Index

Back Top Print

[AR - BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HE - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Konstitusio ya kidogma juu ya 
ufunuo wa kimungu
 

Paulo Askofu
Mtumishi wa watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

  

UTANGULIZI

1. Katika kusikiliza kwa uchaji NENO LA MUNGU (Dei Verbum) na kulitangaza kwa tumaini thabiti, Mtaguso Mkuu unaungana na Mtakatifu Yohane asemaye: “Tunawahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu: hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi, ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi, na ushirika wetu ni pamoja na Baba na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo” (1Yoh. 1:2-3). Kwa hiyo, [Mtaguso huu], ukifuata nyayo za Mtaguso wa Trento na Vatikano I, unadhamiria kueleza mafundisho halisi juu ya ufunuo wa kimungu na kurithishwa (transmissione) kwake. Mtaguso unataka ulimwengu usikie mbiu ya wokovu, ili kwa kusikia uweze kusadiki, na kwa kusadiki uweze kutumaini, na kwa kutumaini uweze kupenda[1].

Sura ya Kwanza

UFUNUO WENYEWE

Maumbile na maana ya ufunuo

2. Ilimpendeza Mungu, katika wema na hekima yake, kujifunua mwenyewe na kulidhihirisha fumbo la mapenzi yake (taz. Efe 1:9); katika fumbo hilo, kwa njia ya Kristo, Neno la Mungu aliyefanyika mwili, katika Roho Mtakatifu, wanadamu wanapata njia ya kumwendea Baba na kushirikishwa hali ya kimungu (taz. Efe 2:18; 2Pet 1:4). Kwa njia ya ufunuo huo Mungu asiyeonekana (taz. Kol 1:15; 1Tim. 1:17) katika upendo wake usio na mipaka anaongea na wanadamu kama na marafiki (taz. Kut 33:11; Yn 15:14-15), tena hukaa nao (taz. Bar 3:38) ili kuwaalika na kuwapokea katika ushirika naye. Mpango huu wa ufunuo hutimizwa kwa matukio na kwa maneno. Haya yameunganika kwa ndani kabisa, kiasi kwamba kazi zilizotimizwa na Mungu katika historia ya wokovu zinaonyesha na kuthibitisha mafundisho na yale yote yaliyomo katika maneno; na maneno yanatangaza kazi na kuliangaza fumbo lililomo ndani yake. Aidha, kwa njia ya ufunuo huo, ukweli kamili juu ya Mungu na juu ya wokovu wa wanadamu unang’ara kwetu katika Kristo, ambaye Yeye mwenyewe ndiye mshenga na utimilifu wa ufunuo wote[2].

Matayarisho ya ufunuo wa kiinjili

3. Mungu, anayeviumba na kuvihifadhi vitu vyote kwa njia ya Neno [wake] (taz. Yn 1:3), anaendelea kuwapatia wanadamu ushuhuda juu yake mwenyewe katika vitu vilivyoumbwa (taz. Rum 1:19-20). Tena, alipotaka kuifungua njia ya wokovu wa kimungu, tangu mwanzo alijidhihirisha kwa wazazi wetu wa awali. Baada ya kuanguka kwao, aliwainua tena katika tumaini la wokovu kwa ahadi ya ukombozi (taz. Mwa 3:15), naye alikuwa na utunzo wa daima kwa jamii ya wanadamu, ili awapatie uzima wa milele wale wote ambao wanautafuta wokovu kwa saburi katika kutenda mema (taz. Rum 2:6-7). Kwa wakati wake alimwita Ibrahimu, ili kumfanya yeye kuwa taifa kubwa (taz. Mwa 12:2-3), ambalo baada ya Mababu, alilifundisha kwa njia ya Musa na Manabii, ili wamtambue Mungu kuwa ndiye Mungu peke yake, mwenye uhai na ukweli, Baba mwenye kuwatunza na hakimu mwenye haki. Tena aliwafundisha kumngojea Mwokozi aliyeahidiwa. Kwa jinsi hii Mungu aliiandaa njia ya Injili katika mwenendo wa karne.

Kristo anakamilisha ufunuo

4. Mungu, baada ya kusema zamani katika Manabii mara nyingi na kwa njia nyingi, “mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana” (Ebr 1:1-2). Maana alimtuma Mwanawe, yaani Neno wa milele, anayewaangazia watu wote, ili akae kati ya wanadamu na kuwafunulia siri za Mungu (taz. Yn 1:1-18). Kwa hiyo Yesu Kristo, Neno aliyefanyika mwili, aliyetumwa kwetu kama “mwanadamu kwa wanadamu”[3], “huyanena maneno ya Mungu” (Yn 3:34) na kutimiza kazi ya wokovu ambayo Baba alimpa ili aitende (taz. Yn 5:36; 17:4). Kwa hiyo Yeye mwenyewe, ambaye tumwonapo twamwona Baba (taz. Yn 14:9), alitimiza na kukamilisha ufunuo na kuuthibitisha kwa ushuhuda wa kimungu. Hayo aliyafanya kwa uwepo wake kamili, kwa kujidhihirisha mwenyewe, kwa maneno na matendo, kwa ishara na miujiza na hasa kwa kifo na ufufuko wake mtukufu kutoka katika wafu, na hatimaye kwa kumtuma Roho wa kweli. Alitufunulia kwamba Mungu yupo pamoja nasi ili atukomboe kutoka katika giza la dhambi na mauti na kutufufua kwa uzima wa milele.

Kwa hiyo azimio la kikristo, kwa sababu ni Agano Jipya na la mwisho, halitapita kamwe. Na hakuna ufunuo mwingine mpya wa hadharani unaongojewa kabla ya ujio mtukufu wa mwisho wa Bwana wetu Yesu Kristo (taz. 1Tim 6:l4 na Tit 2:13).

Ufunuo upokelewe kwa imani

5. Utii wa imani lazima apewe Mungu anayejifunua (Rum 16:26; taz. Rum 1:5; 2Kor 10:5-6). Kwa imani mwanadamu hujikabidhi kikamilifu na kwa uhuru mikononi mwa Mungu, akitoa kwa Mungu mwenye kufunua “heshima kuu ya akili na utashi”[4], na akikubali kwa hiari ufunuo anaopewa na Yeye. Ili imani hii iweze kutekelezwa, mtu hana budi kutanguliwa na kusaidiwa na neema ya Mungu. Kadhalika hana budi kuwa na msaada wa ndani wa Roho Mtakatifu anayesukuma moyo na kumwelekeza kwa Mungu, na anayefunua macho ya akili na anayewapa “watu wote utamu katika kuukubali na kuuamini ukweli”[5]. Roho Mtakatifu huyohuyo hukamilisha imani daima kwa njia ya mapaji yake ili ufunuo ueleweke kwa undani zaidi.

Kweli zilizofunuliwa

6. Kwa njia ya ufunuo wa kimungu, Mungu alitaka kujifunua na kujishirikisha nasi na pia kutufunulia na kutushirikisha maazimio ya mapenzi yake ya milele kuhusu wokovu wa wanadamu, “yaani kushirikisha fadhili za kimungu, ambazo zinapita kabisa ufahamu wa akili za kibinadamu”[6].

Mtaguso Mkuu hukiri kwamba “Mungu, asili na utimilifu wa vitu vyote, anaweza kufahamika kwa hakika kwa mwanga wa kawaida wa akili ya kibinadamu kwa njia ya ulimwengu ulioumbwa (taz. Rum 1:20); tena [Mtaguso Mkuu] hufundisha ya kuwa ni kwa sababu ya ufunuo wake Mungu kwamba “mambo yale ya kimungu ambayo kwa yenyewe hayavuki upeo wa akili ya kibinadamu, yanaweza pia katika hali ya siku hizi ya wanadamu, kufahamika kwa wote upesi, kwa hakika thabiti na bila mchanganyiko wa kosa”[7].

Sura ya Pili

URITHISHAJI WA UFUNUO WA KIMUNGU

Mitume na waandamizi wao ni watangazaji wa Habari Njema

7. Kwa wema wake mkuu, Mungu alipanga kwamba yale aliyoyafunua kwa ajili ya wokovu wa mataifa yote yadumu daima kama yalivyo na yarithishwe kwa vizazi vyote. Kwa hiyo Kristo Bwana, ambaye ndani yake ufunuo wote wa Mungu Mwenyezi unatimilika (taz. 2Kor 1:30 na 3:16-4:6), aliwaamuru Mitume kuwahubiria wote Injili ambayo iliisha ahidiwa kwa njia ya Manabii, na ambayo aliitimiliza mwenyewe na kuitangaza kwa kinywa chake [8]. Kwa njia hii waliwashirikisha watu wote vipaji vya kimungu. Injili hii iliwekwa kama chemchemi ya kila ukweli uletao wokovu na ya kila nidhamu yenye maadili. Tendo hilo lilitimizwa kiaminifu na Mitume, ambao kwa kuhubiri kwa maneno, kwa mifano na kwa kuunda jumuiya mbalimbali waliwajulisha watu wote yale waliyopokea kutoka katika kinywa cha Kristo, kwa kuishi pamoja naye na kwa matendo yake; na pia yale waliyojifunza kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Tena, tendo hilo lilitimizwa pia na wale, Mitume na wengine walioishi nao, ambao, kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu mwenyewe, waliandika ujumbe wa wokovu[9].

Mitume waliweka Maaskofu kuwa waandamizi wao ili Injili ihifadhiwe daima ikiwa nzima na yenye uhai katika Kanisa, “wakiwakabidhi nafasi zao wenyewe za mamlaka-fundishi (magisterii)”[10]. Hivyo basi, Mapokeo hayo Matakatifu pamoja na Maandiko Matakatifu ya Maagano yote mawili ni kama kioo ambacho, kwa njia yake, Kanisa linalohiji hapa duniani humtazama Mungu, ambaye kutoka kwake hupewa yote mpaka litakapomwona uso kwa uso kama alivyo (taz. 1Yoh 3:2).

Mapokeo Matakatifu

8. Kwa hiyo, mahubiri ya kitume, yanapatikana kwa namna ya pekee katika Vitabu Vitakatifu, ilikuwa lazima yaendelee kuhifadhiwa kwa mfululizo wa kupokezana mpaka mwisho wa nyakati. Hivyo basi, Mitume, wanapowarithisha wengine yale waliyopokea, wanawasihi waamini wahifadhi mapokeo waliyopewa ama kwa maneno au kwa maandishi (taz. 2The 2:15). Na pia waliwasihi wapiganie imani waliyopewa mara moja tu na kwa daima (taz. Yda 3)[11]. Yale ambayo Mitume waliyarithisha, ndani yake yamo yote yenye kulifanya Taifa la Mungu kuishi katika utakatifu na kukuza imani yake. Hivyo Kanisa, katika mafundisho yake na katika maisha na ibada zake, linaendeleza daima na kuvirithisha vizazi vyote ukweli juu yake, na pia juu ya yale anayoyaamini.

Mapokeo hayo yanayotoka kwa Mitume hukua katika Kanisa kwa msaada wa Roho Mtakatifu[12]: unakua, kwa kweli, utambuzi wa mambo na pia wa maneno yanayorithishwa. Nao, unakua kwa tafakuri na kusoma kwa moyo kwa waamini, ambao wanayaweka na kuyafikiri mioyoni mwao (Lk 2:19 na 51). Na pia unakua kwa njia ya ujuzi wa ndani wa mambo ya kiroho wanaoung’amua; na kwa mahubiri ya wale waliopewa fadhili halisi ya ukweli kwa njia ya uandamizi wa kiaskofu. Yaani Kanisa, katika mfululizo wa karne, linaelekea kwenye utimilifu wa ukweli wa kimungu hadi maneno ya Mungu yatakapotimia ndani yake.

Mafundisho ya Mababa watakatifu yanathibitisha uwepo hai wa Mapokeo hayo. Hazina ya Mapokeo hayo inamiminwa ndani ya matendo na maisha ya Kanisa linaloamini na kusali. Mapokeo yenyewe yanalijulisha Kanisa kanoni, au orodha, nzima ya Vitabu Vitakatifu (integer Sacrorum Librorum canon), na kuwezesha kuvielewa kwa undani zaidi. Na pia yanasaidia Maandiko Matakatifu ili yaendelee kutenda kazi daima; hivyo Mungu, aliyeongea zamani, hakomi kuongea na Bibiarusi wa Mwanae mpendwa. Na Roho Mtakatifu, ambaye kwa njia yake sauti hai ya Injili husikika katika Kanisa, na kwa njia ya Kanisa katika ulimwengu, anawaingiza waamini katika ukweli wote na kufanya Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yao (taz. Kol 3:16).

Uhusiano hai baina ya Mapokeo na Maandiko

9. Kwa hiyo Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yameshikamana pamoja na kushirikiana. Kwa sababu yote mawili yanabubujika kutoka katika chemchemi ileile ya kimungu na hivyo huungana na kuwa kitu kimoja na kuelekea lengo moja. Kwa kweli, Maandiko Matakatifu ndilo Neno la Mungu ambalo liliandikwa kwa uvuvio wa Roho wa Mungu. Neno la Mungu lililokabidhiwa kwa Mitume na Kristo Bwana na Roho Mtakatifu linarithishwa li zima na Mapokeo Matakatifu kwa waandamizi wao, ili, wakiangazwa na Roho wa kweli, kwa njia ya kuhubiri kwao, walihifadhi kiaminifu, walifafanue na kulieneza. Hivyo Kanisa halichoti uhakika wake juu ya mambo yote yaliyofunuliwa kutokana na Maandiko Matakatifu peke yake. Kwa hiyo Maandiko Matakatifu na Mapokeo Matakatifu lazima yapokelewe na kuheshimiwa kwa hisia sawa, za uchaji na heshima[13].

Uhusiano kati ya Mapokeo, Maandiko Matakatifu, Kanisa lote na Uongozi wake

10. Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yanaunda hazina moja takatifu ya Neno la Mungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Taifa lote takatifu pamoja na Wachungaji wake likishikamana na hazina hiyo, linadumu daima aminifu katika Mafundisho ya Mitume na katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali (taz. Mdo 2:42), ili, katika kuitunza, kuiishi na kuikiri imani iliyorithishwa, uwepo umoja wa pekee wa kiroho kati ya Maaskofu na waamini[14].

Jukumu (Munus) la kutoa ufafanuzi halisi wa Neno la Mungu lililoandikwa au kupokewa[15] umekabidhiwa tu kwa Majisterio hai ya Kanisa[16], ambayo mamlaka yake inatekelezwa kwa jina la Yesu Kristo. Lakini Majisterio hiyo ya kufundisha haiko juu ya Neno la Mungu, bali [Majisterio] ni mtumishi wa Neno hilo, na hufundisha yale tu iliyorithi. Kwani, kwa amri ya Mungu na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, hulisikiliza Neno kwa uchaji, hulihifadhi kitakatifu na kulielezea kiaminifu, na huchota katika hazina hii moja ya imani yale yote inayoyatangaza ili yaaminiwe kwa kuwa yalifunuliwa na Mungu.

Ni dhahiri kwamba Mapokeo Matakatifu, Maandiko Matakatifu na Majisterio ya Kanisa, kwa maamuzi yenye hekima sana ya Mungu, yameshikamana na kuunganika pamoja kiasi kwamba moja haliwezi kusimama peke yake bila mengine. Bali, yote kwa pamoja, na kila moja kwa namna yake, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliye mmoja, hutoa mchango wake kwa wokovu wa watu.

Sura ya Tatu

UVUVIO WA KIMUNGU NA UFAFANUZI WA MAANDIKO MATAKATIFU

Uvuvio na ukweli katika Maandiko Matakatifu (Biblia)

11. Kweli zilizofunuliwa na Mungu zilizomo na zinazoelezwa katika matini ya Maandiko Matakatifu, zimeandikwa chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Mama Kanisa mtakatifu, akitegemea imani ya [nyakati za] Mitume, anavipokea rasmi kama vitakatifu vitabu vyote vizima vya Agano la Kale na Jipya, tena katika sehemu zao zote, kwa misingi hii kwamba, kwa vile viliandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu (taz. Yn 20:31; 2Tim 3:16; 2Pet 1:19-21; 3:15-16), Mungu mwenyewe ndiye mtunzi wake; na katika hali hiyo vimekabidhiwa kwa Kanisa lenyewe[17]. Kwa kutunga Vitabu Vitakatifu, Mungu aliwachagua watu fulani aliowatumia, katika vipaji na nguvu zao[18], ili, akifanya kazi ndani yao na kwa njia yao[19] kama watunzi wa kweli waandike kila kitu alichotaka kiandikwe bila kitu cha ziada[20].

Kwa vile yale yote ambayo watunzi waliovuviwa au waandishi watakatifu (hagiographi) wanayasema, inabidi yapokelewe kama yanasemwa na Roho Mtakatifu, lazima kukiri kwamba vitabu vya Maandiko Matakatifu vinafundisha kwa nguvu, kwa uaminifu thabiti na bila hitilafu ukweli ambao Mungu alitaka ukabidhiwe kwa Maandiko Matakatifu kwa ajili ya wokovu wetu[21]. Kwa hiyo “kila Andiko lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2Tim 3:16-17).

Mwongozo kuhusu ufafanuzi wa Biblia

12. Maadam Mungu katika Maandiko Matakatifu ameongea kwa njia ya wanadamu na kwa mtindo wa kibinadamu[22], mfafanuzi wa Maandiko Matakatifu, ili afahamu vizuri yale Mungu aliyotaka kutushirikisha, lazima atafute kwa makini yale ambayo waandishi watakatifu walitaka kumaanisha na yale ambayo Mungu alitaka kutufunulia kwa njia ya maneno yao.

Ili kuelewa nia ya waandishi watakatifu lazima tujali pia, kati ya mengine, mitindo ya fasihi yao (genera litteraria).

Maana ukweli unaelezwa na kuonyeshwa kwa namna tofauti katika matini za kihistoria, za kinabii au za kishairi au za mitindo mingine ya kifasihi. Kwa hiyo ni lazima mfafanuzi atafute maana ile iliyoandikwa, aliyotaka kueleza mwandishi mtakatifu katika nafasi fulani, kadiri ya hali ya wakati na utamaduni wake, kwa njia ya mitindo ya fasihi iliyotumika wakati ule[23]. Maana, ili kuelewa kwa hakika alichotaka kusema mwandishi mtakatifu katika maandishi, lazima kujali sana jinsi alivyoguswa na mambo mbalimbali, alivyojieleza na kusimulia kadiri ya utamaduni na nyakati za mwandishi mtakatifu, na pia kadiri ya mitindo iliyokuwa imeenea kati ya jamii mbalimbali[24].

Lakini, Maandiko Matakatifu lazima yasomwe na kufunuliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu mwenyewe ambaye kwa njia yake yaliandikwa[25]. Kwa sababu hiyo, ili kupata kwa hakika maana ya matini takatifu, hatuna budi kujali sana na kwa makini yale yaliyomo katika Maandiko Matakatifu yote na umoja wake, pamoja na kutilia maanani Mapokeo hai ya Kanisa lote na ulinganifu wa imani (analogiae fidei). Ni wajibu wa wafafanuzi kusaidia, kadiri ya mwongozo huu, kuelewa na kufasiri kwa undani zaidi maana ya Maandiko Matakatifu ili, kwa chunguzi zilizo za namna ya matayarisho, uamuzi wa Kanisa uthibitike. Kwa kweli hayo yote yanayohusu jinsi ya kufasiri Maandiko Matakatifu yapo chini ya uamuzi wa Kanisa, ambaye hutimiza amri ya Mungu na huduma yake ya kuhifadhi na kulifafanua Neno la Mungu[26].

Kushirikishwa kwa wanadamu Hekima ya Mungu

13. Katika Maandiko Matakatifu, ukweli na utakatifu wa Mungu ukiwa imara daima, hisani (condescensio) ya ajabu ya Hekima ya milele inadhihirishwa, “ili tufahamu ukarimu usioelezeka wa Mungu na pia jinsi Yeye, ambaye yupo tayari daima kuyashughulikia maumbile yetu, alivyojishusha katika maneno yetu”[27]. Maana, maneno ya Mungu yaliyotamkwa kwa lugha za kibinadamu yameingia katika maneno ya wanadamu, kama vile Neno wa Baba wa Milele alivyojifanya mtu, akichukua udhaifu wa maumbile ya kibinadamu.

Sura ya Nne

AGANO LA KALE

Historia ya wokovu yahifadhiwa katika vitabu vya Agano la Kale

14. Mungu, katika upendo wake mkuu, akiazimu na kutayarisha kwa makini wokovu wa watu wote, alijichagulia kwa mpango wa pekee Taifa, ili alikabidhi ahadi zake. Maana, baada ya kufunga Agano na Ibrahimu (taz. Mwa 15:18), pia na Taifa la Israeli kwa njia ya Musa (taz. Kut 24:8), alijifunua kwa maneno na matendo kwa taifa alilojipatia, kama Mungu mmoja wa kweli na hai, ili [Taifa la] Israeli ling’amue njia za Mungu kati ya wanadamu; pia Mungu mwenyewe alinena kwa vinywa vya Manabii ili Israeli azielewe kwa undani na kwa wazi zaidi, tena azijulishe kwa upana zaidi kwa Mataifa yote (taz. Zab 22:27-28; 96:1-3; Isa 2:1-4; Yer 3:17). Mpango wa wokovu uliotabiriwa, ukasimuliwa na kuelezwa na watunzi watakatifu, unajitokeza (exstat) kama Neno la kweli la Mungu katika vitabu vya Agano la Kale. Ndiyo sababu vitabu hivyo vilivyoandikwa kwa uvuvio wa kimungu vinahifadhi thamani ya daima: “Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya Maandiko tupate kuwa na tumaini” (Rum 15:4).

Ulazima wa Agano la Kale kwa Wakristo

15. Mpango wa Agano la Kale ulikusudia hasa kutayarisha, kutangaza kiutabiri (taz. Lk 24:44; Yn 5:39; 1Pet 1:10) na kuashiria kwa jinsi za mifano (taz. 1Kor 10:11) ujio wa Kristo Mkombozi wa ulimwengu na ujio wa Ufalme wa kimasiya. Aidha, vitabu vya Agano la Kale, kadiri ya hali ya jamii ya wanadamu kabla ya nyakati za wokovu ulioletwa na Kristo, vinawadhihirishia watu wote ujuzi juu ya Mungu na juu ya binadamu na pia jinsi Mungu mwenye haki na huruma anavyojihusisha na watu. Vitabu hivyo, ingawa vina ndani yake mambo ambayo hayajakamilishwa na ya muda, ni dhahiri kwamba vinaonyesha mafundisho (paedagogia) halisi ya kimungu[28]. Kwa hiyo waamini ni lazima wapokee kwa heshima vitabu hivyo ambavyo vinaonyesha jinsi ya kumcha Mungu, mafundisho makuu juu ya Mungu, hekima iletayo wokovu kwa maisha ya binadamu, na pia hazina za ajabu za sala. Ndani ya vitabu hivyo limefichika fumbo la wokovu wetu.

Umoja wa Maagano yote mawili

16. Mungu, mvuviaji na mtunzi wa vitabu vya Maagano yote mawili, alipanga kwa hekima ili Agano Jipya lifichike ndani ya Agano la Kale na Agano la Kale lifunuliwe katika Agano Jipya[29]. Kwa sababu hiyo, hata kama Kristo alifanya Agano Jipya katika damu yake (taz. Lk 22:20; 1Kor 11:25), vitabu vyote vya Agano la Kale, vikichukuliwa katika hali yao nzima[30] katika ujumbe wa Injili, vinapata na kuonyesha maana yao timilifu katika Agano Jipya (taz. Mt 5:17; Lk 24:27; Rum 16:25-26; 2Kor 3:14-16), navyo [vitabu vya Agano la Kale] pia, kwa upande wao, vinaliangaza na kulieleza Agano Jipya.

Sura ya Tano

AGANO JIPYA

Ubora wa Agano Jipya

17. Neno la Mungu, ambalo ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye (taz. Rum 1:16), linajidhihirisha na kuonyesha nguvu yake kikamilifu katika Maandiko ya Agano Jipya. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati (taz. Gal 4:4), Neno alifanyika mwili akakaa kwetu akiwa amejaa neema na kweli (taz. Yn 1:14). Kristo alileta Ufalme wa Mungu hapa duniani, akamfunua Baba yake na pia akajifunua mwenyewe kwa matendo na maneno. Pia alikamilisha kazi yake kwa kifo, ufufuko na kupaa kwake kwa utukufu mbinguni na kumpeleka Roho Mtakatifu. Akiinuliwa juu ya nchi anawavuta wote kwake (taz. Yn 12:32), Yeye tu aliye na maneno ya uzima wa milele (taz. Yn 6:68). Fumbo hili havikujulishwa vizazi vingine kama walivyofunuliwa Mitume wake watakatifu na Manabii zamani hizi katika Roho Mtakatifu (taz. Efe 3:4-6), ili waihubiri Injili na kuchochea imani katika Yesu Kristo na Bwana na kulikusanya Kanisa. Maandishi ya Agano Jipya ni ushuhuda wa daima na wa kimungu wa mambo hayo yote.

Asili ya kitume ya Injili

18. Wote wanafahamu kwamba kati ya Maandiko yote, pia ya Agano Jipya, Injili kwa haki zina ubora wa pekee kwa sababu ni ushuhuda mahsusi wa maisha na mafundisho ya Neno aliyefanyika mwili, Mwokozi wetu.

Kanisa daima na popote huamini na kukiri kwamba Injili zote nne zina asili yao kutoka kwa Mitume. Yale ambayo Mitume walihubiri kwa kuagizwa na Kristo, baadaye, kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu (Divino afflante Spiritu), wao wenyewe na wengine walioishi nao walitupatia sisi, kama msingi wa imani, [ujumbe uleule waliouhubiri,] katika maandishi. Huo ndiyo Injili inayosimuliwa kwa namna nne kadiri ya Mathayo, Marko, Luka na Yohane[31].

Tabia ya kihistoria ya Injili

19. Mama Kanisa mtakatifu, kwa nguvu na daima amesadiki na hukiri kwamba Injili nne zilizotajwa hapo juu, ambazo anaamini bila kusita kwamba ni za kweli, zinasimulia kiaminifu yale ambayo Yesu Mwana wa Mungu aliyatenda kwelikweli na kufundisha kwa ajili ya wokovu wa milele, wakati alipoishi kati ya wanadamu hadi siku ile alipopaa mbinguni (taz. Mdo 1:1-2). Mitume, baada ya Bwana kupaa mbinguni, waliwatangazia watu yale aliyokuwa ameyasema na kuyatenda, kwa ujuzi kamili waliojaliwa[32] baada ya kufundishwa na matukio matukufu ya Kristo na kuangazwa na mwanga wa Roho wa ukweli[33]. Hatimaye watunzi watakatifu waliandika Injili nne wakichagua mengine kati ya mengi yaliyokuwa yamesimuliwa kwa maneno au kwa maandishi, wakifupisha mambo mengine, au kuyafafanua wakilenga hasa hali ya Makanisa. Tena waliandika wakilinda mtindo uleule wa kuhubiri, lakini daima wakisimulia mambo ya kweli na kwa uaminifu kuhusu Yesu[34]. Wao wenyewe, wakichota kutoka katika kumbukumbu yao na pia ushuhuda wa wale ambao “tangu mwanzo walikuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno”, waliandika kusudi watujulishe “ukweli” (taz. Lk 1:2-4) wa mambo tuliyoelezewa.

Maandishi mengine ya Agano Jipya

20. Kanoni ya Agano Jipya, zaidi ya Injili nne, ina pia nyaraka za Mtume Paulo na maandiko mengine ya Mitume yaliyotungwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Maandiko hayo, kwa azimio lenye hekima la Mungu, yale yote yamhusuyo Kristo Bwana yanathibitishwa, mafundisho yake halisi yanaelezwa kinaganaga zaidi, na uweza uletao wokovu wa kazi ya kimungu ya Kristo unahubiriwa. Tena, maisha ya kwanza ya Kanisa na kuenea kwake kwa ajabu vinasimuliwa, na utimilifu wake mtukufu unatabiriwa.

Maana, Bwana Yesu alitenda kazi pamoja na Mitume wake kama alivyoahidi (taz. Mt 28:20) na akawapelekea Roho Mtakatifu Msaidizi, mwenye kuwaongoza na kuwaingiza kwenye kweli yote (taz. Yn 16:13).

Sura ya Sita

MAANDIKO MATAKATIFU KATIKA MAISHA YA KANISA

Kanisa huheshimu Maandiko Matakatifu

21. Kanisa limeheshimu daima Maandiko Matakatifu kama lilivyoheshimu Mwili wa Bwana, wala halikukosa kamwe, hasa katika Liturujia takatifu, kujilisha mkate wa uzima na kuwapa waamini kutoka katika meza moja ya Neno la Mungu na pia ya Mwili wa Kristo. Kanisa limeyaamini daima na linaendelea kuyaamini Maandiko Matakatifu, pamoja na Mapokeo Matakatifu, kuwa ndiyo kanuni kuu kuliko zote ya maisha yake ya imani; kwa kweli Maandiko hayo, yaliyovuviwa na Mungu na kutungwa mara moja kwa daima, yanatushirikisha bila hitilafu yoyote Neno la Mungu mwenyewe; tena yanatusikiza sauti ya Roho Mtakatifu katika maneno ya Manabii na Mitume. Kwa hiyo mahubiri yote ya Kanisa, kama vile na dini yenyewe ya kikristo, lazima yalishwe na kuongozwa na Maandiko Matakatifu. Maana katika Vitabu Vitakatifu Baba aliye mbinguni anawajia watoto wake kwa upendo mkubwa na anaongea nao. Katika Neno la Mungu umo uweza na nguvu nyingi, kiasi kwamba Neno hilo huwa ni egemeo na nguvu kwa Kanisa na pia uthabiti wa imani, chakula cha roho na chemchemi safi na ya daima ya maisha ya kiroho kwa watoto wa Kanisa. Kwa hiyo, haya yaliyoandikwa ya kwamba “Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu” (Ebr 4:12), “laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa” (Mdo 20:32; taz. 1The 2:13), haya basi huyahusu kabisa Maandiko Matakatifu.

Tafsiri za Biblia lazima ziwe sahihi na aminifu

22. Ni lazima waamini wafunguliwe kwa wingi Maandiko Matakatifu. Kwa sababu hiyo Kanisa la awali lilipokea kama mali yake tafsiri ya zamani ya kigriki ya Agano la Kale iitwayo ya LXX [Septuajinta au “Watu Sabini”]; pia liliheshimu daima tafsiri nyingine za Mashariki na za Kilatini, hasa ile iitwayo Vulgata. Kwa vile Neno la Mungu lazima lipatikane kwa watu wote wa nyakati zote, basi Kanisa, kwa upendo wa kimama, linafanya kila jitihada ili zitayarishwe tafsiri zifaazo na zenye kuaminika katika lugha mbalimbali hasa kutoka lugha za asili za Vitabu Vitakatifu. Kama itaonekana kuwa inafaa kutayarisha tafsiri hizo pamoja na wakristo waliojitenga, kwa kibali cha mamlaka ya Kanisa, basi tafsiri hizo zinaweza kutumiwa na wakristo wote.

Wajibu wa kitume wa wataalamu

23. Bibiarusi wa Neno aliyefanyika mwili, yaani Kanisa, akifundishwa na Roho Mtakatifu, hujibidisha kufikia zaidi na zaidi ujuzi wa ndani wa Maandiko Matakatifu ili kuwalisha watoto wake kila wakati kwa maneno ya kimungu. Kwa hiyo, kwa haki anahimiza kuwajua zaidi Mababa Watakatifu wa Mashariki na wa Magharibi na aina mbalimbali za Liturujia takatifu. Ni lazima wafafanuzi Wakatoliki na pia wanateolojia wengine washirikiane kwa bidii na kujitahidi kusoma na kufasiri Maandiko Matakatifu kwa namna ifaayo chini ya uangalizi wa Majisterio takatifu. Kwa njia hii wahudumu wengi zaidi wa Neno la Mungu waweze kwa mafanikio zaidi kulipatia Taifa la Mungu chakula chake, yaani Maandiko yaangazayo akili, yanayoimarisha utashi na kuwasha mioyo ya wanadamu ili wampende Mungu[35]. Mtaguso Mkuu unawahimiza wana wa Kanisa wapenzi wa taaluma za kibiblia, ili wadumu katika kutimiza kwa nguvu mpya na kwa juhudi kubwa kazi ile waliyoianza vizuri kadiri ya lengo la Kanisa[36].

Ulazima wa Maandiko Matakatifu kwa Teolojia

24. Teolojia Takatifu hutegemea, kama msingi wake wa daima, Neno la Mungu lililoandikwa, pamoja na Mapokeo Matakatifu. Na juu ya msingi huo wa Neno, inapata kuimarishwa kwa nguvu na kufanywa upya zaidi ikitazama katika mwanga wa imani kila kweli iliyomo katika fumbo la Kristo. Maandiko Matakatifu yote yana Neno la Mungu ndani yake, na kwa vile yaliandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, ni Neno la Mungu kweli kweli. Kwa hiyo, kujifunza Maandiko Matakatifu kitakuwa ndicho kiini na roho ya Teolojia Takatifu[37]. Pia huduma ya Neno inajilisha kwa manufaa na kupania utakatifu kutoka kwa Neno la Maandiko. Huduma hiyo ni: mahubiri ya kichungaji, katekesi na mafundisho yote ya kikristo, na ndani yake homilia katika Liturujia lazima ipewe nafasi ya pekee.

Kusoma Biblia kunahimizwa

25. Kwa hiyo makleri wote, hasa mapadre wa Kristo, mashemasi au makatekista wanaoshiriki kwa rasmi huduma ya Neno, lazima wajizamishe katika Maandiko Matakatifu kwa kuyasoma bila kuchoka na kwa makini, ili kati yao asiwepo “mhubiri mtupu wa Neno la Mungu na wa nje tu, asiyezingatia Neno hilo moyoni mwake”[38], yeye ambaye inabidi awashirikishe waamini waliokabidhiwa kwake hazina tele ya Neno la Mungu, hasa katika Liturujia takatifu. Vilevile Mtaguso Mkuu unawasihi kwa nguvu na kwa bidii sana waamini wote, hasa watawa, wajifunze “uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu” (Flp 3:8) kwa kusoma mara kwa mara Maandiko Matakatifu. Maana “kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo”[39]. Kwa hiyo wakaribie kwa furaha na upendo Kitabu kitakatifu chenyewe [cha Biblia] kwa njia ya Liturujia takatifu yenye utajiri wa Maneno ya Mungu; pia wakikaribie kwa kukisoma kwa uchaji na kwa njia ya mazoezi yafaayo kwa lengo hilo na kwa njia ya misaada mingine, ambayo, kwa kibali na kwa uangalizi wa Wachungaji wa Kanisa, inaenea pote katika siku zetu kwa namna ya kusifika. Lakini waamini wakumbuke kwamba kusoma Maandiko Matakatifu lazima kuwe katika mazingira ya sala, ili Mungu na binadamu waweze kuongea pamoja; kwa sababu “tunaongea naye tunaposali na tunamsikiliza tunaposoma Maneno Matakatifu”[40].

Ni juu ya Maaskofu, “walio warithi wa mafundisho ya kitume”[41], kuwafundisha waamini waliokabidhiwa kwao matumizi sahihi ya Vitabu Vitakatifu, hasa Agano Jipya ambalo ndani yake Injili inashika nafasi ya kwanza. Watafanya hilo kwa kuwapa waamini tafsiri za Maandiko Matakatifu zenye maelezo ya lazima na ya kutosha, ili wana wa Kanisa waweze kuzoea kushinda na Maandiko Matakatifu kwa hakika na kwa manufaa na pia ili wakolezwe na roho zake.

Kisha, yatayarishwe matoleo ya Maandiko Matakatifu yenye maelezo ya kufaa kwa matumizi pia ya wale wasio wakristo yalinganayo na hali yao. Lakini Wachungaji wa kiroho na pia Wakristo wote waangalie ili matoleo hayo yaenezwe kwa busara.

Hitimisho

26. Kwa njia hii, kwa kusoma na kujifunza Vitabu Vitakatifu “Neno la Bwana liendelee na kutukuzwa” (2The 3:1), na hazina ya ufunuo iliyokabidhiwa kwa Kanisa ijaze zaidi na zaidi mioyo ya waamini. Kama vile kushiriki mara nyingi fumbo la Ekaristi kunavyokuza maisha ya Kanisa, vivyo hivyo tunaweza kutumaini mwamko mpya wa maisha ya kiroho kutokana na kuheshimu zaidi Neno la Mungu “linalodumu milele” (Isa 40:8; taz. 1Pet 1:23-25).

  

Mambo yote yaliyoamuliwa katika konstitusio hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mtakatifu Petro, 18 Novemba 1965

 

Mimi mwenyewe Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)

 

 

 

[1] Taz. Mt. Augustinus, De Catechizandis Rudibus 4,8: PL 40, 316.
[2] Taz. Mt 11:27; Yn 1:14 na 17; 14:6; 17:1-3; 2Kor 3:16 na 4:6; Efe 1:3-14.
[3] Epist. ad Diognetum 7,4: Funk, Patres Apostolici, I, uk. 403.
[4] Conc. Vat. I, Const. Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap.3: Denz. 1789 (3008).
[5] Conc. Araus. II, can. 7: Denz. 180 (377); Conc. Vat. I, l.c. :Denz. 1791 (3010).
[6] Conc. Vat. I, Const. Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap.2: Denz. 1786 (3005).
[7] Ibid.: Denz. 1785 na 1786 (3004 na 3005).
[8] Taz. Mt 28:19-20 na Mk 16:15. Conc. Trid., Decr. De Canonicis Scripturis: Denz. 783 (1501).
[9] Taz. Conc. Trid., l.c.; Conc. Vat. I, Const. Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap. 2: Denz. 1787 (3006).
[10] Mt. Ireneus, Adv. Haer., III, 3, 1: PG 7, 848; Harvey, 2, uk. 9.
[11] Taz. Conc. Nic. II: Denz. 303 (602). Conc. Const. IV, Sess. X, can. 1: Denz. 336 (650-652).
[12] Taz. Conc. Vat. I, Const. Dogm. de fide catholica, Dei Filius, cap. 4: Denz. 1800 (3020).
[13] Taz. Conc. Trid., Decr. De canonicis Scripturis: Denz. 783 (1501).
[14] Taz. Pius XII, Const. Apost. Munificentissimus Deus, 1 nov. 1950: AAS 42 (1950) uk. 756, collatis verbis Mt. Cypriani, Epist. 66, 8: CSEL 3, 2, 733: “Ecclesia plebs Sacerdoti adunata et Pastori suo grex adhaerens”.
[15] Taz. Conc. Vat. I, Const Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap. 3: Denz. 1792 (3011).
[16] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Humani Generis, 12 ago. 1950: AAS 42 (1950) uk. 568-569: Denz. 2314 (3886).
[17] Taz. Conc. Vat. I, Const. Dogm. de fide catholica Dei Filius, cap. 2: Denz. 1787 (3006). Pont. Comm. Biblica, Decr. 18 juni 1915: Denz. 2180 (3629); EB 420, S.S.C.S. Officii, Epist. 22 des. 1923: EB 499.
[18] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Divino afflante Spiritu, 30 sep.1943: AAS 35 (1943) uk. 314; EB 556.
[19] In et per hominem: Taz. Ebr 1:1 na 4:7 ( in): 2Sam 23:2; Mt 1:22 na passim ( per); Conc. Vat. I: Schema de doctr. cath, nota 9: Coll. Lac. VII, 522.
[20] Leo XIII, Litt. Encycl. Providentissimus Deus, 18 nov. 1893: Denz. 1952 (3293); EB 125.
[21] Taz. Mt. Augustinus, De Gen. ad litt., 2, 9, 20: PL 34, 270-271; CSEL 28, 1, 46-47 na Epist. 82, 3: PL 33,277; CSEL 34, 2, 354. – Mt. Thomas, De Ver., q. 12, a. 2, C. – Conc. Trid., Decr. De canonicis Scripturis: Denz. 783 (1501). – Leo XIII, Litt. Encycl. Providentissimus Deus: EB 121, 124, 126-127. – Pius XII, Litt. Encycl. Divino afflante Spiritu: EB 539.
[22] Taz. Mt. Augustinus, De Civ. Dei, XVII, 6, 2: PL 41, 573; CSEL 40, 2, 228.
[23] Taz. Mt. Augustinus, De Doctr. Christ., III, 18, 26: PL 34, 75-76; CSEL 80, 95.
[24] Taz. Pius XII, l.c.: Denz. 2294 (3829-3830); EB 557-562.
[25] Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Spiritus Paraclitus, 15 sep. 1920: EB 469. - Mt. Hieronymus, In Gal. 5, 19-21; PL 26, 417 A.
[26] Taz. Conc. Vat. I, Const. Dogm. de fide catholica, Dei Filius, cap. 2: Denz. 1788 (3007).
[27] Mt. Ioannes Chrysostomus, In Gen. 3, 8 (hom. 17, 1): PG 53, 134. “Attemperatio” kigiriki: sugkatabasij.
[28] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Mit brennender Sorge, 14 machi 1937: AAS 29 (1937) uk. 151.
[29] Taz. Mt. Augustinus, Quaest. in Hept. 2, 73: PL 34, 623.
[30] Taz. Mt. Irenaeus, Adv. Haer., III, 21, 3: PG 7, 950; (25,1: Harvey, 2, uk. 115). Mt. Cyrillus Hieros., Catech., 4, 35: PG 33, 497. Theodorus Mops., In Soph., 1, 4-6: PG 66, 452D-453A.
[31] Taz. Mt. Irenaeus, Adv. Haer., III, II, 8: PG 7, 885; ed. Sagnard uk.194.
[32] Taz. Yn 2:22; 12:16; na pia 14:26; 16:12-13; 7:39.
[33] Taz. Yn 14:26; 16:13.
[34] Taz. Instructio Sancta Mater Ecclesia a Pontificio Consilio Studiis Bibliorum provehendis edita: AAS 56 (1964) uk. 175.
[35] Taz. Pius XII, Litt. Encycl. Divino afflante Spiritu, 30 sep. 1943: EB 551, 553, 567. Comm. Biblica, Instructio de S. Scriptura in Clericorum Seminariis et Religiororum Collegiis recte docenda, 13 mei 1950: AAS 42 (1950) uk. 495-505.
[36] Taz. Pius XII, ibidem: EB 569.
[37] Taz. Leo XIII, Litt. Encycl. Providentissimus Deus: EB 114; Benedictus XV, Litt. Encycl. Spiritus Paraclitus, 15 sep. 1920: EB 483.
[38] Mt. Augustinus, Serm. 179, 1: PL 38, 966.
[39] Mt. Hieronimus, Comm. in Is., Prol.: PL 24, 17. - Taz. Benedictus XV, Litt. Encycl. Spiritus Paraclitus: EB 475-480. Pius XII, Litt. Encycl. Divino afflante Spiritu: EB 544.
[40] Mt. Ambrosius, De officiis ministrorum, I, 20, 88: PL 16, 50.
[41] Mt. Irenaeus, Adv. Haer., IV, 32, 1: PG 7, 1071; (= 49, 2) Harvey, 2, uk. 255.