[AR - BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]
Konstitusio juu ya liturujia
SACROSANCTUM CONCILIUM
Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso mkuu
ataka haya yakumbukwe daima
UTANGULIZI
1. Mtaguso Mkuu (Sacrosanctum Concilium) umeazimu kukuza kila siku zaidi na zaidi maisha ya kikristo kati ya waamini; kuzilinganisha taratibu zile zinazobadilika na mahitaji ya siku hizi; kuyahimiza mambo yale yote yanayosaidia kuleta umoja kati ya wote wanaomwamini Kristo; kuyaimarisha yale yote yanayofaa kwa kuwaita wote kundini mwa Kanisa. Mtaguso huu Mkuu unaona ni wajibu wake kujali kwa namna ya pekee kurekebisha na kukuza Liturujia.
Nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa
2. Maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu”[1]. Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waonyeshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kuhiji. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea[2]. Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho[3], mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo[4]. Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumhubiri Kristo; na kwa njia hiyo inawaonyesha wale walio nje [nalo,] Kanisa lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya mataifa[5], ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja[6], mpaka liwepo zizi moja na mchungaji mmoja[7].
Hati hii juu ya Liturujia na Riti mbalimbali
3. Kwa hiyo Mtaguso Mkuu unadhamiria kwamba inabidi kukumbusha kanuni zifuatazo kuhusu ukuzaji na marekebisho ya Liturujia, na kutoa miongozo ya utekelezaji.
Kati ya kanuni na sheria hizo, zipo nyingi zinazoweza kutumika na lazima zitumike katika Riti*[, au madhehebu,] ya Kiroma (Ritum romanum) na pia Riti nyinginezo. Miongozo ya utekelezaji ifuatayo, lakini, ni kwa ajili ya Riti ya Kiroma tu, isipokuwa kama ni mambo ambayo, kwa maumbile yake yenyewe, yanahusu pia Riti nyingine.
Heshima kwa Riti zote zilizo halali
4. Mwishowe, Mtaguso Mkuu, kwa kuheshimu kiaminifu Mapokeo, unathibitisha kwamba Mama Kanisa anastahi kwa heshima moja Riti zote (omnes Ritus) zilizokubaliwa kuwa halali. Tena Mtaguso unatamani kwamba [Riti hizo] zihifadhiwe kwa baadaye na kuendelezwa kwa hali na mali. Aidha, Mtaguso unatamani zitengenezwe upya, kama ni lazima, kwa utaratibu na kadiri ya Mapokeo halisi na pia zipewe nguvu mpya kulingana na mazingira ya sasa.
Sura ya Kwanza
KANUNI ZA JUMLA ZA MAREKEBISHO NA UKUZAJI WA LITURUJIA TAKATIFU
I - MAUMBILE YA LITURUJIA NA UMUHIMU WAKE KATIKA MAISHA YA KANISA
5. Mungu, “ambaye hutaka watu wote waokolewe na kupata kujua yaliyo kweli” (1Tim 2:4), “ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi” (Ebr 1:1), ulipofika utimilifu wa nyakati akamtuma Mwanawe, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, aliyetiwa mafuta kwa Roho Mtakatifu, ili awahubiri maskini habari njema, awagange waliovunjika moyo[8], yeye aliye “mganga wa mwili na wa roho”[9], Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu[10]. Maana ubinadamu wake, katika kuungana na Neno, ulikuwa chombo cha wokovu wetu. Kwa hiyo “katika Kristo ulitokea utimilifu halisi wa upatanisho wetu, nasi tulipewa ukamilifu wa ibada kwa Mungu”[11].
Tendo hilo la ukombozi wa wanadamu na la kutukuzwa kwake kamili, lenye utangulizi wake katika miujiza iliyotendeka kwa taifa la Agano la Kale, lilitimizwa na Bwana Yesu hasa kwa njia ya fumbo la Pasaka ya mateso yake yenye heri, ufufuko wake kutoka kuzimu, na kupaa kwake mbinguni kwa utukufu; fumbo ambalo kwa ajili yake “kwa kufa aliangamiza mauti na alipofufuka akaturudishia uzima”[12]. Maana, kutoka ubavuni mwa Kristo akilala msalabani ilitoka sakramenti ya ajabu ya Kanisa lote[13].
Tendo la wokovu linaloendelezwa na Kanisa hutimizwa katika Liturujia
6. Kama vile Kristo alivyotumwa na Baba, kadhalika naye aliwatuma Mitume, waliojaa Roho Mtakatifu.Alifanya hivyo sio tu ili watangaze, kwa kuhubiri Injili kwa kila kiumbe[14], kwamba Mwana wa Mungu, kwa kifo na ufufuko wake, ametuokoa kutoka mamlaka ya shetani[15]na ya mauti na kutuleta katika ufalme wa Baba yake; bali, pia alitaka kazi hiyo ya ukombozi, ambayo walikuwa wakiitangaza, waitekeleze kwa njia ya Sadaka na Sakramenti, ambazo ni kiini cha maisha ya kiliturujia. Hivyo, kwa njia ya Ubatizo, wanadamu wanaingizwa katika fumbo la Pasaka ya Kristo: wanakufa pamoja naye, wanazikwa na kufufuka pamoja naye[16], wanapokea roho ya kufanywa wana “ambayo kwa hiyo twalia: Aba, yaani Baba” (Rum 8:15); na hivyo wanapata kuwa wale waabuduo halisi ambao Baba awatafuta[17]. Kadhalika, kila wailapo karamu ya Bwana, waitangaza kifo cha Bwana hata ajapo[18]. Kwa hiyo, siku ileile ya Pentekoste, ambapo Kanisa lilidhihirishwa ulimwenguni, “wale waliolipokea neno” la Petro “wakabatizwa”. Nao “wakawa wakidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali ... wakimsifu Mungu kwa pamoja, na kuwapendeza watu wote” (Mdo 2:41-42.47 Vulg.). Tokea hapo, Kanisa halijaacha kamwe kujumuika pamoja ili kuliadhimisha fumbo la Pasaka: kwa kuyasoma yote “katika Maandiko yanayomhusu Yeye [Kristo]” (Lk 24:27), kwa adhimisho la Ekaristi, ambapo “vimefanyika wazi tena mafanikio na ushindi mkuu wa kifo chake”[19], na kwa kumshukuru “Mungu kwa sababu ya kipawa chake tusichoweza kukisifu kama ipasavyo” (2Kor 9:15), katika Yesu Kristo, “kwa sifa ya utukufu wake” (Efe 1:12), kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Uwepo wa Kristo katika Liturujia
7. Kusudi kutimiza tendo kubwa namna hii, Kristo yupo daima katika Kanisa lake, kwa jinsi ya pekee katika maadhimisho ya kiliturujia. Yupo kwenye Sadaka ya Misa katika nafsi ya kasisi, “Yeye ambaye, akijitoa mara moja msalabani, anajitoa tena mwenyewe kwa huduma ya mapadre”[20]. Yupo hasa chini ya maumbo ya Ekaristi. Yupo kwa nguvu yake katika sakramenti, ili kwamba mtu anapobatiza, ni Kristo mwenyewe anayebatiza[21]. Yupo katika Neno lake, kwa kuwa ni Yeye anayesema wakati Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Kanisa. Yupo, tena, wakati Kanisa linaposali (supplicat) na kuimba zaburi (psallit), kwa vile aliahidi: “Walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu nami nipo papo hapo katikati yao” (Mt 18:20).
Kwa kweli, katika tendo kubwa namna hii, ambalo kwa njia yake Mungu hutukuzwa kikamilifu na wanadamu wanatakatifuzwa, Kristo daima hulishirikisha Kanisa; naye Kanisa ni Bibiarusi yake mpendwa sana, ambaye anamwomba Bwana wake na kwa njia yake anamwabudu Baba wa milele.
Kumbe, kwa haki Liturujia hutazamwa kama utekelezaji wa kazi ya kikuhani ya Yesu Kristo. Katika Liturujia, kwa ishara zinazoonekana, huo-nyeshwa na kutendeka kutakatifuzwa kwake binadamu, kila ishara ikiwa na maana ya pekee. Katika Liturujia, ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa fumbo wa Yesu Kristo, yaani na Kichwa na viungo vyake.
Kwa hiyo kila adhimisho la kiliturujia, kwa kuwa ni tendo la Yesu Kristo Kuhani na la Mwili wake, ndilo Kanisa, ni tendo takatifu kupita yote na hakuna tendo jingine la Kanisa linalofanana nalo kwa manufaa kwa kiwango kilekile na kwa daraja ileile.
Liturujia ya duniani na ile ya mbinguni
8. Katika Liturujia ya hapa duniani sisi tunashiriki, tukiionja, Liturujia ya mbinguni, iadhimishwayo katika Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, tunaouelekea kama wasafiri, ambako Kristo ameketi mkono wa kuume wa Mungu kama mhudumu wa patakatifu na wa ile hema ya kweli[22]. Tunaungana na wapiganaji wa jeshi la mbinguni kumwimbia Bwana wimbo wa utukufu. Tukiwakumbuka kwa heshima watakatifu, twatumaini kupata ushirika nao; twamngojea kwa shauku Mkombozi, Bwana wetu Yesu Kristo, mpaka atakapojidhihirisha, Yeye aliye uzima wetu, ndipo na sisi tutakapodhihirishwa pamoja naye katika utukufu[23].
Liturujia takatifu haimalizi utendaji wote wa Kanisa
9. Liturujia takatifu haimalizi utendaji wote wa Kanisa. Maana, kabla wanadamu hawajaikaribia Liturujia, yabidi waalikwe kwenye imani na toba: “Wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije wasipopelekwa?” (Rum 10:14-15).
Kwa hiyo Kanisa laihubiri habari njema ya wokovu kwa wale wasioamini, kusudi watu wote wamjue Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo aliyemtuma, na pia, wakitubu, waongoke kutoka njia zao[24]. Aidha, Kanisa lazima lihubiri daima imani na toba kwa waamini; lazima pia liwatayarishe kwa Masakramenti, liwafundishe kuyashika yote yaliyoamriwa na Kristo[25], na pia liwahimize kwenye matendo yote ya mapendo, ya ibada na ya utume, ambayo huonyesha ya kuwa waamini wa Kristo si wa ulimwengu huu, lakini wao ni nuru ya ulimwengu na lazima wamtukuze Baba mbele ya watu.
Liturujia ni kilele na chemchemi ya maisha ya Kanisa
10. Hata hivyo Liturujia ni kilele ambapo kazi ya Kanisa inaelekea, na papo hapo ni chemchemi zinamotoka nguvu zake zote. Maana, bidii zote za kazi za kitume hukusudiwa ili wote, waliofanywa watoto wa Mungu kwa njia ya imani na Ubatizo, wakusanyike pamoja, wamtukuze Mungu katika Kanisa, washiriki sadaka na kuila karamu ya Bwana.
Kwa upande wake, Liturujia huwasukuma waamini, waliolishwa kwa “sakramenti za kipasaka”, kuishi katika “umoja wa utakatifu”[26]. Tena huwaombea “waonyeshe katika maisha yao yale waliyopewa katika imani”[27]. Aidha, kufanyika upya kwa agano la Bwana na wanadamu katika Ekaristi kuwavuta na kuwasha ndani ya waamini upendo wenye bidii wa Kristo. Kwa hiyo kutokana na Liturujia, hasa Ekaristi, humiminwa ndani yetu neema, kama toka chemchemi, na pia hupatikana kikamilifu lengo la utendaji wote wa Kanisa ambalo ni utakatifu ule wa wanadamu na tukuzo la Mungu, katika Kristo.
Umuhimu na maelekeo ya kila mtu katika Liturujia
11. Lakini, ili kufikia lengo hilo kamili, sharti waamini washiriki Liturujia takatifu kwa maelekeo ya moyo mnyofu, walinganishe akili zao na sauti, wafanye kazi pamoja na neema ya Mungu ili wasiipokee bure[28]. Kwa hiyo wachungaji watukufu wanapaswa kuangalia kuwa katika tendo la Liturujia zishikwe sheria zifanyazo maadhimisho yawe thabiti na halali. Wachungaji pia lazima wahakikishe kuwa waamini wanaelewa kinachofanyika na wanashiriki kikamilifu na kufaidi matunda ya maadhimisho hayo.
Liturujia na sala ya binafsi
12. Lakini maisha ya kiroho hayaishii katika kuishiriki Liturujia takatifu tu. Maana mkristo, anayealikwa kushiriki sala ya pamoja, anapaswa pia aingie chumbani mwake kumwomba Baba katika siri[29]. Aidha, kadiri ya mafundisho ya Mtume anapaswa kusali bila kukoma[30]. Naye Mtume mwenyewe hutufundisha kuchukua sikuzote katika mwili wetu mateso yake Yesu, ili uzima wa Yesu nao hudhihirishwe katika mwili wetu wenye kufa[31]. Kwa sababu hiyo katika sadaka ya Misa twamwomba Bwana kwamba “anapopokea sadaka ya dhabihu ya kiroho” atufanye sisi wenyewe kuwa kwake “sadaka ya milele”[32].
Ibada mbalimbali za wakristo zielekee kwenye Liturujia
13. Ibada mbalimbali za watu wakristo, mradi zilingane na kanuni na taratibu za Kanisa, zinahimizwa sana, hasa zinapofanyika kwa agizo la Kiti cha Kitume.
Ibada mbalimbali za Makanisa maalum (particularium) zina hadhi ya pekee, hasa zinapofanyika kwa agizo la Maaskofu, kadiri ya desturi au vitabu vilivyoidhinishwa kihalali.
Ibada hizo, lakini, sharti zipangwe kwa kulingana vipindi vya mwaka wa kiliturujia, zilingane na Liturujia takatifu, zitokane nayo kwa namna fulani, na kuwaelekeza watu kwenye Liturujia yenyewe, kwa sababu, kwa tabia yake, Liturujia ina hadhi ya juu zaidi kuliko ibada za watu.
II - UMUHIMU WA KUHIMIZA MALEZI YA KILITURUJIA NA KUSHIRIKI HAI KWA WAAMINI
14. Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya kiliturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji. Jambo hili linadaiwa na tabia ya Liturujia yenyewe na pia – kwa sababu ya Ubatizo [wao], ni haki na wajibu wa watu wakristo, ambao ni “mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu” (1Pet 2:9; taz. 2:4-5).
Katika kurekebisha na kukuza Liturujia lazima kujali kwa namna ya pekee kushiriki huko kwa utimilifu na utendaji kwa waamini wote: maana [Liturujia] ni chemchemi ya kwanza na ya lazima ambayo toka kwake waamini wanaweza kuchota roho kweli ya kikristo. Kwa hiyo wachungaji wa roho, katika kazi zao zote za kitume, wanapaswa kuishughulikia bila kukoma kwa njia ya mafundisho yafaayo.
Lakini haiwezekani kutumaini kuyatimiza hayo, kama wachungaji wenyewe hawajawa na roho na nguvu ya Liturujia, na kabla hawajajielimisha ili wawaelimishe na wengine. Kwa hiyo ni muhimu kabisa, awali ya yote, makleri wapate mafundisho juu ya Liturujia. Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu unaagiza yafuatayo.
Malezi ya maprofesa wa Liturujia
15. Walimu wanaochaguliwa kufundisha Liturujia katika seminari, katika vituo vya malezi ya kitawa, na katika vyuo vya elimu ya Teolojia, ni lazima wapate elimu inayoifaa kazi yao katika vyuo vinavyofundisha haya kwa namna ya pekee.
Ufundishaji wa Liturujia
16. Liturujia takatifu katika seminari na nyumba za malezi ya kitawa, lazima ihesabiwe kati ya masomo ya lazima na ya muhimu zaidi. Aidha, katika vyuo vya Teolojia ihesabiwe kati ya masomo ya maana zaidi, na ifundishwe kadiri ya muono wa kiteolojia, wa kihistoria, wa kiroho, wa kichungaji na wa kisheria. Aidha, walimu wa masomo mengine, hasa walimu wa Dogma, Maandiko Matakatifu, Teolojia ya maisha ya kiroho na ya kichungaji, wajitahidi kusisitiza, kila mmoja kadiri ya matakwa ya masomo yake, fumbo la Kristo na historia ya wokovu ili uonekane wazi uhusiano wake na Liturujia, na jinsi masomo hayo yanavyohusiana katika malezi ya kipadre.
Malezi ya waseminari kuhusu Liturujia
17. Waseminari wakubwa, katika seminari na katika nyumba za kitawa, waelimishwe juu ya Liturujia katika maisha ya kiroho; yaani waingizwe polepole ili waweze kuelewa maana ya madhehebu takatifu na kushiriki kwa moyo wote, na pia wapate kuadhimisha mafumbo matakatifu na ibada nyingine zenye roho ya kiliturujia. Pia wajifunze kuzishika sheria za kiliturujia, ili maisha katika seminari na katika nyumba za malezi za kitawa zitawaliwe na roho ya kiliturujia.
Kuwasaidia mapadre mintarafu Liturujia 18. Mapadre, wanajimbo na pia watawa, wanaofanya kazi tayari katika shamba la mzabibu la Bwana, wasaidiwe kwa kila namna ifaayo ili waelewe zaidi na zaidi yale watendayo katika ibada takatifu, tena wasaidiwe kuishi maisha ya kiliturujia na kuwashirikisha waamini waliokabidhiwa.
Kuwaelimisha waamini juu ya Liturujia 19. Wachungaji wa roho wajitahidi, kwa bidii na saburi, ili waamini waelimishwe juu ya Liturujia na pia waweze kuishiriki kikamilifu, katika mwili na katika roho, kulingana na umri wao, hali yao, aina ya maisha yao na elimu yao ya kidini. Kwa njia hii wachungaji hawa watatimiza moja ya majukumu yao ya kwanza, yaani kuwa wagawaji waaminifu wa mafumbo ya Mungu. Aidha, waliongoze kundi lao katika mambo hayo, si kwa maneno tu, bali pia kwa mifano.
Vyombo vya upashanaji habari na Liturujia 20. Kama zinatumiwa redio na televisheni kutangaza ibada takatifu, hasa Misa, matumizi ya vyombo hivyo yawe ya heshima na utaratibu, chini ya uongozi na udhamini wa mtu mwenye ujuzi, ambaye ameteuliwa na Maaskofu kwa kazi hiyo.
III - MAREKEBISHO YA LITURUJIA TAKATIFU 21. Mama Kanisa anatamani kufanya kwa uangalifu marekebisho ya Liturujia yenyewe, ili kuhakikisha kuwa wakristo wanapata wingi wa neema katika Liturujia takatifu. Katika Liturujia ipo sehemu isiyobadilika, kwa sababu imewekwa na Mungu; na pia zipo sehemu zinazoweza kubadilika, nazo ni zile ambazo, kufuatana na mwenendo wa nyakati, zinaweza au pia zinapaswa kubadilika, endapo ndani yake yameingia mambo yasiyolingana na maumbile halisi ya Liturujia yenyewe, au inapoonekana kutofaa tena.
Katika marekebisho hayo, inabidi kuratibu matini na madhehebu za ibada ili zionyeshe kinaganaga zaidi mambo matakatifu zinayoisharisha, nao wakristo waweze kuyaelewa kwa urahisi iwezekanavyo na kuyashiriki kikamilifu, kwa bidii na kama jumuiya.
Kwa sababu hiyo, Mtaguso Mkuu unaweka kanuni za jumla zifuatazo.
A) Kanuni za jumla
Kuratibu Liturujia ni juu ya Hierarkia
22. § 1. Kuratibu Liturujia takatifu ni juu ya mamlaka ya Kanisa tu, ambayo ipo katika Kiti Kitakatifu na, kadiri ya sheria, kwa Maaskofu.
§ 2. Kwa uwezo unaotokana na sheria, kuratibu Liturujia, kadiri ya mipaka iliyokubaliwa, ni juu ya Mabaraza mbalimbali ya Maaskofu ya nchi fulani yaliyoundwa kwa mujibu wa sheria kusimamia nchi hizo.
§ 3. Kwa hiyo, mtu mwingine yeyote yule, hata akiwa padre, hawezi kuongeza, kuondoa au kubadili jambo lolote kwa uamuzi wake mintarafu Liturujia.
Mapokeo na maendeleo 23. Ili kuyahifadhi mapokeo mema, na hapohapo lakini kufanyiza maendeleo ya halali yasitawi, marekebisho ya kila sehemu ya Liturujia lazima yatanguliwe na uchunguzi wa kina wa kiteolojia, wa kihistoria na wa kichungaji. Aidha, marekebisho hayo yazijali kanuni za jumla zinazohusu muundo na roho ya Liturujia. Tena yajali mang’amuzi yatokanayo na marekebisho ya Liturujia ya hivi karibuni na ruhusa (indultis) zilizokubaliwa mahali mbalimbali. Mwishowe, mabadiliko yasifanywe isipokuwa inapodaiwa na manufaa ya kweli ya Kanisa, kwa uangalifu ili mambo mapya yatokane kwa mpangilio na yale yaliyopo.
Pia, kadiri iwezekanavyo, kusiwe na tofauti kubwa kati ya ibada katika nchi zilizo jirani.
Biblia na Liturujia
24. Jambo muhimu kuliko yote katika adhimisho la Liturujia ni Maandiko Matakatifu, maana katika hayo huchukuliwa masomo ya kusomwa na kufafanuliwa katika mahubiri, na pia zaburi zinazoimbwa. Sala, maombi na nyimbo hupata uvuvio toka Maandiko, kama vile toka Maandiko matendo na ishara hupata maana. Kwa hiyo, ili kufaulu kufanya marekebisho na maendeleo na malinganisho ya Liturujia, ni lazima kuhimiza ule upendo mtamu na hai wa Maandiko Matakatifu, ambao unashuhudiwa na mapokeo mastahiki ya Makanisa ya Mashariki na ya Magharibi.
Marekebisho ya vitabu vya Liturujia 25. Vitabu vya kiliturujia virekebishwe upesi iwezekanavyo; kazi hiyo ifanywe na watu wenye ujuzi, na maoni ya Maaskofu wa nchi mbalimbali yasikilizwe.
B) Kanuni zitokanazo na tabia ya kidaraja na ya kijumuiya ya Liturujia 26. Matendo ya kiliturujia si matendo ya kila mmoja peke yake, bali ni maadhimisho ya Kanisa, ambalo ni “sakramenti ya umoja”, yaani taifa takatifu linalokusanywa na kuratibishwa chini ya uongozi wa Maaskofu[33].
Kwa sababu hiyo matendo hayo ni ya mwili wote kabisa wa Kanisa, nayo huudhihirisha na kuuimarisha. Aidha, kila mmoja wa wanakanisa anahusika kwa namna tofauti, kadiri ya utofauti wa daraja, wa majukumu, na wa ushiriki kiutendaji
Ubora wa adhimisho la pamoja 27. Kila mara ibada, kulingana na maumbile ya kila moja, zinapodai adhimisho la pamoja kwa mahudhurio ya waamini wanaoshiriki kimatendo, ihimizwe kwamba adhimisho hilo ni la kupendelewa zaidi, kadiri inavyowezekana, kuliko adhimisho la mtu peke yake, kana kwamba lingekuwa ibada ya binafsi.
Hayo yanahusu hasa adhimisho la Misa – hata kama kila Misa ni daima tendo la hadhara na la kijumuiya – na pia maadhimisho ya sakramenti.
Nafasi ya kila mmoja katika adhimisho la Liturujia 28. Katika maadhimisho ya liturujia kila mmoja, mhudumu au mwamini, aliye na kazi ya kufanya, atekeleze yote na sehemu zile tu zinazohusu wajibu wake, kulingana na maumbile ya ibada na kanuni za Liturujia.
29. Pia watumishi wa altare, wasomaji, wenye kueleza ibada na wanakwaya wote, wanatekeleza huduma kweli ya kiliturujia. Kwa hiyo inawapasa watekeleze kazi yao kwa ule uchaji wa kweli na adabu inayofaa huduma muhimu namna hii, na ambayo taifa la Mungu kwa haki linadai kwao.
Hivyo inabidi wajawe kwa makini na roho ya kiliturujia, kila mmoja kadiri ya hali yake; na pia wafundishwe kutenda yote kufuatana na kanuni za utaratibu zilizowekwa.
Kushiriki kikamilifu kwa waamini 30. Ili kuwawezesha waamini washiriki kimatendo, mashangilio ya waamini, maitikio, kuimba zaburi, antifona, nyimbo, vitendo, ishara na mkao wa mwili vitiliwe maanani. Unyamavu mtakatifu utumike pia, wakati unapodaiwa.
31. Katika marekebisho ya vitabu vya kiliturujia, iangaliwe kwa makini kwamba maelekezo (rubricae) yanayowahusu waamini pia yawekwe wazi kabisa.
Liturujia na usawa wa waamini 32. Katika Liturujia usiwepo upendeleo wowote kwa watu binafsi ama cheo, iwe katika maadhimisho au katika fahari ya nje, isipokuwa kwa cheo kitokanacho na kazi ya kiliturujia na Daraja takatifu; au pia heshima zinazowapasa viongozi wa serikali kwa kadiri ya sheria za kiliturujia.
C) Kanuni zitokanazo na tabia ya kiliturujia ya kuelimisha na kuwalea waamini 33. Ingawa Liturujia takatifu ni hasa ibada kwa Mungu Mkuu, yamo pia ndani yake mafundisho tele kwa waamini[34]. Maana katika Liturujia Mungu anaongea na watu wake; naye Kristo anaendelea kuhubiri Injili. Waamini kwa upande wao wanamwitikia Mungu kwa nyimbo na sala.
Sala zinazoinuliwa kwa Mungu na padre, aongozaye ibada katika nafsi ya Kristo, zinasemwa kwa niaba ya taifa zima takatifu na wote waliopo. Na zile ishara zinazoonekana, ambazo Liturujia huzitumia kwa kuyaashiria yale mambo ya kimungu yasiyoonekana, zilichaguliwa na Kristo au na Kanisa. Kwa hiyo si yanaposomwa tu “yaliyoandikwa kwa kutufundisha sisi” (Rum 15:4), lakini pia Kanisa linaposali au kuimba au kutenda, imani ya wale wanaoshiriki inalishwa, akili zao zinainuliwa kwa Mungu, ili kumtolea heshima ipasayo na kupokea kwa wingi zaidi neema yake.
Kwa hiyo, katika kufanya marekebisho ya Liturujia kanuni za jumla zifuatazo hazina budi kuzingatiwa.
Ukamilifu na kueleweka kwa ibada 34. Ibada zing’ae kwa heshima na urahisi, ziwe fupi, wazi na bila marudio ya bure. Zilingane na uwezo wa ufahamu wa waamini, bila kuhitaji, kwa kawaida, maelezo mengi.
Biblia, homilia na katekesi kuhusu Liturujia 35. Ili ionekane wazi kwamba katika Liturujia matendo ya ibada na Neno vimeunganika kiundani:
1) Katika ibada takatifu, masomo ya Maandiko Matakatifu yapangwe kwa wingi zaidi, kutoka sehemu mbalimbali na kwa jinsi inayofaa zaidi.
2) Wakati ufaao zaidi kwa mahubiri, kama sehemu ya adhimisho la Liturujia, kwa kadiri ya ibada yenyewe inavyoruhusu, uwekwe na kutajwa pia katika rubrika (maelekezo). Huduma ya kuhubiri itimizwe kwa uaminifu kamili na jinsi ifaavyo. Aidha, mahubiri yachotwe hasa kutoka chemchemi ya Maandiko Matakatifu na ya Liturujia, kwani ni tangazo la matendo makuu ya Mungu katika historia ya wokovu, iliyo fumbo la Kristo, fumbo ambalo daima lipo na linatenda kazi ndani yetu, hasa katika maadhimisho ya kiliturujia.
3) Mafundisho kuhusu Liturujia yenyewe yatolewe kwa njia mbalimbali. Katika ibada zenyewe yatolewe maelezo mafupi, ikiwa ni lazima. Hayo yafanywe kwa maneno yaliyotayarishwa au kwa mengine yanayofanana nayo, na padre au mhudumu mwenye uwezo. Lakini hayo yote yafanywe tu katika nafasi zifaazo zaidi.
4) Ibada ya Neno la Mungu ihimizwe, hasa katika makesha ya sherehe, au siku za Majilio na Kwaresima, siku za Dominika na sikukuu, hasa pale asipokuwepo padre. Ikiwa ni hivyo, ibada iongozwe na shemasi au mtu mwingine aliyeruhusiwa na Askofu.
Lugha ya Liturujia 36. § 1. Matumizi ya lugha ya kilatini yahifadhiwe katika madhehebu za ibada za kilatini, licha ya sheria za pekee zikiwemo.
§ 2. Lakini, mara nyingi zaidi itumike lugha ya nchi kwani yaweza kuwafaa sana waamini, iwe katika Misa, katika kuadhimisha Sakramenti, na pia katika sehemu nyingine za Liturujia. Katika masomo na maelekezo, katika baadhi ya sala na nyimbo, lugha ya nchi ipate nafasi zaidi. Kanuni zinazohusu jambo hili zimetolewa peke yake katika sura zifuatazo.
§ 3. Kadiri ya kanuni hizo, kutoa uamuzi mintarafu matumizi ya lugha ya nchi ni juu ya mamlaka ya kikanisa husika ya kila nchi, kama ilivyoandikwa katika ibara 22 § 2. Na ikiwa inafaa, maoni ya Maaskofu wa nchi jirani zinazotumia lugha hiyo yasikilizwe. Maamuzi hayo lazima yapate kibali, yaani idhini, cha Kiti cha Kitume.
§ 4. Tafsiri ya vitabu vya Liturujia vya kilatini lazima ikubaliwe na mamlaka ya kikanisa husika ya nchi ile, kama yalivyotajwa hapo juu.
D) Kanuni za marekebisho ya Liturujia kulingana na hali za watu na mapokeo yao 37. Kanisa, katika yale yasiyogusa imani au manufaa ya jumuiya nzima ya waamini, halipendi kuwabana wote kwa mtindo moja, wala katika Liturujia. Kanisa huheshimu na kuhimiza vipawa na tunu za mila za kila taifa na jamii. Katika tamaduni za mataifa, yale ambayo hayafungamani kabisa na ushirikina au makosa, Kanisa huyachunguza kwa wema na pia, kama inawezekana, huyahifadhi yalivyo. Na mara nyingine huyaingiza hata katika Liturujia yenyewe, iwapo tu yanalingana na roho ya kweli na halisi ya kiliturujia.
38. Pasipo kuvunja umoja wa Riti ya Kiroma, katika marekebisho ya vitabu vya Liturujia, iachwe nafasi kwa ajili ya tofauti zilizo halali na kwa marekebisho yanayoweza kufanywa na jamii, nchi na mataifa mbalimbali, hasa katika nchi za misioni. Hayo yatiliwe maanani katika mipangilio ya ibada na katika kuandaa maelekezo (rubricis) ya jinsi ibada zinavyofanyika.
39. Kadiri ya maagizo yaliyomo katika matoleo halisi (editionibus typicis) ya vitabu vya kiliturujia, mamlaka ya kufanya marekebisho ni juu ya Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2; marekebisho hayo yahusu hasa utoaji wa Sakramenti, visakramenti, maandamano, lugha na muziki na sanaa za kiliturujia kadiri ya kanuni za msingi zilizomo katika hati hii.
Jinsi ya kufanya marekebisho ya Liturujia 40. Kwa kuwa katika nchi mbalimbali marekebisho ya kina ya Liturujia yanatakiwa upesi, nayo yanaleta ugumu zaidi, basi, kwa sababu hiyo:
1) Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2, yachunguze kwa makini na busara mambo yaliyomo katika mila na desturi ya kila jamii ambayo yanaweza kuingizwa, kwa namna ifaayo, katika ibada kwa Mungu. Hatimaye, marekebisho yanayodhaniwa kuwa ni ya kufaa au ya lazima, yapelekwe kwa Baba Mtakatifu kusudi yaingizwe kwa idhini yake.
2) Kusudi marekebisho hayo yafanyike kwa tahadhari inayotakiwa, Baba Mtakatifu atatoa idhini kwa Mabaraza ya Maaskofu ili yaruhusu na kuongoza, ikiwa inafaa, majaribio ya kwanza yatakiwayo katika vikundi vilivyoandaliwa kwa kusudi hilo na kwa muda wa kupangwa.
3) Kwa vile sheria za kiliturujia mara nyingi huleta matatizo mintarafu marekebisho, hasa katika misioni, ni lazima wataalamu wahusishwe katika kuzitunga sheria hizo.
IV - KUKUZA MAISHA YA KILITURUJIA JIMBONI NA PAROKIANI 41. Askofu lazima atazamwe kama kuhani mkuu wa kundi lake na ambaye maisha ya waamini wake katika Kristo kwa namna fulani yanatoka kwake na yanamtegemea.
Kwa hiyo ni lazima waamini wote wakaze sana umuhimu wa maisha ya kiliturujia ya jimbo pamoja na Askofu, hasa katika kanisa katedrali (cathedrali): wote waelewe kwamba Kanisa ladhihirika hasa katika ushirikiano kamili na wa kimatendo wa taifa lote takatifu la Mungu katika maadhimisho yaleyale ya kiliturujia, hasa katika Ekaristi ileile moja, sala ileile na altare ileile anapoongoza Askofu pamoja na mapadre wake na watumishi[35].
Maisha ya kiliturujia katika parokia 42. Maadam Askofu hawezi mwenyewe kuongoza daima na popote kundi lake zima katika Kanisa lake, basi Askofu hana budi kuwagawanya waamini katika makundi mbalimbali, na kati ya hayo yana umuhimu wa maana sana maparokia yanayoundwa kila mahali chini ya uongozi wa mchungaji amwakilishaye Askofu; maana, hayo yanawakilisha kwa namna fulani Kanisa lionekanalo ambalo limewekwa katika dunia nzima.
Kwa hiyo maisha ya kiliturujia ya parokia na uhusiano wake na Askofu lazima visitawishwe katika roho na matendo ya waamini na wakleri; pia lazima kufanya jitihada ili hisia ya jumuiya katika parokia ichanue hasa katika kuadhimisha pamoja Misa ya Dominika.
V - KUKUZA KAZI YA KICHUNGAJI MINTARAFU LITURUJIA 43. Hamasa ya kukuza na kurekebisha Liturujia inatazamwa kwa haki kama ishara ya Maongozi ya Mungu katika nyakati zetu, na pia kama mpito wa Roho Mtakatifu katika Kanisa lake; tena inapiga chapa mahsusi kwa maisha ya Kanisa na pia kwa mwelekeo mzima wa dini kimawazo na kimatendo kwa wakati huu.
Kwa sababu hiyo, kwa lengo la kuongeza zaidi na zaidi katika Kanisa kazi hiyo ya kichungaji mintarafu Liturujia, Mtaguso Mkuu unaamua yafuatayo:
Kamati ya Liturujia kitaifa 44. Yafaa Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2, yaunde kamati ya Liturujia ambayo itafanya kazi ikisaidiwa na wataalamu wa Liturujia, muziki, sanaa takatifu pamoja na uchungaji. Kama inawezekana, kamati hiyo isaidiwe na aina ya taasisi ya kichungaji ya Liturujia yenye wataalamu katika uwanja huo, bila kuwatenga walei pale inapotakiwa. Itakuwa ni wajibu wa kamati yenyewe, chini ya uongozi wa Mabaraza ya Maaskofu, kama ilivyoelezwa hapo juu, kuratibu kazi ya kichungaji mintarafu Liturujia katika sehemu yake iliyokabidhiwa, na pia kuhimiza utafiti na majaribio yanayotakiwa kila panapokuwa na suala la kupeleka kwa Baba Mtakatifu.
Kamati ya Liturujia ya jimbo 45. Vilevile katika kila jimbo iundwe kamati ya Liturujia kwa lengo la kuhimiza, chini ya uongozi wa Askofu, utume wa kiliturujia.
Ikiwa inafaa, majimbo kadhaa yaunde kamati moja ili kuhimiza Liturujia kwa makubaliano ya pamoja.
Kamati nyinginezo 46. Licha ya kamati ya Liturujia, kadiri iwezekanavyo, katika kila jimbo iundwe pia kamati ya muziki na ya sanaa takatifu.
Kamati hizo tatu lazima zishirikiane katika kazi zao, na, ionekanapo kuwa inafaa, ziunganike na kuunda kamati moja.
Sura ya Pili
FUMBO TAKATIFU LA EKARISTI
Misa na fumbo la Pasaka 47. Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza Sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibiarusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: sakramenti ya utakatifu (sacramentum pietatis), ishara ya umoja, kifungo cha mapendo[36], karamu ya Pasaka “ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na hutolewa amana ya uzima wa milele”[37].
Kushiriki kiutendaji kwa waamini katika Misa 48. Kwa sababu hiyo, Kanisa anajibidisha kwa namna nyingi kusudi waamini wasihudhurie fumbo hilo la imani kama wageni au watazamaji bubu, bali waishiriki ibada takatifu kwa akili, kwa moyo na kwa matendo, wakielewa vizuri fumbo hilo kwa njia ya matendo ya kiliturujia na sala. Waamini waelimishwe katika Neno la Mungu; walishwe katika karamu ya Mwili wa Bwana; wamtolee Mungu shukrani; wakitolea hostia isiyo na doa, siyo kwa mikono ya padre tu, bali pia pamoja naye, wajifunze kujitolea wenyewe. Tena, siku kwa siku, kwa njia ya Kristo mshenga, wakamilishwe katika umoja na Mungu na kati yao[38], ili hatimaye Mungu awe yote katika wote.
49. Kwa hiyo, ili sadaka ya Misa ilete manufaa kamili ya kichungaji pia kwa njia ya umbo la ibada, Mtaguso Mkuu unaagiza yafuatayo kwa ajili ya Misa ziadhimishwazo pamoja na waamini, hasa Dominika na Sikukuu.
Marekebisho ya kanuni ya Misa
50. Kanuni ya ibada ya Misa itengenezwe upya ili kiini halisi cha kila sehemu ya ibada na uhusiano kati ya sehemu mbalimbali vionekane wazi zaidi, na kuwawezesha waamini kushiriki kwa moyo na kwa matendo.
Kwa sababu hiyo madhehebu za ibada zirahisishwe, lakini kiini chake kihifadhiwe; yaachwe mambo yale ambayo yalifanyika maradufu na yale yaliyoongezwa bila umuhimu, kadiri nyakati zilivyopita; na mengine yaliyoachwa bila haki yaingizwe tena, kadiri ya kanuni ya kale ya Mababa watakatifu, kadiri itakavyoonekana kufaa au kuwa lazima.
Masomo ya Biblia katika Misa yaongezeke
51. Ili meza ya Neno la Mungu iandaliwe kwa wingi zaidi kwa ajili ya waamini, hazina za Biblia zizidi kufunguliwa, kusudi katika muda wa miaka kadhaa ya kuagizwa waamini wasomewe sehemu kubwa zaidi ya Maandiko Matakatifu.
Homilia
52. Inatiliwa sana maanani homilia, kama sehemu ya Liturujia yenyewe; kwani, kwa njia yake, katika mwaka wa kiliturujia, mafumbo ya imani na miongozo ya maisha ya kikristo vinafafanuliwa kutoka Maandiko Matakatifu. Katika Misa ziadhimishwazo pamoja na waamini siku ya Dominika na Sikukuu zilizoamriwa, homilia isiachwe isipokuwa kwa sababu nzito.
Sala ya waamini 53. “Sala za pamoja” au “sala za waamini” ziingizwe tena baada ya Injili na homilia, hasa Dominika na Sikukuu zilizoamriwa, kusudi, kwa ushirikiano na waamini, yatolewe maombi kwa ajili ya Kanisa takatifu, wale wanaotuongoza, wanaosongwa na mahitaji mbalimbali, kwa ajili ya watu wote na ukombozi wa ulimwengu mzima[39].
Matumizi ya kilatini na lugha ya mahali katika Misa
54. Katika Misa zinazoadhimishwa pamoja na waamini, matumizi ya lugha ya nchi inayohusika yaruhusiwe kwa jinsi ifaavyo, hasa katika masomo na “sala za waamini”, na pia katika sehemu ziwahusuzo waamini, kufuatana na mazingira ya kila nchi, kadiri ya ibara 36 ya hati hii.
Lakini bidii ifanyike ili waamini waweze kusali na kuimba pamoja sehemu za ibada ya Misa ziwahusuzo wao pia katika lugha ya kilatini.
Aidha, ikionekana kwamba inafaa katika nchi nyingine kutumia zaidi lugha ya nchi ile katika Misa, yafuatwe maagizo yaliyotolewa katika ibara 40 ya hati hii.
Komunyo katika maumbo yote mawili 55. Njia kamilifu zaidi ya kushiriki Misa inakazwa sana: nayo ni pale waamini wanapopokea Mwili wa Bwana Yesu, baada ya komunyo ya Padre, kutoka katika sadaka ileile.
Bila kupingana na maagizo ya kidogma ya Mtaguso Mkuu wa Trento[40], inaruhusiwa komunyo katika maumbo mawili kwa makleri na watawa, na pia walei, katika nafasi zinazopangwa na Baba Mtakatifu na kufuatana na maoni ya Askofu, kama vile wanaopewa Daraja takatifu, katika Misa ya kupewa Daraja; wanaoweka nadhiri za kitawa, katika Misa ya kuweka nadhiri; na wanaobatizwa (neophytis), katika Misa ya Ubatizo wao.
Umoja wa Misa 56. Ibada ya Misa ina sehemu mbili, yaani Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi; hizo zote zimeunganika sana kati yake kiasi kwamba zinafanya ibada moja tu. Kwa hiyo Mtaguso Mkuu unawasihi kwa dhati wachungaji wa roho wawaelimishe kwa makini waamini wao, katika katekesi, ili washiriki Misa nzima, hasa siku ya Dominika na Sikukuu zilizoamriwa.
Konselebrasio 57. § 1. Misa ya kushirikiana mapadre wengi pamoja, au ‘Konselebrasio’, ambayo huonyesha vizuri umoja wa upadre, imebaki mpaka leo katika desturi ya Kanisa la Mashariki na pia la Magharibi. Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu umependa kutoa kibali chake kwa konselebrasio katika nafasi zifuatazo:
1° a) Siku ya Alhamisi Kuu ya Karamu ya Mwisho, katika Misa ya Krisma na pia katika Misa ya jioni;
b) katika Misa wakati wa Mitaguso, mikutano ya Maaskofu na Sinodi;
c) katika Misa ya kumbariki Abate.
2° Aidha, kwa idhini ya Mkuu wa mahali anayehusika, ambaye tu anaweza kuamua kuhusu kufaa kwa konselebrasio, [basi idhini inatolewa kwa nafasi hizi]:
a) katika Misa “ya shirikani” (conventualem) na katika Misa kubwa makanisani, ikiwa manufaa ya waamini hayahitaji mapadre wote waliopo waadhimishe Misa kila mmoja peke yake;
b) katika Misa wakati wa mikutano mbalimbali ya Mapadre wa jimbo na pia wa mashirika.
§ 2. 1° Ni juu ya Askofu kupanga utaratibu wa konselebrasio katika jimbo.
2° Lakini kila padre anaweza kuadhimisha Misa bila mapadre wengine, ila si wakati uleule na mahali palepale [konselebrasio inapofanyika]; wala Alhamisi Kuu.
58. Ibada mpya ya konselebrasio itungwe na kuingizwa katika Pontifikale na katika Misale ya Kiroma.
Sura ya Tatu
SAKRAMENTI NYINGINE NA VISAKRAMENTI
Maana ya Sakramenti 59. Sakramenti zimewekwa ili kuwatakatifuza wanadamu, kuujenga Mwili wa Kristo, na mwishowe kumtolea Mungu ibada. Kwa kuwa ni ishara zinazowafundisha waamini, kwa upande moja zinadai imani, na kwa upande mwingine zinalisha imani yenyewe kwa maneno na matendo ya ibada; tena zinaimarisha na kuidhihirisha imani hiyo. Ndiyo sababu zinaitwa “Sakramenti za imani”. Ni kweli kwamba zinawapatia waamini neema, lakini pia maadhimisho yake yanawaandaa kikamilifu ili neema yenyewe wanayoipokea itoe matunda; pia yawawezeshe kumheshimu Mungu jinsi ipasavyo na kufanya matendo ya huruma.
Kwa sababu hiyo ni muhimu sana waamini wazielewe kwa urahisi ishara za Sakramenti, nao wazikaribie kwa makini sana Sakramenti zile zilizowekwa ili kuyalisha maisha ya kikristo. Visakramenti
60. Mama Kanisa takatifu aliweka pia visakramenti, ambavyo ni alama takatifu ambazo kwazo, kutokana na kufanana kwa namna fulani na Sakramenti, vinaashiria matunda, hasa ya kiroho, ambayo hupatikana kwa maombi ya Kanisa. Kwa njia ya visakramenti hivi watu hutayarishwa kupokea tunda la msingi la Sakramenti, na mazingira mbalimbali ya maisha hutakaswa.
61. Hivyo liturujia ya Sakramenti na Visakramenti inawawezesha waamini wenye moyo mnyofu kuyatakatifuza matukio karibu yote ya maisha kwa njia ya ile neema ya kimungu inayobubujika toka fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kutokana na fumbo hilo Sakramenti na Visakramenti hupata nguvu yao; na kwa msaada wa nguvu hiyo matumizi manyofu ya mambo ya kidunia yaweza kuelekezwa katika kumtakatifuza binadamu na kumsifu Mungu.
Umuhimu wa marekebisho ya adhimisho ya Sakramenti 62. Katika mwenendo wa nyakati katika ibada ya Sakramenti na Visakramenti yameingizwa mambo kadhaa yaletayo ugumu katika kuelewa maumbile na lengo la ibada hizo. Kwa hiyo marekebisho, ili kulinganisha ibada na matakwa ya siku hizi, ni ya lazima. Kwa kusudi hilo Mtaguso unaagiza yafuatayo.
Lugha katika ibada 63. Mara nyingi katika kutoa Sakramenti na Visakramenti, kwa manufaa ya waamini, lugha ya nchi husika inaweza kutumiwa katika nafasi kubwa zaidi kadiri ya mwongozo ufuatao:
a) Katika utoaji wa Sakramenti na Visakramenti inawezekana kutumia lugha ya nchi husika kufuatana na ibara 36.
b) Kufuatana na toleo jipya la Rituale ya Kiroma, Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2 ya hati hii, yatayarishe upesi iwezekanavyo Rituale faridi zinazolinganishwa na mahitaji ya kila nchi, pia kuhusu lugha; kisha Rituale hizo zitatumika katika nchi zinazohusika baada ya kuchunguzwa na Kiti cha Kitume. Katika kutunga Rituale hizo, au mikusanyo maalum mingine ya ibada, yasiachwe maelezo yaliyomo kabla ya kila madhehebu katika Rituale ya Kiroma, yale yenye tabia ya kichungaji au ya maelekezo (rubricis), na yale yenye umuhimu wa pekee wa kijamii pia.
Ukatekumeni
64. Uwekwe tena ukatekumeni kwa watu wazima, uliogawanywa katika hatua nyingi, wa kutekeleza kadiri ya mwongozo wa Mkuu wa mahali. Hivyo, muda wa ukatekumeni, uliowekwa kwa ajili ya mafundisho yafaayo, uweze kutakatifuzwa kwa njia ya ibada takatifu zitakazoadhimishwa kwa nyakati mbalimbali.
Marekebisho ya adhimisho la Ubatizo 65. Katika nchi za misioni iruhusiwe kuyapokea, sambamba na mambo yote ya mapokeo ya kikristo, pia yale ya unyago ulivyo katika mila za kila taifa kwa kiasi kiwezekanacho kufungamana na ibada ya kikristo, kadiri ya ibara 37-40 za hati hii.
66. Ibada zote mbili za Ubatizo wa wakubwa zitengenezwe, ile ya kawaida na ile ya Ubatizo wa sherehe zaidi, kwa kuzingatia kuwekwa tena kwa ukatekumeni. Katika Misale ya Kiroma Misa maalum “katika utoaji wa Ubatizo” iingizwe.
67. Ibada ya Ubatizo wa watoto itengenezwe upya, nayo izingatie hali halisi ya watoto. Katika ibada hiyo jukumu na wajibu wa wazazi na wasimamizi vitiliwe mkazo zaidi.
68. Katika ibada ya Ubatizo iwepo pia mibadala fulani ya utaratibu, ya kutumia wakati wanaobatizwa ni wengi, kadiri ya mwongozo wa Mkuu wa mahali. Itungwe pia ibada iliyo fupi zaidi ambayo wanaweza kutumia, hasa katika nchi za misioni, makatekista au pia, katika hatari ya kufa, waamini, ikiwa anakosekana Padre au Shemasi.
69. Badala ya “Ibada ya kukamilisha yaliyoachwa katika Ubatizo wa watoto”, itungwe ibada mpya ambayo nayo ionyeshe waziwazi zaidi kwamba mtoto, aliyekwisha kubatizwa kwa ibada fupi, ameshapokelewa katika Kanisa.
Itungwe pia ibada maalum kwa wale ambao wameshabatizwa kwa halali na baadaye wanaliongokea Kanisa Katoliki. Katika ibada hiyo kusisitizwe kupokelewa kwao katika ushirika wa Kanisa.
70. Nje ya kipindi cha Pasaka, maji ya Ubatizo yaweza kubarikiwa katika ibada yenyewe ya Ubatizo kwa formula fupi maalum iliyoidhinishwa.
Marekebisho ya adhimisho la Kipaimara
71. Ibada ya Kipaimara itengenezwe upya ili ionyeshe vizuri zaidi uhusiano wa ndani wa Sakramenti hii na zingine za kumwingiza mtu katika ukristo. Kwa hiyo, kurudia ahadi za Ubatizo kutangulie kupokea Sakramenti hii.
Ikiwa inafaa, Sakramenti ya Kipaimara inaweza kutolewa wakati wa Misa. Kama ibada itaadhimishwa nje ya Misa, itayarishwe formula ya kutumia kama utangulizi.
Marekebisho ya adhimisho la Kitubio 72. Ibada na formula za Kitubio zitengenezwe upya ili zionyeshe waziwazi zaidi maumbile na matokeo ya Sakramenti hii.
Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa 73. Sakramenti ya “Mpako wa Mwisho”, ambayo inaweza kuitwa vizuri zaidi “Mpako wa wagonjwa”, si Sakramenti kwa wale tu walio katika hali ya kuaga dunia. Kwa hiyo, wakati ufaao kwa kuipokea ni ule mwamini aanzapo kuwa katika hatari ya kufa kwa sababu ya ugonjwa na uzee.
74. Licha ya ibada mbili tofauti, yaani ya Mpako wa wagonjwa na ya Komunyopamba, itungwe pia utaratibu wenye mfululizo, ambamo Mpako utatolewa kwa mgonjwa baada ya Kitubio na kabla ya kuipokea Komunyopamba.
75. Idadi ya mipako irekebishwe, kadiri inavyoonekana inafaa; pia sala za ibada ya Mpako wa wagonjwa zirekebishwe ili zilingane na hali tofauti ya kila mgonjwa anayepewa Sakramenti.
Marekebisho ya adhimisho la Daraja 76. Ibada na matini yanayohusu Sakramenti ya Daraja yarekebishwe. Mawaidha (Allocutiones) ya Askofu mwanzoni mwa kila ibada ya Daraja yaweza kutolewa katika lugha ya nchi.
Katika ibada ya kumweka wakfu Askofu, Maaskofu wote waliopo waweza kumwekea mikono yao juu yake.
Marekebisho ya adhimisho la Ndoa 77. Ibada ya Sakramenti ya Ndoa, iliyomo katika Rituale ya Kiroma, irekebishwe na itajirishwe zaidi ili neema ya Sakramenti iashirishwe waziwazi zaidi, na pia majukumu ya wafunga ndoa yakazwe sana.
Katika adhimisho la Sakramenti ya Ndoa, “kama katika mila na desturi za taifa zipo mila na sherehe nyingine za kufaa, Mtaguso unatamani kabisa hizo zihifadhiwe”[41].
Aidha, Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali, kama ilivyoelezwa katika ibara 22 § 2 ya hati hii, yanaweza kutayarisha kwa mujibu wa ibara 63, ibada maalum, nayo ilingane na mila za taifa; lakini kwa sharti itunzwe sheria ya kwamba Padre anayesimamia Ndoa aombe na kupokea ukubaliano wa wafunga ndoa.
78. Kawaida Ndoa iadhimishwe wakati wa Misa, baada ya Injili na homilia, kabla ya “sala za waamini”. Sala ya kumwombea bibiarusi irekebishwe ili iwaeleze vizuri wanaarusi wote wawili wajibu wao wa kuwa waaminifu wao kwa wao; lugha ya nchi inaweza kutumika katika sala hii.
Lakini, ikiwa Sakramenti ya Ndoa inaadhimishwa bila Misa, mwanzoni mwa ibada usomwe waraka na Injili ya Misa ya Ndoa; vilevile kila mara baraka ya wanandoa itolewe.
Marekebisho ya Visakramenti 79. Visakramenti virekebishwe, kadiri ya kanuni ya msingi kwamba waamini wawezeshwe kushiriki kwa ufahamu, matendo, na kwa urahisi. Tena vilinganishwe na mahitaji ya siku hizi. Katika kurekebisha miongozo yao, kadiri ya ibara 63, kama ikifaa, yawezekana kuongeza pia Visakramenti vipya.
Baraka za pekee ziwe chache sana, na kwa ajili ya Maaskofu na Wakuu [wa mahali] tu.
Jitihada zifanyike ili Visakramenti vingine vitolewe na walei wenye uwezo na sifa zinazotakiwa, walau katika nafasi za pekee na kwa uamuzi wa Mkuu anayehusika.
Nadhiri za kitawa 80. Ibada ya kuweka wakfu mabikira iliyomo katika Pontifikale ya Kiroma irekebishwe.
Itungwe pia ibada ya kuweka nadhiri, au uprofesi (professionis religiosae), na ya kurejea nadhiri (renovationis votorum), yenye kuonyesha kwa wazi zaidi umoja, usahili na heshima. Nayo itumiwe na wale wanaoweka nadhiri za maisha au za muda wakati wa Misa, isipokuwa kwa nafasi ya pekee.
Ni vema nadhiri ziwekwe wakati wa Misa.
Marekebisho ya ibada ya Mazishi 81. Ibada ya Mazishi ionyeshe kinaganaga zaidi tabia ya kipasaka ya kifo cha kikristo. Pia mintarafu rangi ya kiliturujia hiyo, na ilingane zaidi na mazingira na mapokeo ya kila kanda.
82. Irekebishwe pia ibada ya Mazishi ya watoto na itungwe Misa maalum kwa ajili ya hiyo.
Sura ya Nne
LITURUJIA YA VIPINDI
Liturujia ya Vipindi ni tendo la Kristo na la Kanisa 83. Kuhani Mkuu wa Agano Jipya na la milele, Yesu Kristo, kwa kutwaa maumbile ya kibinadamu, ameingiza katika ugeni huu wa hapa duniani wimbo ule unaoimbwa daima katika makao ya mbinguni. Yeye anaunganisha naye jumuiya ya wanadamu wote mpaka washiriki naye katika kuuinua wimbo huo wa kimungu na wa sifa.
Kwa kweli, Yesu huendeleza tendo hili la kikuhani kwa njia ya Kanisa lake, ambalo humsifu Bwana Mungu bila kukoma na kumwomba kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu mzima, si kwa njia ya kuadhimisha Ekaristi tu, bali pia kwa namna nyingine, na hasa kwa kusali “Kazi ya Mungu” (Officio divino), yaani Liturujia ya Vipindi.
84. Liturujia ya Vipindi, kadiri ya mapokeo ya zamani ya kikristo, imewekwa ili mfululizo wa mchana na usiku utakatifuzwe kwa njia ya sifa ya Mungu. Wakati wenye kuadhimisha wimbo ule wa sifa na wa ajabu ni mapadre, au wengine waliowekwa kwa ajili hiyo na sheria ya Kanisa, au pia waamini wanaosali pamoja na Padre kwa jinsi inavyokubalika, hapo kweli ni sauti ya Bibiarusi mwenyewe anayeongea na Bwanaarusi. Kwa kweli ni sala ya Kristo ambaye, pamoja na Mwili wake, humwomba Baba.
85. Wote wanaotimiza tendo hilo wanatekeleza wajibu wa Kanisa, na pia wanashiriki heshima kubwa sana ya Bibiarusi wa Kristo kwa sababu, wanapomsifu Mungu, hukaa mbele ya kiti cha enzi cha Mungu kwa niaba ya Mama Kanisa.
Umuhimu wa Liturujia ya Vipindi katika uchungaji 86. Mapadre wanaotekeleza huduma takatifu ya kichungaji watasali masifu ya Vipindi kwa juhudi kubwa zaidi kiasi ambacho kitawasukuma kushika onyo la Mtume Paulo: “Ombeni bila kukoma” (1The 5:17). Kwa maana Bwana peke yake tu anaweza kuleta na kukuza matunda ya kazi wanayofanya, yeye aliyesema: “Bila mimi hamwezi kufanya lolote” (Yn 15:5). Kwa sababu hiyo Mitume, walipowawekea mikono mashemasi, walisema: “Na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno” (Mdo 6:4).
87. Ili mapadre na waamini wengine waweze kusali vizuri na kikamilifu zaidi Liturujia ya Vipindi katika nafasi mbalimbali, Mtaguso Mkuu, ukiendeleza marekebisho yaliyoanzishwa na Kiti cha Kitume, unapenda kuagiza yafuatayo kuhusu Liturujia ya Vipindi, kufuatana na Riti ya Kiroma.
Marekebisho ya utaratibu wa Liturujia ya Vipindi 88. Kwa vile lengo la Liturujia ya Vipindi ni kutakatifuza siku nzima, utaratibu wa kimapokeo wa vipindi urekebishwe ili Sala za Vipindi zifanywe kwa wakati wake, kadiri inavyowezekana. Vilevile hali ya maisha ya siku hizi, na hasa ya wale wanaojibidisha katika matendo ya kitume, iangaliwe.
Mwongozo kwa marekebisho ya Liturujia ya Vipindi 89. Kwa hiyo, katika kurekebisha Liturujia ya Vipindi, ufuatwe mwongozo huu:
a) Masifu ya Asubuhi (Laudes), kama sala ya asubuhi, na Masifu ya Jioni (Vesperae), kama sala ya jioni, kadiri ya mapokeo yenye heshima ya Kanisa lote ni bawaba maradufu ya Liturujia ya Vipindi ya kila siku. Hivyo yatazamwe kama Vipindi muhimu zaidi na yaadhimishwe kufuatana na umuhimu wake;
b) Utaratibu wa Sala ya Usiku, au Kompleto (Completorium), urekebishwe ili ulingane inavyofaa na mwisho wa siku;
c) Sala ya Kipindi kiitwacho Mikesha (Matutinum), ingawa kinaendelea kuwa kipindi cha sala kwa ajili ya usiku kisaliwapo pamoja katika kwaya (in choro), irekebishwe ili iweze kutumika wakati wowote wa siku, tena iwe na zaburi chache na masomo marefu zaidi;
d) Kipindi cha Kwanza (Prima) kifutwe;
e) Katika kwaya Vipindi vidogo vya Kabla ya Adhuhuri au Tersia (Tertia), Adhuhuri au Sesta (Sexta) na Baada ya Adhuhuri au Nona (Nona) vihifadhiwe. Nje ya kwaya inaruhusiwa kuchagua kimoja kati ya hivyo vitatu, kadiri ya majira ya siku.
Liturujia ya Vipindi ni chemchemi ya uchaji 90. Licha ya hayo, Liturujia ya Vipindi ni sala ya hadhara ya Kanisa na chemchemi ya uchaji na chakula cha sala ya binafsi. Kwa hiyo, mapadre na waamini wengine wote wanaoshiriki Liturujia ya Vipindi tunawasihi ili, katika kusali, akili na sauti zao viungane; kwa kufikia lengo hilo wahusika wajipatie ufahamu wa kina zaidi wa Liturujia na wa Biblia hasa kuhusu zaburi.
Katika kufanya marekebisho hayo, hazina yenye heshima na ya zamani iliyomo katika Breviari ya Kiroma irekebishwe ili waliokabidhiwa waweze kuitumia zaidi na kwa urahisi.
Mgawanyo wa Zaburi 91. Ili utaratibu wa Vipindi uliopendekezwa katika ibara 89 uweze kutekelezwa kweli, zaburi zigawanywe sio tena katika juma moja, bali katika muda mrefu zaidi.
Kazi hii ya kurekebisha mgawanyo wa zaburi, iliyoanzishwa vizuri, imalizwe kwa haraka, bila kusahau Kilatini kinachotumiwa na wakristo, na matumizi yake ya kiliturujia katika nyimbo. Vivyo hivyo mapokeo yote ya Kanisa la Kiroma yasisahauliwe.
Utaratibu wa masomo 92. Kuhusu masomo, mwongozo ufuatao uzingatiwe:
a) Usomaji wa Maandiko Matakatifu upangwe ili hazina za Neno la Mungu zipatikane katika wingi wake kwa urahisi zaidi;
b) Masomo yachukuliwayo kutoka maandiko ya Mababa, Waalimu na Waandishi wa Kanisa, yachaguliwe vizuri zaidi;
c) Masimulizi ya mateso ya watakatifu, yaani maisha yao, yarudishwe katika ukweli wa kihistoria.
Marekebisho ya tenzi 93. Pia tenzi zirudishwe katika mtindo wao wa asili, kwa kiasi kifaacho; na yale yaliyo katika hali ya visasili (mythologiam) au yasiyofaa kwa uchaji wa Mungu yaondolewe au yabadilishwe. Aidha, zichukuliwe tena tenzi nyingine, kadiri ifaavyo, zilizomo katika mikusanyo mbalimbali.
Wakati wa kusali kila Kipindi 94. Ili kutakatifuza kweli siku na kusali Vipindi vyenyewe kwa matunda ya kiroho, Sala za Vipindi zifanywe kulingana na majira yake, yaani sambamba na wakati halisi wa kila Kipindi.
Ulazima wa Liturujia ya Vipindi 95. Jumuiya zenye sharti la kusali pamoja zinatakiwa kusali katika kwaya Liturujia ya Vipindi kila siku, zaidi ya Misa ya shirikani; na hasa:
a) Jumuiya za Wakanoniki, Mashirika ya Wamonaki wa kike na wa kiume na wale watawa wote (Regularium) wanaotakiwa kusali pamoja katika kwaya, kadiri ya sheria na katiba zao, wanapaswa kusali Vipindi vyote.
b) Kapitulo za Makanisa Makuu na za Kolejata zinapaswa kusali sehemu zile za Ofisyo zinazoamriwa katika sheria za kawaida au za pekee.
c) Wanashirika wote waliotajwa juu, ambao wamepewa Daraja kuu (Ordinibus maioribus) au wameweka nadhiri za maisha, isipokuwa ndugu watawa walei (conversis), wanapaswa kusali peke yao Vipindi vile wasivyosali katika kwaya.
96. Makleri wasiopasika kusali katika kwaya, kama wamepewa Daraja kuu, wanapaswa kusali sala zote za Vipindi kila siku peke yao au kwa pamoja, kadiri ya ibara 89.
97. Mwongozo wa kushiriki ibada nyingine kama mibadala ya kufaa ya Liturujia ya Vipindi uratibiwe.
Katika nafasi za pekee na kwa sababu halali, Wakuu wa mahali wanaweza kuwaruhusu wale walio chini yao kutofungwa na ulazima wa kusali Liturujia ya Vipindi, ama kufanya ibada nyingine badala yake.
98. Wanashirika wa taasisi yoyote ya kitawa ambao kwa mujibu wa Katiba husali sehemu kadhaa za Liturujia ya Vipindi, huonyesha sala ya hadhara ya Kanisa.
Vilevile wanaonyesha sala ya hadhara ya Kanisa kama, kwa mujibu wa Katiba, wakisali “Ofisyo fupi”, mradi zimetungwa kulingana na mpango wa Liturujia ya Vipindi ya kawaida na kuidhinishwa inavyotakiwa.
Kusali pamoja Liturujia ya Vipindi99. Liturujia ya Vipindi ni sauti ya Kanisa, yaani ya Mwili wote wa fumbo unaomsifu Mungu hadharani. Kwa hiyo, Mtaguso unawasihi makleri wasiopasika kusali katika kwaya na hasa mapadre wanaoishi au kukutana pamoja, wasali pamoja walau sehemu kadhaa za Liturujia ya Vipindi.
Aidha, wale wote wanaosali Liturujia ya Vipindi kwa pamoja au katika kwaya, watimize, kikamilifu iwezekanavyo, wajibu waliokabidhiwa kwa uchaji wa rohoni na pia kwa vitendo vya nje.
Pia ni vema, kama inawezekana, Liturujia ya Vipindi katika kwaya au kwa pamoja iimbwe.
Kushiriki kwa waamini katika Liturujia ya Vipindi 100. Wachungaji wa roho wajitahidi kwamba Vipindi vikuu vya sala, hasa Masifu ya Jioni (Vesperae), viadhimishwe kanisani pamoja na waamini siku ya Dominika na Sikukuu kubwa zaidi. Walei pia wanahimizwa wasali Liturujia ya Vipindi au pamoja na mapadre, au wakiungana kati yao, au kila mmoja peke yake.
Lugha katika Liturujia ya Vipindi 101. § 1. Kadiri ya mapokeo ya zamani ya riti ya kilatini, wakleri wanapaswa kuhifadhi lugha ya kilatini katika Liturujia ya Vipindi. Lakini Mkuu wao ana uwezo wa kuruhusu matumizi ya tafsiri katika lugha ya nchi, iliyoandaliwa kadiri ya ibara 36, kwa wale wakleri mmoja mmoja (singulis pro casibus) ambao kwao matumizi ya lugha ya kilatini ni kizuio kikubwa kwa kusali Liturujia ya Vipindi ipasavyo.
§ 2. Kwa wamonaki wa kike (monialibus) na wanajumuiya wa mashirika ya kitawa, au wasio wakleri, au wa kike, Mkuu wao anayehusika anaweza kuruhusu matumizi ya lugha ya nchi katika Liturujia ya Vipindi, hata ikiadhimishwa katika kwaya, lakini tafsiri iidhinishwe.
§ 3. Kila mkleri anayepaswa kusali Liturujia ya Vipindi, akisali katika lugha ya nchi pamoja na waamini, au pamoja na wale waliotajwa katika § 2, anatimiza wajibu wake. Hata hivyo, tafsiri inayotumika iwe imeidhinishwa.
Sura ya Tano
MWAKA WA LITURUJIA
Maana ya Mwaka wa Liturujia102. Mama Kanisa takatifu huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanaarusi wake aliye Mungu, katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kila juma Kanisa, katika siku aliyoiita “Dominika”, yaani “Siku ya Bwana”, anaadhimisha kumbukumbu ya ufufuko wa Bwana. Kwa namna ya pekee anauadhimisha ufufuko huo pamoja na mateso yake yenye heri mara moja kwa mwaka katika Sikukuu ya Pasaka, iliyo kubwa kuliko Sherehe zote.
Katika mzunguko wa mwaka mzima, [Mama Kanisa] analikunjua fumbo la Kristo, tangu umwilisho na kuzaliwa, hadi kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana.
Anapokumbuka namna hii mafumbo ya ukombozi, Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii, uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu.
103. Kwa kuadhimisha katika mzunguko huo wa [kila] mwaka mafumbo ya Kristo, Kanisa humheshimu kwa upendo wa pekee Maria mwenye heri, Mama wa Mungu, ambaye ameunganika na Mwana wake kwa namna isiyoweza kutengwa, katika kazi ya wokovu. Tena, ndani ya Maria, Kanisa hustahi na kutukuza tunda bora kuliko yote la ukombozi, na pia hutazama kwa furaha, kama katika mfano usio na doa, yale anayoyatamani na kuyatumaini kwa ajili yake lote.
Kumbukumbu za Mashahidi na za Watakatifu 104. Kanisa limeingiza pia katika mwaka wa Liturujia kumbukumbu za Mashahidi na za Watakatifu wengine ambao, baada ya kufikia ukamilifu kutokana na neema ya Mungu iliyo ya namna nyingi, na wakishapata ukombozi wa milete, wanaimba sifa kamili ya Mungu kule mbinguni na kutuombea.
Kwa kuadhimisha siku za kuzaliwa [mbinguni] kwa Watakatifu Kanisa latangaza fumbo la Pasaka lionekanalo katika Watakatifu walioteswa pamoja na Kristo na kutukuzwa pamoja naye, na lawaonyesha waamini mifano yao inayowavutia wote kwa Baba kwa njia ya Kristo. Pia linawaombea fadhili za Mungu kwa njia ya mastahili yao.
105. Kanisa, katika vipindi mbalimbali vya mwaka na kadiri ya utaratibu wa kimapokeo, linatimiza wajibu wake wa kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya kiroho na kimwili, mafundisho, sala pamoja na matendo ya toba na ya huruma.
Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu kwa dhati unaamua yafuatayo.
Umuhimu wa Dominika 106. Kadiri ya mapokeo ya Mitume, yanayopata asili yake katika siku ya ufufuko wa Kristo, Kanisa huadhimisha fumbo la Pasaka kila siku ya nane, katika siku ile iitwayo kwa haki kabisa Siku ya Bwana au Dominika. Katika siku hii waamini wanapaswa kujumuika pamoja ili, wanaposikiliza Neno la Mungu na kushiriki Ekaristi, wafanye ukumbusho wa mateso, ufufuko na utukufu wa Bwana Yesu. Na pia watoe shukrani kwa Mungu “aliyewazaa upya katika tumaini lenye uhai kwa njia ya ufufuko wa Yesu Kristo katika wafu” (1Pet 1:3). Kwa hiyo, siku ya Dominika ni Sikukuu ya kwanza ambayo ni lazima ielezwe vizuri na kuingizwa, kwa kadiri inavyowezekana, katika maisha ya kidini ya wakristo, ili iweze kuwa pia siku ya furaha na ya kuacha kazi. Sherehe nyingine zisitiliwe mkazo sana, isipokuwa zile zenye umuhimu zaidi, kwa sababu siku ya Dominika ni msingi na kiini cha mwaka mzima wa Liturujia.
Marekebisho ya Mwaka wa Liturujia 107. Mwaka wa Liturujia urekebishwe ili zihifadhiwe au ziingizwe tena desturi na taratibu za vipindi vitakatifu kadiri ya hali ya nyakati zetu. Pia maana yao ya asili ihifadhiwe ili kulisha ipasavyo uchaji wa waamini katika kuadhimisha mafumbo ya ukombozi wa Kristo, na hasa fumbo la Pasaka. Aidha, ikiwa ni lazima, marekebisho yafanywe kulingana na hali ya kila mahali kadiri ya ibara 39 na 40.
108. Roho za waamini zielekezwe kwanza kabisa kwenye sikukuu za Bwana, ambamo, katika mwaka, yanaadhimishwa mafumbo ya wokovu. Kwa hiyo Vipindi vya Mwaka (Proprium de Tempore) vipewe umuhimu wake kuliko sikukuu za Watakatifu, ili mfululizo mzima wa mafumbo ya wokovu uadhimishwe ipasavyo.
Kwaresima 109. Maana mbili zinazofanya kipekee Kipindi cha Kwaresima, ukumbusho wa Ubatizo au matayarisho yake, na toba, zitiliwe mkazo wa pekee katika Liturujia na katekesi ya Liturujia. Nazo zinasaidia kuwaandaa waamini kuadhimisha fumbo la Pasaka, wakisikiliza mara nyingi zaidi Neno la Mungu na kujibidisha katika kusali. Kwa hiyo:
a) Mambo yote yadokezayo Ubatizo yaliyomo katika Liturujia ya Kwaresima yapewe nafasi kubwa zaidi, na pia, kama inafaa, yaingizwe tena mengine yatokanayo na mapokeo ya zamani;
b) Vivyo hivyo ifanywe kuhusu mambo ya toba. Mintarafu katekesi, juhudi ifanywe ili iweze kuingizwa rohoni mwa waamini, pamoja na matokeo ya kijamii ya dhambi, maumbile halisi ya toba yenye kuchukia dhambi kwa sababu ni kumtukana Mungu; nafasi ya Kanisa katika tendo la toba isisahauliwe kamwe, na pia sala kwa ajili ya wakosefu ihimizwe.
110. Toba ya wakati wa Kwaresima isiwe ni tendo la ndani na la binafsi tu, bali pia lionekanalo kwa nje na katika maisha ya jamii. Matendo ya toba na kujinyima, kadiri ya uwezekano wa nyakati zetu na mahali mbalimbali, na pia kadiri ya hali ya waamini, yasisitizwe na kuhimizwa na wale wenye mamlaka, kama ilivyoelezwa katika ibara 22.
Lakini tendo la kufunga chakula wakati wa Pasaka litakuwa takatifu, nalo liadhimishwe popote siku ya Ijumaa ya Mateso na Kifo cha Bwana na kuendelea, kama inawezekana, siku nzima ya Jumamosi Kuu, ili kufikia furaha na shangwe ya Dominika ya Ufufuko kwa moyo wazi na ulioinuliwa.
Sherehe za Watakatifu 111. Katika Kanisa, kadiri ya mapokeo, Watakatifu huheshimiwa; vivyo hivyo masalia yao halisi na picha zao huhifadhiwa kwa heshima. Maana sherehe za Watakatifu zinatangaza matendo ya ajabu ya Kristo ndani ya watumishi wake, na pia zinawaonyesha waamini mifano bora ya kuiga.
Ili sikukuu za Watakatifu zisipewe umuhimu zaidi kuliko zile zinazokumbusha mafumbo ya wokovu, nyingi kati ya sikukuu hizo [za Watakatifu] ziadhimishwe tu katika Kanisa faridi, au Taifa au Shirika. Sikukuu zile tu zinazowakumbuka Watakatifu wenye umuhimu kwa wote ziadhimishwe katika Kanisa zima.
Sura ya Sita
MUZIKI MTAKATIFU
Umuhimu wa muziki wa kiliturujia 112. Mapokeo ya kimuziki ya Kanisa lote ni hazina yenye thamani isiyopimika, inayozidi aina nyingine ya sanaa, hasa kwa sababu kuimba kutakatifu, kukiunganika na maneno, ni sehemu ya lazima na ya ndani ya Liturujia ya sherehe.
Hakika kuimba kutakatifu kumesifiwa katika Maandiko Matakatifu[42]na pia na Mababa wa Kanisa na Mapapa wa Kanisa la Kiroma, ambao nyakati hizi kwanzia na Mt. Pius X, wamesisitiza kwa dhati karama na huduma ya kuimba kutakatifu katika ibada ya Liturujia.
Kwa hiyo, muziki mtakatifu utazidi kuwa mtakatifu pale uunganikapo na tendo la Liturujia; maana utafanya sala kuwa tamu zaidi na kuonyesha umoja wa mioyo, pia utaleta heshima zaidi katika maadhimisho matakatifu. Tena Kanisa linakubali na kuingiza katika ibada kwa Mungu mitindo yote ya sanaa ya kweli, lakini yenye sifa zinazotakiwa.
Kwa hiyo, Mtaguso Mkuu unahifadhi kanuni na sheria zilizokubalika na za mapokeo ya Kanisa, na pia unalenga shabaha ya muziki mtakatifu, ambayo ni utukufu wa Mungu na kutakatifuzwa kwa waamini. Ili kutekeleza kusudi hilo, Mtaguso Mkuu unaamua yafuatayo.
Liturujia ya Sikukuu 113. Tendo la Liturujia hupata kuwa na heshima zaidi wakati linapoadhimishwa katika sherehe kwa kuimba, wakiwepo makasisi na kwa ushirikiano hai wa waamini.
Kuhusu matumizi ya lugha, ibara 36 izingatiwe; juu ya Misa, kama ilivyoelezwa katika ibara 54; kwa Sakramenti, ifuatwe ibara 63, na mintarafu Liturujia ya Vipindi, ifanywe kama isemavyo ibara 101.
114. Hazina ya mapokeo ya muziki mtakatifu ihifadhiwe na kukuzwa kwa uangalifu sana. Shule za Kwaya (Scholae cantorum) zihimizwe, hasa katika Makanisa Makuu. Aidha, Maaskofu na wachungaji wengine wa roho wafanye jitihada ili katika kila ibada iadhimishwayo kwa kuimba, waamini wote waweze kushiriki kikamilifu, kadiri ya ibara 28 na 30.
Uandaaji wa wanamuziki 115. Jitihada kubwa ifanyike ili kuhamasisha elimu na mazoezi ya muziki katika seminari, katika nyumba za unovisi za mashirika ya kiume na ya kike, katika nyumba za wanafunzi, kama vile vyuo na shule za kikatoliki; ili kupata elimu hii, walimu waandaliwe kwa bidii kubwa, kisha watumwe kufundisha muziki mtakatifu.
Ikiwa inafaa, uundaji wa Taasisi za Juu za muziki mtakatifu uhimizwe.
Wanamuziki, wanakwaya, na juu ya wote watoto, wapewe elimu halisi ya kiliturujia.
Nyimbo za kigregoriani na nyinginezo 116. Kanisa anautambua uimbaji wa mtindo wa kigregoriani kuwa ndio ulio rasmi wa Liturujia ya Kiroma: kwa hiyo, katika matendo ya Liturujia ushike nafasi ya kwanza, isipokuwa kwa sababu maalum.
Mitindo mingine ya muziki mtakatifu, hasa ile itumiayo sauti nyingi (polyphonia), isiondolewe katika maadhimisho ya ibada kwa Mungu, lakini ilingane na roho ya tendo la Liturujia, kadiri ya ibara 30.
117. Toleo halisi (Editio typica) la vitabu vya nyimbo za kigregoriani lichapwe; tena ni afadhali litayarishwe toleo halisi zaidi kuliko vitabu vilivyochapwa baada ya matengenezo ya Mt. Pius X.
Licha ya toleo hilo, bora litayarishwe toleo jingine lenye tuni zilizo rahisi zaidi, la kutumia katika makanisa madogo.
Nyimbo za kidini za mahali 118. Nyimbo za kidini za [wakristo] wenyeji zihimizwe kwa bidii, ili katika ibada mbalimbali za watu na pia katika matendo ya Liturujia sauti za waamini ziweze kusikika vizuri, kadiri ya utaratibu na madai ya miongozo.
Muziki ya kiliturujia katika misioni 119. Katika nchi kadha wa kadha, hasa zile za Misioni, yapo mataifa yenye mapokeo yao ya muziki ambayo yana maana kubwa katika maisha yao ya kidini na ya kijamii. Muziki huu upewe heshima na nafasi inayofaa katika kuyaelimisha mataifa hayo kidini, na pia katika kutengeneza ibada kwa kulingana na tabia yao, kadiri ya ibara 39 na 40.
Kwa hiyo, katika kuwaelimisha wamisionari juu ya muziki, jitihada ifanyike ili, kadiri inavyowezekana, waweze kuendeleza muziki wa kimapokeo wa mataifa yanayohusika, katika mashule na katika ibada takatifu.
Organi na ala nyingine za muziki 120. Katika Kanisa la Kiroma, organi ya mianzi ipewe nafasi ya heshima, kama ala ya kimapokeo ya muziki ambayo kwayo muziki huongeza fahari ya ajabu kwa ibada za Kanisa, na pia huinua roho za waamini kwa Mungu na kwa mambo ya mbinguni.
Ala nyingine za muziki pia zinaweza kutumika katika ibada kwa Mungu, kwa uamuzi na kibali cha Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali, kadiri ya ibara 22 § 2, 37 na 40. Lakini sharti ziwe za kufaa kwa matumizi matakatifu au zigeuzwe ili zifae kwa lengo hili. Tena, zilingane na heshima ya hekalu na zisaidie kujenga [uchaji wa] waamini.
Wajibu wa watunga muziki 121. Watunga muziki, wakisukumwa na roho ya kikristo, wajione kuwa wameitwa kuustawisha muziki mtakatifu na kukuza hazina yake.
Pia watunge melodia zinazolingana na sifa za muziki mtakatifu na ambao unaweza kuimbwa si tu na kwaya kubwa, bali pia na kwaya ndogo. Tena ziwasaidie waamini wote kushiriki kikamilifu.
Maneno yaliyomo katika nyimbo yalingane na mafundisho ya Kanisa katoliki, zaidi yachukuliwe hasa katika Maandiko Matakatifu na vitabu vya liturujia.
Sura ya Saba
SANAA TAKATIFU NA VIFAA VITAKATIFU
Hadhi ya sanaa takatifu 122. Mambo ya sanaa (artes ingenuae) yanahesabika kwa haki kati ya kazi za maarifa ya kibinadamu zenye heshima zaidi. Kati ya hizo, sanaa ya kidini na kilele chake ambacho ni sanaa takatifu zinaheshimiwa kwa namna ya pekee. Hizo, kwa maumbile yao, huhusiana na uzuri usiopimika wa Mungu, ambao lazima udhihirishwe kwa namna fulani katika kazi za mwanadamu. Tena, huelekea kwa Mungu na kwa kukuza sifa na utukufu wake, kwa sababu hazina lengo jingine isipokuwa kuzielekeza kwa nguvu na kikamilifu, kwa njia ya matunda yao, akili za wanadamu kwa Mungu.
Kwa sababu hizo, Mama Kanisa takatifu daima amependelea sanaa na kutafuta huduma yao yenye heshima, ili mambo yahusuyo ibada takatifu yapewe kweli heshima na uzuri, kwani hayo ni alama na ishara za yale ya mbinguni. Kwa hiyo, Kanisa pia amejitahidi kuwalea wanasanaa. Tena Kanisa, tangu awali na kwa haki, amejiona kuwa mwamuzi juu ya mambo ya sanaa, akichagua kati ya kazi za wanasanaa zile zilinganazo na imani, uchaji na kanuni za mapokeo, ili zifae kwa matumizi ya kidini.
Kwa bidii ya pekee Kanisa amejitahidi ili vifaa vitakatifu vitumike kadiri ya heshima na uzuri wa ibada; na pia amekubali mabadiliko yale ya malighafi, ya maumbo na ya madoido yaliyoingizwa na maendeleo ya mbinu za sanaa katika mwenendo wa karne.
Kwa hiyo, Mababa wamependa kuamua yafuatayo.
Matumizi ya mitindo mbalimbali ya sanaa 123. Kanisa hana mtindo wake maalum wa sanaa, lakini amekubali mitindo ya sanaa ya kila karne, kadiri ya tabia na mila za mataifa, na pia kufuatana na matakwa ya kila ibada. Hivyo, katika mwenendo wa karne, Kanisa ameandaa hazina ya sanaa ambayo lazima kuhifadhi kwa uangalifu mkubwa. Sanaa ya siku hizi na ya mataifa yote na ya nchi zote ipate uhuru wa kujionyesha katika Kanisa, mradi tu iwe kwa ajili ya heshima na matakwa ya majengo matakatifu na maadhimisho ya kiliturujia. Kwa njia hii, [sanaa takatifu ya siku hizi] iwezeshwe kuunganisha sauti yake na kwaya ile ya ajabu [ya masifu kwa ajili] ya utukufu ambayo wanasanaa maarufu katika karne zilizopita waliimba kwa imani katoliki.
124. Katika kuhimiza na kuhamasisha sanaa takatifu halisi, wenye mamlaka katika Kanisa watafute uzuri wenye heshima kuliko fahari tupu. Vivyo hivyo ifanywe mintarafu mavazi na vifaa vitakatifu.
Maaskofu wasikubali kamwe matendo ya sanaa yapinganayo na imani na maadili na uchaji wa kikristo katika nyumba ya Mungu na mahali pengine patakatifu. Pia wakatae yale yanayovunja heshima halisi ya kidini kwa sababu ni mapotovu kwa upande wa maumbo au kwa sababu ya utovu wa uzuri wa kisanaa, au ya uhafifu wake au hila.
Katika kujenga majengo matakatifu jitihada ifanyike ili yafae kwa ajili ya kuadhimisha Liturujia na kwa kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu.
125. Desturi ya kuonyesha picha na sanaa takatifu katika makanisa, kusudi waamini waweze kuziheshimu, iimarishwe. Hata hivyo, idadi yake iwe ya kiasi kifaacho, na mahali zinapowekwa pafuate utaratibu unaotakiwa, ili kutowakwaza baadhi ya waamini na kutohimiza uchaji usio halali.
Sanamu takatifu 126. Katika kuhakiki kazi za sanaa, Wakuu wa mahali wasikilize mapendekezo ya Kamati ya Sanaa takatifu ya Jimbo; na pia, kama inatakiwa, wapokee mapendekezo kutoka kwa wale wenye ujuzi maalum, na kwa zile kamati zilizotajwa katika ibara 44, 45 na 46.
Wenye mamlaka wakae macho ili vifaa vitakatifu au vitu vya thamani, kwa vile ni urembo wa nyumba ya Mungu, visichukuliwe au kuharibiwa.
Malezi ya wanasanaa 127. Maaskofu, wenyewe au kwa njia ya mapadre wanaofaa ambao wanajua na kupenda sanaa, wawaangalie wanasanaa kwa namna ya pekee, ili kuwaelimisha juu ya roho ya sanaa takatifu na ya Liturujia takatifu.
Pia inatamaniwa kuanzisha shule au idara za sanaa takatifu katika nchi zile ambazo inaonekana inafaa, ili kuwalea wanasanaa.
Wanasanaa wote ambao, wakiongozwa na maarifa yao, wanataka kutumikia utukufu wa Mungu katika Kanisa takatifu, daima wakumbuke kwamba wanafanya kazi ambayo ni mtindo wa igizo takatifu la Mungu Mwumbaji. Na pia matunda ya kazi yao yatakuwa kwa ajili ya ibada katoliki, kukuza imani na uchaji na malezi ya kidini ya waamini. Marekebisho ya sheria za sanaa takatifu
128. Sheria za Kanisa na miongozo ya Kanisa inayohusu mambo ya nje yahusuyo ibada takatifu, pamoja na vitabu vya Liturujia, vitengenezwe upya upesi iwezekanavyo, kadiri ya ibara 25. Hasa yatazamwe tena mambo yafuatayo: ujenzi unaostahili na wa kufaa wa majengo matakatifu; umbo na utengenezaji wa altare; heshima, mahali na usalama wa tabernakulo ya Ekaristi; kufaa kwa mahali pa kubatizia na heshima yake; sehemu ifaayo kwa kuweka sanamu, picha takatifu na mapambo yote. Kutokana na msingi huo, sheria zile zisizolingana na marekebisho ya Liturujia zisahihishwe au kufutwa; lakini zile zinazoinufaisha zitunzwe au kuingizwa tena vipya.
Kwa jambo hilo, na hasa kuhusu malighafi na mitindo ya vifaa vitakatifu na mavazi, Mabaraza ya Maaskofu ya kila mahali yanaruhusiwa kufanya marekebisho yanayotakiwa kadiri ya mahitaji na mila za mahali panapohusika na kufuatana na ibara 22 ya hati hii.
Uandaaji wa makleri mintarafu sanaa 129. Makleri, wakati wa masomo ya falsafa na teolojia, waelimishwe pia kuhusu historia na maendeleo ya sanaa takatifu, kama vile kanuni halisi zinazoongoza utengenezaji wa vitu vya sanaa na hivyo waweze kuheshimu na kulinda majengo na matendo matakatifu (venerabilia monumenta) na pia kutoa ushauri kwa wanasanaa, ili watimize vema kazi yao.
Zana za kiaskofu 130. Inafaa ishara za kiaskofu zitumiwe na watu wa Kanisa tu wenye Daraja ya kiaskofu au mamlaka ya pekee.
Nyongeza
TANGAZO LA MTAGUSO MKUU VATIKANO II KUHUSU
MATENGENEZO YA KALENDA
Mtaguso Mkuu Vatikano II hutilia maanani sana matakwa ya wengi, yaani ya kutaka Sikukuu ya Pasaka iangukie daima Dominika fulani na hivyo kudai matumizi ya kalenda isiyobadilika. Kwa sababu hiyo, baada ya kuchunguza kwa makini yale yanayoweza kutokana na matumizi ya kalenda mpya ya namna hii, Mtaguso Mkuu unatangaza yafuatayo:
1. Mtaguso Mkuu hauna kizuizi chochote kwa kuichagua Dominika fulani ya Kalenda ya Kigregoriani kuwa Sikukuu ya Pasaka. Ila kiwepo kibali cha wale wanaohusika, hasa ndugu zetu waliojitenga na Kiti cha Kitume.
2. Vilevile Mtaguso Mkuu hauwapingi wale ambao wangependa kuingiza aina tofauti ya kalenda ya kudumu katika maisha ya kijamii.
Lakini, kati ya aina hizo mbalimbali za kalenda za kudumu zinazopendekezwa ili ziingizwe katika maisha ya kijamii, Kanisa linadai juma moja liendelee kuwa na jumla ya siku saba pamoja na Dominika. Kwa hiyo, zisiongezwe siku nyingine zaidi ya zile saba za juma, ili mfululizo wa majuma usibadilike; isipokuwa kama zipo sababu nzito mno. Nazo hazina budi kukubaliwa na Kiti cha Kitume.
Mambo yote yaliyoamuliwa katika konstitusio hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuliwa kwa pamoja katika Sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa utukufu wa Mungu.
Roma, katika Kanisa la Mtakatifu Petro, 4 Desemba 1963
Mimi mwenyewe Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki
(zinafuata sahihi za Mababa)