozi, wahimizi na waangalizi wa maisha yote ya kiliturujia katika Kanisa lililokabidhiwa kwao [23].

Wajitahidi daima kwa bidii ili waamini wafahamu na kuishi kwa njia ya Ekaristi kwa undani zaidi fumbo la kipasaka, ili kupata kuwa mwili mmoja uliofungamana katika umoja wa upendo wa Kristo[24]. “Wakidumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno” (Mdo 6:4), wafanye bidii sana ili wote wanaoshughulikiwa nao waweze kuwa na nia moja katika kusali[25], ili pia, kwa kuzipokea Sakramenti, wakue katika neema na wawe mashahidi waaminifu wa Bwana.

Kama wakamilishi, Maaskofu wajitahidi kukuza utakatifu wa Mapadre wao, wa watawa na wa walei, kulingana na wito wa pekee wa kila mmoja[26]; hali wakikumbuka kuwa wao wenyewe watakiwa kuwa kielelezo cha utakatifu, katika upendo, katika upole na unyenyekevu wa maisha. Watakatifuze Makanisa yaliyokabidhiwa kwao hadi tabia ya Kanisa lote zima la Kristo lipate kung’aa wazi. Kwa hali hiyo, wachochee kwa kiasi kikubwa miito ya kipadre na ya kitawa, na kwa juhudi ya pekee, ya kimisionari.

Jukumu la kuongoza kama wachungaji wa roho

16. Katika kutekeleza jukumu lao kama baba na kama wachungaji, Maaskofu wawe kati ya kundi lao kama wale watumikao[27], wawe kama wachungaji wema wajuao kondoo zao na kujuliwa nao; kama baba kweli watendao kutokana na moyo wao wa mapendo na wa bidii kwa ajili ya wote. Na kwa mamlaka yao, ambayo kweli walipokea kutoka kwa Mungu, waamini wote wanawanyenyekea kwa furaha. Wakusanye familia nzima ya kundi lao na wailee ili kila mmoja, akiwa amefahamishwa wajibu wake, aishi na kutenda katika ushirika wa mapendo.

Ili kulifikia lengo hilo Maaskofu, wakiwa “tayari kwa kila kazi iliyo njema” (2Tim 2:21) na “wakistahimili mambo yote kwa ajili ya wateule” (2Tim 2:10), waratibishe maisha yao, ili yaendane na mahitaji ya nyakati.

Wawatendee mapadre kwa hisani, kama watu ambao, kwa upande wao, wanajibebesha majukumu na mahangaiko kwa uangalizi wa makini katika maisha ya kila siku. Wawatambue kama wanao na marafiki[28], hivyo wawe tayari kuwasikiliza na kuwatendea kwa uaminifu na wema. Aidha wajitahidi kusukuma utekelezaji wa kazi ya kichungaji katika jimbo zima.

Washughulike hali zote za kiroho, za kielimu na za kimwili, za mapadre wao, ili nao wenyewe, kwa njia ya maisha ya utakatifu na ya utauwa, waweze kutekeleza huduma yao kiaminifu na kwa manufaa. Kwa lengo hilo, wasimamie asasi zilizopo na waanzishe upya ile mikutano ambamo mapadre mara kwa mara waweza kupata nafasi ya kukutana ama kwa ajili ya upyaisho wa maisha yao, kwa njia ya kozi ndefu kidogo za mazoezi ya kiroho, ama kwa ajili ya kujiendeleza katika taaluma za kikanisa, hasa Maandiko Matakatifu na teolojia, masuala ya kijamii yenye uzito zaidi, na mbinu mpya za uchungaji. Wawafuatilie kwa huruma ya kimatendo mapadre wale ambao kwa sababu fulani wako hatarini, au waliepa kwa namna yoyote wajibu wao.

Ili kufaulu kuwapatia waamini yaliyo mema, kadiri ya hali ya kila mmoja, wafanye bidii sana ili kufahamu kwa ndani mahitaji yao katika mazingira wanamoishi, wakitumia mbinu zote zenye kufaa kwa madhumuni hayo, hasa utafiti wa kijamii. Wajitahidi kuwa waangalifu kwa watu wote, bila ubaguzi wa umri, cheo, wala utaifa; kwa wazalendo sawa kama kwa wageni au wapitaji. Katika kutekeleza tendo hilo la uchungaji waheshimu kiwango cha uwajibikaji wa wanajimbo wao katika mambo ya Kanisa, wakiwakubalia wajibu na haki za kushirikiana kimatendo katika kujenga Mwili wa fumbo wa Kristo.

[Maaskofu pia] wawafuatilie kwa upendo ndugu Wakristo waliojitenga, vilevile wawahimize waamini wao ili wawatendee kwa ukarimu na mapendo. Hali kadhalika, wasimamie shughuli za kiekumeni, kulingana na mwongozo wa Kanisa [29]. Wawapende kwa dhati pia wale wasiobatizwa, ili upendo wa Kristo Yesu, ambao Maaskofu ni mashahidi mbele ya watu wote, udhihirike pia kwao.

Shughuli nyinginezo za kitume

17. Aina mbalimbali za utume zisitawishwe katika jimbo kwa ujumla, na pia katika sehemu zake pekee, na matendo hayo yote ya kitume yaratibishwe na kuunganika kwa ndani, chini ya uongozi wa Askofu. Kwa hali hiyo, uanzishaji na utekelezaji wote wa katekesi, wa umisioni, wa matendo ya huruma, wenye tabia ya kijamii, ya kifamilia, kuhusu elimu, na kazi zozote zingine zenye lengo la kichungaji, ziunganike kuwa tendo lenye nia moja, ambalo lasaidia pia ili umoja wa jimbo uonekane wazi.

Wawakazie kwa bidii waamini wenyewe kwamba, kulingana na hali na mali zao, wana wajibu wa kufanya kazi ya kitume, na wawahimize kushiriki na kuchangia katika asasi mbalimbali za kitume za walei, na hasa katika Aksio Katoliki. Aidha, waongeze idadi na wasimamie umoja na vyama ambavyo moja kwa moja, au kwa mzunguko, vinaelekeza kwenye mambo ya milele: yaani vinasaidia au kujipatia maisha matakatifu, au kutangaza Injili ya Kristo kati ya watu wote, au kueneza mafundisho ya kikristo na kukuza ibada za hadhara, au kupata maendeleo katika mambo ya kijamii, au katika kutekeleza matendo ya huruma na ya mapendo.

Kazi hizo za kitume lazima zilinganishwe na mahitaji ya siku hizi, kwa kuzingatia hali na matarajio ya watu: siyo yale ya kiroho na ya kimaadili tu, bali pia yale yahusuyo jamii, demografia na uchumi. Na ili kufanikiwa kulifikia kwa manufaa lengo hilo, kuwe na msaada kutokana na tafiti za elimujamii za kidini, zifanywazo kwa mujibu wa ofisi za elimujamii za kichungaji, ambazo zapendekezwa kwa bidii sana kuwepo.

Uangalifu wa pekee kwa makundi maalum ya waamini

18. Inatakiwa kuwepo uangalifu wa pekee kwa waamini wale ambao, kutokana na hali ya maisha yao, hawawezi kufaidia kikamilifu misaada ya kawaida ya kichungaji kutoka kwa maparoko, au wanaikosa kabisa; k.v. wahamiaji walio wengi, wakimbia kwao, wakimbizi, mabaharia, wahudumu wa usafiri wa anga, wahamahamaji na watu wa aina kama hizo. Zihamasishwe mbinu za kichungaji ziwezazo kusaidia maisha ya kiroho ya watalii.

Mabaraza ya Maaskofu, hasa ya kitaifa, yatazame kwa uangalifu mah-susi matabaka hayo ya watu, na kwa vyombo na asasi zifaazo yashughulikie na kusisimua utunzo wa mambo yao ya kiroho, katika maafikiano ya nia na bidii. Hayo yafanyike kwa kutazama kwanza miongozo iliyotolewa na itakayotolewa na Kiti cha Kitume [30], baada ya kuyalinganisha na mazingira ya nyakati, ya mahali na ya wahusika.

Uhuru wa Maaskofu na mahusiano yao na mamlaka ya kiserikali

19. Katika kutekeleza jukumu lao la kitume, linalonuia wokovu wa roho [za watu], Maaskofu kwa haki wanafaidi uhuru wa kujitawala kamili na timilifu mbali na mamlaka yoyote ya kiserikali. Ndiyo sababu si halali kukinza, kwa wazi au kwa kuficha, utekelezaji wa majukumu yao ya kikanisa, wala kuwazuia wasiwasiliane kwa uhuru na Kiti cha Kitume, na mamlaka nyinginezo za kikanisa, pia na waamini wao.

Bila shaka Wachungaji Watukufu, wakati wanaposhughulikia mema ya kiroho ya kundi lao, papo hapo wanasukuma pia maendeleo ya kijamii na ya kiserikali na fanaka ya umma. Hivyo katika mipaka ya wajibu wao na kulingana na hali yao ya uaskofu, wanaunganisha harakati zao za utendaji na nia za serikali ya umma kwa kuwakazia waamini utii wa sheria zilizo za haki, na heshima kwa mamlaka iliyoidhinishwa kihalali.

Uhuru katika uteuzi wa Maaskofu

20. Kwa vile wadhifa wa kitume wa Maaskofu uliasisiwa na Kristo Bwana na hulenga shabaha za kiroho na zisizo za ulimwengu huu, Mtaguso Mkuu huu umeazimia kwamba haki ya kuteua na ya kutawaza Maaskofu ni haki halali na maalum ya mamlaka ya kikanisa husika peke yake.

Kwa hiyo, ili kulinda, ilivyo haki, uhuru wa Kanisa, na kuhamasisha zaidi na zaidi na kwa namna ya kufaa mema ya waamini wakristo, Mtaguso Mkuu huu unatarajia kuwa wakati unaokuja, mamlaka ya kiserikali isipewe tena haki au fadhila za kuchagua, kuteua, kupendekeza, wala kuidhinisha wadhifa wa Uaskofu. Mtaguso huu mkuu, pamoja na kutoa shukrani, na sifa za dhati kwa heshima iliyoonyeshwa kwa Kanisa, unawaomba kwa radhi ya moyo wenye mamlaka wale ambao mpaka sasa, kwa mujibu wa makubaliano au kawaida za pekee, walishika haki au mapendeleo hayo, ili baada ya kufanya maafikiano na Kiti cha Kitume, sasa wakubali kuyaacha kwa hiari yao.

Kujiuzulu kutoka katika huduma ya kiaskofu

21. Kwa vile wadhifa wa kichungaji wa Maaskofu una umuhimu wa pekee na unabeba majukumu mazito, linatolewa ombi kunjufu kwa Maaskofu wa jimbo na kwa wale wenye dhima ileile kwa mujibu wa sheria, ili kwamba, wangekuja kushindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na umri mkubwa au kwa sababu nzito nyingineyo yote, wajiuzulu kutoka katika ofisio yao, kwa hiari au kwa kualikwa na mamlaka husika. Kwa upande wake, mamlaka hiyo, ikiwa inakubali kujiuzulu [kwa Askofu], ihakikishe ya kuwa matunzo yafaayo yanatolewa kwa waliostaafu, pamoja na kuwakubalia haki maalum.

II - MAENEO YA MAJIMBO

Marekebisho ya mipaka ya majimbo

22. Kwa madhumuni ya kulifika lengo halisi la jimbo inabidi kwamba tabia ya Kanisa ionekane waziwazi katika watu wa Mungu wanaoishi katika eneo la jimbo lile; tena kwamba Maaskofu waweze kutimiza kwa manufaa majukumu yao ya kichungaji; hatimaye, kwamba huduma ya kiroho ya watu wa Mungu itolewe kikamilifu inavyowezekana.

Kutokana na hayo yote, pamoja na mipaka ya eneo la jimbo kupambanuliwa kwa namna ya kufaa, inatakiwa pia wakleri na mali zigawanywe kirazini (rationem consentaneam), kulingana na madai ya utume. Na hayo yote hayatakuwa kwa faida ya wakleri na waamini wakristo wahusika fika tu, lakini pia kwa faida ya Kanisa Katoliki kwa ujumla.

Kwa hiyo, kwa habari za maeneo ya majimbo, Mtaguso Mkuu huu unaagiza kwamba, mema ya roho yanapodai hivi, mapema iwezekanavyo marekebisho yafanyike kwa busara, ama kwa kugawa au kugawanya au kuunganisha, ama kwa kubadili mipaka yenyewe, ama kwa kuhamishia panapofaa zaidi makao ya Askofu, ama mwishowe, hasa kwa habari za majimbo yenye miji mikubwa, kwa kuyapa utaratibu mpya wa ndani.

Utaratibu wa marekebisho

23. Katika marekebisho ya maeneo ya majimbo kuwepo na uangalifu katika kuhifadhi hasa umoja wa mfumo wa kila jimbo, kwa habari za watu, maofisi, taasisi, kwa mithili ya mwili maridhawa ulio hai. Kila mara, baada ya kutathmini kwa makini hayo yote, vigezo hivi vya jumla vizingatiwe:

1) Katika kudizaini eneo la jimbo, suala la mchanganyiko wa watu wa Mungu lizingatiwe kadiri inavyowezekana, kwa sababu hilo linasaidia utekelezaji wa kazi za kichungaji. Wakati huohuo, zitafutwe njia za kuweza kuwianisha maeneo ya kidemografia ya watu hao na maofisi ya kiserikali na taasisi za kijamii, ambazo ni zana za mfumo wake wenyewe. Hivyo eneo la kila jimbo lisitenganike kamwe.

Kama mazingira yaruhusu, mipaka ya maeneo ya kiserikali ifuatwe, na vilevile hali ya pekee, k.m. ya kisaikolojia, ya kiuchumi, ya kijiografia na kihistoria ya watu na ya mahali.

2) Kwa kawaida, ukubwa wa eneo la jimbo na idadi ya wakazi wake ziwe za kiasi ambacho, kwa upande mmoja, Askofu – hata kama anasaidiwa na wengine – aweze kuongoza mwenyewe maadhimisho ya sikukuu maalumu (pontifikali), aweze kutimiza ipasavyo ziara za kichungaji, kuongoza na kuratibisha kazi zote za kichungaji jimboni, na hasa kuwafahamu mapadre wake, watawa na walei wanaoshiriki kwa namna moja au nyingine katika utendaji jimboni. Kwa upande mwingine, liandaliwe ‘shamba’ kubwa la kutosha na la kuridhisha, ambamo Askofu kwa mapadre waweze kujitolea kwa faida kwa nguvu zao zote katika huduma, wakizingatia mahitaji ya Kanisa zima.

3) Hatimaye, ili huduma ya wokovu itolewe jimboni kwa manufaa zaidi, kwa kawaida wawepo katika kila jimbo mapadre wa kutosha kwa idadi na idhini, kwa ajili ya uangalizi wa kiroho wa watu wa Mungu. Maofisi, taasisi na amali za kawaida katika kila Kanisa faridi zisikosekane, yaani, zile ambazo zahitajika kwa ajili ya uongozi wake thabiti na ya utekelezaji wa utume wake. Mwisho, mipango ifanyike ili ziweze kupatikana, kama bado hazipo, mali za kuweza kutegemeza bila kukosa maslahi ya watu na udumifu wa taasisi za kijimbo.

Kwa ajili ya hayo, pale ambapo wanakuwepo waamini wa riti tofauti, Askofu anatakiwa kuwashughulikia mahitaji ya kiroho, au kwa njia ya mapadre na maparokia ya riti hiyohiyo; ama kwa njia ya vika wa kiaskofu aliyepewa madaraka mahsusi, ambaye, ikiwa itafaa, apewe hadhi ya uaskofu pia; ama kwa njia yake binafsi, akitimiza jukumu la mkuu wa riti mbalimbali. Lakini, ikiwa hayo yote, kwa uamuzi wa Kiti cha Kitume, kulingana na sababu maalum, hayafuatiliki, hapo hierarkia mahsusi iundwe kwa kila riti[31].

Hali kadhalika, kwa mazingira kama hayo, waamini wa lugha tofauti washughulikiwe ama kwa njia ya mapadre na maparokia ya lugha hiyo; ama kwa njia ya vika wa kiaskofu, mwenye kujua vizuri lugha hiyo na akiwa pia, kama itafaa, mwenye hadhi ya uaskofu; ama kwa mbinu nyingineyo yote yenye kufaa.

Kushauriana na Mabaraza ya Maaskofu

24. Kabla ya kuchukua mabadiliko au upyaisho kuhusu majimbo kulingana na mwongozo wa namba 22 na 23, pasipo kuathiri utaratibu wa Makanisa ya Mashariki, yafaa maoni yapelekwe kuchunguzwa na Mabaraza ya Maaskofu halali kwa eneo husika. Nayo, yakiamua kuwa inafaa, yatakubali kusaidiwa na kamati maalum ya kiaskofu, na kila mara yatapokea maoni ya Maaskofu wa provinsi au wa kanda husika. Baada ya hapo [Mabaraza] yatapeleka mawaidha na mapendekezo yao kwa Kiti cha Kitume.

III - WASAIDIZI WA ASKOFU WA JIMBO

I - MAASKOFU WAANDAMIZI NA MAASKOFU WASAIDIZI

25. Kwa habari ya uongozi wa majimbo, huduma ya kichungaji ya Maaskofu iandaliwe ili lengo lake kuu liwe mema ya kundi la Bwana. Kusudi mema hayo yapatikane kwa njia iliyo bora, sio mara chache ni vema kusimika Maaskofu wasaidizi, kwa sababu Askofu wa jimbo, ama kwa ajili ya upana wa eneo la jimbo lake, ama kwa idadi kubwa mno ya wakazi wake, ama kwa visa vya pekee vya kitume au vingine vya aina mbalimbali, hawezi kutimiza wajibu wake wote wa kiaskofu kadiri ya madai ya mema ya roho. Tena, pengine, mahitaji ya pekee yasababisha kuwa Askofu wa jimbo mwenyewe apewe kama msaidizi Askofu Mwandamizi. Hao Maaskofu, Msaidizi kwa Mwandamizi, lazima wapewe uwezo maalum ili kwamba, pasipo kuathiri umoja wa uongozi katika jimbo, utendaji wao uwe wa mafanikio, na hadhi yao, iliyo halisi ya kiaskofu, ilindwe zaidi.

Maaskofu waandamizi na wasaidizi, basi, kwa vile wanavyoitwa kuushiriki uangalizi wa Askofu wa jimbo, wanatakiwa kutimiza majukumu yao kwa namna ambayo, katika mambo yote watatenda daima kwa maafikiano kamili naye. Aidha, waonyeshe daima utii na heshima kwa Askofu wa jimbo; naye, kwa upande wake, awapende na awaheshimu kama ndugu.

Uwezo wa Maaskofu wasaidizi na waandamizi

26. Endapo mema ya roho yanadai hivyo, Askofu wa jimbo asione tatizo kuomba kwa Mamlaka halali, msaidizi mmoja au kadhaa, yaani wale ambao wasimikwa kwa ajili ya jimbo, lakini hawana haki ya kurithi.

Kama haijaagizwa kwenye barua ya uteuzi, Askofu wa jimbo amfanye Msaidizi wake, au Wasaidizi, kuwa Makamu wake, au walau Vika wa kiaskofu, wenye kutegemea mamlaka yake tu, na apende kushauriana nao kila anapodaiwa kutafakari masuala yenye umuhimu mkubwa, hasa ya aina ya kichungaji.

Isipokuwa mipango mingine ilifanywa na Mamlaka halisi, uwezo na madaraka waliyo nayo Maaskofu Wasaidizi kwa mujibu wa sheria havimalizwi pamoja na kwisha huduma ya Askofu wa jimbo. Bali, ni afadhali kwamba pindi kiti cha kiaskofu kiwapo wazi, wadhifa wa kusimamia jimbo – isipokuwa mipango mingine imelazimishwa na sababu nzito – apewe Askofu Msaidizi au, kama wapo zaidi ya mmoja, mmojawapo wa hao.

Askofu Mwandamizi, yaani yule aliyeteuliwa na kupewa haki ya kurithi, daima hana budi kuteuliwa na Askofu wa jimbo awe ni Makamu wake. Na Mamlaka halisi yanaweza kumpa hata uwezo mkubwa zaidi, kwa sababu za pekee.

Kwa ajili ya kutunza mema ya sasa na ya baadaye ya jimbo, Askofu wa jimbo na Askofu Mwandamizi wake, katika masuala yenye umuhimu mkubwa zaidi, wasikose kushauriana wao kwa wao.

II - KURIA NA HALMASHAURI ZA JIMBO

27. Katika Kuria ya jimbo ni muhimu hasa ofisio ya Makamu wa Askofu. Hivyo, kwa kadiri utawala sahihi wa jimbo unavyodai, Askofu anaweza kumteua [pia] Vika wa kiaskofu mmoja, au Mavika kadhaa, ambao kwa dhati ya sheria huwa na madaraka sawa na yale ambayo sheria ya jumla humpa Makamu wa Askofu, iwe katika eneo maalum ya jimbo, au katika fani fulani ya shughuli, au juu ya waamini wa riti fulani.

Kati ya wenzi wa Askofu katika uongozi wa jimbo wahesabika pia wale mapadre wanaounda ‘senato’ yake na halmashauri yake: k.v. wale wa kapitulo ya katedrali, na wa jopo la washauri, au wa halmashauri nyinginezo, kulingana na mazingira na tabia ya kila mahali. Taasisi hizo, hasa kapitulo za katedrali, zipewe, kadiri inavyofaa, utaratibu mpya unaolingana na mahitaji ya siku hizi.

Mapadre na walei ambao wamo katika Kuria wazingatie kwamba wanashiriki katika huduma ya kichungaji ya Askofu.

Kuria ya jimbo iratibishwe kwa jinsi ambavyo itaweza kuwa chombo chenye kufaa cha kumsaidia Askofu katika kukidhi uongozi wa jimbo, na vilevile katika utendaji wa kazi za kitume.

Imependekezwa kwa dhati kwamba katika kila jimbo Halmashauri mah-susi ya kichungaji iwepo, ambayo mwenyekiti wake ni Askofu wa jimbo, na inafanywa na mapadre, watawa na walei wanaochaguliwa kwa uangalifu wa pekee. Ni juu ya halmashauri hiyo kuchunguza yote yanayohusiana na kazi za kichungaji, kuyatafakari na kupendekeza mambo ya kutendea kazi.

III - WAKLERI WA JIMBO

28. Mapadre wote, wa kijimbo au wa kitawa, wanashiriki na wanautimiza upadre ulio mmoja wa Kristo pamoja na Askofu. Kwa sababu hiyo wawekwa kuwa wasaidizi waangalifu wa Daraja ya Maaskofu. Katika kutimiza uangalizi wa roho, majukumu ya kwanza yana mapadre wa jimbo, kama wale ambao, kwa tabia ya kuwa waingizwa (inkadinati) au wahudumu wa Kanisa faridi, wamejiweka wakfu kwa kutoa huduma kikamilifu ndani ya jimbo, kwa ajili ya kuchunga sehemu maalum ya kundi la Bwana. Kwa sababu hiyo wao hufanya presbiterio ( presbyterium) moja na familia moja, ambamo Askofu ni baba. Naye, ili kuweza kugawa kwa manufaa na haki huduma takatifu kati ya mapadre anatakiwa kufaidika na uhuru kamili katika kukabidhi ofisio au benefizio. Kwa hiyo, haki na mapendeleo yafutwa, ambayo kwa namna yoyote yauwekea mipaka uhuru huo.

Mahusiano kati ya Askofu na mapadre wa kijimbo yanatakiwa kujengwa hasa katika vifungo vya upendo wa kimungu, ili umoja wa makusudi kati ya mapadre na Askofu usitawishe kazi zao za kitume. Kwa sababu hiyo, ili huduma ya roho ifae zaidi na zaidi, Askofu awaite mapadre kwa mazungumzo, hata ya pamoja, ili kuongea hasa juu ya masuala ya kichungaji; nalo lifanyike kadiri inavyowezekana, kila baada ya muda maalum, wala siyo mara chache.

Zaidi ya hayo, mapadre wote wa jimbo wawe wameunganika kati yao, na hivyo wajisikie wanasukumwa na uangalifu kwa ajili ya mema ya rohoni ya jimbo zima. Aidha, wakikumbuka kuwa malimwengu wanayopata katika utekelezaji wa huduma yao ya kikanisa yatokana na wajibu wao mtukufu, basi walisaidie jimbo kwa ukarimu, kwa upande wa mahitaji ya kidunia pia, kulingana na maagizo ya Askofu na kufuatana na uwezo wao.

Mapadre wanaoshughulikia kazi za kimaparokia

29. Kati ya wasaidizi wa jirani sana wa Askofu ni mapadre wale, ambao yeye anawakabidhi jukumu la kichungaji au kazi za kitume zenye tabia ya kuwa kwa ajili ya parokia nyingi, ama kuhusu sehemu maalum ya jimbo, ama kwa ajili ya tabaka mahsusi ya waamini, ama kuhusu utendaji wa pekee.

Wanatoa msaada wenye thamani kubwa mapadre wale ambao Askofu anawakabidhi huduma ya kitume, au shuleni, au katika taasisi au vyama mbalimbali. Mapadre wanaoshughulikia miradi ya kimajimbo pia, kwa vile wanatimiza kazi muhimu za kitume, wastahili heshima ya pekee, hasa kutoka kwa Askofu wa jimbo ambamo wanayo makao yao.

Maparoko

30. Lakini, wasaidizi hasa wa Askofu ni maparoko, ambao, kama wachungaji halisi, wamekabidhiwa uangalizi wa roho, katika eneo fulani la jimbo, chini ya mamlaka ya Askofu.

1) Katika utekelezaji wa uangalizi huo, maparoko pamoja na wasaidizi wao wanatakiwa kutimiza majukumu yao ya kufundisha, kutakatifuza na kuongoza kwa namna ambayo itasaidia waamini na jumuiya ya kiparokia kujisikia ni viungo vya kweli sio vya jimbo tu, lakini pia vya Kanisa zima. Kwa sababu hiyo washirikiane na maparoko wengine na vilevile na mapadre wanaohudumia kichungaji eneo lile (kama vile, k.m., Wakuu wa vikaria, au Madekani), ama wanaoshughulikia kazi za parokia kadhaa, kusudi uangalizi wa kichungaji usikose maafikiano, nao uwe na mafanikio zaidi.

Aidha, uangalizi wa roho unatakiwa kuchochewa na roho ya kimisioni, ili uwafikie kwa namna ya kufaa, wote wanaokaa katika parokia. Na kama maparoko wanashindwa kuwafikia watu wa tabaka fulani, basi waombe msaada wa wengine, walei pia, ili wawasaidie katika utume.

Ili kuleta mafanikio zaidi katika uangalizi wa roho, maisha ya pamoja ya mapadre yanapendekezwa sana, hasa ya wahudumu wa parokia ileile, kwa sababu maisha ya aina hiyo, pamoja na kusitawisha utendaji wa kitume, huwaonyesha waamini mfano wa mapendo na umoja.

2) Kuhusu jukumu la kufundisha, maparoko watakiwa kuhubiri neno la Mungu kwa waamini wote, ili wakiwa na mizizi katika imani, tumaini na mapendo, watimilike katika Kristo, na jumuiya ya kikristo itoe ushuhuda ule ua mapendo ambao Kristo aliamuru[32]; hali kadhalika, kwa njia ya malezi ya kikatekesi yanayolingana na umri wa kila mmoja, wanatakiwa kuongoza waamini kwenye ufahamu kamili wa fumbo la wokovu. Katika kuyatoa malezi hayo, wasitafute tu msaada kutoka kwa watawa, bali pia waombe ushirikiano na walei, wakiunda pia “udugu wa mafundisho ya kikristo”.

Katika kutekeleza jukumu la kutakatifuza, maparoko wahakikishe kuwa adhimisho la Sadaka ya Ekaristi linakuwa kiini na kilele cha maisha yote ya jumuiya ya kikristo. Wafanye bidii pia ili waamini walishe maisha yao ya kiroho wakizipokea kwa uchaji na mara kwa mara sakramenti takatifu na pia kujua na kushiriki kwa mwamko katika liturujia. Maparoko wakumbuke pia kuwa sakramenti ya Kitubio inachangia sana katika kuchochea maisha ya kikristo: kwa hiyo wajionyeshe wako tayari daima kupokea kitubio cha waamini, wakiwaita hata mapadre wengine wenye ufahamu wa lugha mbalimbali kusaidia, ikitakiwa.

Katika kutekeleza wajibu wa uchungaji, kwanza kabisa maparoko wafanye bidii kuwafahamu kundi lao. Na kwa vile ni watumishi wa kondoo wote, wakuze maisha ya kikristo katika kila mwamini, katika kila familia, na pia katika vyama vyenye lengo mahsusi la kichungaji, kama vile katika jumuiya ya parokia kwa jumla pia. Kwa sababu hiyo, wazitembelee nyumba na shule, kadiri huduma ya kichungaji inavyodai; wawashughulikie kwa makini wabaleghe na vijana; wawafuatilie maskini na wagonjwa kwa mapendo ya kibaba; wawe na uangalizi wa pekee kwa ajili ya wafanyakazi, na wafanye bidii ili waamini wasaidie katika kazi za kitume.

3) Mavika wa kiparokia, yaani wasaidizi wa paroko, wanatoa siku kwa siku msaada muhimu wa kimatendo katika huduma ya kichungaji, chini ya mamlaka ya paroko. Kwa sababu hiyo, kati ya maparoko na wasaidizi wao kuwepo na uhusiano wa kidugu, na kudumu kupendana na kuheshimiana daima. Paroko na wasaidizi wategemezana kwa ushauri, msaada na mfano; na wakabili kwa pamoja kazi za kiparokia kwa nia moja na jitihada zenye maafikiano.

Kuteuliwa, kuhamishwa, kuondolewa na kujiuzulu kwa maparoko

31. Askofu, katika kuamua kama padre anastahili kusimamia parokia, asizingatie tu suala la elimu ya mteule mhusika, bali pia utauwa wake, bidii yake ya kitume, na vipawa na sifa nyingine ambazo kwa haki zadaiwa katika utekelezaji wa uangalizi wa roho.

Aidha, kwa vile lengo kuu la wadhifa wa paroko ni manufaa ya roho, ili Askofu aweze kutimiza kwa urahisi na kwa kufaa uteuzi wa maparoko, haki zote za kupendekeza, za kuteua, za kuzuia, kama vile sheria za mashindano pia, ya wazi au ya peke yake, zikomeshwe; isipokuwa itunzwe haki ya watawa.

Maparoko katika parokia yao wanatakiwa kufaidi ule uthabiti katika ofisio, unaodaiwa na mema ya roho. Kwa hiyo, pamoja na kufuta ubaguzi wowote kati ya maparoko wa kuhamishika na wasiohamishika, katika kuhamisha au kuondoa maparoko, ukubaliwe na kurahisishwa zaidi na zaidi mtindo unaomwezesha Askofu kushughulika mahitaji ya mema ya roho, licha ya kuhifadhi usawa wa asili na wa kisheria.

Maparoko ambao, kwa sababu ya umri wao mkubwa, ama kwa sababu nzito nyinginezo, hawawezi kutimiza kazi yao kwa namna ya kufaa na iletayo matunda, wanaombwa sana ili wao wenyewe, kwa hiari yao au kwa mwaliko wa Askofu, wakubali kujiuzulu kutoka katika ofisio yao. Askofu kwa upande wake ahakikishe kuwa maparoko waliojiuzulu wanapata matunzo yanayofaa.

Kuanzishwa na kufutwa kwa parokia

32. Hatima, iwe tu kwa sababu ya wokovu wa roho za watu kwamba unafanyika na kutambulika uamuzi wa kuanzishwa na kufutwa parokia au mabadiliko kama hayo, ambayo Askofu anaweza kutenda kwa mujibu wa mamlaka yake.

IV - WATAWA

Watawa na kazi za kitume

33. Watawa wote – na pamoja nao wanahesabiwa pia, katika mwongozo unaofuata hapa, wanachama wote wa vyama vingine vyenye kushika mashauri ya kiinjili – kulingana na wito wa pekee wa kila shirika, wana faradhi ya kufanya kazi kwa makini na bidii yote kwa ajili ya kujenga na kukuza Mwili mzima wa fumbo wa Kristo, na kwa ajili ya mema ya Makanisa faridi.

Nao watakiwa kuhamasisha lengo hilo hasa kwa sala, matendo ya toba na mfano wa maisha yao. Mtaguso huu Mkuu unawahimiza sana [watawa] kukuza zaidi na zaidi heshima na utunzaji wa mambo hayo ya kiroho. Hata hivyo, wakati huohuo inabidi washiriki kwa nguvu katika kazi za kitume za nje pia, kwa kuzingatia karama ya pekee ya kila shirika.

Watawa kama wasaidizi wa Maaskofu katika utume

34. Watawa walio mapadre, waliowekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya kipadre ili wao nao wawe wasaidizi halisi wa Daraja ya Maaskofu, siku hizi wanaweza kuwa bado msaada mkubwa kwa Maaskofu, kulingana na mahitaji ya roho za watu yalivyoongezeka. Kwa hiyo, kadiri wanavyoshiriki uangalizi wa roho na kazi za kitume chini ya mamlaka ya Wachungaji watukufu, ndivyo wanavyotakiwa kuhesabiwa kwa namna fulani kuwemo kweli miongoni mwa wakleri wa jimbo.

Watawa wengine pia, wanaume kwa wanawake, ambao nao wamo katika familia ya kijimbo kwa namna moja au nyingine, wanaleta msaada mkubwa kwa hierarkia takatifu na, kulingana na mahitaji ya utume yanavyoongezeka, wanaweza na wanatakiwa kuuleta hata zaidi katika siku za mbeleni.

Misingi ya utume wa watawa katika jimbo

35. Lakini, kusudi kazi za kitume katika majimbo mbalimbali zitimizwe daima kwa moyo mmoja, na kusudi utunzwe umoja wa nidhamu ya kijimbo, zinawekwa kanuni hizi za msingi:

1) Watawa wote, kwa kuwatazama Maaskofu kuwa waandamizi wa Mitume, wawatendee daima kwa utiifu na heshima. Aidha, kila wanapokuwa wamekabidhiwa kihalali kazi za kitume, inawapasa kutekeleza majukumu yao wakijionyesha kama wasaidizi watiifu wa Maaskofu[33]. Zaidi ya hayo, watawa wakubalie hima na kiaminifu maombi na mapendekezo ya Maaskofu, wapate kuchukua zaidi na zaidi madaraka katika huduma ya wokovu wa wanadamu, kufuatana na karama na Katiba za kila Shirika. Nazo (Katiba), kama inahitajika, zilinganishwe na kusudi hilo, kwa kuzingatia maagizo ya Dikrii hii ya Mtaguso.

Hasa, kwa sababu ya mahitaji ya kiroho [ya watu] na ya uhaba wa wakleri wa kijimbo, Mashirika ya kitawa, yasiyo ya maisha ya kitaamuli tu, yanaweza kuitwa na Maaskofu kushiriki katika huduma mbalimbali za kitume, kwa kuzingatia lakini kawaida za kila Shirika. Na Wakuu wa Mashirika wahamasishe utekelezaji wa ushirikiano huu inavyowezekana, hata kwa kupokea uongozi wa parokia, hata kwa muda tu.

2) Watawa wanaojishughulisha katika utume wa nje, wahifadhi roho ya Shirika lao na wadumu waaminifu katika kuishika kanuni yao, na katika kutii Wakuu wao. Maaskofu wenyewe wasikose kuwakumbushia kwa nguvu watawa faradhi hiyo.

3) Uruhusisho (Exemptio), ambao unawafanya watawa wanategemea moja kwa moja Baba Mtakatifu au mamlaka nyingine ya kikanisa, na wako wameruhusiwa mbele ya mamlaka ya kisheria ya Maaskofu, una maana hasa katika utaratibu wa ndani wa Mashirika, ili mambo yote yaendane na kuunganika kwa lengo la kueneza na kukamilisha maisha ya kitawa katika hayo Mashirika[34]. Huo uruhusisho unakuwa mikononi mwa Baba Mtakatifu njia ya kuweza kuwatumia watawa kwa ajili ya mema ya Kanisa zima[35]; tena utawaruhusu mamlaka nyingine husika kuwatumia kwa ajili ya Makanisa yaliyo chini yao kisheria.

Lakini uruhusisho huo hauzuii watawa wa jimbo fulani wasiwe chini ya mamlaka ya kisheria ya Askofu, kwa mujibu wa sheria, kadiri inavyotakiwa na utekelezaji wa jukumu la kichungaji la Maaskofu, pia na utaratibu wa uangalizi makini wa roho[36].

4) Watawa wote, wa kipapa (exemptorum) au wasio wa kipapa, wako chini ya mamlaka ya Wakuu wa mahali, katika yale yahusuyo maadhimisho ya hadhara ya ibada kwa Mungu, isipokuwa kuna utofauti wa riti; uangalizi wa roho; mahubiri kwa watu; malezi ya kidini na ya kimaadili ya waamini, hasa ya watoto; mafundisho ya katekesi na malezi ya kiliturujia; matunzo ya cheo na hadhi ya ukleri; na, hatima, aina mbalimbali za utendaji unaohusiana na utume mtakatifu. Pia shule za kikatoliki za watawa ziko chini ya Mkuu wa mahali, kwa habari za utaratibu wao wa jumla na ukaguzi wao, isipokuwa ni haki ya watawa wenyewe kuziongoza iwapendezavyo. Vilevile watawa wanatakiwa kuyashika maagizo yote yaliyowekwa kihalali kwa wote na Maaskofu katika Mitaguso au katika Mabaraza.

5) Kati ya Mashirika mbalimbali ya kitawa, na kati yao na wakleri wa kijimbo, usitawishwe ushirikiano wenye utaratibu. Aidha, bidii ifanyike ili utendaji na kazi zozote za kichungaji ziwianishwe kati yao: nayo inategemea hasa ile tabia ya kimungu ya mioyo na ya akili iliyo na misingi yake katika mapendo. Kuhamasisha uwianisho huo ni juu ya Kiti cha Kitume kwa habari ya Kanisa zima; ni juu ya wachungaji watukufu katika majimbo yao pekee; hatimaye ni juu ya Sinodi ya Mapatriarka na juu ya Mabaraza ya Maaskofu katika maeneo yao husika.

Kuhusu kazi za kitume zinazotekelezwa na watawa, Maaskofu au Mabaraza ya Maaskofu kwa upande mmoja, na Wakuu wa Mashirika au Mabaraza ya Wakuu wa Mashirika kwa upande mwingine, wote watekeleze wajibu wao baada ya kushauriana pamoja.

6) Ili kukuza moyo wa umoja na uhusiano (mutuas relationes) kwa manufaa kati ya Maaskofu na watawa, mara kwa mara na kila inapohitajika, Maaskofu na Wakuu wa Mashirika wakutane ili kujadili juu ya masuala yahusuyo utume kwa ujumla katika eneo fulani.

Sura ya III

MAASKOFU WANAOSHIRIKI KAZI KWA MANUFAA YA MAJIMBO KADHAA

I - SINODI, MITAGUSO NA MABARAZA YA MAASKOFU

Sinodi na mitaguso pekee

36. Tangu awali ya karne za Kanisa, Maaskofu wanaosimamia Makanisa faridi, katika ushirika wa mapendo na wakisukumwa na bidii ya utume kwa ulimwengu mzima waliokabidhiwa Mitume, waliunga nguvu na nia zao, kwa ajili ya kukuza mema ya wote na ya Makanisa pekee. Kwa lengo hilo, Sinodi na Mtaguso ya kiprovinsi viliundwa, na hapo baadaye pia Mitaguso ya wote, ambamo Maaskofu waliweza kufanya uamuzi juu ya mifumo iliyo sawa kwa Makanisa mbalimbali, ya kuitunza katika kufundisha kweli za imani na katika kuratibu nidhamu ya kikanisa.

Hivyo basi, Mtaguso Mkuu huu unapendekeza sana kwamba asasi bora ya Sinodi na ya Mitaguso ipewe nguvu mpya, ili kuweza kusaidia kwa manufaa na mafanikio katika kukuza imani na kulinda nidhamu katika Makanisa mbalimbali, kulingana na mazingira ya nyakati.

Umuhimu wa Mabaraza ya Maaskofu

37. Maaskofu, hasa siku hizi, wanapata magumu katika kutimiza kwa usawa na manufaa utume wao, pasipokuwepo ushirikiano wa ndani na wa pamoja na Maaskofu wengine. Na kwa vile Mabaraza ya Maaskofu – ambayo katika nchi nyingi yalikwisha kuundwa – yameonyesha dalili za utume wenye matunda mengi, Mtaguso Mkuu huu unafikiria kuwa inafaa sana kwamba, katika dunia nzima Maaskofu wa taifa moja au wa eneo fulani waunde taasisi moja na wakutanike mara kwa mara kati yao, ili katika kubadilishana mang’amuzi na maoni kuwepo na ushirikiano mtakatifu wa nguvu kwa ajili ya mema ya Makanisa yote.

Kwa sababu hiyo, Mtaguso huu, unaagiza haya yafuatayo kuhusu Mabaraza ya Maaskofu.

Maana, muundo, uwezo wa kisheria, na ushirikiano wa Mabaraza ya Maaskofu

38. 1) Baraza la Maaskofu ni kama taasisi ambamo Wachungaji wakuu (Antistites) watukufu wa taifa au eneo fulani, hutimiza majukumu yao ya kichungaji kwa pamoja, kwa ajili ya kukuza mema ambayo Kanisa humpa mwanadamu, hususan kwa njia ya miundo na mbinu za kitume, ambazo zaendana na mazingira ya nyakati.

2) Baraza la Maaskofu hufanywa na wale wote wanaoongoza Makanisa ya mahali ya riti mbalimbali – wasipokuwepo Mavika jenerali – Waandamizi, Wasaidizi na Maaskofu wengine wa cheo waliokabidhiwa jukumu mahsusi na Kiti cha Kitume au na Baraza la Maaskofu. Maaskofu wengine wa cheo, na Mabalozi wa Baba Mtakatifu – kulingana na tabia ya ofisio waliyo nayo katika eneo lile –, si wanachama wa Baraza la Maaskofu, kwa sheria.

Maaskofu wa jimbo na Waandamizi wao huwa na kura ya uamuzi katika Baraza. Maaskofu Wasaidizi na Maaskofu wengine walio wanachama wa Baraza huwa na kura au ya uamuzi au ya ushauri kufuatana na katiba ya Baraza.

3) Kila Baraza la Maaskofu litayarishe katiba yake, ambayo inapaswa kupitiwa na Kiti cha Kitume, na ambamo – kati ya mambo mengine – zinapangwa ofisi zinazofaa zaidi kwa madhumuni yake, k.v. Kamati tendaji ya Maaskofu, Tume (Commissiones) za kiaskofu, na Ukatibu Mkuu.

4) Maamuzi ya Mabaraza ya Maaskofu, yakiwa yamefanywa kihalali na kwa walau theluthi mbili za kura za Maaskofu wanabaraza wenye kura ya uamuzi, na baada ya kuangaliwa na Kiti cha Kitume, yana nguvu ya kisheria katika mambo yale tu ambayo sheria ya jumla inataja, au likiruhusu hivi agizo maalum la Kiti cha Kitume, lililotolewa au kwa Uamuzi wa [Kiti] chenyewe (motu proprio) au kutokana na ombi la Baraza.

5) Endapo mengine ya pekee yanashauri hivi, Maaskofu wa nchi kadhaa, kwa idhini ya Kiti cha Kitume, wanaweza kuunda Baraza moja.

Kwa vyovyote, mawasiliano kati ya Mabaraza ya nchi mbalimbali yarahisishwe, ili kupata kuhamasisha na kuhifadhi mema makubwa zaidi.

6) Maaskofu wa Makanisa ya Mashariki wanaonywa sana ili, katika kuhamasisha nidhamu ya Kanisa lao katika Sinodi zao, na kukuza kwa manufaa utendaji wote wenye lengo la kusaidia mafaa ya dini, wazingatie vilevile mema ya wote katika eneo zima, ambamo yamo Makanisa kadha wa kadha ya riti tofauti, wakijadili rai zao katika mikutano baina ya riti mbalimbali (interritualibus), kulingana na kanuni zitakazowekwa na mamlaka husika.

II - MAENEO YA PROVINSI NA KUSIMIKWA KWA KANDA ZA KIKANISA

Kanuni za msingi kwa ajili ya kurekebisha mipaka

39. Manufaa ya roho yanadai lithibitike eneo maalum, silo la majimbo tu, bali pia la provinsi za kikanisa; naam, nao unasukuma ziasisiwe kanda za kikanisa pia, kusudi mahitaji ya utume yashughulikiwe kwa urahisi na mafanikio zaidi kulingana na mazingira ya kijamii na ya mahali; pia mikutano ya Maaskofu wao kwa wao, na pamoja na Mametropolita, pamoja na Maaskofu wa nchi ileile, vilevile mikutano ya Maaskofu pamoja na mamlaka ya kiserikali ikawe rahisi na yenye manufaa.

Mwongozo

40. Hivyo, Mtaguso Mkuu huu, ili kuyafikia malengo yaliyodokezwa hapo juu, unaagiza mwongozo huu:

1) Yafaa yakaguliwe upya maeneo ya provinsi za kikanisa, na zipangwe kwa sheria za kufaa haki na mapendeleo ya Mametropolita.

2) Iwe kanuni ya kawaida kwamba majimbo yote na maeneo mengine yenye hadhi moja na ile ya jimbo kwa mujibu wa sheria, yawekwe chini ya provinsi ya kikanisa mojawapo. Kwa hiyo, yale majimbo ambayo mpaka sasa yako moja kwa moja chini ya mamlaka ya Kiti cha Kitume, wala hayajaunganika na jimbo jingine, basi, yaungane kuwa provinsi mpya ya kikanisa, ikiwezekana, au yaunganike na provinsi iliyo jirani au ya kufaa, na yawekwe chini ya sheria za kimetropolita za Askofu Mkuu, kulingana na kanuni za sheria za kawaida.

3) Endapo mafaa yataka hivi, basi, provinsi za kikanisa ziunganike katika kanda za kikanisa, ambazo zapewa utaratibu wa kisheria.

Kuhoji Mabaraza ya Maaskofu

41. Inafaa kwamba Mabaraza ya Maaskofu husika yatathmini masuala kuhusu maeneo ya provinsi na kuasisiwa kwa kanda, kulingana na utaratibu uliowekwa katika vipengele namba 23 na 24 kwa ajili ya majimbo, na baadaye yapeleke maoni yao na mapendekezo kwa Kiti cha Kitume.

III - MAASKOFU WENYE OFISIO ZA KIMAJIMBO

Ushirikiano na Maaskofu

42. Kwa vile haja za kichungaji zinadai zaidi na zaidi kwamba huduma kadhaa za kichungaji ziwe zina mwelekeo na uongozi ulio mmoja na sawa, inafaa ziundwe ofisi kadhaa ili ziweze kuwa za msaada kwa majimbo yote au baadhi, ya kanda au nchi fulani: ofisi hizo zaweza kukabidhiwa kwa Maaskofu pia.

Mtaguso Mkuu huu unawasihi wote ili kwamba kati ya Maprelati au Maaskofu, waliowekwa katika ofisi hizo, na Maaskofu wa jimbo na Mabaraza ya Maaskofu udumu ushirika wa kidugu na maafikiano ya mioyo katika umoja, kwa ajili ya utendaji wa kichungaji, ambao utaratibu wa msingi unatakiwa pia kuwekwa kwa njia ya sheria za kawaida.

Mavika wa kijeshi

43. Kwa vile huduma ya kiroho kwa wanajeshi, kulingana na hali ya pekee ya maisha yao, inadai uangalifu wa hali ya juu, Uvika wa kijeshi ( Vicariatus Castrensis), kadiri inavyowezekana, usimikwe katika kila taifa. Na Vika, na Machapleni ( cappellani) vilevile, wajishughulishe kwa bidii na makini katika kazi hii ngumu, kwa ushirikiano mzuri na Maaskofu wa majimbo [37].

Kwa sababu hiyo Maaskofu wa majimbo wampatie Vika wa kijeshi mapadre wa kutosha wafaao kwa huduma nzito hii, na wasaidie katika utendaji wowote wenye lengo la kunufaisha mema ya roho za wanajeshi[38].

UTUME WA JUMLA

44. Mtaguso Mkuu huu unaagiza kwamba, katika matengenezo ya Kodisi ya sheria za Kanisa (Codex Iuris Canonici) zitungwe sheria za kufaa, kulingana na kanuni za msingi zilizowekwa katika hati hii na kwa kuzingatia pia mapendekezo yaliyotolewa na Tume au na Mababa wa Mtaguso.

Mtaguso Mkuu huu unaagiza pia kwamba iandaliwe miongozo ya jumla juu ya uangalizi wa roho ya kutumiwa na Maaskofu na maparoko pia, kwa lengo la kuwasaidia kuratibu mbinu za kutekeleza jukumu lao la kichungaji kwa manufaa na urahisi zaidi.

Vilevile uandaliwe mwongozo mahsusi kwa ajili ya uangalizi wa roho kwa ajili ya matabaka ya pekee za waamini, baada ya kuzingatia tabia na hali tofauti za nchi au kanda mbalimbali; na mwongozo kwa ajili ya mafundisho ya katekesi kwa wakristo, ambao ndani yake yawemo maelezo kuhusu kanuni za msingi za mafundisho hayo na za mwelekeo wake, pia za utungaji wa vitabu vihusuvyo mada hiyo. Katika kuandaa miongozo hiyo, vilevile yazingatiwe mapendekezo yaliyotolewa na Tume mbalimbali au na Mababa wa Mtaguso.

 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 28 Oktoba 1965

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa) 



[1] Taz. Mt 1:21.
[2] Taz. Yn 20:21.
[3] Taz. Conc. Vat.I, Const. dogm.I, de Ecclesia Christi, Pastor aeternus, c. 3. Denz. 1828 (3061).
[4] Taz. Conc. Vat. I, Const. dogm. I, de Ecclesia Christi, Prooem.: Denz. 1821 (3050).
[5] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, Lumen Gentium, cap.III, nn. 21,24,25: AAS 57 (1965), uk. 24-25, 29-31.
[6] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, Lumen Gentium, cap.III, nn. 21: AAS 57 (1965), uk.24-25.
[7] Taz. Ioannes XXIII, Const. Apost. Humanae salutis, 25 des. 1961: AAS 54 (1962), uk. 6
[8] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, Lumen Gentium, cap.III, nn. 22: AAS 57 (1965), uk.25-27.
[9] Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, ibid.
[10] Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, ibid.
[11] Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, ibid.
[12] Taz. Paulus VI, Motu proprio Apostolica sollicitudo, 15 sept. 1965: AAS 57 (1965), uk. 775-780.
[13] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, Lumen Gentium, cap.III, nn. 23: AAS 57 (1965), uk.27-28.
[14] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Fidei donum, 21 apr. 1957: AAS 49 (1957), uk. 237; taz. pia: Benedictus XV, Epist.Ap. Maximum illud, 30 nov. 1919: AAS 11 (1919), uk. 440; Pius XI, Litt. Encycl. Rerum Ecclesiae, 28 febr. 1926: AAS 18 (1926), uk. 68 ss.
[15] Taz. Paulus VI, Allocutio ad Em. mos Patres Cardinales. Exc. mos Presules, Rev. mos Prelatos ceterosque Romanae Curiae Officiales, 21 sept. 1963: AAS 55 (1963), uk. 793 ss.
[16] Taz. Conc. Vat. II, Decr. de Ecclesiis Orientalibus Catholicis, Orientalium Ecclesiarum, nn. 7-11: AAS 57 (1965) uk. 79-80
[17] Taz. Conc.Trid., Sess. V, Decr. De reform., c. 2, Mansi 33,30; Sess. XXIV, Decr. De reform., c. 4, Mansi 33,159; Conc. Vat. II, Const. Dogm. de Ecclesia, Lumen Gentium, Cap. III, n. 25: AAS 57 (1965) uk. 29 ss.
[18] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, Lumen Gentium, Cap. III, nn. 25: AAS 57 (1965), uk.29-31.
[19] Taz. Ioannes XXIII, Litt.Encycl. Pacem in terris, 11 apr. 1963, passim: AAS 57 (1963), uk. 257-304.
[20] Taz. Paulus VI, Litt. Encycl. Ecclesiam suam, 6 ago. 1964: AAS 56 (1964) uk. 639.
[21] Taz. Paulus VI, Litt. Encycl. Ecclesiam suam, 6 ago. 1964: AAS 56 (1964) uk. 644-645.
[22] Taz. Conc. Vat. II, Decr. de Instrumentis communicationis socialis, Inter mirifica, AAS 56 (1964) uk. 145-153.
[23] Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium: AAS 56 (1964) uk. 97 ss.; Paulus VI, Motu proprio Sacram Liturgiam, 25 jan. 1964: AAS 56 (1964) uk. 139 ss.
[24] Taz. Pius XII, Litt.Encycl. Mediator Dei, 20 nov. 1947: AAS 39 (1947) uk. 521 ss.; Paulus VI, Litt. Encycl. Mysterium Fidei, 3 sept. 1965: AAS 57 (1965) uk. 753-774.
[25] Taz. Mdo 1:14 na 2:46.
[26] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm., de Ecclesia, Lumen Gentium, cap.IV, nn. 44-45: AAS 57 (1965), uk.50-52.
[27] Taz. Lk 22:26-27.
[28] Taz. Yn 15:15.
[29] Taz. Conc. Vat.II, Decr. de Oecumenismo, Unitatis redintegratio: AAS 57 (1965) uk. 90-107.
[30] Taz. Mt. Pius X, Motu proprio Iampridem, 19 mar. 1914: AAS 6 (1914) uk. 173 ss.; Pius XII, Const. Ap. Exsul Familia, 1 ago. 1952: AAS 44 (1952) uk. 649 ss.; Leges Operis Apostolatus Maris, auctoritate Pii XII conditae, 21 nov. 1957: AAS 50 (1958) uk. 375-383.
[31] Taz. Conc. Vat. II, Decr. de Ecclesiis Orientalibus Catholicis, Orientalium Ecclesiarum, nn. 4: AAS 57 (1965) uk. 77.
[32] Taz. Yn 13:35.
[33] Taz. Pius XII, Allocutio, 8 des. 1950: AAS 43 (1951) uk. 28; Paulus VI, Allocutio, 23 mei 1964: AAS 56 (1964) uk. 571.
[34] Taz. Leo XIII, Const. Ap. Romanos Pontifices, 8 mei 1881: Acta Leonis XIII, vol.II, (1882) uk. 234 ss.
[35] Taz. Paulus VI, Allocutio, 23 mei 1964: AAS 56 (1964) uk. 570-571.
[36] Taz. Pius XII, Allocutio, 8 des. 1950: AAS 43 (1951) uk. 28.
[37] Taz. S. C. Consistorialis: Instructio de Vicariis Castrensibus, 23 apr. 1951: AAS 43 (1951) uk. 562-565; Formula servanda in relatione de statu Vicariatus Castrensis conficienda, 20 okt. 1956: AAS 49 (1957) uk. 150-163; Decr. De Sacrorum Liminum visitatione a Vicariis Castrensibus peragenda, 28 feb. 1959: AAS 51 (1959) uk. 272-274; Decr. Facultas audiendi confessiones militum Cappellanis extenditur, 27 nov. 1960: AAS 53 (1961) uk. 49-50 – Taz. pia S.C. de Religiosis: Instructio de Cappellanis militum religiosis, 2 feb. 1955: AAS 47 (1955) uk. 93-97.
[38] Taz. S. C. Consistorialis: Epistula ad Em.mos PP. DD. Cardinales atque Exc.mos PP. DD.Archiepiscopos, Episcopos ceterosque Ordinarios Hispanicae Ditionis, 21 juni 1951: AAS 43 (1951) uk. 566.