SINODI YA MAASKOFU
________________________________________________________
MKUTANO WA JUMLA WA KAWAIDA WA 14
Wito na utume wa familia
katika Kanisa na ulimwengu mamboleo
LINEAMENTA
Mji wa Vatikano
2014
YALIYOMO
DIBAJI
RELATIO SYNODI ya Mkutano wa Tatu wa Jumla usio wa Kawaida
Utangulizi
SEHEMU YA KWANZA.
Usikivu: Mazingira na changamoto juu ya familia.
Mazingira ya kijamii na kitamaduni.
Umuhimu wa maisha ya upendo.
Changamoto kwa uchungaji.
SEHEMU YA PILI.
Kumtazama Kristo: Injili ya familia.
Mtazamo juu ya Yesu na malezi ya Mungu katika historia ya wokovu.
Familia katika mpango wa Mungu wa wokovu.
Familia katika hati za Kanisa.
Tabia ya kutokuvunjika ya ndoa na furaha ya kuishi pamoja.
Ukweli na uzuri wa familia, na huruma kwa familia dhaifu na zilizojeruhiwa.
SEHEMU YA TATU.
Kukabiliana na hali halisi: mitazamo ya kichungaji
Kutangaza Injili ya familia leo, katika mazingira mbalimbali.
Kuwaongoza wachumba katika safari ya maandalizi kwa sakramenti ya ndoa.
Kuisindikiza miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa.
Uangalizi wa kiuchungaji kwa ajili ya wanaoishi katika ndoa ya kiserikali, au wanaoishi pamoja bila ndoa.
Kuwatibu familia zilizojeruhiwa (wanandoa waliotengana, waliotalakiana, waliotalakiana na kuoa au kuolewa tena, familia zenye mzazi mmoja tu)
Uangalizi wa kichungaji kuhusu watu wenye mwelekeo wa kupendana jinsia moja.
Kuzaa watoto na changamoto ya udhibiti wa uzazi.
Changamoto ya malezi na wajibu wa familia katika uinjilishaji.
Hitimisho.
MASWALI kwa ajili ya upokeaji na tafakari ya kina juu ya Relatio Synodi.
Swali tangulizi la ujumla linalohusu sehemu zote za Relatio Synodi
Sehemu ya Kwanza Usikivu: Mazingira na changamoto juu ya familia
Mazingira ya kijamii na kitamaduni (na. 5-8).
Umuhimu wa maisha ya upendo (na. 9-10)
Changamoto kwa uchungaji (n. 11).
Sehemu ya Pili Kumtazama Kristo: Injili ya familia.
Mtazamo juu ya Yesu na malezi ya Mungu katika historia ya wokovu (na. 12-14).
Familia katika mpango wa Mungu wa wokovu (na. 15-16).
Familia katika hati za Kanisa (na. 17-20).
Tabia ya kutokuvunjika ya ndoa na furaha ya kuishi pamoja (na. 21-22).
Ukweli na uzuri wa familia, na huruma kwa familia dhaifu na zilizojeruhiwa (na. 23-28).
Sehemu ya 3 Kukabiliana na hali halisi: mitazamo ya kichungaji
Kutangaza Injili ya familia leo, katika mazingira mbalimbali (na. 29-38).
Kuwaongoza wachumba katika safari ya maandalizi kwa sakramenti ya ndoa (na. 39-40).
Kuisindikiza miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa (n. 40).
Uangalizi wa kiuchungaji kwa ajili ya wanaoishi katika ndoa ya kiserikali, au wanaoishi pamoja bila ndoa (na. 41-43).
Kuwatibu familia zilizojeruhiwa (wanandoa waliotengana, waliotalakiana, waliotalakiana na kuoa au kuolewa tena, familia zenye mzazi mmoja tu) (nn. 44-54).
Uangalizi wa kichungaji kuhusu watu wenye mwelekeo wa kupendana jinsia moja (na. 55-56)
Kuzaa watoto na changamoto ya udhibiti wa uzazi (na. 57-59).
Changamoto ya malezi na wajibu wa familia katika uinjilishaji (na. 60-61).
DIBAJI
Mwishoni mwa Mkutano wa Tatu wa Jumla usio wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu wenye kauli mbiu isemayo Changamoto za kichungaji kuhusu familia mintarafu Uinjilishaji, ulioadhimishwa mwaka 2014, Papa Fransisko aliamua kutangaza hadharani Relatio Synodi, ambayo ni hati ya hitimisho la kazi ya kisinodi. Wakati huohuo, Baba Mtakatifu alidokeza kuwa hati hiyo itakuwa Lineamenta (“Mwongozo wa kazi”) kwa ajili ya Mkutano wa Jumla wa Kawaida wenye kauli mbiu: Wito na utume wa familia katika Kanisa na ulimwengu mamboleo, utakaofanyika kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.
Relatio Synodi, inayosambazwa kama Lineamenta, ilihitimishwa kwa maneno haya: “Matafakari haya yaliyopendekezwa, yaliyo tunda la kazi ya Sinodi iliyoadhimishwa kwa uhuru mkubwa na kwa mtindo wa kusikilizana, yanakusudia kutoa maswali na kuonyesha matazamio yanayotakiwa kukomazwa na kuwekwa bayana kutokana na tafakari ya Makanisa mahalia katika mwaka huu hadi kuufikia adhimisho la Mkutano wa Jumla wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu” (Relatio Synodi, n. 62).
Kwenye Lineamenta huambatanishwa maswali dodoso kadhaa ili kujua hali ya upokeaji wa hati hiyo na kuhimiza mchakato wa kupenya zaidi katika kazi iliyoanza wakati wa Mkutano wa Jumla usio wa Kawaida. Inabidi “kutafakari tena kwa utanashati na ari mpya ufunuo wa kimungu – unaorithishwa katika imani ya Kanisa – unatuambia nini juu ya uzuri, dhima na hadhi ya familia” (Relatio Synodi, n. 4). Kwa mtazamo huo, tunaitwa kuishi “mwaka mzima ili kuendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu mapendekezo yaliyotolewa, ili kupata mwanga zaidi wa maisha ya kiroho, ili hatimaye, kupata suluhu ya kweli katika kukabiliana na matatizo na changamoto ambazo familia zinakumbana nazo” (Papa Fransisko, Hotuba ya kuhitimisha Mkutano wa Sinodi, tarehe 18 Oktoba 2014). Ujumla wa majibu yatakayotolewa kwa maswali dodoso hayo, pamoja na Relatio Synodi, utasaidia kuandaa Instrumentum laboris (“Hati ya kutendea kazi”) kwa ajili ya Mkutano wa Jumla wa Kawaida wa 14 wa mwaka 2015.
Mabaraza ya Maaskofu hualikwa kuchagua namna na mbinu zinazofaa ili kufikia lengo hilo, kwa kushirikisha watendaji wote wa Makanisa mahalia, ikiwa ni pamoja na taasisi za kitaaluma, vyama na mashirika, vyama vya kitume vya walei, na wadau wengine wa kikanisa.
RELATIO SYNODI
ya
Mkutano wa Tatu wa Jumla usio wa Kawaida
(tarehe 5 hadi 19 Oktoba 2014)
Utangulizi
1. Sinodi ya Maaskofu iliyokusanyika mbele ya Papa inaelekeza uangalizi wake kwa familia zote duniani, pamoja na furaha zao, magumu yao na matumaini yao. Kwa namna ya pekee inajisikia ina wajibu wa kumshukuru Bwana kwa jinsi familia nyingi za Kikristo zinavyoitikia kwa uaminifu mkubwa wito na utume wao. Zinafanya hivyo kwa furaha na imani, hata pale ambapo safari ya kifamilia inaziweka mbele na vikwazo, kutokuelewana na mateso. Sinodi hii na Kanisa zima huwapongeza, kuwashukuru na kuwapa moyo wanafamilia hizo. Katika kesha la sala lililoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro siku ya Jumamosi, tarehe 4 Oktoba, 2014 katika maandalizi ya Sinodi juu ya familia Papa Fransisko amekumbusha kwa namna rahisi na ya kugusia umuhimu wa mang’amuzi ya kifamilia katika maisha ya kila mtu, akisema hivi: “Giza la usiku linaanza kushuka juu ya kusanyiko letu. Muda huu ndio muda ambao kila mtu hutamani kurudi nyumbani ili kukutana tena katika meza moja ileile, ndipo ilipo hali ya kupendana, ya kutendeana mema, ya mikutano yenye kuwasha mioyo na kuukuza, mithili ya divai nzuri inayodokeza mbele katika maisha ya binadamu furaha ya sherehe isiyo na mwisho. Saa hii ndiyo pia saa nzito kuliko zote kwa yule anayejikuta yuko mpweke kabisa, katika machweo yenye huzuni ya ndoto na miradi iliyovunjika: watu wangapi wanajikokotea siku kwa siku katika kichochoro chenye uchungu cha kukata tamaa, cha kutelekezwa, na pengine cha chuki; nyumba ngapi zimeishiwa divai ya furaha, na hivyo, ladha – yaani hekima yenyewe – ya maisha [...] Jioni hii tunajifanya sauti ya hao wote kwa njia ya sala yetu, sala iliyo kwa ajili ya wote”.
2. Kitalu cha furaha na majaribu, cha mahusiano ya upendo wa kina na cha mahusiano ambayo, mara nyingine, yamejeruhiwa, familia ndiyo “shule ya kujitajirisha kibinadamu” (rej. Gaudium et Spes, 52), ambayo wote tunaihitaji sana. Licha ya kuwepo alama nyingi za migogoro kwenye taasisi ya familia katika mazingira mbalimbali ya “kijiji cha utandawazi”, hamu ya mtu ya kuwa na familia inadumu kuwa hai, hasa kati ya vijana. Hamu hiyo inasababisha Kanisa, lililo hodari kuhusu ubinadamu na aminifu kwa utume wake, liitangaze daima na kwa uhakika thabiti “Injili ya familia” ambayo ilikabidhiwa kwake kwa ufunuo wa pendo la Mungu katika Yesu Kristo na kufundishwa bila kukoma na Mababa wa Kanisa, Walimu wa kiroho na Majisterio ya Kanisa. Familia, kadiri ya mtazamo ya Kanisa, inachukua umuhimu wa pekee kabisa, na wakati huu ambapo waamini wote wamealikwa kuachana na ubinafsi na kutoka nje, ni lazima familia ijitambue tena kuwa mtendaji wa msingi wa uinjilishaji. Mawazo yanarejea kwa ushuhuda wa kiutume wa familia nyingi.
3. Askofu wa Roma ameiitisha Sinodi ya Maaskofu katika Mkutano wake wa Jumla usio wa Kawaida wa mwezi wa Oktoba 2014, kusudi itafakari juu ya hali halisi ya familia, iliyo ya msingi na ya thamani, ili hapo baadaye kuendeleza kwa kina zaidi matafakari kwenye Mkutano wa Jumla wa Kawaida ambao utafanyika mwezi wa Oktoba 2015, kisha kuichambua mada hiyo kwa muda wa mwaka mzima ulio kati ya matukio hayo mawili. “Hata tendo la kukusanyika katika umoja ('convenire in unum') kandokando ya Askofu wa Roma ni tayari tukio la neema, ambamo hali ya urika wa Maaskofu inajionyesha katika mwendo wa upambanuzi wa kiroho na wa kiuchungaji”: jinsi hii ndivyo Papa Fransisko alivyofafanua mang’amuzi ya kisinodi, huku akielezea kuwa wajibu wake ni usikivu maradufu wa ishara za Mungu na za historia ya wanadamu, na pia uaminifu, maradufu na mmoja, unaotokana nao.
4. Tukinurishwa na hotuba hiyohiyo tumejumuisha matokeo ya matafakari yetu na ya mazungumzano yetu katika sehemu hizi tatu zinazofuata. Ya kwanza, usikivu, ili kuangalia hali halisi ya siku hizi ya familia, katika mchangamano wa mianga yake na giza lake; ya pili, kumtazama Kristo, ili kutafakari tena kwa utanashati na ari mpya ufunuo wa kimungu – unaorithishwa katika imani ya Kanisa – unatuambia nini juu ya uzuri, dhima na hadhi ya familia; na ya tatu, mjadala, tukiwa chini ya nuru ya Bwana wetu Yesu Kristo, ili tuzibaini njia za kufanya upya azma za Kanisa na jamii kwa ajili ya familia yenye kujengwa juu ya ndoa ya mwanamume na mwanamke.
SEHEMU YA KWANZA
Usikivu: Mazingira na changamoto juu ya familia
Mazingira ya kijamii na kitamaduni
5. Huku tukiwa waaminifu kwa mafundisho ya Kristo tunaangalia hali halisi ya familia wakati huu, katika mchangamano wa miali yake ya mwanga na vivuli vya giza. Tunawafikiria wazazi, akina babu na bibi, akina kaka na akina dada, ndugu wa karibu na wa mbali, na pia uhusiano kati ya familia mbili ambao unajengwa na kila ndoa. Mabadiliko ya kianthropolojia na kitamaduni yanaathiri leo hali zote za maisha na kudai yatazamwe kwa kutumia mbinu mbalimbali za kiuchambuzi. Lazima kusisitiza kwanza yaliyo mazuri: kwa mfano, kuwepo kwa uhuru mkubwa zaidi wa kutoa maoni, na utambuzi wa kina zaidi wa haki za wanawakw na watoto, walau katika nchi nyingine. Lakini, kwa upande mwingine, ni lazima kuzingatia pia hatari inayozidi kuongezeka ya ubinafsi wa kupita kiasi, unaopotosha mahusiano ya kifamilia hadi kusababisha kumtazama kila mwanafamilia kuwa sawa na kisiwa, ukishabikia, mara nyingine, picha ya mtu anayejijenga kadiri ya mapenzi yake yanayochukuliwa kama mali kamilifu yenye kujitosheleza. Na kwa ziada, kunaongezeka pia hali ya wasiwasi katika imani, inayowagusa wakatoliki wengi na, mara nyingi, ni asili ya migogoro katika ndoa na familia.
6. Katika utamaduni wa leo upweke ndio sura kuu mmojawapo wa umaskini, nao unasababishwa na kumweka Mungu mbali na maisha ya watu, pia na udhaifu wa mahusiano. Kuna pia hisi ya jumla ya kutoweza kitu mbele ya hali halisi ya kijamii na kiuchumi, ambayo, mara nyingi, inafikia hatua ya kuzigandamiza familia. Ndivyo ilivyo kwa hali ya umaskini unaoongezeka na hali ya kukosa ajira ya hakika, hali ambayo mara nyingine hukabiliwa kama jinamizi, au kwa sababu ya shinikizo zito mno la kodi ambalo bila shaka haliwatii vijana hamu ya kufunga ndoa. Mara nyingi familia zinajihisi kuwa zimeachwa kwa sababu ya kutojali na mapungufu ya uangalifu kwa upande wa taasisi za kiserikali. Matokeo hasi, kwa mtazamo wa mpangilio wa kijamii, ni wazi: kuanzia mpunguo wa kupita kiasi wa uzazi na shida katika kulea, ugumu wa kupokea uzazi wa mtoto, kuwaona wazee kama mzigo, hadi kuenea kwa fadhaa za kimapendo zinayoweza kumfikisha mtu hata katika kutenda jeuri. Ni wajibu wa Serikali ya Nchi kutunga sheria na kuongeza nafasi za ajira ili kuhakikisha mustakabali mzuri kwa vijana, na kuwasaidia kutekeleza mpango wa kuunda familia yao.
7. Yapo mazingira ya kiutamaduni na kidini yenye changamoto za pekee. Kwenye baadhi ya jamii bado kuna ndoa ya mitara na kwenye baadhi ya mazingira ya kijadi kuna mazoea ya “ndoa kwa hatua”. Katika mazingira mengine zipo bado ndoa za kupangwa. Katika nchi ambako uwepo wa Kanisa Katoliki ni mdogo kuna ndoa za mseto nyingi na za utofauti wa imani, pamoja na magumu yote zinayoyabeba kuhusu hali ya kisheria, ya ubatizo na ya malezi ya watoto, pia ya kuheshimiana kwa wenza kwa upande wa tofauti za imani. Katika ndoa hizi inaweza kutokea hatari ya kuhalalisha kila kitu au kutojali, lakini pia inawezekana yakatengenezwa mazingira mazuri ya kiekumene na mazungumzano mwanana miongoni mwa makundi ya watu wa imani tofauti wanaoishi katika jamii moja. Katika mazingira mengi, na si tu yale ya Magharibi, inazidi kuenea tabia ya mume na mke kuishi pamoja kabla ya ndoa au hata kuishi pamoja bila ya kuwa na mpango wowote wa kufunga ndoa. Zaidi ya hayo, mara nyingi zinatungwa sheria za kiraia ambazo zinadhoofisha ndoa na familia. Kutokana na tabia ya kutukuza malimwengu (secularization) katika sehemu nyingi za dunia rejea kwa Mungu imepungua sana, na imani huwa si kitu kinachoshirikishwa tena kijamii.
8. Katika baadhi ya nchi, watoto wanaozaliwa nje ya ndoa ni wengi, na wale ambao baadaye wanalelewa na mzazi mmoja au katika mazingira ya familia pana au yaliyoundwa upya, nao ni wengi. Idadi ya talaka inaongezeka na si haba kuona kuwa maamuzi hayo yanatokana na sababu za kiuchumi tu. Watoto mara nyingi wanabishaniwa baina ya wazazi, nao ndio wahanga halisi wa matengano ya kifamilia. Akina baba mara nyingi hawapo, si tu kwa sababu za kiuchumi, wakati ambapo wangetakiwa kuwajibika zaidi kwa watoto na familia. Hadhi ya mwanamke inahitaji bado kulindwa na kuinuliwa. Leo hii, katika mazingira mengi, kuwa mwanamke bado ni sababu ya kubaguliwa na, hata zawadi ya umama (uzazi) mara nyingi inachukuliwa kama adhabu badala ya kuheshimiwa kama kitu cha thamani kubwa. Hayawezi kusahauliwa hata matendo ya ukatili yanayozidi kuwapata wanawake, na bahati mbaya wakati mwingine hata ndani ya familia, na ule ukatili mkubwa wa kuwakeketa wanawake ulioenea katika baadhi ya tamaduni. Moja ya kashfa kubwa na jambo linalodhihirisha kupotoka kwa jamii ya sasa ni udhalilishaji wa kingono wa watoto. Hata jamii zilizojeruhiwa kwa vita, ugaidi au uwepo wa mfumo wa uhalifu, zinajikuta zikiwa katika hali ya kifamilia iliyodhoofika, na hasa katika miji mikubwa na vichochoro vyake idadi ya watoto wanaoitwa ‘wa mitaaani’ inazidi kuongezeka. Ukimbizi na uhamaji ni ishara nyingine ya nyakati inayotakiwa kutazamwa na kuielewa kwa kuzingatia athari zake kwa maisha ya kifamilia.
Umuhimu wa maisha ya upendo
9. Kwa picha hii ya kijamii iliyooneshwa, inaonekana kuwa, katika sehemu nyingi za dunia, mtu anajisikia haja zaidi ya kujijali, kujitambua toka ndani, kuishi vizuri zaidi sawia na mihemuko yake na vionjo vyake, kutafuta mahusiano bora ya kimapendo. Tamaa hiyo njema inaweza kusaidia kutengeneza mahusiano ya kujitoa mmoja kwa mwingine, yenye kuwajibisha na yenye mshikamano kama yalivyo yale ya familia. Hatari ya mtu kujiangalia tu mwenyewe na kuishi kwa ubinafsi ni kubwa. Changamoto kwa Kanisa ni kuyasaidia majozi katika makuzi yao hususan katika nyanja za mihemuko na ukomavu wa upendo kwa njia ya kuhimiza mazungumzo kati yao, maisha ya fadhila na kutumainia upendo wenye huruma wa Mungu. Uwajibikaji kamili unaohimizwa katika ndoa ya Kikristo unaweza kuwa dawa muhimu dhidi ya kishawishi cha ubinafsi.
10. Katika dunia ya leo haikosekani mielekeo ya kitamaduni inayotaka kulazimisha mapendo bila mipaka, ambayo hutaka kupekua kila kitu, hata vile vilivyo tata. Kwa kweli swala la udhaifu wa kimapendo lipo sana leo: mapendo ya kutafuta faida binafsi, yasiyo ya kudumu na yenye kubadilika, ambayo hayawasaidii watu kufikia ukomavu mkubwa zaidi. Kunatiisha kuenea kwa ponografia (picha za ngono) na biashara ya ngono, kunakochangiwa hata na matumizi mabaya ya mtandao wa intaneti, na inatakiwa ilaaniwe ile hali ya watu kulazimishwa kufanya ukahaba. Katika mazingira haya, majozi mara nyingine yanayumba, yanasita na yanapata shida kuona njia ya kukua. Wengi wanaelekea kubaki katika hatua za chini kabisa kimihemuko na kimapenzi. Mgogoro katika jozi unayumbisha familia, na kutokana na matengano na talaka, athari kubwa zinawapata watu wazima, watoto na jamii, na hivyo hudhoofisha mtu na mahusiano ya kijamii. Hata kushuka kwa idadi ya vizazi kunakotokana na fikra na mitazamo ya kupunguza uzazi iliyoenezwa na siasa za kiulimwengu juu ya afya ya uzazi, si tu kwamba kunatengeneza mazingira ambamo kubadilishana kwa vizazi hakuna uhakika, bali kuna hatari ya kutufikisha kwenye zama za umasikini mkubwa wa kiuchumi na kupoteza matumaini ya wakati ujao. Maendeleo ya biotekinolojia nayo yameathiri sana uzazi.
Changamoto kwa uchungaji
11. Katika mazingira haya, Kanisa linaonja umuhimu wa kusema neno la kweli na la matumaini. Ni lazima tuanze kwa kuamini kwamba mtu anatoka kwa Mungu, na, kutokana na hilo, pia kwamba tafakari inayoweza kupendekeza tena maswali makubwa juu ya maana ya kuwa watu, iweze kuwa jibu sahihi kwa matazamio yaliyo makubwa zaidi ya ubinadamu. Tunu kubwa ya ndoa na ya familia ya Kikristo zinawiana na kile kinachotafutwa siku zote za maisha ya mwanadamu hata wakati huu unapotawala ubinafsi na starehe. Inatakiwa kuwapokea watu katika hali halisi ya maisha yao, kujua kuwaunga mkono katika kutafuta kwao, kuhamasisha tamaa ya Mungu na nia ya kujisikia sehemu ya Kanisa kikamilifu hata katika wale walioshindwa au wapo kwenye hali fulani yenye utata. Ujumbe wa Kikristo unabeba daima ndani yake huruma na ukweli, vitu ambavyo katika Kristo vinaendana.
SEHEMU YA PILI
Kumtazama Kristo: Injili ya familia
Mtazamo juu ya Yesu na malezi ya Mungu katika historia ya wokovu
12. Ili “kutathmini mwendo wetu katika kukabiliana na changamoto za siku za leo, kitu cha lazima ni kukazia macho yetu juu ya Yesu Kristo, kutulia katika kutafakari na katika kuabudu uso wake [...]. Kwa maana, kila tunaporudi kwenye chemchemi ya maisha ya Kikristo hufunguka mbele yetu njia zilizo mpya na nafasi tusizofikiria kabla” (Papa Fransisko, Hotuba ya tarehe 4 Oktoba 2014). Yesu aliwaangalia kwa upendo na upole wanawake na wanaume aliokutana nao, akiwasindikiza hatua zao kwa ukweli, subira na huruma, katika kuwahubiria madai ya Ufalme wa Mungu.
13. Kwa vile utaratibu wa uumbaji huratibishwa na mwelekeo wa viumbe vyote kwa Kristo, inabidi kupambanua – bila kuzitenganisha – hatua mbalimbali ambazo kwa njia yake Mungu huwashirikisha wanadamu wote neema ya agano naye. Kwa sababu ya malezi ya Mungu, ambayo kadiri yake utaratibu wa uumbaji hukua hatua kwa hatua hadi kuufikia utaratibu wa ukombozi, inatupasa kuutambua ule upya wa sakramenti ya ndoa ya Kikristo kuwa mfulizo wa ndoa ya asili ilivyokuwa mwanzoni. Kwa namna hiyo inawezekana kuelewa jinsi Mungu inavyotenda wokovu, katika uumbaji na katika maisha ya Kikristo pia. Katika uumbaji: kwa kuwa vitu vyote viliumbwa kwa njia yake Kristo, na kwa ajili yake (rej. Kol 1:16), basi, Wakristo “huzigundua kwa furaha na heshima zile mbegu za Neno la Mungu zilizofichama ndani ya hivyo; pia inawapasa kutazama kwa makini mabadiliko makubwa yanayotukia kati ya mataifa” (Ad Gentes, 11). Katika maisha ya Kikristo: kwa vile kila mwamini, kwa njia ya Ubatizo, anaunganishwa na Kanisa kwa kupitia lile Kanisa la nyumbani ambalo ni familia yake, na kuanza safari ya maisha ambayo inaendelea, hatua kwa hatua, katika kujaliwa na kupokea zaidi na zaidi karama za Mungu” (Familiaris Consortio, 9), kwa njia ya kuurudia daima upendo ule wenye kuokoa katika dhambi na kutuza ukamilifu wa uzima.
14. Yesu mwenyewe, akirejea kwenye mpango wa asili kuhusu jozi la kibinadamu, alisisitiza upya muungano usiovunjika baina ya mwanamume na mwanamke, ijapo alisema pia kwamba “Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu, lakini tangu mwanzo haikuwa hivi” (Mt 19:8). Tabia ya kutokuvunjika ya ndoa (“Aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” Mt 19:6), haitakiwi kutafsiriwa kwanza kama “mzigo” mzito uliobebeshwa juu ya watu, bali kama “zawadi” waliojaliwa wale waliounganishwa katika ndoa. Kwa namna hiyo, Yesu anaonyesha jinsi uhisani wa Mungu unavyosindikiza sikuzote safari ya mtu, na unavyouponya moyo ulio mgumu na kuugeuza kwa neema yake, akiuelekeza kwa Yule aliye asili yake, kwa kupitia njia ya msalaba. Katika Injili tunapata mfano dhahiri ya Yesu, ambao ni kielelezo kamili kwa Kanisa. Maana, Yesu aliishi katika familia moja, akafanya chanzo cha ishara zake katika sherehe ya arusi huko Kana, akahubiri ujumbe kuhusu maana ya ndoa kama utimilifu wa ufunuo unaorejea kwa namna mpya kwenye mpango wa asili wa Mungu (rej. Mt 19:3). Lakini wakati huohuo halitekeleza hayo mafundisho aliyokuwa akifundisha, kwa kuonyesha wazi maana ya kweli ya huruma. Hilo linaonekana wazi katika kukutana kwake na mwanamke Msamaria (rej. Yn 4:1-30), pia na mwanamke mzinifu (rej. Yn 8:11). Hapo Yesu, kwa upendo mkubwa kwa yule aliyekosa, anamwelekeza kwenye majuto na toba (“Enenda zako; wala usitende dhambi tena”), ambayo ni njia ili kusamehewa.
Familia katika mpango wa Mungu wa wokovu
15. Maneno ya uzima wa milele ambayo Yesu aliwaachia wanafunzi wake yalikuwa ni pamoja na mafundisho kuhusu ndoa na familia. Mafundisho hayo ya Yesu yanatusaidia kufafanua mpango wa Mungu kuhusu ndoa na familia kama wenye hatua tatu za msingi. Hapo mwanzo, kulikuwa na familia ya asili, pale Mungu muumbaji alipoweka ndoa ya awali baina ya Adamu na Hawa, kama msingi thabiti ya familia. Si tu kwamba Mungu alimwumba mtu mwanamume na mwanamke (rej. Mwa 1:27), bali aliwabariki pia ili wazae na kuongezeka (rej. Mwa 1:28). Kwa hiyo, “mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Mwa 2:24). Muungano huo uliharibiwa na dhambi na umekuwa muundo wa ndoa katika historia ya Watu wa Mungu, ambao Musa aliwajalia ruhusa ya kuandika hati ya talaka (rej. Kum 24:1nk). Muundo huo ndio uliokuwa wa kawaida wakati wa Yesu. Kwa kuja kwake na kufanya upatanisho wa ulimwengu ulioanguka kwa njia ya ukombozi aliotenda mwenyewe, kipindi cha agano lililoanzishwa kwa Musa kilikomea.
16. Yesu, aliyepatanisha vitu vyote ndani yake, alirejesha upya ndoa na familia kwenye muundo wake wa asili (rej. Mk 10:1-12). Familia na ndoa zimekombolewa na Kristo (rej. Efe 5:21-32), na kutengenezwa upya kwa mfano wa Utatu Mtakatifu, fumbo ambalo kila upendo wa kweli hutoka kwake. Agano la ndoa, lililoanzishwa katika uumbaji na kufunuliwa katika historia ya wokovu, hupata ufunuo kamili wa maana yake katika Kristo na Kanisa lake. Kutoka kwa Kristo kwa njia ya Kanisa, ndoa na familia hupewa neema inayohitajika ili kuushuhudia upendo wa Mungu na kuishi maisha ya ushirika. Injili (Habari Njema) ya familia imo ndani ya historia ya ulimwengu tangu kuumbwa kwa mtu kwa mfano na sura ya Mungu (rej. Mwa 1:26-27) hadi ukamilifu wa fumbo la Agano katika Kristo mwisho wa dahari katika arusi ya Mwanakondoo (rej. Ufu 19:9; Yohane Paulo II, Katekesi juu ya upendo wa kibinadamu).
Familia katika hati za Kanisa
17. “Katika mkondo wa karne, Kanisa halikuacha kamwe kutoa mafundisho yake juu ya ndoa na familia. Kwenye Majisterio yake, tamko moja kati ya yaliyo muhimu zaidi lilitolewa na Mtaguso Mkuu Vatikano II, katika Konstitusyo ya Kichungaji Gaudium et Spes, ambayo imechukua sura moja nzima ili kuelezea uhamasishaji na hadhi ya ndoa na familia (rej. Gaudium et Spes, 47-52). Mtaguso umeelezea ndoa kuwa ushirikiano wa maisha na upendo (rej. Gaudium et Spes, 48), kwa kuweka upendo kama kiini cha familia, na kwa kuonyesha, wakati huohuo, ukweli wa upendo huo mbele ya fikra mbalimbali zilizopo katika utamaduni wa kisasa, zinazolenga kupunguza umuhimu wake. “Upendo wa kweli kati ya mume na mke” (Gaudium et Spes, 49) ni kujitoa kila mmoja kwa mwenzake, pia hujumuisha na kukamilisha matumizi ya tendo la ndoa na mapendo mororo, kadiri ya mpango wa kimungu (rej. Gaudium et Spes, 48-49). Aidha, kipengere che 48 cha Gaudium et Spes kinasisitiza kuwa wanandoa wana mzizi katika Kristo: Kristo Bwana “anawajia Wakristo wanandoa kwa njia ya sakramenti ya ndoa”, na kudumu kukaa pamoja nao. Katika umwilisho wake, Yesu anachukua upendo wa kibinadamu, anautakasa na kuukamilisha, na anawajalia wanandoa, pamoja na Roho wake, uwezo wa kuuishi, akiwajazia maisha yao yote kwa imani, matumaini na mapendo. Kwa namna hiyo, wanandoa ni kama wakfu na, kwa kupewa neema ya pekee, hujenga Mwili wa Kristo na kuliunda Kanisa la nyumbani (rej. Lumen Gentium, 11). Nalo Kanisa, ili lipate kutambua kikamilifu fumbo lake, linaitazama familia ya Kikristo, ambayo inalidhihirisha fumbo lake kwa uwazi na ukweli” (Instrumentum Laboris, 4).
18. “Kwa kufuata mkondo wa Mtaguso wa Vatikano II, Majisterio ya kipapa ilichanganua zaidi mafundisho kuhusu ndoa na familia. Hususan Papa Paulo VI, kwa Insiklika yake Humanae Vitae, aliweka wazi kifungo cha ndani kinachounganisha mapendo ya ndoa na uzazi wa mtoto. Mt. Yohane Paulo II alizingatia kwa makini hali ya familia, katika katekesi zake juu ya mapendo ya kibinadamu, katika Barua kwa familia zote (Gratissimam Sane) na hasa katika Wosia wa Kitume Familiaris Consortio. Katika hati hizo, Papa huyo alitaja familia kama “njia ya Kanisa”; akatoa picha ya ujumla ya wito wa mapendo ya mwanamume na mwanamke; na kupendekeza mwongozo wa msingi kwa ajili ya uchungaji wa familia na kuhusu majukumu ya familia katika jamii. Hususan, alipoandika kuhusu mapendo katika ndoa (taz. Familiaris Consortio, 13), alifafanua jinsi wanandoa, katika kupendana, wanavyopokea kipaji cha Roho wa Kristo na kuishi wito wao wa utakatifu” (Instrumentum Laboris, 5).
19. “Papa Benedikto XVI, katika Insiklika Deus Caritas Est (Mungu ni Upendo), alirejea kwenye dhamira ya hali halisi ya mapendo baina ya mwanamume na mwanamke, ambayo hung’arizwa kikamilifu katika nuru tu ya upendo wa Kristo msulibiwa (taz. Deus Caritas Est, 2). Yeye alisisitiza jinsi “ndoa yenye msingi katika mapendo ya kudumu kwa mwenzi mmoja yanakuwa ikona (picha, mfano) ya uhusiano wa Mungu na watu wake, na tena kwamba namna ya Mungu ya kupenda watu inakuwa kipimo cha mapendo ya kibinadamu” (Deus Caritas Est, 11). Aidha, katika Insiklika Caritas in Veritate (Mapendo katika Ukweli), anasisitiza umuhimu wa mapendo kama asili ya uzima katika jamii (taz. Caritas in Veritate, 44), mahali ambapo hufundishwa kung’amua mafaa ya wote” (Instrumentum Laboris, 6).
20. “Papa Fransisko, katika Insiklika Lumen Fidei (Mwanga wa Imani) akichunguza uhusiano kati ya familia na imani, ndivyo alivyoandika: “Kukutana na Kristo, kukubali kushikwa na kuongozwa na upendo wake, hupanua upeo wa maisha, na kuyajalia tumaini imara lisilodanganya. Imani si makimbilio ya watu wasio na moyo hodari, bali ni uwezo wa maisha kupanuka. Imani inasaidia kugundua wito mkuu, wito wa mapendo, na inahakikisha kuwa mapendo haya ni ya kuaminiwa, kwamba inafaa kujikabidhi kwake, kwa sababu msingi wake upo katika uaminifu wa Mungu, ambao una nguvu kuliko udhaifu wetu wowote ule” (Lumen Fidei, 53)” (Instrumentum Laboris, 7).
Tabia ya kutokuvunjika ya ndoa na furaha ya kuishi pamoja
21. Kujitoa kila mmoja kwa mwenzake ni tendo la msingi la sakramenti ya ndoa. Nayo inatokana na neema ya Ubatizo, ambao unaweka agano la awali la kila mtu na Kristo katika Kanisa. Katika kukaribishana, na kwa neema ya Kristo, wana arusi wanaahidiana kujitoa kikamilifu kila mmoja kwa mwenzake, kuaminiana, na kuwa wazi kupokea watoto. Wanavitambua kama mambo maalum ya ndoa vile vipaji ambavyo Mungu anawajalia, wakitilia maanani azma waliyojichukulia kila mmoja mbele ya mwenzake, kwa jina la Mungu na mbele ya Kanisa Hivyo, katika imani inawezekana kupokea mema ya ndoa kama wajibu unaobebeka kwa msaada wa neema ya sakramenti. Mungu anaweka wakfu mapendo ya wanandoa na kuithibitisha tabia yake ya kutokuvunjika, akiwapa msaada ili waweze kuishi katika uaminifu, katika kukamilishana na kwa kuwa wazi kuwapokea watoto. Kwa hiyo, Kanisa linawatazama wanandoa kama moyo wa familia nzima inayoelekeza – nayo pia – macho yake kwa Yesu.
22. Kwa mtazamo huohuo, kwa kushika maneno ya Mtume yanayofundisha kuwa viumbe vyote viliumbwa kwa njia ya Kristo na kwa ajili yake (rej. Kol 1:16), Mtaguso wa Vatikano II ulipenda kutamka sifa za ndoa ya asili na za mambo mema yaliyopo katika dini nyinginezo (taz. Nostra Aetate, 2) na katika tamaduni mbalimbali, licha ya mapungufu na makasoro (taz. Redemptoris Missio, 55). Kuwepo kwa mbegu za Neno la Mungu katika tamaduni (taz. Ad Gentes, 11) kungeweza kuzingatiwa pia, kwa namna fulani, kuhusu hali halisi ya ndoa na ya familia kadiri ya tamaduni nyingi na watu wasio Wakristo. Kwa maana ya kwamba kuna mambo kadhaa ambazo zi halali pia katika namna zilizo nje ya ndoa ya Kikristo – ikiwa zina msingi wake katika uhusiano wa kudumu na wa kweli baina ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja - , ambazo, kwa vyovyote, tunazitambua kuwa zinaielekea hiyo. Kwa kutazama hekima ya kibinadamu iliyoenea kati ya mataifa na tamaduni mbalimbali, Kanisa linatambua pia familia hiyo kama umoja wa asili na wa msingi unaotakiwa ili kuishi kwa pamoja kwa watu kuwe na usitawi mzuri.
Ukweli na uzuri wa familia, na huruma kwa familia dhaifu na zilizojeruhiwa
23. Kanisa linazitazama kwa furaha ya ndani na faraja kubwa familia zinazodumu kuwa aminifu kwa mafundisho ya Injili, likizishukuru na kuzipa moyo kwa ushuhuda zinaotoa. Maana, kwa njia ya hizo, huaminika uzuri wa ndoa isiyovunjika na inayodumu aminifu sikuzote. Katika familia, ambayo “ingeweza kuitwa Kanisa la nyumbani” (Lumen Gentium, 11), hukomaa mang’amuzi ya kwanza ya kikanisa ya ushirika kati ya watu, ambamo huakisika, kwa neema, fumbo la Utatu Mtakatifu. “Ni hapa ambapo mmoja hujifunza uvumilivu na furaha ya kazi, mapendo ya kindugu, msamaha wenye ukarimu, unaofanywa upya tena na tena, na juu ya yote ibada kwa Mungu, kwa njia ya sala na toleo la maisha ya kila mmoja” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 1657). Familia Takatifu ya Nazareti ni mfano wake mkuu, na katika shule yake sisi “tunagundua kwa nini tunatakiwa kushika nidhamu ya kiroho, ikiwa tunapenda kufuata mafundisho ya Injili na kuwa wanafunzi wake Kristo” (Paulo VI, Hotuba huko Nazareti, 5 Januari 1964). Injili ya familia, inazilisha pia zile mbegu zinazotarajia kuota na kukomaa, nayo haina budi kuitunza miti ile iliyokauka na inayohitaji kupaliliwa.
24. Kanisa, kwa vile lilivyo mwalimu wa hakika na mama mwenye bidii, pamoja na kwamba linatambua kuwa kwa walio Wakristo hakuna kifungo kingine cha ndoa zaidi ya kile cha sakramenti, na kwamba kukivunja ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu, linaelewa pia kwamba wanae wengi ni dhaifu katika mwendo wao wa imani. “Kwa hiyo, bila kupunguza thamani ya mtazamo wa kiinjili, inatakiwa kusindikiza kwa huruma na subira hatua zinazowezekana za ukuaji wa watu zinavyojitokeza siku kwa siku. [...] Hatua ndogo, kati ya vipingamizi vingi vya kibinadamu, inaweza kumpendeza Mungu zaidi kuliko maisha yanayoonekana kwa nje kuwa sawa lakini yanamaliza siku nzima bila kupambana na mambo yenye ugumu mkubwa. Kila mmoja anastahili kuguswa na faraja na mvuto wa upendo wa Mungu wenye kuokoa, ambao kwa kimuujiza hutenda kazi ndani ya kila mtu, licha ya kasoro na makosa yake” (Evangelii Gaudium, 44).
25. Kwa lengo la kuwashughulikia kiuchungaji watu waliofunga ndoa kiserikali, wanye talaka waliofunga ndoa tena, au wale ambao wanaishi tu pamoja, ni juu ya Kanisa kuwafunulia malezi ya kimungu yanayohusu kazi ya neema katika maisha yao, na kuwasaidia kuufikia utimilifu wa mpango wa Mungu ndani yao. Kwa kufuata mtazamo wa Kristo, ambaye mwanga wake humtia nuru kila mtu (rej. Yn 1:9; Gaudium et Spes, 22), Kanisa linawaangalia kwa upendo wale wanaoshiriki maisha yake kwa namna isiyotimilika, likitambua kuwa neema ya Mungu hufanya kazi pia katika maisha yao kwa kuwapa moyo wa kutenda mema, kwa kutunzana kwa upendo, na kuihudumia jumuiya yenyewe ambamo wanaishi na kufanya kazi.
26. Kanisa linaangalia kwa uchungu ile hali ya kukata tamaa ya vijana wengi mbele ya azma ya ndoa, na linateswa na jinsi waamini wengi wanavyoamua haraka haraka kukivunja kifungo cha ndoa, wakianzisha uhusiano na mwenzi mwingine. Waamini hawa, walio sehemu ya Kanisa, wanahitaji uangalizi wa kiuchungaji wenye huruma na kutia moyo, kwa kupambanua inavyotakiwa hali mbalimbali za watu. Vijana waliobatizwa wanahitaji kutiwa moyo ili wasisite mbele ya utajiri ambao mipango yao ya upendo inaletewa na sakramenti ya ndoa. Kwa sababu wanapokea kutoka hiyo neema ya Kristo na uwezo wa kushiriki kikamilifu zaidi katika maisha ya Kanisa.
27. Kwa maana hiyo, mtazamo mpya ya uchungaji wa familia wa siku hizi ni kujali kwa makini hali halisi ya ndoa za kiserikali baina ya mwanamume na mwanamke, ya ndoa ya kimila, na, kwa kuzingatia tofauti zilizopo, pia hali ya kuishi pamoja bila ndoa. Pale ambapo muungano unafikia uthabiti mkubwa wa kutosha kwa njia ya kifungo cha hadharani, ukiwa unaonyesha kuwepo upendo mkuu, uwajibikaji mbele ya watoto, uwezo wa kukabiliana na magumu, huweza kutazamwa kama fursa ya kusindikizwa ili ichanue hadi kufikia hatua ya kuadhimisha sakramenti ya ndoa. Lakini mara nyingi kuishi pamoja kunaanza si kwa kutazamia ndoa hapo mbele, bila nia yoyote ya kufunga uhusiano wa kudumu uliotambulika mbele ya jamii.
28. Kwa mtazamo wenye huruma wa Yesu, Kanisa linatakiwa kuwasindikiza kwa makini na kwa upendo wanae dhaifu zaidi, walioathirika na upendo uliojeruhiwa na kupotewa, kwa kuwatia moyo na tumaini, kama vile mwanga unaomulika juu ya mnara, au mwenge unaopelekwa kati ya watu ili kuwaangazia waliopoteza njia au wanaokumbwa na tufani. Kwa kujua kwamba rehema iliyo kubwa zaidi ni kusema ukweli kwa upendo, tuzidi kuvuka hata mipaka ya huruma tupu. Upendo wenye rehema, pamoja na kuvutia na kuunganisha, una uwezo wa kugeuza na kuinua pia. Hualika kutubu. Kwa jinsi ya utendaji wa Bwana Yesu mwenyewe, ambaye hakuhukumu yule mwanamke mzinifu, bali alimwalika asitende dhambi tena (rej. Yn 8:1-11).
SEHEMU YA TATU
Kukabiliana na hali halisi: mitazamo ya kichungaji
Kutangaza Injili ya familia leo, katika mazingira mbalimbali
29. Mazungumzano ndani ya Sinodi yamesisitiza juu ya baadhi ya masuala ya kichungaji ya lazima zaidi ya kukabidhiwa kwa Makanisa mahalia ili yayatendee kazi katika ushirika “na Petro na chini ya Petro” (“cum Petro et sub Petro”). Kutangaza Injili ya familia ni haja ya lazima kwa ajili ya uinjilishaji mpya. Kanisa limeitwa kukutekeleza kwa upole wa kimama na kwa uwazi wa mwalimu (rej. Efe 4:15), katika uaminifu kwa “kujihinisha” (kenosis) kwa huruma kwa Kristo. Ukweli unachukua mwili katika udhaifu wa kibinadamu si kwa lengo la kuulaani, bali ili uuokoe. (rej. Yn 3:16-17).
30. Kuinjilisha ni wajibu wa taifa zima la Mungu, kila mmoja kufuatana na huduma yake na karama yake. Bila ushuhuda wa furaha ya wanandoa na familia, zilizo makanisa ya nyumbani, tangazo la Injili, hata kama ni sahihi, litakuwa katika hatari ya kutoeleweka au kuzama katika bahari ya maneno mengi ambayo ni kawaida ya jamii yetu (rej. Novo Millennio Ineunte, 50). Mababa wa Sinodi wamesisitiza mara nyingi kwamba familia za kikatoliki, kwa nguvu ya neema ya sakramenti ya ndoa, zimeitwa kuwa, zao zenyewe, wahudumu hai katika uchungaji wa familia.
31. Itakuwa muhimu sana kusisitiza ukuu wa neema, na kwa hiyo uwezo unaojaliwa na Roho Mtakatifu katika sakramenti. Inatakiwa kusaidia kung’amua kwamba Injili ya Familia ni furaha ambayo “huijaza mioyo na maisha yote”, kwa sababu katika Kristo tumewekwa “huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke” (Evangelii Gaudium, 1). Katika mwanga wa mfano wa mpanzi (rej. Mt 13:3-9), wajibu wetu ni kushirikiana katika kupanda: mengine yote ni kazi ya Mungu. Inapaswa isisahaulike kwamba Kanisa, ambalo linahubiri juu ya familia, ni ishara ya ukinzani.
32. Kwa sababu hiyo, wajibu huo unalidai Kanisa zima kuongoka kimisionari: ni lazima kutosimama katika kutangaza habari iliyo ya kinadharia tu, na iliyotenganika na matatizo halisi ya watu. Inapaswa kutosahau kamwe kwamba mgogoro wa imani ndio uliosababisha mgogoro wa ndoa na familia na, kama matokeo yake, umekatika mfululizo wa uwasilishaji wa imani kutoka kwa wazazi hadi watoto. Mbele ya imani thabiti, kulazimisha kwa mitazamo fulani ya kitamaduni, ambayo huweza kuzidhoofisha familia na ndoa, hakuna nguvu.
33. Uongofu unaohitajika ni pia ule unaohusu msamiati unaotumika, ili uwe wenye maana kwelikweli. Tangazo hilo lazima liwezeshe kung’amua kwamba Injili ya familia ni jibu kwa matarajio ya ndani kabisa ya mtu: ni jibu kwa hadhi yake, na kwa ukamilifu wake katika kutendeana, katika kushiriki na katika kuzaa. Si suala la kuweka sheria tu, bali ni kuonyesha tunu, ili kuitika hitaji la hizo ambalo linaonekana leo pia katika nchi zilizoacha zaidi imani.
34. Neno la Mungu ni chanzo cha uzima na cha maisha ya kiroho kwa familia. Uchungaji wote wa familia unapaswa kufinyangwa kwa ndani na kuwalea wanakanisa la nyumbani kwa njia ya kuyasoma Maandiko Matakatifu katika mazingira ya sala na chini ya uongozi wa Kanisa. Neno la Mungu si habari njema tu kwa maisha ya binafsi ya watu, bali ni pia kigezo cha hukumu na mwanga wa upambanuzi wa changamoto mbalimbali ambazo wanandoa na familia wanakabiliana nazo.
35. Wakati huohuo Mababa wengi wa Sinodi wamesisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na mtazamo ulio chanya zaidi kwa utajiri wa mang’amuzi mbalimbali ya kidini, bila kuficha matatizo yaliyomo. Katika mazingira haya mbalimbali ya kidini na katika tofauti ya kiutamaduni ambayo ni sifa ya Mataifa, kwanza ni lazima kuyaheshimu mambo chanya mbalimbali yaliyomo na katika mwanga wa hayo kutambua mipaka na mapungufu yake.
36. Ndoa ya Kikristo ni wito ambao unapokelewa baada ya mafundisho na maandalizi ya kutosha katika safari ya kiimani, kwa utambuzi uliokomaa, na ile ndoa haipaswi kueleweka kama desturi ya kitamaduni au haja ya kijamii au kisheria. Kwa hiyo inahitajika kubuni mbinu maalum zinazomsindikiza mtu na pia jozi ili, pamoja na kutoa mafundisho ya mambo ya imani, ziunganishe pia mang’amuzi ya maisha inayotolewa na jumuiya zima ya kikanisa.
37. Mara nyingi imetajwa haja ya kufanywa upya kwa utendaji wa kichungaji katika mwanga wa Injili ya familia, kwa kuondokana na mitazamo ya kibinafsi ambayo bado inashika utendaji huo. Kwa sababu hiyo, mara nyingi imesisitizwa juu ya hitaji la kufanywa upya kwa malezi ya mapadre, mashemasi, makatekista na wahudumu wengine wa kichungaji, kwa njia ya ushirikiano zaidi wa familia zenyewe.
38. Sambamba, imesisitizwa haja ya uinjilishaji ambao unazishtaki bila kuficha shuruti za kitamaduni, za kijamii, za kisiasa na za kiuchumi, na ile nafasi kubwa mno iliyopewa mantiki ya soko, hali ambazo zinazuia maisha ya kweli ya kifamilia, na kusababisha hali na matendo ya ubaguzi, umaskini, unyanyapaa, ujeuri. Kwa sababu hiyo ni lazima vikuzwe mazungumzano na ushirikiano na miundo ya kijamii; pia ni lazima kuwatia moyo na kuwaunga mkono walei ambao wanajitahidi kufanya kazi, kama Wakristo, katika mazingira ya kitamaduni na kisiasa na kiuchumi.
Kuwaongoza wachumba katika safari ya maandalizi kwa sakramenti ya ndoa
39. Hali halisi ya kijamii ilivyo ngumu na changamoto ambazo familia leo inaitwa kupambana nazo hudai juhudi zaidi katika jumuiya nzima ya Kikristo kwa ajili ya maandalizi ya wachumba kuelekea ndoa. Lazima kukumbuka umuhimu wa fadhila. Kati ya fadhila zote usafi wa moyo inatambulika kama fadhila yenye thamani ya pekee kwa ajili ya kukomaza kwelikweli mapendo baina ya watu. Kuhusu haja hii, Mababa wa Sinodi waliafikiana katika kusisitiza umuhimu wa kushirikisha zaidi jumuiya nzima kwa kutanguliza ushuhuda wa familia zenyewe, licha ya kukita mizizi kwa maandalizi ya ndoa katika safari ya kisakramenti ya kuingizwa katika Ukristo, kwa kusisitiza uhusiano kati ya ndoa na ubatizo na sakramenti nyinginezo. Sambamba imesisitizwa haja ya kuweka mikakati maalum kwa ajili ya maandalizi ya hivi karibuni ya ndoa ambayo iwe mang’amuzi ya kweli ya ushirikiano katika maisha ya kikanisa na ichambue mada mbalimbali za maisha ya kifamilia.
Kuisindikiza miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa
40. Miaka ya kwanza ya ndoa ni kipindi muhimu na tete ambacho kwacho wanandoa wanakua katika ufahamu wa changamoto na wa maana ya ndoa. Papo hapo kuna haja ya kuendelea kuwasindikiza kichungaji wanandoa baada ya adhimisho la sakramenti (rej. Familiaris Consortio, Sehemu ya 3). Basi ni muhimu sana katika kazi hiyo ya kichungaji uwepo wa majozi yenye uzoefu. Parokia imetambulika kama mahali ambapo wanandoa wenye uzoefu wanaweza kuwekwa karibu na wale ambao ni wapya, wakisaidiwa pia na misaada ya vyama vya kitume, harakati za kikanisa na jumuiya mpya. Ni lazima kuwahimiza wanandoa wawe na msimamo wa pekee kuhusu kuwa tayari kupokea zawadi kubwa ya watoto. Ni muhimu kusisitiza umuhimu wa maisha ya kiroho ya kifamilia, wa sala na wa kushiriki Ekaristi siku ya Dominika, kwa kuhamasisha majozi yajumuike mara kwa mara ili kukuza maisha ya kiroho na mshikamano katika majukumu halisi ya maisha. Ibada, matendo ya kiuchaji na Ekaristi, vya kuadhimishwa kwa ajili ya familia, hasa katika kumbukumbu ya siku ya ndoa, vimetajwa kama muhimu ili kukuza uinjilishaji kwa njia ya familia.
Uangalizi wa kichungaji kwa ajili ya wanaoishi katika ndoa ya kiserikali, au wanaoishi pamoja bila ndoa
41. Sinodi, huku ikiendelea kutangaza na kuhamasisha ndoa ya Kikristo, inahimiza pia ifanyike upambanuzi wa kichungaji juu ya watu ambao hawaishi hali hii. Ni muhimu kuanzisha mazungumzo ya kichungaji na watu hao kwa lengo la kuangalia vitu vilivyomo kwenye maisha yao vinavyoweza kusaidia kuwaongoza kupokea Injili ya ndoa katika ukamilifu wake. Wachungaji wajitahidi kugundua katika maisha ya watu hao viashiria vya uwezekano wa uinjilishaji na ukuaji wa kibinadamu na kiroho. Hisia mpya ya uchungaji wa leo, imo katika kang’amua mambo chanya yaliyomo kwenye ndoa za kiserikali, na, licha ya tofauti zake, yale yaliyomo katika maisha ya pamoja bila ndoa. Inatakiwa kwamba katika pendekezo la Kanisa, pamoja na kukazia kwa uwazi ujumbe wa Kikristo, tuonyeshe pia mambo yanayoweza kujenga katika hali ambazo haziwiani nao bado au zimeacha kufanya hivyo.
42. Imegundulika pia kuwa katika nchi nyingi “idadi ya majozi yanayoishi pamoja kwa majaribio, bila ndoa yoyote wala ya kikanisa, wala ya kiserikali, inazidi kuongezeka” (Instrumentum Laboris, 81). Katika baadhi ya nchi hili linatokea hasa katika ndoa za jadi, zilizopangwa na familia husika na mara nyingi za kuadhimishwa kwa hatua kadhaa. Katika nchi nyingine kumbe inaendelea kukua idadi ya majozi ambayo baada ya kuishi pamoja kwa muda mrefu, wanaomba kuadhimisha ndoa kanisani. Kuchagua kuishi pamoja bila ndoa mara nyingi hutokana na kasumba ya jumla inayopingana na wajibu wowote ulio rasmi na wa kudumu, lakini pia unatokana na subira ya uhakika wa maisha kiuchumi (kazi na mshahara wa kudumu). Mwisho, miungano isiyo rasmi katika baadhi ya nchi ni mingi si tu kutokana na kukataza tunu za familia na ndoa, bali hasa kutokana na ukweli kwamba, kwa wanaoishi katika hali ya chini kijamii, kuoana kunatazamwa kama starehe, kiasi kwamba umasikini wa mali unawasukuma kuiishi miungano isiyo rasmi.
43. Hali zote hizi zishughulikiwe kwa mtindo wa kujenga, kwa kujaribu kuzigeuza ziwe fursa za makuzi kuelekea utimilifu wa ndoa na familia katika mwanga wa Injili. Yaani, inatakiwa kuzipokea hali hizo na kuzisindikiza kwa uvumilivu na umakini. Ili kutimiza lengo hilo ushuhuda unaovutia wa familia halisi za Kikristo ni muhimu sana, kama wainjilishaji wa familia.
Kuwatibu familia zilizojeruhiwa (wanandoa waliotengana, waliotalakiana, waliotalakiana na kuoa au kuolewa tena, familia zenye mzazi mmoja tu)
44. Wakati wanandoa wanapopatwa na matatizo katika mahusiano yao, lazima waweze kutegemea msaada na ufuatiliaji wa Kanisa. Uchungaji wa mapendo na huruma, vinaelekea kurekebisha watu na mahusiano. Mang’amuzi huonyesha kwamba, kwa msaada ufaao na kwa kitendo cha upatanisho, kwa neema, asilimia nyingi za migogoro ya kindoa zinapita kwa namna inayoridhisha. Kujua kusamehe na kujisikia kusamehewa ni mang’amuzi ya msingi katika maisha ya kifamilia. Msamaha kati ya wanandoa huwezesha kung’amua upendo ambao ni wa daima wala haupiti kamwe (rej. 1Kor 13:8). Mara nyingine lakini, huonekana kuwa vigumu, kwa yule aliyepokea msamaha wa Mungu, kutoa msamaha wa kweli unaompa tena binadamu furaha na nguvu ya kuishi.
45. Katika Sinodi mara nyingi limeonekana wazi hitaji la maamuzi jasiri ya kichungaji. Mababa wa Sinodi, wakiuthibitisha tena kwa nguvu uaminifu kwa Injili ya familia na wakitambua kwamba kutengana na kupeana talaka daima ni jeraha lisababishalo uchungu mkubwa kwa wanandoa wanaoishi hali hizo, na kwa wanao, wameona umuhimu wa kuvumbua njia mpya za kichungaji zinazoanzia kwenye hali halisi ya madhaifu ya kifamilia, kwa kujua kwamba, iliyo mara nyingi, wanandoa wanatendewa hayo kwa uchungu badala ya kuyachagua kwa hiari ya dhati. Yapo mazingira na hali tofauti kwa sababu za kibinafsi au za kiutamaduni na za kijamii na kiuchumi. Unahitajika mtazamo unaoelewa utofauti wa mazingira hayo kama alivyodokeza Mt. Yohane Paulo II (rej. Familiaris Consortio, 84).
46. Kwanza kabisa inabidi kusikiliza kila familia kwa heshima na upendo kwa kujifanya wenzi wa mwendo kama Kristo alivyofanya na wanafunzi njiani kwenda Emau. Katika nafasi za namna hiyo ni ya maana sana maneno ya Papa Fransisko: “Itakuwa lazima Kanisa liwaelimishe watu wake – mapadre, watawa na walei – katika “usanii huo wa kusindikiza”, ili wote wajifunze daima kuvua viatu mbele ya nchi takatifu iliyo mtu mwingine (rej. Kut 3:5). Tunatakiwa kuupa mwendo wetu mdundo safi wa ukaribu, pamoja na mtazamo wenye heshima na uliojaa huruma, ambao lakini, wakati huohuo, uponye, uweke huru na kutia moyo ili watu wakomae katika maisha ya Kikristo” (Evangelii Gaudium, 169).
47. Kupambanua kwa pekee kunahitajika sana ili kuwasindikiza kichungaji waliotengana, waliopeana talaka, waliotelekezwa. Hasa upokewe na kuthaminika uchungu wa walioachwa, waliopewa talaka au kutelekezwa bila kosa lao, au waliolazimishwa kuvunja maisha ya pamoja kwa sababu ya kupigwa na mwenzi wao. Kusamehe wakati mtu hajatendewa haki si kitu chepesi, lakini ni mwendo ambao neema inauwezesha. Hapo inaonekana hitaji la utume wa upatanisho na wa ushenga hata kwa kutumia vituo maalum vya kuwasikiliza wanandoa wenye matatizo vya kusimikwa katika majimbo. Vilevile inabidi kusisitiza daima kwamba ni jambo la msingi kuyabeba kwa namna iliyo na nia njema na ijengayo matokeo ya kutengana au ya kupeana talaka yanayoathiri watoto, ambao kwa vyovyote ni wahanga wasio na kosa wa tukio lile. Wao hawawezi kuwa “mali” ya kuigombania, na inabidi kutafuta taratibu zilizo nzuri zaidi ili waweze kusonga mbele baada ya mshtuko mkubwa wa kutengana kwa familia na waweze pia kukua kwa namna iliyo ya utulivu zaidi. Kwa vyovyote Kanisa litatakiwa kuonyesha wazi hali isiyo ya haki inayotokana mara nyingi na tendo la talaka. Mtazamo wa pekee unahitajika katika kuwasindikiza familia za mzazi mmoja, hasa inabidi wasaidiwe wanawake ambao wanatakiwa kubeba peke yao jukumu la kuendesha nyumba na malezi ya watoto.
48. Idadi kubwa ya Mababa wamesisitiza hitaji la kufanya taratibu za kutambua kisheria ubatili wa ndoa ziweze kupatikana kwa urahisi zaidi na zenyewe ziwe nyepesi zaidi, ikiwezekana zisiwe na ada. Kati ya mapendekezo yaliyotolewa yapo haya: kutambua hitaji la hukumu mbili zilizo sawa kuwa limepitwa na nyakati; uwezekano wa kuthibitisha njia ya kiutawala chini ya mamlaka ya Askofu wa Jimbo; kesi nyepesi zianzishwe kila mara ubatili ulipo wazi kabisa. Baadhi ya Mababa lakini hawakubaliani na mawazo hayo kwa sababu – kadiri yao – hayawezi kuhakikisha hukumu ya kuaminika. Lazima kusema tena kwamba katika nafasi hizo zote kisa ni kuhakikisha ukweli juu ya uhalali wa kifungo cha ndoa. Kadiri ya mapendekezo mengine ingebidi pia kuufikiria uwezekano wa kuitilia maanani zaidi nafasi ya imani ya wanaotarajia kufunga ndoa ili kuhalalisha sakramenti ya ndoa, kwa kushikilia kwamba, kati ya waliobatizwa, ndoa mara zote ni sakramenti.
49. Kuhusu kesi za ndoa, kurahisisha utaratibu – kama wengi walivyoomba – licha ya kudai kuwaandaa wafanyakazi wa kutosha (mapadre na walei wanaotakiwa kujituma kama kazi yao ya kwanza), kunadai pia kusisitiza juu ya wajibu wa Askofu wa jimbo, ambaye katika jimbo lake angeweza kukabidhi kazi hii kwa washauri watakaoandaliwa ipasavyo, ambao wataweza kushauri bure, pande zote mbili kuhusu uhalali wa ndoa yao. Kazi hiyo inaweza kutendwa na ofisi maalum, au na watu wenye utaalamu. (rej. Dignitas Connubii, kip. 113, 1).
50. Watu ambao wamepeana talaka lakini hawajaolewa au kuoa tena, ambao iliyo mara nyingi ni mashahidi wa uaminifu wa ndoa, wapewe moyo katika kutafuta kwenye Ekaristi chakula kinachowategemeza katika hali yao. Jumuiya mahalia na Wachungaji lazima wawasindikize watu hao kwa kuwajali, hasa kama wanakuwepo watoto au hali yao ya umaskini ni nzito.
51. Hata nafasi za waliopeana talaka halafu wakaoa au kuolewa tena zinadai kupambanuliwa kwa umakini sana na kusindikizwa kwa heshima kubwa, kwa kuacha kila lugha au msimamo ambao unawafanya wajisikie wanatengwa, na kwa kuhimiza ushiriki wao katika maisha ya jumuiya. Kwa jumuiya ya Kikristo kuwasaidia ndugu hawa si alama ya kudhoofika kwa imani na kwa ushuhuda wake kuhusu tabia ya kutokuvunjika kwa ndoa, bali jumuiya inaonyesha kabisa mapendo yake katika kutoa misaada hiyo.
52. Mababa wametafakari juu ya uwezekano wa kuwaruhusu kuungama na kupokea Ekaristi wale waliopeana talaka na baadaye wakaoa au kuolewa tena. Baadhi ya Mababa wa Sinodi wameusisitiza utaratibu uliopo sasa, kulingana na uhusiano wa msingi uliopo kati ya kushiriki Ekaristi na ushirika na Kanisa na mafundisho yake juu ya tabia ya kutokuvunjika ya ndoa. Wengine wamekubali kuwapokea kwenye meza ya Bwana baadhi ya wenye tatizo hilo, walio katika mazingira ya pekee na katika hali maalum, hasa kama ni nafasi ambapo haiwezekani kurudi nyuma na kama kuna faradhi za kimaadili juu ya wana ambao wangepata uchungu usio na haki. Kama kutakuwa na kurudi kwenye Sakramenti ingefaa iwepo safari ya toba chini ya madaraka ya Askofu wa Jimbo. Tena inabidi kupenya zaidi katika suala hili, kwa kuzingatia utofauti kati ya hali halisi ya dhambi na mazingira yanayopunguza uzito wa hatia, kwa vile “kumpa mtu kosa na wajibu katika kukosa vinaweza kupunguzwa au kuondolewa” na “sababu mbalimbali za kisaikolojia au kijamii” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 1735).
53. Mababa kadhaa wamesema kwamba watu waliopeana talaka na kuoa au kuolewa tena au wanaoishi unyumba bila ndoa wanaweza kutumia kwa faida komunyo ya kiroho. Wengine wamejiuliza kwa nini, basi, wasiweze kupokea hata ile ya kisakramenti. Kwa hiyo umesisitizwa haja ya kupenya zaidi katika mada hii ili kuonyesha zaidi upekee wa misimamo hiyo miwili na uhusiano wake na theolojia ya ndoa.
54. Masuala yahusuyo ndoa za mseto yameongelewa mara nyingi katika mazungumzo ya Mababa wa Sinodi. Utofauti wa utaratibu wa ndoa wa Makanisa ya Kiorthodoksi unaibua masuala nyeti katika nafasi fulani, ambayo yanadai kutafakariwa katika mazingira ya kiekumeni. Vilevile kuhusu ndoa za watu wa dini tofauti, utakuwa muhimu mchango wa mazungumzano na dini nyingine.
Uangalizi wa kichungaji kuhusu watu wenye mwelekeo wa kupendana jinsia moja
55. Familia nyingine wanaishi na mang’amuzi ya kuwa nao miongoni mwao watu ambao wana mwelekeo wa usenge. Kuhusu hilo kumekuwa na kujiuliza ni uangalizi gani wa kichungaji unaoweza kufaa mbele ya hali hiyo kwa kurejea jinsi Kanisa linavyofundisha: “Hakuna msingi wowote kwa ajili ya kuingiza au kuimarisha mfanano walau wa mbali, kati ya miungano ya kisenge na mpango wa Mungu juu ya ndoa na juu ya familia”. Papo hapo, wanaume na wanawake wenye mwelekeo wa usenge wanatakiwa kupokelewa kwa heshima na moyo. “Kuhusu hawa kila alama ya kubaguliwa kusiko kwa haki iachwe” (Idara kwa ajili ya Mafundisho ya Imani, Nadhari zihusuzo miradi ya utambuzi kisheria ya miungano kati ya wasenge, 4).
56. Na kwa vyovyote haikubaliki Wachungaji wa Kanisa washinikizwe toka nje katika hoja hizi na kwamba mashirika ya kimataifa yaziwekee Nchi maskini masharti katika mikopo ya kifedha ili zianzishe sheria za “ndoa” za watu wa jinsia moja.
Kuzaa watoto na changamoto ya udhibiti wa uzazi
57. Ni rahisi kugundua kuwepo kwa uenezi wa fikra zinazopunguza uzito wa kuzaa watoto hadi kuwa jambo mojawapo kati ya mengi katika mpango wa maisha wa mtu binafsi au wa jozi. Visa vya kiuchumi mara nyingine vinasukumiza kufanya uamuzi unaochangia kwenye kupunguza uzazi, jambo ambalo linadhoofisha mfumo wa jamii, na kutilia wasiwasi uhusiano kati ya vizazi na kusababisha kutokuwa na uhakika wa mtazamo wa zama zijazo. Utayari wa kupokea watoto ni hitaji la ndani kabisa la mapendo ya wanandoa. Katika mwanga huu, Kanisa linazitegemeza familia zinazowapokea, kuwalea na kuwakumbatia kwa upendo watoto wanaoonyesha kilema fulani.
58. Hata katika suala hili inatakiwa kuanza kwa kuwasikiliza watu, na kuwapa sababu za uzuri na ukweli za kuwa wazi bila masharti kupokea watoto, kwa vile upendo wa mwanadamu ndicho unachohitaji ili kuuishi katika utimilifu. Na kwa msingi huu inawezekana kuanzisha mafundisho yanayofaa juu ya njia za asili za uzazi mwajibifu. Hayo yatasaidia kuishi kwa mapatano na utambuzi umoja kati ya wanandoa, katika mapana yake yote, pamoja na wajibu wa uzazi. Ujumbe wa ile Insiklika Humanae Vitae ya Paulo VI, unaoweka mkazo wa ulazima wa kujali hadhi ya mtu katika kuzitathmini kimaadili njia za kupanga uzazi unatakiwa kufunuliwa upya. Kuasili watoto, yatima, na waliotelekezwa, wakichukuliwa kama watoto wao, ni njia ya pekee ya utume wa familia (rej. Apostolicam Actuositatem, 11), inayotajwa na kuhimizwa mara nyingi na Majistero (rej. Familiaris Consortio, 41; Evangelium Vitae, 93). Kuchagua kuasili au kukabidhiwa kwa muda mtoto ni namna ya pekee ya kuonyesha uwezo wa uzazi wa wanandoa, si pale tu ambapo familia hiyo inaathiriwa na utasa. Chaguo hilo ni alama wazi ya upendo wa kifamilia, fursa ya kushuhudia imani ya wazazi, na ya kurudisha hadhi ya kimwana kwa wale ambao hawakujaliwa kuwa nayo.
59. Inatakiwa kusaidia ili kuuishi upendo, hata katika vifungo vya kindoa, kama njia ya ukomavu, iliyo kumpokea zaidi na zaidi mwenzi na kujitoa daima kwa utimilifu zaidi. Ikumbukwe, kwa hali hiyo, kuwa kuna lazima ya kutoa njia za kimalezi zinazolisha maisha ya kindoa, pia ni muhimu kuwa na walei wanaotoa msaada wa usindikizaji kwa njia ya ushuhuda ulio hai. Bila shaka, mifano ya upendo aminifu na wa kina wenye matendo ya mahaba, ya heshima, unaoweza kuongezeka siku kwa siku, na ambao katika kujifunua hasa kwa tendo la uzazi wa watoto unang’amua fumbo linalozidi mipaka yetu, inatoa msaada mkubwa sana.
Changamoto ya malezi na wajibu wa familia katika uinjilishaji
60. Kwa hakika, moja ya changamoto za msingi zinazozikabili familia za leo ni ile ya malezi. Inadai kujishughulisha sana, kwa vile inavyokuwa na magumu mengi zaidi kutokana na hali halisi ya kiutamaduni wa sasa na athari kubwa za vyombo vya habari. Inatakiwa yazingatiwe kwa makini mahitaji na matarajio ya familia ambazo zinafanya bidii katika maisha ya kila siku kuwa mahali pa makuzi, pa kuzipokeza kwa namna hai na rahisi zile fadhila zinazofanya maisha ya mtu yawe na muundo unaokubalika na kupendeza. Kwa hiyo wazazi waweze kuchagua kwa hiari aina ya malezi na elimu ya kuwapa watoto wao kadiri ya kuamini kwao.
61. Kanisa lina jukumu lenye thamani la kuzitegemeza familia, likianzia na uingizwaji katika Ukristo, kwa njia ya jumuiya zenye kuzipokea. Kanisa lina wajibu, leo zaidi kuliko jana, katika mazingira tatanishi kama katika yale ya kawaida, wa kuwasaidia wazazi katika juhudi zao za kulea, wa kuwasindikiza watoto na vijana katika ukuaji wao kwa kupitia njia zinazogusa kila mmoja, zenye uwezo wa kuingiza katika maana kamili ya maisha na kuibua machaguo sahihi na uwajibikaji, ya kufanywa katika mwanga wa Injili. Maria, katika upendo wake mwororo, huruma, vionjo vya kimama, anaweza kulisha njaa ya ubinadamu na ya uhai, na kwa ajili ya hilo anaombwa na familia na taifa la Kikristo. Kazi ya kichungaji na ibada kwa Bikira Maria ni hatua ya kuanzia inayofaa kwa ajili ya utangazaji wa Injili wa familia.
Hitimisho
62. Matafakari haya yaliyopendekezwa, yaliyo tunda la kazi ya Sinodi iliyoadhimishwa kwa uhuru mkubwa na kwa mtindo wa kusikilizana, yanakusudia kutoa maswali na kuonyesha matazamio yatakayotakiwa kukomazwa na kuwekwa bayana kutokana na tafakari ya Makanisa mahalia katika mwaka huu hadi kuufikia adhimisho la Mkutano wa Jumla wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu unaotarajiwa kufanywa mnamo mwezi wa Oktoba 2015, wenye dhamira kuu ya wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu wa leo. Haya si maamuzi yaliyokamilika tayari, wala si matarajio mepesi. Hata hivyo safari ya kiurika ya maaskofu na kuhusika kwa taifa lote la Mungu chini ya utendaji wa Roho Mtakatifu, kwa kuangalia kielelezo cha Familia Takatifu, vinaweza kutuongoza kupata njia za ukweli na za huruma kwa ajili ya wote. Ni matashi mema ambayo Papa Fransisko, tangu mwanzo wa kazi zetu za kisinodi, ametuelekezea akitualika kujipa moyo wa imani na kuwa wazi kuupokea, kwa unyenyekevu na unyofu, ukweli katika mapendo.
MASWALI kwa ajili ya upokeaji
na tafakari ya kina
juu ya Relatio Synodi
Swali tangulizi la ujumla linalohusu sehemu zote za Relatio Synodi
Taswira ya hali halisi ya familia kadiri inavyotolewa na Relatio Synodi ndiyo ile inayoonekana wazi katika Kanisa na katika jamii ya leo? Kuna mambo mengine ambayo inawezekana kuyaongeza?
Sehemu ya Kwanza
Usikivu: Mazingira na changamoto juu ya familia
Kama ilivyoelezwa katika utangulizi (na. 1-4), Sinodi isiyo ya kawaida ilinuia kuzielekea familia zote za ulimwengu, na kutaka kushiriki katika furaha, magumu na matumaini yao. Halafu Sinodi iliziangalia kwa mtazamo wa shukrani za pekee familia zilizo nyingi za Kikristo ambazo zinaishi kiaminifu wito wao, na kuzihimiza kujituma hata zaidi katika wakati huu wa “Kanisa litokalo nje yake”, kwa kujitambua kuwa mtendaji wa msingi wa uinjilishaji, hasa katika kuichochea ndani yao na ndani ya familia zenye matatizo ile “hamu ya kuwa na familia” inayodumu kuwa hai daima na ambayo ni msingi ya kuamini kuwa ni ya lazima sana “kuanzia tena na familia” ili kukitangaza kwa mafanikio kiini cha Injili.
Mwendo mpya uliowekwa na Sinodi isiyo ya kawaida umo ndani ya mazingira mapana zaidi ya kikanisa yaliyoelezwa na Wosia wa Kitume Evangelii Gaudium wa Papa Fransisko, yaani, kwa kuanzia na “mahali ambapo watu huishi pembezoni” (watu waliosahaulika), kwa kufanya uchungaji wenye kauli mbiu ya “utamaduni wa kukutana”, ulio na uwezo wa kutambua kazi huru ya Bwana hata nje ya miundo yetu ya fikra za kawaida, na kushikilia, bila kusita, hali ya “hospitali ya mkoba”, hali ambayo inafaa sana kwa tangazo la huruma ya Mungu. Namba za sehemu ya kwanza ya Relatio Synodi zinatoa majibu kwa changamoto hizo. Nazo zinatoa picha ya jumla kuhusu hali halisi ya familia za leo inayoweza kusaidia ili kuendeleza tafakari ya kina.
Maswali yanayotolewa hapa chini, yenye kurejea yaliyotamkwa katika sehemu ya kwanza ya Relatio Synodi, yanakusudia kurahisisha kazi ya Mabaraza ya Maaskofu katika kutafakari kwao, ili kuepukana na mtindo wa kutoa majibu kadiri ya fikra na matazamio yanayoendana na uchungaji wenye lengo tu la kutekeleza mafundisho, jambo ambalo lisingeheshimu mahitimisho ya Mkutano wa kisinodi uliofanyika, na kuisogeza tafakari yao mbali na mwendo uliokwisha kuwekwa tayari.
Mazingira ya kijamii na kitamaduni (na. 5-8)
1. Ni mipango mkakati gani inayotumika na ile inayopendekezwa kwa mbeleni ili kukabiliana na changamoto juu ya familia zinazotokana na ukinzani wa kitamaduni (rej. na. 6-7): ile inayoelekea kuamsha utambuzi wa uwepo wa Mungu katika maisha ya familia; ile inayolenga kulea na kuimarisha mahusiano thabiti kati ya watu; ile inayokusudia kuchochea sera za kijamii na kiuchumi zinazozifaa familia; ile inayopunguza magumu yanayojitokeza wakati wa kuwatunza watoto, wazee na ndugu walio wagonjwa; ile inayosaidia kukabiliana na mazingira maalum ya kitamaduni ambamo Kanisa mahalia huishi?
2. Mbinu gani za kufanyia uchambuzi hutumiwa, na matokeo muhimu gani yamepatikana kuhusiana na mabadiliko (hasi na chanya) ya kianthropolojia na kitamaduni?(rej. na. 5) Kati ya matokeo yaliyoainishwa inawezekana kugundua kuwepo mambo ya pamoja katika uwingi wa tamaduni?
3. Pamoja na kuihubiri Injili na kukosoa hali zenye matatizo, Kanisa limechagua njia gani ili kuwa karibu “kama Kanisa” na familia zenye hali tata hizo? (rej. na. 8). Je, kuna mikakati gani ya kimalezi ili kuzuia hali hizo zisijitokeze? Inawezekana kufanya nini ili kuzitegemeza na kuimarisha familia za wakatoliki, walio waaminifu kwa kifungo cha ndoa?
4. Kwa namna gani Kanisa katika utendaji wake wa kichungaji linajibu changamoto za utamaduni unaohalalisha kila kitu unaoenea katika jamii iliyoacha imani kwa Mungu, pia na taswira ya familia iliyoundwa na mwanamume na mwanamke walioungana kwa kifungo cha ndoa na iliyo tayari kuzaa watoto?
Umuhimu wa maisha ya upendo (na. 9-10)
5. Kwa namna gani, na kwa kufanya nini familia za Kikristo zinashirikishwa katika kutoa ushuhuda mbele ya vizazi vipya juu ya maendeleo katika ukomavu wa upendo? (rej. na. 9-10). Kuhusiana na mada hizo, kwa namna gani itawezekana kuboresha malezi ya wahudumu wenye Daraja takatifu? Ni watendaji gani wa kiuchungaji, walioandaliwa kwa namna maalumu, ambao wanahitajika hasa?
Changamoto kwa uchungaji (n. 11)
6. Kwa kiwango gani, na kwa mbinu gani, uchungaji wa kawaida wa familia huwaelekea walio mbali na Kanisa? (rej. na. 11). Mchakato gani wa kiutendaji umeandaliwa ili kuchochea na kuhimiza ile “hamu ya kuwa na familia” iliyopandwa na Mungu Muumbaji katika moyo wa kila mtu – na iliyo hai hasa katika vijana – pia moyoni mwa walio katika hali ya kifamilia zisizoendana na mtazamo wa Kikristo? Hawa wanauitikia kwa namna gani utume wa Kanisa kwa ajili yao? Ni kubwa kiasi gani idadi ya ndoa za asili kati ya wasiobatizwa, pia kuhusiana na hamu ya vijana ya kuwa na familia?
Sehemu ya Pili
Kumtazama Kristo: Injili ya familia
Injili ya familia, inayohifadhiwa kiaminifu na Kanisa katika mkondo wa Ufunuo wa Kikristo ulioandikwa na uliorithishwa, hudai kutangazwa katika ulimwengu wa leo kwa furaha na matumaini mapya, kwa kumkazia daima macho Yesu. Wito na utume wa familia una nafasi kamilifu katika mpango wa uumbaji unaotimilika katika ule wa ukombozi, kwa jinsi ambavyo Mtaguso ulipendekeza kimuhtasari kwa kutamka kwamba: “wanandoa wenyewe, walioumbwa kwa sura ya Mungu aliye hai na waliowekwa katika hadhi halisi ya kila mtu, waunganishwe kwa upendo ulio sawa wa kila mmoja kwa mwenzie, na nia moja na hatimaye utakatifu wa pamoja. Na hivyo watamfuata Kristo aliye asili ya uzima katika furaha na majitoleo ya wito wao. Na kwa njia ya upendo wao mwaminifu wapate kuwa mashahidi wa lile fumbo la pendo ambalo Bwana amelifunua kwa ulimwengu, kwa njia ya kifo na ufufuko wake” (Gaudium et Spes, 52; taz. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 1533-1535).
Katika mwanga huo, maswali yanayotokana na Relatio Synodi yanakusudia kuwahimiza Wachungaji na watu wa Mungu ili watoe majibu aminifu na hodari kwa ajili ya kutangaza upya Injili ya familia.
Mtazamo juu ya Yesu na malezi ya Mungu katika historia ya wokovu (na. 12-14)
Kwa kupokea mwaliko wa Papa Fransisko, Kanisa linamtazama Kristo katika ukweli wake unaodumu daima na katika upya wake usio na kikomo, mwenye kuangaza pia kila familia. Kristo ndiye "Injili ya milele" (Ufu 14:6) ;yeye "ni yuleyule jana na leo na hata milele" (Ebr 13:8), lakini utajiri wake na uzuri wake haviwezi kwisha. Yeye daima ni kijana na ni chanzo endelevu cha upya” (Evangelii Gaudium, 11).
7. Kumtazama Kristo kunafungua nafasi zilizo mpya. “Kwa maana, kila tunaporudi kwenye chemchemi ya maisha ya Kikristo hufunguka mbele yetu njia zilizo mpya na nafasi tusizofikiria kabla” (na. 12). Mafundisho ya Maandiko Matakatifu hutumiwa kwa namna gani katika kazi ya kichungaji kwa ajili ya familia? Kwa kiasi gani mtazamo huo juu ya Kristo unasitawisha uchungaji wa familia ulio hodari na aminifu?
8. Vijana na wanandoa wanaona kuwa katika maisha yao zimetimilizwa tunu gani za ndoa na za familia? Na tunu hizo zinachukua sura na muundo gani? Zipo tunu ambazo zaweza kuangazwa? (rej. na. 13). Ni nyanja gani za dhambi zinazotakiwa kuepukana nazo na kuzishinda?
9. Malezi na mafundisho gani ya kibinadamu yanatakiwa kuzingatiwa – kwa kulandana na malezi na mafundisho ya Mungu – ili kuelewa kwa usahihi zaidi ni nini ambacho uchungaji wa Kanisa unapaswa kuwa kwa ajili ya ukomavu wa maisha ya pamoja ya mwanamume na mwanamke, kuelekea ndoa hapo mbeleni? (rej. na. 13).
10. Nini kifanyike ili kuonyesha ukuu na uzuri wa zawadi ya ndoa isiyovunjika, ili kuweza kuchochea hamu ya kuiishi na kuijenga zaidi na zaidi? (rej. na. 14)
11. Kwa namna gani watu wangeweza kusaidiwa kuelewa kuwa uhusiano na Mungu huwezesha wanandoa kuyashinda madhaifu yaliyomo pia katika mahusiano ya kindoa? (rej. na. 14). Kwa namna gani utolewe ushuhuda kwamba baraka ya Mungu inasindikiza kila ndoa iliyo kweli? Kwa jinsi gani idhihirishwe kuwa neema ya kisakramenti inawategemeza wanandoa katika mwendo mzima wa maisha yao?
Familia katika mpango wa Mungu wa wokovu (na. 15-16)
Wito wa mapendo uliomo katika mwanamume na mwanamke kutokana na uumbaji wao, hupata namna yake kamilifu kutoka kwa tukio la Pasaka ya Kristo Bwana, aliyejitoa kikamilifu, akafanya Kanisa kuwa Mwili wake katika fumbo. Ndoa ya Kikristo, kwa kuchota neema ya Kristo, inakuwa njia ambayo wale wenye wito huo, wanatembea juu yake kuelekea ukamilifu wa mapendo, ulio utakatifu.
12. Kwa namna gani inawezekana kusaidia kuelewa kwamba ndoa ya Kikristo ni kadiri ya agizo la asili la Mungu, na kwamba - kutokana na hilo - ni nafasi ya kung'amua utimilifu, wala si mipaka? (rej. na. 13).
13. Kwa namna gani familia inaweza kutambuliwa kama “Kanisa la nyumbani” (rej. LG 11), mtendaji na mlengwa wa kazi ya uinjilishaji kwa kuutumikia Ufalme wa Mungu?
14. Kwa jinsi gani inawezekana kuhimiza juhudi hiyo ya kimisionari ya familia?
Familia katika hati za Kanisa (na. 17-20)
Majisterio (Mafundisho rasmi) ya Kanisa inatakiwa kujulikana kwa kina zaidi kwa Watu wa Mungu katika utajiri wake wote. Maisha ya kiroho ya wanandoa hulishwa na mafundisho endelevu wa Wachungaji, wenye kuwachunga kundi la waamini, na hukomazwa kwa kusikiliza Neno la Mungu bila kuchoka, kwa kupokea sakramenti za imani, na kwa kuishi mapendo.
15. Familia za Kikristo huishi mbele ya mtazamo wa upendo wa Bwana na katika uhusiano na Yeye hukua kama ushirika wa maisha na upendo. Kwa namna gani inawezekana kusitawisha maisha ya kiroho ya familia, na kwa jinsi gani familia zisaidiwe ili ziwe mahali pa maisha mapya katika Kristo? (rej. na. 21).
16. Mbinu gani za kikatekesi zibuniwe na kuhamasishwa zenye kujulisha na kusaidia kuishi mafundisho ya Kanisa kuhusu familia, kwa lengo la kupunguza umbali uliopo baina ya maisha halisi ya watu na imani inayoungamwa, pamoja na kuongoza kwenye miendo ya toba?
Tabia ya kutokuvunjika ya ndoa na furaha ya kuishi pamoja (na. 21-22)
“Upendo halisi wa kindoa unachukuliwa ndani ya upendo wa kimungu na unategemezwa na kutajirishwa na nguvu yenye kukomboa ya Kristo pamoja na utendaji wa wokovu wa Kanisa. Hivyo, wanandoa kweli wanaongozwa kwa Mungu, wanasaidiwa na kuimarishwa katika jukumu lao bora la kuwa baba na mama. Kwa sababu hiyo, wakristo wanandoa wanatiwa nguvu na kama kuwekwa wakfu na sakramenti maalumu kwa ajili ya wajibu na hadhi ya hali yao. Nao wanapata kutekeleza wajibu wao wa kindoa na wa kifamilia kwa nguvu ya sakramenti hii, wakipenyezwa na Roho wa Kristo ambaye kwake maisha yao yote yanajazwa imani, tumaini na mapendo. Na hatimaye wanaelekea kuufikia ukamilifu wao, kila mmoja akimtakatifuza mwenzake; na hivyo wanashirikiana pamoja katika kumtukuza Mungu” (Gaudium et Spes, 48).
17. Njia gani zitumike ili kufahamisha thamani ya ndoa isiyovunjika na yenye kuzaa kama mwendo wa utimilizaji kamili wa mtu? (rej. na. 21).
18. Inawezekana kufanya nini ili kuonyesha kwamba familia – kwa namna nyingi – ndiyo mahali pa pekee pa kung’amua furaha kama wanadamu?
19. Mtaguso wa Vatikano II ulipenda kutamka sifa za ndoa ya asili, kwa kuendeleza mafundisho ya kimapokeo ya awali ya kikanisa. Kwa kiasi gani utendaji wa kichungaji katika majimbo unaweza kuthamini pia hekima hii ya watu, kama kitu cha msingi katika utamaduni na jamii ya kawaida? (rej. na. 22).
Ukweli na uzuri wa familia, na huruma kwa familia dhaifu na zilizojeruhiwa (na. 23-28)
Baada ya kutazama uzuri wa ndoa zilizofanikiwa na wa familia zilizo thabiti, pamoja na kufurahi kwa ushuhuda madhubuti wa wale waliodumu waaminifu kwa kifungo cha ndoa hata baada ya kuachwa na mwenzie, Wachungaji waliokusanyika katika Sinodi wamejiuliza – kwa wazi na uhodari, wala si bila uchungu na uangalifu – ni kwa mtazamo gani Kanisa linatakiwa kuwashughulikia wale wakatoliki ambao wamefunga ndoa ya kiserikali tu, wale ambao bado wanaishi pamoja tu bila ndoa, na kwa wale ambao, baada ya kuwa walifunga ndoa halali kanisani, halafu wakatalakiana na kufunga ndoa tena ya kiserikali.
Pamoja na kutambua mipaka na mapungufu yaliyo wazi katika hali hizo mbalimbali, Mababa wa Sinodi walishika kwa mtazamo chanya njia aliyodokeza Papa Fransisko, ambayo kadiri yake “bila kupunguza thamani ya mtazamo wa kiinjili, inatakiwa kusindikiza kwa huruma na subira hatua zinazowezekana za ukuaji wa watu zinavyojitokeza siku kwa siku” (Evangelii Gaudium, 44).
20. Kwa namna gani inawezekana kuwasaidia watu kutambua kwamba hakuna mtu yeyote aliyetengwa mbali na huruma ya Mungu? Na inawezekanaje kueleza ukweli huo katika utendaji wa kichungaji wa Kanisa kwa ajili ya familia, hasa zile dhaifu na zilizojeruhiwa? (rej. na. 28).
21. Kwa habari ya watu ambao hawajafikia hatua ya kuelewa kikamilifu zawadi ya upendo wa Kristo, waamini wanaweza kuwaonyesha kwa jinsi gani moyo wa kuwapokea na kuwasindikiza kwa tumaini, bila kuachana kamwe na wajibu wa kutangaza madai ya Injili? (rej. na. 24).
22. Inawezekana kufanya nini ili watu wanaoishi katika aini mbalimbali ya maisha ya pamoja – ambamo huwezekana kugundua uwepo wa thamani za kiutu – mwanamume na mwanamke wahisi kuwepo katika Kanisa heshima, imani na nia ya kuwatia moyo ili wazidi kukua katika wema, na wapate kuufikia utimilifu wa ndoa ya Kikristo? (rej. na. 25).
Sehemu ya 3
Kukabiliana na hali halisi: mitazamo ya kichungaji
Katika kutafakari kwa kina sehemu ya tatu ya Relatio Synodi, ni muhimu wote waongozwe na mageuzi ya kichungaji ambayo Sinodi isiyo ya kawaida imeanza kuyadokeza, huku ikiweka misingi yake katika Mtaguso Mkuu wa Vatikano II na katika majisterio (mafundisho rasmi) ya Papa Fransisko. Ni wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu kuzidi kuitafakari kwa kina sehemu hiyo, kushirikisha kama ipasavyo viungo vyote vya kikanisa katika kazi hiyo, hadi kupendekeza maoni kutokana na mazingira yao maalum. Lazima wote tujitahidi sana tusije tukajikuta tena mwanzoni mwa safari, bali tutambue hatua zilizopigwa katika Sinodi isiyo ya kawaida, na tuendelee toka huko.
Kutangaza Injili ya familia leo, katika mazingira mbalimbali (na. 29-38)
Kutokana na haja ya kuwa na familia, lakini pia kutokana na changamoto nyingi na ngumu zilizomo katika ulimwengu wa sasa, Sinodi imesisitiza umuhimu wa kuwa na ari mpya kwa ajili ya kutangaza Injili ya familia, kwa namna wazi na yenye maana.
23. Katika malezi ya mapadre na ya wahudumu wengine wa kichungaji, ina uzito gani maisha ya kifamilia? Je, familia zenyewe zinahusishwa katika malezi hayo?
24. Je, tunao utambuzi kwamba mabadiliko ya haraka ya jamii yetu yanadai kuwa waangalifu daima kuhusu msamiati wa kutumiwa katika mawasiliano ya kichungaji? Kwa jinsi gani inawezekana kushuhudia kwa mafanikio ukuu wa neema, ili maisha ya kifamilia yapangwe na kutimizwa kama nafasi ya kumpokea Roho Mtakatifu.
25. Katika kutangaza Injili ya familia, tufanye nini kusudi kuwa na mazingira ambapo kila familia iwe kadiri ya mapenzi ya Mungu, na pia itambulike kijamii katika hadhi yake na utume wake? “Uongofu wa kichungaji” na uchunguzi mpya na wa kina upi hutakiwa kutekeleza ili kufikia lengo hilo?
26. Je, tunatambua umuhimu wa ushirikiano na asasi za kijamii na za kisiasa katika kazi ya kuhudumia familia? Ushirikiano huo unatekelezwa vipi? Twapaswa kuvifuata vigezo gani? Kwa jinsi gani vyama vya familia vyaweza kuchangia katika hayo? Ushirikiano huo uendane vipi na haja ya kuzilaumu shurutu za kitamaduni, za kiuchumi na za kisiasa, zinazokwaza maisha halisi ya kifamilia?
27. Jinsi gani inawezekana kusaidia uhusiano kati ya familia, jamii na siasa kwa manufaa ya familia? Kwa jinsi gani kuhamasisha tegemeo la jumuiya ya kimataifa na la Dola kwa familia?
Kuwaongoza wachumba katika safari ya maandalizi kwa sakramenti ya ndoa (na. 39-40)
Sinodi imetambua hatua zilizopigwa katika miaka hii ya mwisho ili kuyasaidia maandalizi ya kufaa ya vijana kwa sakramenti ya ndoa. Lakini Sinodi imesisitiza pia haja ya juhudi kubwa zaidi za jumuiya nzima ya Kikristo si kwa maandalizi tu, bali pia kwa miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa.
28. Je, hatua za maandalizi kwa sakramenti ya ndoa ziweje ili kusisitiza wito na utume wa familia kadiri ya imani katika Kristo? Hatua hizo ni msaada kweli ili watu wapate kushiriki maisha halisi ya kikanisa? Inawezekana kufanya nini ili kuzipyaisha na kuziboresha?
29. Jinsi gani katekesi ya kisakramenti ya kuingizwa katika Ukristo inajumuisha pia safari kuelekea wito na utume wa familia? Hatua gani ni za dharura zaidi? Kwa namna gani inawezekana kuonyesha uhusiano wa Ubatizo - Ekaristi na Ndoa? Kwa jinsi gani isisitizwe kwamba mara nyingi hatua za maandalizi kwa sakramenti ya ndoa zina kwa kweli tabia ya ukatekumeni na ya mistagojia (mafundisho juu ya mafumbo ya imani)? Kwa jinsi gani inawezekana kuhusisha jumuiya ya Kikristo katika maandalizi hayo?
Kuisindikiza miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa (n. 40)
30. Katika maandalizi kwa sakramenti ya ndoa na katika kusindikiza miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa, mchango muhimu wa ushuhuda na wa tegemeo ambao familia, harakati na vyama vya kifamilia vinaweza kuutoa, je, unatumiwa kama ipasavyo? Kuhusu hayo, je, mang’amuzi chanya gani yanastahili kutajwa?
31. Katika majadiliano ya kisinodi imesisitizwa kwamba uchungaji wa kuwasindikiza majozi miaka ya kwanza ya ndoa inabidi uendelezwe zaidi. Kuhusu hilo, mambo gani yenye maana zaidi yamekwisha kutimizwa? Tena, mambo gani lazima yaendelezwe katika ngazi ya parokia na ya jimbo, na pia katika vyama na harakati?
Uangalizi wa kiuchungaji kwa ajili ya wanaoishi katika ndoa ya kiserikali, au wanaoishi pamoja bila ndoa (na. 41-43)
Katika majadiliano ya kisinodi, imesisitizwa kwamba pana hali zenye kutofautiana, kutokana na mambo mbalimbali ya kitamaduni, na ya kiuchumi, desturi zenye mizizi katika mila na mapokeo, ugumu wanaoona vijana katika kufanya maamuzi yanayowafunga kwa maisha yote.
32. Kwa ajili ya kufanya upambanuzi sahihi wa kichungaji kuhusu hali hizo mbalimbali za watu, vigezo gani vizingatiwe katika mwanga wa mafundisho ya Kanisa, ambayo yanakazia kuwa mambo ya msingi ya ndoa ni umoja, tabia ya kutokuvunjika na kuwa tayari kuzaa watoto?
33. Jumuiya ya Kikristo ipo tayari kuhusishwa kichungaji katika hali hizo? Kwa jinsi gani jumuiya ya Kikristo inawasaidia watu wanaoishi katika ndoa ya kiserikali wapate kupambanua mambo chanya yaliyotajwa hapo juu na yale hasi katika maisha yao, kwa namna ya kuwaelekeza na kuwategemeza katika mwendo wa ukuaji na uongofu kuelekea sakramenti ya ndoa? Kwa namna gani kuwasaidia watu wanaoishi pamoja bila ndoa waamue kufunga ndoa?
34. Hususan, jibu gani litolewe kwa masuala yanayohusiana na kuwepo hadi leo kwa aina za ndoa za jadi katika hatua, tena zinazopangwa na wazee wa koo husika?
Kuwatibu familia zilizojeruhiwa (wanandoa waliotengana, waliotalakiana, waliotalakiana na kuoa au kuolewa tena, familia zenye mzazi mmoja tu) (nn. 44-54)
Katika majadiliano ya kisinodi, imetiliwa mkazo juu ya uchungaji unaoendeshwa na “usanii wa kusindikiza”, kwa kuupa “mwendo wetu mdundo safi wa ukaribu, pamoja na mtazamo wenye heshima na uliojaa huruma, ambao lakini, wakati huohuo, uponye, uweke huru na kupa moyo ili watu wakomae katika maisha ya Kikristo” (Evangelii Gaudium, 169).
35. Je, jumuiya ya Kikristo ipo tayari kuzijali familia zilizojeruhiwa, zipate kuonja huruma ya Baba? Juhudi gani zaweza kufanyika ili kuondoa mambo yale ya kijamii na kiuchumi ambayo mara nyingi yanasababisha jeraha hizo? Jumuiya ya Kikristo imepiga hatua gani kwa ajili ya ukuaji wa kazi hiyo na wa utambuzi wa kimisionari unaoitegemeza? Tena ni hatua gani ambazo bado inapaswa kuzifanya?
36. Kwa jinsi gani inawezekana kuhamasisha kazi ya kutafuta njia za kichungaji zinazokubalika katika ngazi ya Makanisa mahalia? Na kuhusu njia hizo, kwa jinsi gani inawezekana kuendeleza mazungumzano kati ya Makanisa mahalia “pamoja na Petro na chini ya Petro”?
37. Kwa namna gani taratibu za kutambua kisheria ubatili wa ndoa zaweza kufanywa zipatikane kwa urahisi zaidi na zenyewe ziwe nyepesi zaidi, ikiwezekana bila ada? (na. 48).
38. Uchungaji wa kisakramenti kuhusu watu waliopeana talaka na baadaye wakaoa au kuolewa tena, unahitaji uchunguzwe zaidi, kwa kutathmini pia utaratibu wa ndoa wa Makanisa ya Kiorthodoksi, na “kwa kuzingatia utofauti kati ya hali halisi ya dhambi na mazingira yanayopunguza uzito wa hatia” (na. 52). Matazamio gani yauelekeze uchungaji? Inawezekana kupiga hatua gani? Je, mapendekezo gani yafaa ili kuondoa vizuizi visivyo vya lazima, wala visivyohitajika?
39. Je, utaratibu wa sasa unawezesha kutoa majibu ya kufaa kwa changamoto zilizotoka katika ndoa ya watu wa dini tofauti, tena katika ndoa za mseto? Au inabidi kuzingatia mambo mengine?
Uangalizi wa kichungaji kuhusu watu wenye mwelekeo wa kupendana jinsia moja (na. 55-56)
Uangalizi wa kichungaji kuhusu watu wenye mwelekeo wa kupendana jinsia moja unaleta leo changamoto mpya, ambazo zinatokana pia na jinsi haki zao zinavyopendekezwa kijamii.
40. Jinsi gani jumuiya ya Kikristo inaelekeza uangalizi wake wa kichungaji kwa familia walio nao miongoni mwao watu wenye mwelekeo wa usenge? Kwa jinsi gani, katika mwanga wa Injili, na kwa kuepuka kila alama ya ubaguzi, inabidi kuwajali watu walio katika hali hiyo? Kwa namna gani kuwaonyesha madai ya mapenzi ya Mungu katika hali yao?
Kuzaa watoto na changamoto ya udhibiti wa uzazi (na. 57-59)
Kuzaa watoto ni jambo la msingi la wito na utume wa familia: “Wanandoa wanajua kuwa ni washiriki wa upendo wa Mungu Muumba na wafasiri wake kwa njia ya wajibu wa kuuendeleza uhai wa binadamu na kuulea; nao hauna budi kutazamwa kama utume wao maalumu” (Gaudium et Spes, 50).
41. Hatua zipi, zilizo za maana zaidi zimepigwa ili kutangaza na kuhamasisha kwa mafanikio utayari wa kuzaa watoto na uzuri na hadhi ya kibinadamu ya kuwa mama au baba, katika mwanga, kwa mfano, wa Insiklika Humanae Vitae ya Mwenyeheri Paulo VI? Kwa jinsi gani inawezekana kuhamasisha mazungumzano na ulimwengu wa sayansi na tekinolojia za biomedikali, kusudi isivukwe mipaka ya namna ya kimaumbile ya binadamu ya kuzaa?
42. Umama na ubaba usiojinyima watoto huhitaji kutegemezwa kwa njia ya miundo na vyombo vya kijamii. Je, jumuiya ya Kikristo inaonyesha moyo wa mshikamano na ushirikiano kwelikweli? Kwa jinsi gani? Je, jumuiya ya Kikristo ina ujasiri katika kupendekeza majawabu yenye nguvu kijamii na kisiasa pia? Kwa njia gani kuhamasisha kuasili au kukabidhiwa kwa muda watoto kama alama kuu ya ukarimu wenye kuzaa? Kwa jinsi gani kuhamasisha matunzo na heshima kwa watoto?
43. Kwa mkristo kuwa mama au baba ni kuujibu wito. Wito huo unatiliwa mkazo katika katekesi kwa namna ya kutosha? Njia gani za malezi zinatolewa ili wito huo uongoze kwa kweli dhamiri za wanandoa? Pana utambuzi juu ya matokeo mazito ya mabadiliko ya kidemografia (habari za idadi ya watu)?
44. Kwa jinsi gani Kanisa linapiga vitu dhidi ya balaa ya kutoa mimba kwa kueneza utamaduni wenye nguvu wa uhai?
Changamoto ya malezi na wajibu wa familia katika uinjilishaji (na. 60-61)
45. Kwa wazazi, utume wa kulea si daima jukumu lililo rahisi: je, katika jumuiya ya Kikristo wanapata mshikamano na tegemeo? Njia gani za malezi zipendekezwe? Tupige hatua gani ili jukumu la wazazi la kuwalea watoto litambuliwe pia kijamii na kisiasa?
46. Kwa namna gani wazazi na familia za Kikristo huweza kusaidiwa kutambua kwamba wajibu wa kurithisha imani ni jambo halisi la kuwa Mkristo?
© Haki nakili 2014 – Ukatibu Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu
Hati hii huweza kunukuliwa na kutafsiriwa na Mabaraza ya Maaskofu au kwa idhini yao, kama yaliyomo hayababilishwi kwa namna yoyote ile, na nakala mbili za yenyewe hupelekwa kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu, 00120 Mji wa Vatikano.
Hati hii imetafsiriwa na hati asili ya Kiitaliano.